Friday, June 14, 2013

Mgombea udiwani TLP atimkia Chadema

Mgombea udiwani Kata ya Elerai Manispaa ya Arusha kwa tiketi ya Chama cha Tanzania Labour(TLP), Boysafi  Peter Shirima jana alitangaza kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akitangaza uamuzi huo mbele ya umati wa watu, waliohudhuria mkutano wa hadhara wa kampeni zinazoendelea  katika kata hiyo, alidai kuwa amejitoa katika chama hicho kutokana na chama kushindwa kuzindua kampeni za kumnadi licha ya kuwa mgombea kwa mkoa mzima wa Arusha.

“Mimi ni mgombea pekee kwa chama hiki  kwa sababu ni peke yangu niliyesimama kwa nia dhabiti na kupeperusha bendera ya TLP lakini viongozi wa chama hiki wameshindwa kabisa kunipa ushirikiano...  sasa naondoka na naomba wapiga kura wangu wote pigieni Chadema (Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),”alisema.

Alisema sababu nyingine iliyomwondoa katika chama hicho ni kukosa ushirikiano kwa viongozi na kumwacha peke yake kunadi sera za TLP.

Alisema kabla ya kuandika barua zake za kujiondoa ambazo atazipeleka kwa Afisa Mtendaji wa kata hiyo, aliangalia sera za mgombea wa Chadema na kuona zinafanana na zake, hivyo ameamua kumwongezea nguvu ili kushinda kwa ajili ya kutekeleza sera hizo kwa wananchi.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema  chama icho kimefurahishwa kuona mgombea huyo ameamua mapema

kujisalimisha mahali salama na kuondokana na propaganda na kwamba wanamkaribisha kwa mikoni miwili wawatumikie wananchi. 

 “Huyu mgombea amesikiliza Chadema ameona sera na maneno yetu yanaendana na ukweli na siyo kama vyama vingine wanaongea mengine

lakini matendo tofauti... tunamkaribisha kupigania haki za wananchi,”alisema.
Baada ya Shirima kujiengua katika kinyanyang'anyito hicho,  Mhandisi Jeremiah Mpinga wa Chadema sasa atachukuana wagombea vyama vya CUF na CCM.

No comments:

Post a Comment