MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ameiponda Bajeti ya Serikali kwa madai kuwa haina jipya na wala haina nia njema ya kupunguza umaskini kwa Mtanzania.
Kauli hiyo aliitoa jana, muda mfupi katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima baada ya kumalizika kusomwa kwa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2013/14 iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa.
Mbowe alisema kuwa bajeti ambayo imesomwa na serikali licha ya kushangiliwa na wabunge wa CCM haina makusudi ya kuwasaidia Watanzania ambao ni maskini na badala yake wamewatwisha mzigo kwa kupandisha bei ya mafuta.
“Tumekuwa tukishuhudia kila mwaka serikali inaweka kodi katika vinywaji pamoja na sigara lakini inashindwa kueleza ni kwa jinsi gani wanaweza kupata mapato kutoka katika rasilimali mbalimbali ambazo zipo nchini kama vile madini, utalii pamoja na vyanzo vingine vya mapato,” alisema Mbowe.
Mbali na hilo, Mbowe alisema serikali bado inaendelea kuwa na matumizi makubwa na hilo wanalifanya kwa makusudi huku wakiwakomoa wananchi ambao wana kipato kidogo kwa kupandisha ushuru wa magari pamoja na mafuta.
Naye Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), alisema kuwa pamoja na nyongeza kidogo ya mapato ya bajeti, serikali bado imeendeleza na utamaduni wa kuongeza bei kwa vyanzo vile vile vya pombe, sigara, mafuta na magari wakati vyanzo vinavyohusu rasilimali za nchi kama madini pamoja na makampuni makubwa, misamaha mingi bado haijaondolewa na mfumo wa kuyabana haujatangazwa.
Alisema kitendo cha serikali kuongeza kodi katika mafuta ya petroli na dizeli za aina tatu kwa wakati mmoja, kitachangia ongezeko la kupanda kwa gharama za maisha ikiwa ni pamoja na kupanda kwa nauli.
Alisema serikali haijaonesha mkakati madhubuti wa kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima katika bajeti ya sh trilioni 18.2 kwenye mapato na matumizi na asilimia 40 kupotea kutokana na matumizi mabaya kama ilivyo kuwa ikitokea katika miaka ya nyuma kutokana na serikali kuwa na tabia ya kufanya matumizi makubwa kuliko thamani ya fedha.
Kwa upande wake Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), alisema bajeti ya serikali bado haikuzingatia umaskini wa Watanzania na badala yake imekuwa bajeti ya kiushabiki.
Cheyo alisema kuna vyanzo vingi vya mapato ambavyo vingeweza kutumika kuliongezea taifa kipato kikubwa tofauti na kuongeza kodi katika vinywaji na ushuru wa magari.
Naye Mbunge wa Kigoma Kusini. David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema Bajeti ya Serikali haizungumzii ajira kwa vijana ambao ndio waathirika wakubwa wa ajira.
Kwa upande wa viongozi wa dini katika Mkoa wa Dodoma, Askofu wa Kanda ya Kati katika Kanisa la PAG, Charels Kanyika, alisema licha ya bajeti kuonekana ina unafuu, serikali siku zote imekuwa ikisema mambo ambayo hayatekelezeki.
“Bajeti inaonesha uchumi umekua, lakini bado Watanzania wengi ni maskini, tena hawajui hata hatima ya mlo wao kwa siku. Kuwapandishia bei ya mafuta moja kwa moja ni kuendelea kuwakomesha,” alisema Askofu Kanyika.
Akizungumzia suala la bodaboda, alisema kuwaondolea ushuru ni jambo la kisiasa, kwani kutapunguza mapato ya taifa na kama wangetozwa angalau kiasi kidogo, wangeweza kuongeza pato la taifa.
No comments:
Post a Comment