Saturday, June 15, 2013

Mnyika awalilia wamachinga wa Ubungo

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) amesema kuendelea kwa mgogoro kati ya serikali na wafanyabiashara ndogo ndogo ‘machinga’ ni matokeo ya kutokutekelezwa kwa wakati mapendekezo ya Bunge na udhaifu wa serikali.
Mnyika alisema mgambo na polisi hawawezi kutatua na kupata ufumbuzi wa mgogoro kati ya serikali na wamachinga badala yake serikali kuu na serikali za mitaa kupitia halmashauri waelekeze nguvu katika kunusuru mgogoro.
Mbunge huyo aliieleza Tanzania Daima Jumamosi kwamba mgogoro uliopo kwa wafanyabiashara wa Ubungo unatokana na serikali kupuuza mapendekezo aliyoyatoa ya kuwapatia wafanyabiashara hao eneo mbadala la kufanyia shughuli zao.
Alisema sababu ya mgogoro huo kuendelea ni kutokana na udhaifu wa serikali katika usimamizi wa mipango miji na kusababisha eneo hilo lenye makazi ya wananchi na mzunguko mkubwa wa watu kutokuwa na soko wala eneo rasmi la biashara.
Alieleza kuwa japo Wizara ya Nishati na Madini imeeleza ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaoishi jirani na mitambo ya umeme Ubungo katika bajeti yake ya mwaka 2012/2013, kiasi kilichotengwa hakihusishi kutafuta eneo mbadala la wafanyabiashara ndogo ndogo.
Katika hatua nyinyine, Mnyika aliitaka ofisi ya rais ieleze hatua iliyofikiwa katika kutekeleza ahadi ya kujenga Machinga Complex Ubungo ili haki ya wafanyabiashara kujiajiri kwa kuuza bidhaa ipatikane.
“Wafanyabiashara ndogo ndogo hawakuibuka ghafla katika eneo la Ubungo, walianza taratibu huku serikali ikiwaachia na hata kuwatambua kwa njia mbalimbali, hivyo kuwaondoa katika eneo linaloitwa hatarishi lazima kutanguliwe na maandalizi ya maeneo mbadala ya kufanyia biashara kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wa maeneo husika,” alisema mbunge huyo.
Hivi karibuni mgambo wakisaidiwa na askari wa Jeshi la Polisi waliendesha operesheni katika eneo la Ubungo kwa wafanyabiashara waliorejea kwa kuwanyang’anya mali na kuwapa vipigo baadhi ya wananchi waliokuwa wakinunua bidhaa toka kwa wamachinga hao.

No comments:

Post a Comment