MBUNGE wa Kawe Halma Mdee (CHADEMA) ametaka kujua iwapo serikali imewaunganisha vijana wanaotoka jeshini na kampuni binafsi za ulinzi ili wapate ajira huko.
Mbunge huyo alikuwa akiuliza swali la nyongeza bungeni jana ambapo alisema, “Vijana wanaopata mafunzo jeshini wengi wao hukosa ajira, sasa nataka kujua mpango wa serikali kuzungumza na sekta binafsi ili vijana hao wapate ajira.”
Akijibu swali hilo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema serikali inayo dhamira ya kuwapatia vijana wake wote ajira kama sera inavyosema; hivyo serikali kupitia wizara hiyo itazungumza na makampuni hayo ili yaweze kuwapatia vijana hao ajira.
Katika swali jingine la nyongeza Mbunge wa Viti Maalumu Ester Bulaya (CCM) alihoji serikali kama haioni haja ya kuhakikisha vijana wanaopata mafunzo ya silaha wawe ni wale tu ambao wataajiriwa na jeshi ili kupunguza vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha.
“Vijana wengi wanaopewa mafunzo ya silaha hawapati ajira na hivyo kujikuta wakiwa na uzoefu wa kutosha wa kutumia silaha ambao huenda nao uraiani na kuleta madhara,” alisema Bulaya.
Akijibu swali hilo alisema wanayo dhamira ya kuwaajiri vijana wote waliopitia mafunzo ya jeshi la ulinzi na usalama lakini uwezo wa serikali si mkubwa.
Awali katika swali la msingi mbunge wa Koani, Amina Clement (CCM), alitaka kujua ni kwa nini utaratibu wa kuwapeleka vijana JKT ulisitishwa.
Pia mbunge huyo alitaka kujua ni sababu gani zilizoifanya serikali kuamua kurudisha utaratibu huo wa kuwapeleka vijana JKT.
Akijibu swali hilo la msingi Nahodha alisema utaratibu wa kuwapeleka vijana JKT kwa mujibu wa sheria ulisitishwa kwa sababu nchi ilikuwa na hali ngumu ya kiuchumi katika kipindi cha miaka ya tisini.
No comments:
Post a Comment