Tuesday, June 11, 2013

CHADEMA WAPATA USHINDI MBIGA

CHADEMA wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma imepata ushindi mnono kabisa kwa kuibwaga CCM kwenye uchaguzi mdogo wa Kitongoji  cha Masangu katika kijiji cha Amani Makolo, Kata ya Mkako.

Akitangaza matokeo hayo jana, Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi huo Bahati Liholile Haule alisema kuwa wapiga kura waliojiandikisha katika uchaguzi huo walikuwa ni 110, waliojitokeza kupiga kura walikuwa 103 ambapo hakuna kura zilizoharibika.

Haule alisema kuwa katika uchaguzi huo Vyama viwili vya Siasa vilisimamisha wagombea ambapo kwa CCM ilimsimamisha Alto Ngonyani wakati CHADEMA ilimsimamisha Nestory Komba.

Alifafanua kuwa katika uchaguzi huo ambao ulitawaliwa na amani kubwa matokeo ya mgombea wa CCM 
yalikuwa ni kura 45 wakati mgombea wa CHADEMA alipata kura 58.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini ya CHADEMA, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya Mkoa wa Ruvuma, Joseph Fuime alisema kuwa ushindi ulikuwa mgumu, na licha ya Serikali ya CCM kutengeneza mazingira mfu ya kujipatia ushindi, walishindwa na nguvu ya umma ya kumpata kiongozi bora.

Fuime alisema kuwa ushindi huo ni salamu tosha kwa watawala wa CCM kuwa wananchi hawahitaji maneno yenye kutia matumaini bali sera za kuwaondoa katika minyororo ya maumivu ya maisha.

Alifafanua kuwa Mkoa wa Ruvuma umejaliwa kuwa na rasilimali nyingi sana ikiwemo makaa ya mawe yaliyopo meta chache kutoka eneo ambalo uchaguzi umefanyika, lakini rasilimali hizo hazitumiki kuwanufaisha wananchi wake bali viongozi wa kifisadi, kwa kusema kuwa ushahidi upo wazi katika Ofisi ya Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji au Kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mkako.

Alifafanua kuwa ukifika kwenye ofisi hizo utakutana na saini za viongozi na ujumbe wao ambao una malengo yenye utata dhidi ya maeneo ambayo yana rasilimali muhimu ambazo zingetumika vizuri zingeweza kusababisha wananchi waishi maisha bora: “Ukifika katika Ofisi hizo utakuta Viongozi hao wametembelea Ofisi hizo mara nyingi kuliko maeneo mengine ambayo yanakabiliwa na changamoto nyingi na wananchi wanawahitaji kwa ajili ya kuwaongoza katika kutatua shida  zao lakini cha ajabu huwa hawatembelei maeneo hayo mpaka muda wao wa Uongozi unakwisha.

Mwenyekiti huyo alimalizia kwa kusema kwa nafasi hiyo, anawashukuru wananchi kwa kutambua sera nzuri ambazo zinapaswa kutekelezwa na Kiongozi mzuri na pia kwa kupuuza ghiliba zilizozeeka za CCM na kutoa ujumbe kwa watawala katika chaguzi za kuelekea mwaka 2014 na 2015 ili kuleta matumaini na mustakabali mpya wa Taifa salama.


1 comment:

  1. we are still taking over>>>>>>>>>>>>>>>>>>>

    ReplyDelete