MBUNGE wa Hai Freeman Mbowe (CHADEMA) ameitaka serikali kutaja idadi ya makampuni ya mafuta na gesi yaliyolipa ada ya kila mwaka kwa ajili ya kuwasomesha watanzania katika sekta ya hiyo.
“Inaonyesha makampuni hayo yanatakiwa kulipa Dola 150,000 za Marekani kila mwaka lakini kuna baadhi ya kampuni hazijalipa ada hiyo mpaka sasa,” alisema Mbowe.
Alihoji jambo hilo alipouliza swali la nyongeza na alitaka kujua ni kwa nini serikali isilete wataalamu kutoka nje kuja kuleta elimu ya mafuta na gesi ili kupunguza gharama.
“Gharama ya dola milioni 6.6 za Marekani kusomesha watu 27 ni kubwa… kwa nini serikali isione umuhimu kuimarisha kitengo cha jiolojia kilichoko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kupunguza gharama?” alihoji Mbowe.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Massele, alisema ana orodha ya makampuni 25 aliyoahidi kumkabidhi mbunge huyo.
Kuhusu suala la gesi alisema kwa sasa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kina kitengo kinachotoa mafunzo ya mafuta na gesi na kwamba wapo wanafunzi wanaolipiwa na serikali.
Maselle alisema serikali itaendelea kuongeza bajeti na kutanua wigo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia kitengo cha Jiolojia ili kupata wataalamu wengi wa mafuta na gesi.
“Ni kweli gharama inayotumika ni kubwa lakini tayari tumeanza kutoa mafunzo hayo hapa nchini kupitia baadhi ya vyuo ili kuweza kupata wataalamu wengi kulingana na umuhimu wa sekata hiyo, pia tutaendelea kuwapeleka nje ya nchi kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi,” alisema.
Awali katika swali la msingi, Mbowe alitaka kujua ni wanafunzi wangapi hadi sasa wamesomeshwa kwa fedha zinazotolewa na makampuni ya mafuta na gesi ya TPDC.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, idadi ya makampuni yaliyoko nchini yenye mikataba ya utafutaji huo ni 25 ambayo hadi sasa yamechangia kiasi cha Dola 12,425,000 za Marekani.
No comments:
Post a Comment