Friday, June 14, 2013

Selasini alilia maji

MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), ameihoji serikali kuhusu mpango wa haraka wa kuwapatia maji wananchi wa Rombo hasa maeneo ya tambarare ambayo hayajapata maji tangu nchi ipate uhuru. Mbunge huyo alihoji hayo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la msingi.
“Tangu tuapate uhuru Wilaya ya Rombo hasa maeneo ya tmbarare – Lower Rombo yanakabiliwa na matatizo ya maji.
“Serikali ina mpango gani wa kuyapatia maji ukizingatia kuwa hakuna mabwawa ya kuhifadhi maji ya mvua na ile nia ya kutumia maji ya Ziwa Chala haipo kutokana na kina kirefu ingawa wenzetu wa Kenya wanaendelea kutumia maji hayo hayo kwa wananchi wake,” alisema.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maji, Dk. Binilith Mahenge, alikiri kuwa wilaya na maeneo hayo yanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.
Alisema katika kumaliza tatizo hilo serikali inatekeleza mradi wa maji kwa vijiji 10 vya Ngoyoni, Ngareni, Shimbi Mashariki, Ushiri, Kireni, Msaranga, Mahorosha, Kahe, Leto na Urauri.
“Utekelezaji umeanza kwa vijiji vya Ushiri na Kahe ambavyo vimepata vyanzo vya maji,” alisema Mahenge.
Naibu waziri huyo alisema ujenzi wa miundombinu ya maji kwa vijiji hivyo unatarajia kuanza Julai mwaka huu.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, vijiji vya Mahorosha, Msaranga, Kiraeni, Ngoyoni, Urauri, Ngareni na Shimbi Mashariki ambavyo havipati vyanzo vya maji, vitapata maji kupitia bomba la East Kilimanjaro Trunk linalopeleka maji Tarakea.
Alibainisha kuwa Kijiji cha Leto kilichobaki kitapatiwa maji kutoka kwenye visima vitano vilivyochimbwa na bonde la Pangani kijijini hapo.
Aidha, makandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya maji kwa visima hivyo watapatikana mwishoni mwa mwezi huu.
“Maeneo hayo ni kwenye makorongo ya mito ya Kikelelwa, Shia, Nalemuru Marwe, Ugwasi, Washi na Tarakea, ambapo kati ya makorongo hayo saba, wilaya kwa kushirikiana na ofisi za umwagiliaji Kanda ya Kaskazini watafanya usanifu wa kina kwa kuanza na makorongo ya Mto Marwe na Ungwasi,” alisema Mahenge.
Akizungumzia chanzo cha maji cha Ziwa Chala, alisema tayari Tanzania na Kenya zimesaini makubaliano ya usimamizi na matumizi ya maji ya ziwa hilo Februari 14, 2013 mjini Kisumu.

No comments:

Post a Comment