Baada ya kusota rumande kwa takriban miezi mitatu, hatimaye Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare ameachiwa kwa dhamana.
Hata hivyo, mwenzake Joseph Ludovick ambaye wanashtakiwa pamoja, alikwama kupata dhamana baada ya wadhamini wake kushindwa kuwa na vielelezo vyenye vigezo kulingana na masharti ya dhamana
hivyo alirejeshwa rumande.
Baada ya Lwakatare kuachiwa, alipokewa kwa shangwe na wafuasi wa Chadema waliokuwa na mabango yenye maandishi mbalimbali ya kuelezea furaha yao na mengine yakikiponda chama tawala CCM, huku wakimshangilia kwa kuimba: “peoples’ power... peoples’ power!” wakiwa na maana ya nguvu ya umma.
Akitoa uamuzi kuhusu dhamana hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Aloyce Katemana alisema imetolewa baada ya kuzingatia kigezo cha washtakiwa kufutiwa mashtaka ya ugaidi ambayo yalikuwa yanaangukia kwenye sheria inayozuia dhamana.
Aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na wanaotoka katika taasisi zinazotambulika kisheria.
Sharti lingine ni kila mdhamini kutia saini hati ya udhamini ya Sh10 milioni pamoja na washtakiwa wenyewe.
Hakimu huyo pia aliwataka washtakiwa kusalimisha hati zao za kusafiria mahakamani na kutokutoka nje ya Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha Mahakama.
Hakimu Katemana aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 24, mwaka huu itakapotajwa tena kwa lengo la kujua iwapo upelelezi umekamilika ili ipangiwe tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Awali, uamuzi huo wa dhamana ulipangwa kutolewa Mei 13, mwaka huu lakini ulikwama baada ya Katemana kuripotiwa kuwa likizo na badala yake, Hakimu Mkazi Sundi Fimbo aliitaja tu kesi hiyo na kuiahirisha.
Mei 27, mwaka huu ilitajwa tena hata hivyo uamuzi wa dhamana haukutolewa.
Awali, Lwakatare kupitia kwa mmoja wa mawakili wanaomtetea, Peter Kibatala aliwasilisha maombi ya dhamana mahakamani hapo Mei 13, mwaka huu wiki moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumfutia mashtaka matatu ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili.
Pamoja na dhamana hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) tayari ameandaa maombi ya marejeo katika Mahakama ya Rufaa akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa Mei 7, mwaka huu kuwafutia mashtaka ya ugaidi washtakiwa hao.
Katika maombi hayo, DPP anaiomba mahakama hiyo iitishe majalada ya kesi hiyo na kuchunguza uhalali wa uamuzi huo wa Mahakama Kuu, uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri.
Anadai kuwa katika hati ya maombi ya washtakiwa hao waliyowasilisha Mahakama Kuu, hapakuwepo na maombi ya kufuta mashtaka na kwamba hapakuwa na taarifa zilizowasilishwa dhidi ya washtakiwa ambazo Mahakama Kuu ingezizingatia katika kufikia uamuzi.
Hata hivyo, jopo la mawakili wa Lwakatare nalo liliwasilisha pingamizi la awali dhidi ya maombi hayo ya DPP, likiainisha hoja mbili ambazo mawakili wake watazitoa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo.
Lwakatare anadai kuwa maombi hayo ya marejeo yana dosari ambazo haziwezi kurekebishwa kutokana na kushindwa kuambatanisha nakala ya mwenendo wa uamuzi unaolalamikiwa ambao ndipo maombi hayo yalipojengwa na kwamba kiapo kinachounga mkono maombi hayo kimehusisha mambo mengine yasiyohusika.
No comments:
Post a Comment