Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini wa Chama hicho, Godbless Lema, wamejipeleka Makao ya Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha na kukataa kuwasilisha ushahidi wanaodai kuwa nao juu ya waliorusha bomu katika mkutano wao ambalo hadi sasa limesababisha vifo vya watu wanne.
Viongozi hao wamechukua uamuzi huo kwa lengo la kushinikiza kuundwa kwaTume huru ya kijaji na Rais Jajaka Kikwete ili wauikabidhi.
Hatua hiyo imekuja siku mbili tu baada ya Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja, kuwataka kujisalimisha vinginevyo jeshi hilo lingewasaka ili wawasilishe ushahidi huo.
Viongozi hao waliwasili kwenye makao makuu ya polisi jana majira ya saa 3.30 asubuhi na kutoka saa 8.10 mchana ksiha kwenda katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Sokoni One, Dayosisi ya Kaskazini Kati, kuhudhuria ibada ya mazishi ya aliyekuwa Katibu wa Chadema Kata ya Sokoni One, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) wa Kata hiyo, Judith Moshi (44 ).
Judith ni miongoni mwa watu wanne waliouawa kwa kulipukiwa na bomu la kurusha kwa mkono katika mkutano wa kuhitimisha kampeni za Chadema za uchaguzi wa udiwani wa kata nne za Halmashauri ya Jiji la Arusha, Jumamosi ya wiki iliyopita, katika viwanja vya Soweto.
Judith ambaye wakati wa uhai wake alijaliwa kupata watoto wanne, watatu wakiwa ni wa kike na mmoja wa kiume.
Akizungumza baada ya kutoka Polisi, Mbowe alisema wamekwenda kwenye makao makuu ya jeshi hilo kwa mambo mawili; la kwanza likiwa ni kuandika maelezo ya kufanya mkusanyiko usio halali, ambao wao wanasisitiza kuwa ni halali kwa kuwa ulikuwa na kibali.
Katika maelezo ya pili, walitakiwa kutoa ushahidi walionao kuwa polisi walihusika kurusha bomu hilo siku ya tukio, ambalo walikataa hadi hapo Rais atakapounda Tume huru ya Kimahakama na Kijaji ndipo watakapotoa usahidi wa picha za kawaida, video na watu walioshuhudia.
Baada ya kuwasili kanisani hapo, Mbowe alipewa fursa ya kuzungumza kama kiongozi wa chama na kuwaomba wananchi kutoogopa kwa mambo magumu wanayopata, huku akisisitiza kuwa yanaashiria ukombozi unakaribia nchini.
“Bomu lile lilirushwa kwa lengo la kukatisha uhai wetu. Lakini likaishia kuangamiza maisha ya watoto wadogo na kina mama kama Judith, ambaye alikuwa Katibu wa Chadema Kata ya Sokoni One,” alisema Mbowe.
Alieleza kusikitishwa na kauli ya serikali iliyotolewa bungeni mjini Dodoma kuwa polisi walikuwa mstari wa mbele kuokoa majeruhi na kuchukua maiti za watu waliokufa hadi hospitalini akidai siyo za kweli kwa sababu walikimbia na kuachia wafuasi wa Chadema wakifanya kazi ya kuokoa maisha ya watu na kukusanya maiti hizo.
Mbowe, ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema wafuasi wao walijitoa kwa hali na mali na kujitolea damu kusaidia majeruhi waliopoteza damu nyingi kwa majeraha waliyopata, huku serikali ikikaa pembeni na kuendelea na Bunge kama hakuna kilichotokea na kushindwa kumpa pole kama Kiongozi aliyenusurika kuuawa katika tukio hilo.
Akizungumzia kuhusu madai kwamba, yeye na Lema walikimbia wakati wa tukio hilo la Juni 18, mwaka huu, alisema siyo ya kweli kwa sababu linapotokea tukio la urushaji wa mabomu na risasi, kitu cha kwanza kila mmoja ana wajibu wa kutunza uhai wake na ndicho walichofanya.
Mbowe alisema anaishangaa serikali kutangaza bingo ya Sh. milioni 100 kwa atakayetoa taarifa za kuwezesha kukamatwa kwa mtu aliyerusha bomu hilo wakati kila kitu kipo wazi na kila mtu anafahamu ukweli.
Mkuu wa KKKT, Jimbo la Arusha Mashariki, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Solomon Massangwa, alitaka ifike mahali watu waseme bila kumung’unya maneno kuwa sasa Tanzania siyo salama tena kwa sababu kuna matukio ya uchomaji makanisa, utekaji wa watu wanaokuwa mstari wa mbele kukosoa serikali na utupaji mabomu na ufyatuaji risasi ovyo.
“Haya mambo yanafanyika bila vyombo vya dola kuchukua hatua na kubaki na wimbo ule ule tunashughulikia na wahusika watakamatwa kila kukicha, huku watu wakipoteza maisha yao, ” alisema.
Alisema walitegemea yanapotokea matukio makubwa kama hayo, wahusika wangetiwa mbaroni, kuchukuliwa hatua haraka, lakini ni kinyume cha matarajio ya watu.
“Tanzania ya sasa tofauti na zamani sababu watu siyo wapumbavu, wanajua kila linalotendeka na wasijidanganye watu wa dola kuwa hatujui,” alisema.
Massangwa alisema kila mmoja ana wajibu wa kutunza na kulinda amani, ambayo kwa sasa inakuwa historia kwa matukio ya kukatisha maisha ya watu wasiokuwa na hatia ovyo.
Aliwataka wananchi waungane bila kujali itikadi za vyama vya siasa na dini kuliombea taifa na watawala wawe na hekima ya kushughulikia mambo.
“Vyombo vya usalama lazima wafike mahali wajitathmini kwa kina kama kweli wanatekeleza wajibu wao au la. Vijiulize kwa nini watu hawaheshimu vyombo vya dola, japo wao wapo katikati yetu kuhakikisha maisha yetu yapo salama,” alisema.
Alitoa wito kwa vyombo vya dola kuacha kutumia nguvu isiyohitajika kati ya watu na kusababisha maafa na majanga.
Alisema hawawezi kuzuia watu wasiseme ukweli wa mambo pale wanapoona mambo yanaenda kombo kwa sababu hata Biblia inasema ukweli huinua taifa, bali dhambi ni aibu.
Aliwataka wananchi wasiogope wanapokumbana na mambo magumu kwa sasa, bali watambue kuwa ni ukombozi umekaribia, kwa kuwa hawawezi kumpiga teke kobe kwa sababu watakuwa wanamuongezea mwendo.
Bonyeza Read More Kuendelea
RPC AMSHANGAA MBOWE
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabasi, alisema anamshangaa Mbowe kusema amekataa kutoa ushahidi wake wakati amedai alichonacho ni maneno ya watu na siyo vinginevyo, huku akisisitiza amenukuliwa vibaya na kutoka nje akidanganya eti anataka tume huru.
“Hii Tume anayotaka ni kupoteza muda na kudanganya umma. Ukweli tunaotaka walete ushahidi hapa na siyo kuanza kubuni mambo mengine ili kuchelewesha mambo. Na hili tutajua hatua za kumchukulia kwa sababu anapotosha umma,” alisisitiza.
Sabas alisema kwa kuwa serikali imetangaza bingo kwa mwenye ushahidi, kama anao apeleke ili akabidhiwe kitita hicho.
Tukio hilo limetokea takriban zaidi ya siku 40 tu baada lingine linalofanana nalo, kutokea kwenye hafla ya uzinduzi wa Parokia ya Olasiti ya Kanisa Katoliki, Mei 5, mwaka huu, jijini Arusha pia.
Katika shambulizi la kanisani, bomu lilirushwa kwenye mkusanyiko mkubwa wa waumini nia ikiwa ni kuangamiza watu wengi, hata hivyo walikufa watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60.
Ingawa hadi sasa polisi hawajatoa taarifa kwa umma juu ya aina ya bomu lililolotumika Olasit, mlipuko wa Jumamosi iliyopita kwenye mkutano wa Chadema, unafanana kwa kila kitu na ule wa Mei 5, mwaka huu.
Kwa upande wa Olsasit, walengwa wakuu alikuwa Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla, na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu, kwenye mkutano huo walengwa walitaka kuwaua pamoja na watu wengine Mbowe na Lema.
Mfululizo wa matukio haya ya ugaidi, mbali ya kusababisha kuahirishwa kwa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata hizo, pia umekifanya Chadema kusitisha mahudhurio ya wabunge wake wote katika vikao vya Bunge kuanzia Jumatatu wiki hii kwenda Arusha kushiriki maziko ya watu wanne waliouawa katika mlipuko wa bomu hilo.
Watu hao, akiwamo mwingine aliyeripotiwa kufa juzi na wengine 66 walijeruhiwa katika mkutano wa hadhara wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi ndogo wa udiwani katika kata hizo.
Wengine waliokufa ni Ramadhani Juma (15) na mtoto aliyejulikana jina moja la Jastin anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (13) na Fahad Jamali.
Wengine walioshambuliwa na kujeruhiwa kisha kulazwa hospitali ni Mbunge wa Arumeru Mashariki wa Chadema, Joshua Nassari, ambaye alikuwa Meneja kampeni wa uchaguzi mdogo wa Kata ya Makuyuni.
Nassari alipigwa vibaya na makada CCM na kujeruhiwa vibaya na kwamba hadi sasa anaendelea na matibabu katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (Moi) jijini Dar es Salaam baada ya kupewa rufaa na Hospitali ya Selian.
Wengine waliojeruhiwa ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, Gabriel Lucas ambaye hali yake ilielezwa kubadilika na kulazwa kwenye wodi ya wagonjwa wanaohuitaji uangalizi maalum (ICU).
Viongozi wengine wa Chadema waliokamatwa na polisi na kuachiwa baada ya kupata dhamana ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustafa Akoonay (Mbulu), Said Arfi (Mpanda Mjini) na Joyce Mukya (Viti Maalum).
Vilevile watu zaidi ya 60 walikamatwa kwa tuhuma za kukusanyika na kufanya mkutano usiokuwa wa halali katika Uwanja Soweto ambao ulizingirwa na wanajeshi na polisi kwa lengo la kuwazuia wananchi wakiwamo wafuasi na viongozi wa Chadema kusanyika kwa ajili ya kuaga mwili wa mmoja wa marehemu huyo ambaye ni kati ya watu watatu waliouawa katika mlipuko wa bomu hilo.
NASSARI ALAZWA MOI
Nassari amelazwa MOI baada ya kuhamishwa kutoka Selian akisumbuliwa na maumivu ya shingo na mgongo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye wadi binafsi namba J ya MOI, Nassari alisema alihamishiwa hapo jana kutoka hospitali hiyo kwa kufuata taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kupata barua ya rufaa.
Alisema alihamishiwa MOI baada ya kushauriana na ndugu zake, Ofisi ya Bunge, viongozi wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, madaktari waliokuwa wanamtibu pamoja na wale waliotoka MOI, ambao kwa pamoja walipitisha uamuzi huo.
Akizungunzia hali yake kwa sasa, Nassari alisema alipofika tu MOI juzi, alifanyiwa vipimo vya X- Ray na madaktari walimwambia kuwa pingili za mgongo haziko sawa na kumshauri asubiri utaratibu wa kumfanyia kipimo cha MRI, tofauti na kile alichofanyiwa, ambacho kitaonyesha hali halisi mwilini mwake.
“Sasa kwa bahati mbaya kipimo hicho kinapatikana kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambacho kimeharibika kwa sasa. Waliniambia kuwa natakiwa niwe chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari kwa kipindi cha wiki mbili. Kwa kweli namshukuru sana Mungu kwani kwa sasa naweza hata kwenda chooni mwenyewe,” alisema.
Akizungumzia habari zilizoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba, alitoroka Hospitali ya Selian alikokuwa amelazwa baada ya kujeruhiwa kwenye uchaguzi wa udiwani, uliofanyika Jumapili iliyopita, Nassari alisema ni kweli alitoroka kwa kuwa hakupita kwenye mlango unaotumiwa na wagonjwa.
Alisema alitoka hospitalini hapo akiwa kwenye kiti cha kubebea wagonjwa, huku akiwa amevalia Kimasai na kutoka kwa kupitia geti la nyuma kwa sababu za kiusalama.
Alisema alifanya hivyo kwa kuwa alikuwa hataki watu wajue, kwani wangejua kuwa anahamishiwa Dar es Salaam, kungekuwa na uwezekano mkubwa wa vurugu kutokea maana wangefikiria hali yake siyo nzuri.
Alisema sababu nyingine ni kutokuwapo kwa usalama wa kutosha katika hospitali hiyo, kwani ilikuwa imejaa wanausalama, ambao walikuwa wanazunguka zunguka kwenye eneo la hospitali kila wakati, jambo lililowafanya wajiulize wanataka nini
No comments:
Post a Comment