Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Abubakary Khamis Bakary, amesema Katiba ya Zanzibar italazimika kufanyiwa marekebisho baada ya kukamilika kwa mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano.
Aliyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi Jaku Hashim Ayoub, wa Jimbo la Muyuni wakati wa Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani mjini hapa jana.
Alisema mabadiliko ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iwapo yatapitishwa kama rasimu ya katiba ilivyopendekeza, lazima na Katiba ya Zanzibar ifanyiwe marekebisho.
Alifafanua kifungu cha 80 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kimetoa uwezo kwa Baraza la Wawakilishi kubadilisha kufungu chochote cha Katiba ya Zanzibar.
Hata hivyo, alisema muswada wa kubadilisha Katiba hautapitishwa na Baraza isipokuwa uwe umeungwa mkono kwa mara ya kwanza na ya pili na theluthi mbili ya kura zote za wajumbe wa Baraza hilo.
Alisema mabadiliko yote ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanyika yamezingatia kifungu hicho ikiwamo Zanzibar kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, haki ya Mzanzibari kupiga kura, kuwapo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka pamoja na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Mheshimiwa Spika, Katiba hii imetokana na wananchi wenyewe ambao waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanawakilisha wananchi wote wa Zanzibar," alisema Abubakary.
Alisema kifungu cha 9(2)(a) cha Katiba ya Zanzibar kimeleeza kuwa mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananchi wenyewe wa Zanzibar.
Awali, Mwakilishi Jaku Hashim Ayoub, alitaka kujua ni lini wananchi wa Zanzibar watapewa haki ya kidemokrasia ya kushirikishwa kuamua aina gani ya Katiba wanataka badala ya kuamliwa na viongozi wa kisiasa Zanzibar.
Alisema kwamba Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kabla ya hapo ilitungwa bila ya wananchi kushirikishwa na kuamua wanataka aina gani ya Katiba kama utaratibu uliyotumika kupata rasimu ya Katiba ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania mwaka huu.
No comments:
Post a Comment