WAJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Tanzania Bara, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, ndiyo wanaotarajiwa kuandika Katiba ya Tanganyika (Tanzania Bara), vyanzo kadhaa vya habari vya Raia Mwema vinaeleza.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu ya habari, tayari maandalizi ya muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yamefikia hatua ya kuridhisha na wakati wowote, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema atawasilisha bungeni muswada huo.
Ingawa vyanzo hivyo vya habari vinathibitisha kuwapo kwa maandalizi hayo, lakini AG Werema hakuweza kupatikana hadi tunakwenda mitamboni, simu yake ikiita bila kujibiwa.
Tayari Jaji Warioba ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akihojiwa kupitia kipindi cha televisheni cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, amesema hakuna haja ya kukusanya upya maoni ya wananchi wa Tanzania Bara kwa kuwa yamekwishakusanywa na Tume yake na kwamba watakaopewa jukumu la kuandika Katiba ya Tanzania Bara, wanaweza kutumia maoni yaliyokwishakusanywa.
Lakini wakati hayo yakiendelea, taarifa za uhakika kutoka vyanzo vyetu vya habari ndani ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CC-CCM) zinabainisha kwamba kikao hicho kilichoitishwa Jumatatu wiki hii mjini Dodoma na kuongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kimesikiliza hoja nzito zikiwamo za kuhoji ni wapi Tume ya Warioba imepata maoni ya kuwapo kwa serikali tatu.
Mjumbe mmoja wa kikao hicho kutoka Zanzibar anaelezea kuchachamaa kwa wajumbe wa kikao hicho kutoka Zanzibar, wakisema maoni ya Katiba kuhusu Muungano kutoka visiwani humo yalikuwa ya aina mbili tu na si tatu.
“Zanzibar tulitoa maoni ya aina mbili. Kwanza ni maoni kuhusu muundo wa Muungano uwe wa serikali mbili kama ilivyo sasa, lakini wengi walitoa maoni ya kuwapo kwa Muungano wa mkataba. Haya ndiyo maoni yaliyopo kule hadi sasa. Kwa hiyo, Warioba na wenzake wamepata wapi haya mawazo ya serikali tatu?” kinaeleza chanzo chetu hicho kutoka Zanzibar, kwa sharti la kutotajwa gazetini jina lake.
Katika hatua nyingine, viongozi na watu wengine mbalimbali nchini wameendelea kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela ambaye akiwa katika wadhifa huo, mjadala wa kuundwa upya kwa Serikali ya Tanganyika ulichukua nafasi kubwa kiasi cha Bunge kuridhia Serikali tatu na kisha Mwalimu Julius Nyerere kufanya kampeni iliyofanikiwa kuzima jaribio hilo, alisema ni vizuri zaidi kwa viongozi wakuu kuacha maoni ya wananchi yasikike badala ya kuharakisha kutoa maoni yao.
“Mimi kwa kweli nadhani ni vizuri kuacha kwanza maoni ya wananchi yasikike, tukizungumza sisi viongozi, kama mimi, kuna hatari watu wakaacha kujadili kilichomo kwenye rasimu na badala yake wakajadili maoni yangu. Si vizuri maoni ya viongozi yatawale wakati wote maoni ya wananchi, kiongozi unapoharakisha kutoa maoni yako ina maana unawagawa watu kimtazamo na uwezekano wa kutumia nguvu kubwa kujadili maoni yako ni mkubwa,” anasema Malecela ambaye alipata kuwania ateuliwe mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, mwaka 1995 na baadaye mwaka 2005.
Naye Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, ambaye ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mazungumzo yake na mwandishi wetu alizungumzia hofu ya uwapo wa serikali tatu kuhatarisha uhai wa Muungano.
“Kwanza serikali tatu si suluhisho la matatizo ya Muungano. Hili suala la ama kuvunja au kutovunjwa kwa Muungano kwa sababu ya serikali tatu kwa kweli kwa sehemu kubwa inategemea na dhamira ya viongozi wanaochaguliwa kuongoza nchi.
“Na kwa sababu ni dhamira ya viongozi ndiyo inayoweza kuvunja Muungano, basi ni jukumu la wananchi kuhakikisha wanachagua viongozi wenye dhamira safi na Muungano, mamlaka ya wananchi sasa ifanye kazi kwa uangalifu sana.”
Hata hivyo, alipoulizwa ni kwa namna gani wananchi wataweza kuwa na utabiri wa mgombea gani mwenye dhamira ya kulinda Muungano kwa kuzingatia ukweli kwamba dhamira si jambo la kudumu kwa anayepewa madaraka, Baregu alisema kwa kuwa viongozi wanatokana na jamii ya Watanzania, wanajulikana wasifu na dhamira zao.
Lakini, Dk. Honest Ngowi, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, mkoani Morogoro anazungumzia rasimu ya Katiba Mpya katika muktadha wa kiuchumi hasa kuhusu deni ya taifa.
“Ni lazima Katiba Mpya iweke ukomo kwenye Deni la Taifa. Ukomo utokane na asilimia ya Pato la Taifa. Kusipokuwa na ukomo, taifa litakuwa na matatizo makubwa ya kiuchumi,”
“Baadhi ya nchi za Ulaya kama vile Ugiriki hivi sasa zina matatizo ya kufilisika kwa sababu kwenye kukopa hawakuwa na ukomo. Katiba ya Marekani imeweka ukomo huu na ndiyo umeisaidia kuvuka kutoka kwenye mdororo wa uchumi,” anasema Dk. Ngowi.
Kuhusu rasimu ya Katiba kuweka idadi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri kuwa 75, Dk. Ngowi anasema ni muhimu kwa wabunge hao 75 kupata mafunzo ya hali ya juu kuhusu masuala ya Deni la Taifa, ili washauri vizuri na kuibana serikali kwenye masuala ni muhimu, wapewe ufahamu wa kutosha kuhusu maana na athari za deni la taifa.
Raia mwema
No comments:
Post a Comment