Saturday, June 1, 2013

Matiko ahoji utendaji kazi wa mashine za maji

MBUNGE wa Viti maalum Ester Matiko (CHADEMA), amehoji kauli ya Serikali kuhusu mashine tatu na mota mbili mpya za maji zilizofungwa katika hospitali ya Shirati kama zina uwezo wa kufanya kazi na kurejesha huduma ya maji kwa wananchi wa eneo hilo.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo bungeni mjini hapa jana wakati alipokuwa akiuliza swali la nyongeza katika kipindi cha maswali na majibu.
“Awali serikali ilifunga mashine katika mji wa Shirati lakini kutokana na mashine hiyo kutokuwa na kiwango iliharibika na kufa baada ya miezi mitatu tu, Nataka serikali inihakikishie itaboresha vipi huduma ya maji katika hospitali ya Shirati kwa kununua pampu imara na zenye viwango,” alihoji Matiko.
Awali katika swali la msingi mbunge huyo aliihoji serikali ni kwa nini imeshindwa kutengeneza mashine iliyoharibika ili kurejesha huduma ya maji kwa wananchi.
Pia Matiko alitaka kujua gharama ya kutengeneza mashine hiyo ni kiasi gani na kama ni kununua mashine nyingine itakuwa kiasi gani cha fedha ambacho serikali haiwezi kumudu tangu mwaka 2004.
Akijibu maswali hayo kwa pamoja Naibu Waziri wa Nchi Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Aggrey Mwanri alikiri kuwepo kwa tatizo hilo lakini alimtaka mbunge kutokuwa ‘tomaso’ na kuacha mashine hizo zifanye kazi kwanza ndipo aone kama hazina ubora.
Alisema wao kama serikali wanaziamini mashine hizo na wamezifanyia uchunguzi wa kutosha na ubora wake unafahamika hivyo hawana wasiwasi katika hilo.
Mwanri akijibu swali la msingi alisema ni kweli kuwa kulikuwepo na tatizo la upatikanaji wa maji kwa wakazi wa mji wa Shirati kutokana na kuharibika kwa mashine.
Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imenunua na kufunga pampu tatu pamoja na mota mbili kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa shirati na hospitali za Shirati na Rao.
"Kazi hizo zimeboresha huduma ya maji katika eneo la shirati na katika hospitali hizo," alisema Mwanri.
Alisema mashine zilizokuwa zikihudumia mji wa Shirati ziliharibika kutokana na kuungua kwa mota zake.
Alisema hata hivyo ilibainika kuwa mashine hizo zilikuwa na uwezo mdogo kukidhi mahitaji ya maji ya sasa kwa wakazi wa mji wa Shirati.

No comments:

Post a Comment