Saturday, June 1, 2013

Kikwete alikoroga mauaji ya Mwangosi

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemvaa Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kumpandisha cheo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, badala ya kumchukulia hatua.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kumpandisha cheo Kamuhanda kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) licha ya shutuma kutoka kwa wadau mbalimbali nchini akielezwa kushindwa kuwazuia askari kumuua kikatili mwandishi wa habari wa televisheni ya Chanel Ten, Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012, katika kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, jana alilieleza gazeti hili mjini hapa jana kuwa uamuzi huo umeonyesha udhaifu mkubwa wa Rais Kikwete.
Alisema Rais Kikwete alipaswa kumchukulia hatua Kamuhanda kufuatia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kumtaja kuwa alikiuka sheria ya vyama vya siasa na kuchangia katika kusababisha mauaji ya Mwangosi.
“Rais Kikwete amefanya hivyo bila kujali kauli iliyotolewa kwa niaba yake na Ikulu kwamba angeeleza hatua yake kuhusu tukio la mauji ya Mwangosi baada ya kupatiwa ripoti ya uchunguzi wa mauji hayo,” alisema.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alisema baada ya Rais Kikwete kupatiwa ripoti mbili: ya Kamati ya Jaji mstaafu Ihema, Emmanuel Nchimbi na Tume ya Haki za Binadamu, hajawahi kueleza hatua alizochukua kama ilivyoahidiwa.
“Rais Kikwete kumpandisha cheo Kamuhanda kunaweza kutafsiriwa kuwa ni ‘zawadi’ kwa kazi yake iliyosababisha mauaji, sio tu ya Mwangosi bali yaliyofanywa pia na askari kwa amri yake kwa vijana wa bodaboda mkoani Ruvuma kabla ya kuhamishiwa mkoani Iringa,” alisema.
Bonyeza Read More Kuendelea


Alimtaka Rais Kikwete ajitokeze kulieleza taifa vigezo alivyotumia kumpandisha cheo Kamuhanda pamoja na tuhuma zote alizonazo.
Mnyika aliongeza kuwa hatua hiyo ya kumpandisha cheo Kamuhanda na makamanda wengine ambao wamelalamikiwa kuhusu utendaji wao akiwemo Isaya Mungulu na Thobias Andengenye katika matukio mbalimbali ya askari wa chini yao kusababisha mauaji inatoa picha kuwa matendo hayo yalikuwa na baraka ya uongozi wa juu zaidi wa serikali.
“Rais Kikwete kuwapandisha vyeo makamanda hao kumetonesha majonzi ya wote ambao ndugu zao waliuawa kikatili na Jeshi la Polisi, sehemu mbalimbali yakiwemo yale yaliyotokea katika mikutano ya kisiasa,” alisema Mnyika.
Mnyika alisisitiza kuwa Rais Kikwete alipaswa kujitokeza kutoa majibu juu ya barua aliyoandikiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ya kutaka aunde tume huru ya kijamii kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Kwamba badala yake Jeshi la Polisi ambalo makamanda wake ni watuhumiwa liliachwa lijichunguze ili kulindana na kutoa mwanya wa kuhusika kupanda vyeo badala ya kupanda mahakamani.
Jukwaa la wahariri lashangazwa
Jukwaa la wahariri nchini, limepokea kwa mshangao mkubwa kupandishwa cheo kwa Kamanda Kamuhanda, bila kujali kwamba alisukumiwa lawama na tume mbili zilizoundwa kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Akihojiwa na Tanzania Daima Jumamosi, Katibu Mkuu wa TEF, Neville Meena, alisema inasikitisha kuona serikali ikipuuza vilio na malalamiko ya wananchi kuhusiana na tukio hilo.
“Huyu mtu aliondoka mkoani Ruvuma akikabiliwa na tuhuma za askari wa chini yake kuwaua waandamanaji wa bodaboda na kaja Iringa amekutana na janga lingine.
“Tulitegemea katika utawala wa sheria, hata baada ya kelele za watu wengi na kutia doa kubwa katika utendaji wa polisi, angewajibishwa mara moja,” alisema Meena.
“Sehemu nyingine makamanda wengine walipendwa sana kama Gewe na Tibaigana ambao walifanikiwa kuteka nyoyo za watu kwani walijitahidi kufanya kazi kwa uadilifu.
Katibu huyo alisema waandishi wa habari wanamtazama Kamuhanda kama mtu mwenye kasoro katika utendaji kazi wake, sio tu wakiwa ni waandishi wa habari bali hata raia wa kawaida.
“Hata kama hakuua yeye, lakini kwa matukio haya hasa hili la Mwangosi kwa sababu alikuwepo tangu mwanzo hadi mwisho wa tukio, tulitegemea aondoke na si kupandishwa cheo.
“Kuwepo kwake kumeendelea kutuumiza katika tukio zima; hakuchukua hatua kuzuia hata alipoambiwa. Inaonekana kwao ni utendaji kazi bora kulingana na walivyotaka. Wametusaidia kujua sisi waandishi kuwa tuanze kuitazama serikali kwa jicho la namna gani.
Meena alisema kuwa serikali ingetumia busara kubwa katika jambo hilo, maana tafsiri itakayopokelewa na wananchi ni kwamba serikali ilifurahia mauaji haya, na labda inalea ukatili na mauaji.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isaac Nantanga, juzi katika taarifa yake alisema kuwa Rais Kikwete amewapandisha vyeo maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi kuwa Makamishna wa Polisi (CP) na Manaibu Kamishna wa Polisi (DCP).
Taarifa hiyo ilieleza kuwa waliopandishwa kuwa Makamishna wa Polisi ni Isaya Juma Mungulu na Suleiman Kova ambao kabla ya vyeo vyao vipya walikuwa Manaibu Kamishna wa Polisi.
Isaya Mungulu yuko Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam, ambapo Suleiman Kova ni Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Dar es Salaam.
Waliopandishwa kuwa Manaibu Kamishna wa Polisi ni Elice Mapunda, Brown Lekey, Hamdani Omar Makame, Keneth Kasseke, Abdulrahman Kaniki, Thobias Andengenye, Adrian Magayane, Sospeter Kondela, Simon Sirro na Ernest Mangu.
Wengine ni Hussein Laisseri, Anthony Joel S. Mwami, Mohamed Mpinga, Adolfina Chialo, Mpinga Michael Gyumi, Ally Mlege, Hezron Gyimbi, Michael Kamuhanda, na Jonas Mugendi.
Kabla ya uteuzi huu, maofisa hao walikuwa Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi. Uteuzi huu umeanza mara moja.

No comments:

Post a Comment