WAUNDA MABARAZA YAO YA KATIBA KUJADILI RASIMU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetofautiana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, katika pendekezo la kutaka muundo wa serikali tatu katika rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni.
Katika kupingana na maoni ya tume ya Jaji Warioba, Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM, imeamua kupeka rasimu hiyo kwa wananchi wake kuanzia ngazi ya matawi na kutaka yaundwe mabaraza ya Katiba ya chama hicho ili kujadili rasimu hiyo hususani muundo wa Serikali ya Muungano.
Wakati CC ikipitisha azimio hilo, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba, amesisitiza kuwa suala la serikali tatu kwa sasa haliepukiki kwani zisipokuwapo kuna hatari ya muungano kuvunjika.
Kauli ya Warioba imekuja huku kukiwa na mbinyo wa ndani na nje ya CCM, wakiwamo viongozi waandamizi wa chama hicho tawala na makundi ya urais 2015, kupinga pendekezo la kutaka kuwe na muundo wa serikali tatu.
Bonyeza Read More Kuendelea
Habari kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa CC kutoka visiwani Zanzibar, waliliambia gazeti hili kuwa wajumbe wa Zanzibar walicharuka na kuhoji kwanini Jaji Warioba aliamua kuingiza pendekezo hilo kwenye rasimu ya Katiba wakati msimamo wa chama anaujua.
Wajumbe hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walimshambulia Warioba kuwa si kweli kwamba Wazanzibari wengi walioulizwa kuhusu muundo wa serikali walipendekeza serikali tatu.
Katika kikao hicho mahususi kwa ajili ya kujadili rasimu ya Katiba kilichofanyika jana chini ya Rais Jakaya Kikwete, Kamati Kuu (CC) ya CCM imeazimia kuipeleka rasimu hiyo kwa wanachama wao kuanzia ngazi ya matawi ili ijadiliwe kwenye mabaraza ya Katiba ya chama kwa kuzingatia maoni yaliyopelekwa awali kwenye tume ya Jaji Warioba.
Hatua ya CC kushindwa kutoa msimamo na kuamua kuipeleka rasimu hiyo kwenye matawi yake imeongeza hofu ya CCM kuhusu muundo wa serikali tatu zilizopendekezwa na tume wakati chama hicho tangu awali msimamo wake ni muundo wa serikali mbili kama ilivyo sasa.
Tayari baadhi ya vigogo waandamizi wa chama hicho akiwamo Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, wamepinga kipengele hicho cha rasimu kinachopendekeza serikali tatu.
Hofu ya Sitta na wenzake wanaopinga ni kwamba mchakato wake umelenga kuvuruga muungano na kuibebesha mzigo serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kauli na misimamo ya kina Sitta ni maoni yao binafsi na kwamba wana haki ya kufanya hivyo kama Watanzania wengine.
Alisema msimamo wa chama utatolewa baada ya rasimu hiyo kujadiliwa na wanachama wao kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa ambapo katika ngazi ya taifa itajadiliwa na vyombo vikuu vya uamuzi vya Sekretarieti, Kamati Kuu na NEC.
Nape alifafanua kuwa wanachama watakachoamua ndicho kitakachochukuliwa na kupelekwa kwenye tume ya Jaji Warioba kama msimamo wa CCM.
“Kamati Kuu imekiagiza chama kijipange kujadili rasimu hiyo ndani ya chama kama baraza la kitaasisi la Katiba na kuwataka wanachama na wapenzi wa CCM wajitokeze kwa wingi na kushiriki kwenye mabaraza,” alisema.
Aliongeza kuwa jumuiya za chama za Umoja wa Vijana (UVCCM), Umoja wa Wanawake (UWT) na Wazazi zimekusudia kushiriki kama mabaraza ya Katiba, hivyo kuongeza ushiriki wa wanachama na wapenzi wa CCM katika mchakato huo.
“CCM kama baraza la Katiba la kitaasisi litapitia rasimu iliyowasilishwa kifungu kwa kifungu na kwa kuzingatia maoni ya chama yaliyotolewa mwanzoni kabisa mwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba, wanachama wenu watashiriki kutoa maoni yao,” alisema.
Nape aliongeza kuwa pamoja na kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, CC inaiomba tume hiyo kueleza vizuri mchakato mzima kutoka rasimu ya kwanza mpaka rasimu ya mwisho ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu ya mchakato mzima hasa baada ya rasimu ya kwanza kutoka.
Alipoulizwa ni kwanini CCM inapata kigugumizi kutoa msimamo kuhusu rasimu hiyo kama walivyokwisha kufanya vyama vingine, Nape alisema wao hawakurupuki pasipo kuwashirikisha wanachama wao.
“Hiki ni chama kikongwe, haiwezekani kila kiongozi kutoa msimamo wake bila utaratibu. Sisi lazima tuoneshe mfano, si umesikia CUF Mwenyekiti wao, Prof. Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif, wanapingana kuhusu muungano,” alisema.
Jaji Warioba apigilia msumari
Wakati pendekezo la kutaka kuwe na serikali tatu limewagawa Watanzania, Jaji Warioba amesisitiza kuwa bila serikali tatu muungano utavunjika.
Jaji Warioba aliyasema hayo juzi usiku wakati alipokuwa akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa hewani na kituo cha televisheni cha ITV, huku akionesha dhahiri kujibu maoni ya vigogo kama Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta na wadau mbalimbali, waliolalamikia muundo wa serikali tatu wakidai kwamba ni gharama kuuendesha.
“Huwezi kung’ang’ania gharama, ulazimishe kwa sababu watu wanaogopa gharama, kuna hatari ya muungano kuvunjika, ni lazima uangalie watu wanataka nini na ndicho ambacho tumefanya kwamba kama tukilazimisha serikali mbili, kuna hatari ya muungano kuvunjika.
“Zanzibar wanataka madaraka yao, uchumi wao waumiliki wao wenyewe na ndiyo mabadiliko waliyokuwa wanataka. Bara wanasema kama Zanzibar wanataka hayo itakuwa imekuwa huru, utawafanya nini, huwezi kufanya mabadiliko? Kwahiyo mimi naona ukifanya hivyo hatari ya kuvunjika ni kubwa zaidi, sasa uone kama unataka muungano gharama zitakuwapo kwani hata tulipoanza gharama zilikuwapo.
“Sasa tumefika hapa tunasema ni afadhali tuwe na serikali tatu lakini tujitahidi kupunguza matumizi. Tunavyoona ni afadhali tuwe na serikali tatu…mi nitakuwa mnyonge sana muungano ukiwa dhaifu,” alisema Jaji Warioba.
Alieleza kwamba ikiwa wananchi wanataka kukwepa gharama muungano uvunjwe, lakini ikiwa wanautaka ni bora gharama ziwepo na kusisitiza kwamba aonavyo yeye ni muhimu zaidi nchi hizo kuwa pamoja kuliko vinginevyo, kwani hali hiyo inasaidia kupunguza gharama kuliko nchi hizo zikiachana, kwani gharama zitakuwa kubwa.
Alisema katika kukusanya maoni yao wamepata mambo mengi muhimu ambayo pengine hata wananchi hawayazungumzi, akatolea mfano suala la maadili ya viongozi.
“Tulipopita tulisikia watu wakisema kuhusu maadili, matatizo mengi yapo hata ya wananchi kutokuwa na imani. Walizungumza wakitaka hatua zichukuliwe.
“Na matatizo mengine yanayotokea ni kwa sababu ya maadili ya viongozi kuporomoka,” alisema Jaji Warioba.
Muundo wa serikali tatu kukopa
Kuhusu suala hilo Jaji Warioba alisema atakayekuwa na jukumu la kukopa kwenye muundo huo ni Serikali ya Muungano.
Alisema hata serikali hizo mbili zikija zitaweza kukopa kwani hata hivi sasa utaratibu huo upo.
“Lakini hata sasa hivi kuna utaratibu kuwa serikali zote wanakopa lakini serikali zote zitakuwa na nafasi yake kwenye kukopa,” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu mpaka wa mkopo kwa nchi, mwenyekiti wa tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba alisema inategemea na serikali yenyewe kwani hata hivi sasa utaratibu huo upo na ikiwa serikali ya Zanzibar inataka kukopa hudhaminiwa na Serikali ya Muungano.
Kukwepa kutaja Serikali ya Tanganyika
Kuhusu kukwepa kusema Serikali ya Tanganyika, Jaji Warioba alisema walikuwa wanatengeneza Katiba ya Muungano ambayo inafahamika kuwa ni Tanzania Bara na Zanzibar.
Alieleza kuwa kwa Katiba ijayo ikiwa suala hilo litawekwa, Zanzibar wanaweza kuchagua majina yao bila kuingiliwa, kwani halikuwa jukumu lao kuwachagulia.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, ikiwa Tanzania Bara watakapotunga katiba yao watataka jina libaki Tanganyika, itakuwa juu yao, lakini kwa Katiba ya sasa inahusu Tanzania Bara na Zanzibar.
Bunge la Katiba Novemba
Kuhusu Bunge la Katiba, Warioba alisema litakaa baada ya tume yake kukamilisha rasimu ya pili ya Katiba ambayo itatokana na mapendekezo ya wananchi.
Alisema wanatarajia kuikamilisha kazi hiyo mwishoni mwa Septemba mwaka huu.
“Mawazo yao yatarudi kwetu na tutaangalia kama kuna umuhimu wa kubadili popote au kuacha kama ilivyokuwa ili kutengeneza rasimu ya mwisho.
“Utaratibu wa kisheria ambao umewekwa tunatakiwa tumalize kazi yetu mwisho wa Oktoba ili Novemba Bunge la Katiba likutane,” alisema Jaji Warioba.
Alieleza matarajio ni kwamba mwishoni mwa Septemba watakuwa wamekamilisha rasimu ya pili ambayo pia wataitangaza na baada ya mwezi mmoja, Bunge la Katiba litakutana.
Pamoja na mambo mengine alisema iwapo katika mapendekezo ya wadau wataona kuna jambo zito wanaweza kuliingiza watafanya hivyo lakini mpaka waliridhie kwamba suala hilo ni bora zaidi.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, sheria inaelekeza kwamba baada ya kuiandaa rasimu waitangaze kwenye gazeti la serikali na umma kisha iende kuzungumzwa na wananchi kwenye mabaraza yao pamoja na makundi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment