Monday, June 10, 2013

Lipumba: Kura ya maoni isubiri rasimu za katiba za Bara, Z'bar

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kura maoni ya katiba ya Muungano isubiri kukamilishwa kwa rasimu ya katiba ya Tanzania Bara pamoja na marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ili wananchi wazijadili zote kwa pamoja.

Alisema lengo ni kuepusha mkinzano na katiba hizo na ya Jamhuri ya Muungano.

Akitoa maoni ya awali ya CUF kuhusu rasimu ya katiba mpya jana jijini Dar es Salaam, alisema hana pingamizi kuwa wajumbe wa tume ya Tanzania Bara waandae rasimu ya katiba ya Bara na wajumbe wa Zanzibar waandae mapendekezo ya marekebisho ya katiba ya Zanzibari.

Hata hivyo, alisema muda wa kuyatekeleza hayo na kubadilisha sheria zifuate matakwa ya katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 haupo.

Lipumba alisema pendekezo la rasimu ya katiba kuwepo Tume Huru ya Uchaguzi ni la msingi na lianze kufanyiwa kazi mara moja na kufanya mabadiliko ya kisheria ya kuunda Tume ya Uchaguzi ili uchaguzi ujao uendeshwe na tume iliyo huru . 

Alisema kutokana na hali hiyo, mchakato wa mabadiliko ya katiba utaendelea baada ya uchaguzi kukamilika na sheria husika kufanyiwa mabadiliko.

Alisema siyo, lazima Mwenyekiti na Makamu wake wa Tume ya Uchaguzi wawe watu waliowahi kushika wadhifa wa Jaji wa Mahakama ya Rufani au Mahakama Kuu na awe ameshika wadhifa huo kwa kipindi kisipo pungua miaka mitano kama rasimu ya katiba inavyoeleza katika kifungu 181(4).

Pia, alisema lazima pawe na mwongozo wa kudhibiti mikopo na kuongezeka kwa deni la Taifa kwani nchi inaweza kuingizwa katika mgogoro wa madeni, endapo kutakuwa na uhuru wa serikali zote tatu kukopa ndani na nje ya nchi. 

Kuhusu suala la kila Mkoa kwa Tanzania Bara na Wilaya kwa Zanzibar kuwa ni jimbo la uchaguzi, Lipumba alisema tume iweke wazi juu ya vigezo vya kufanya mikoa na wilaya kuwa majimbo ya uchaguzi na je majimbo hayo yataundwa na tume au tayari yameishatajwa na katiba?”

Lipumba alisema kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ni muhimu iwepo ndani ya katiba kwani rasimu haina asasi hiyo muhimu ya usimamizi na uwajibikaji.
Aliaema CUF inapendekeza  Tume ya Kupambana na Rushwa iwe na uhuru wa kupeleka kesi mahakamani bila idhini ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Suala rasimu kutoa uhuru kwa serikali zote tatu kuwa na Jeshi la ulinzi, Polisi na Usalamawa Taifa, alisema linaweza kuzua utata ndani ya nchi endapo katiba haitaweka  bayana utaratibu wa kuzuia migongano kati ya vyombo vya dola vya muungano na vile vya washirika, hususan ni pale itakapo tokea serikali ya Muungano ikaongozwa na chama A, serikali ya Zanzibar na chama B na serikali ya Tanzania Bara na chama C na serikali zote zikawa na polisi na usalama wake wa taifa.

Kuhusu masuala ya haki za binadamu, alisema katiba itamke wazi kuwa mwanamke mjamzito ana haki ya kupata lishe bora ba huduma za afya wakati wa ujauzito na kujifungua.

Vilevile watoto bila kujaliu wezowa wazazi wao wana haki ya kupata lishe bora, huduma za msingi za afya na elimu inayomuandaa mtoto kukabiliana na changamoto za maisha.

No comments:

Post a Comment