Rasimu ya Katiba mpya iliyotangazwa wiki iliyopita itakuwa mwiba mkali kwa watumishi wa umma tofauti na ilivyo katika Katiba ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania (1977).
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji, itakuwa na nguvu ya kuwafikisha katika vyombo vya sheria watumishi watakaobainika kuvunja maadili na miiko ya kazi.
Katiba ya sasa ambayo nguvu ya utendaji kazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ilitegemea masharti yaliyowekwa kwenye sheria na siyo kuwa na nguvu ya kuwajibisha kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu hiyo.
Rasimu hiyo ibara ya 188 kifungu cha (1) hadi (5) inaeleza jina la Tume na sifa za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti.
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti watateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma na watashika madaraka yao baada ya kuthibitishwa na Bunge.
Sifa za viongozi hao zimeainishwa kuwa ni mwenye Shahada ya Chuo Kikuu kinachotambulika kwa mujibu wa sheria za nchi, mwenye uzoefu katika utumishi wa umma kwa kipindi kisichopungua miaka kumi na mwenye heshima, weledi, uaminifu, uadilifu na asiye na tabia au mienendo yenye kutiliwa shaka.
Bonyeza Read More Kuendelea
Rasimu hiyo inapendekeza kuwapo kwa Tume ya Maadili ya Viongozi na Uwajibikaji badala ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Tofauti na utendaji kazi wa sekretarieti, Tume hiyo kwa kuzingatia sheria itatangaza kwa umma mambo yote yanayohusiana na uchunguzi iliyoufanya iwapo mazingira yataruhusu.
Rasimu hiyo inaonekana kujibu kilio cha Watanzania cha kutoweka kwa miiko na maadili ya viongozi na sekretarieti kutokuwa na nguvu ya kuwawajibisha na kugeuka kwenye muundo wa kubebana.
Kwa mujibu wa ibara ya 189 kifungu cha (1), majukumu ya jumla ya Tume yatakuwa ni kufuatilia na kuchunguza tabia na mwenendo wa viongozi na watumishi wa umma kwa madhumuni ya kusimamia na kuhakikisha kuwa maadili ya viongozi wa umma na miiko ya uongozi wa umma inazingatiwa, inalindwa na kuheshimiwa katika utumishi wa serikali, Bunge, Mahakaman, Taasisi na idara nyingine zote za umma.
Ibara ya 189 kifungu (2) inaeleza majukumu mahsusi ya Tume hiyo yatakuwa ni kusimamia maadili na uwajibikaji katika utumishi wa umma, kufanya upekuzi na kufuatilia kumbukumbu za wanaoomba nafasi za uongozi wa umma.
Katika ibara hiyo sehemu (a) hadi (o), imefafanua kwa kina majukumu ya tume hiyo ambayo ni, kuchunguza tabia na mwenendo wa mtumishi au kiongozi wa umma na kuchukua hatua pale inapostahili, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Inasema ni Tume hiyo itasimamia sheria itakayotungwa na Bunge kuhusu maadili na uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma na kushughulikia masuala ya ubadhirifu wa fedha na mali za umma.
Rasimu hiyo imependekeza kufanya uchambuzi yakinifu kwa viongozi wa umma wanaopewa dhamana kabla ya kuingia madarakani, kutoa elimu ya maadili kwa umma kuhusu miiko na maadili ya viongozi wa umma.
Pia, kufanya uchunguzi kwa maamuzi yake yenyewe au baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mtu yeyote, kutokana na kutenda au kutokutenda kwa kiongozi au mtumishi yeyote wa umma au wakala wa serikali, ikiwa kitendo alichotenda au kutokutendwa ni kinyume cha maadili ya umma.
Kumuelekeza, baada ya kupata malalamiko au itapoona inafaa, kiongozi au mtumishi wa umma au wakala wa serikali au chombo chochote cha umma kufanya tendo lolote au jambo lolote linalotakiwa na sheria, au kuacha, kuzuia au kusahihisha utendaji mbaya au usiostahihi wa majukumu yake.
Kutoa maelekezo kuhusu kuchukuliwa hatua kiongozi au mtumishi yeyote wa umma, kumuelekeza kiongozi au mtumishi wa umma, kwa mujibu wa sheria kutoa nyaraka zinazohusiana na matumizi ya ofisi, matumizi ya fedha au mali za umma, au kutoa taarifa ya matumizi mabaya kwa Tume kwa hatua stahiki.
Rasimu hiyo imependekeza Tume hiyo kuchunguza jambo au mazingira yoyote yanayokiuka au kusababisha ukiukaji wa maadili na kuandaa kanuni za taratibu na matumizi ya mamlaka au utekelezaji wa kazi na majukumu ya Tume kama itakavyoelekezwa na sheria.
Tofauti na katiba ya sasa ambayo imeeleza uwapo wa Kamishina wa Sekretarieti na wajumbe watakaopendekezwa na sheria, lakini Katiba imetaja idadi ya wajumbe wasiozidi saba, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti.
Ibara ya 16 kifungu cha (1), inayowalazimisha watumishi wa umma kutangaza mali ndani ya siku 30 baada ya kupata au kuacha uongozi pamoja na madeni yake.
Ibara ya 17 kifungu cha (1) inapendekeza kiongozi wa umma kutoshiriki katika jambo au shughuli yoyote ambayo ana maslahi nayo yeye binafsi, mwenza wake, mtoto wake, jamaa yake, rafiki au mtu yeyote wake wa karibu.
Rasimu hiyo imependekeza kuwapo kwa miiko ya uongozi wa umma katika ibara ya 20 kifungu (2) sehemu (a) (i) hadi (vii).
“Kiongozi wa umma hatopaswa kutoa au kupokea rushwa, kujilimbikizia mali kinyume cha sheria, kusema uongo au kutoa taarifa zisizo za ukweli, kutoa siri za serikali kinyume na sheria, kutumia wadhifa, nafasi au cheo chake kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa au marafiki zake au mti yeyote aliye na uhusiano naye wa karibu, kufanya vitendo vya uzembe, uvivu, ubaguzi, kiburi, dharau au unyanyasaji wa kijinsia.”
Ibara ya 21 kifungu cha (1), inapendekeza mtumishi wa umma aliye katika ajira ya kudumu hataruhusiwa kuingia katika ajira nyingine yoyote yenye malipo ya mshahara.
Kifungu cha (3), kinasema mtumishi aliyestaafu na anayepokea malipo ya pensheni kutokana na fedha za umma hataruhusiwa kuwa Mwenyekiti, Mkurugenzi au mtumishi zaidi ya vipindi viwili katika shirika au kampuni inayomilikiwa na kuendeshwa kwa fedha za umma au chombo chochote cha umma.
Hivi karibuni katika Kongamano ya Kigoda cha Mwalimu Nyerere, ililojumuisha wasomi wa ndani na nje ya nchi, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kilio kikubwa kilikuwa ni kutupwa kwa Azimio la Arusha ambalo lilikuwa na miiko na maadili ya viongozi wa umma na kuruhusu watumishi kujilimbikizia mali na kutumia ovyo mali ya umma.
No comments:
Post a Comment