Saturday, June 8, 2013

Barabara Ifakara kujengwa kiwango cha lami

SERIKALI imesema inatambua umuhimu wa barabara ya kutoka Kidatu - Ifakara- Taweta hadi Madeke kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Suzan Kiwanga ( CHADEMA).
Katika swali lake Kiwanga alitaka kujua ni lini barabara kutoka Kidatu- Mlimba hadi Madeke mpakani mwa wilaya ya Njombe itajengwa kwa lami ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima na wananchi kwa ujumla.
Pia Kiwanga alitaka kujua kama serikali haioni kuwa barabara hiyo imekidhi vigezo kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa wa kilimo cha mpunga unaofanywa na KPL kwenye kata ya Mngeta.
Akijibu, Magufuli alisema kuwa serikali imekuwa ikijenga barabara ya Kidatu- Ifakara yenye urefu wa kilomita 73.2 kwa awamu kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Kati ya mwaka 2006 hadi 2008 jumla ya kilomita 16.17 zilijengwa kwa kiwango cha lami katika awamu mbili kuanzia Kiberege hadi Ziginali kilomita 10, na kutoka Kibaoni (Ifakara) hadi Ifakara Mjini kilomita 6.17,” alisema Magufuli.
Aidha  alisema kuwa serikali imeshakamilisha kazi ya usanifu kutoka Kibaoni (Ifakara) hadi Ziginali kilomita 16.8 mwaka wa fedha 2011/2012 na kisha kuendelea kutafuta fedha za ujenzi.
Pia alisema kutokana na mkoa wa Morogoro kuwa ukanda wa kusini wa kilimo nchini, serikali ya Marekani kupitia shirika la Maendeleo la USAID imekubali kugharamia kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mikumi - Kidatu- Ifakara yenye urefu wa Kilomita 103.3 na mkataba wa msaada wa fedha ulishasainiwa Januari 23 mwaka huu.
Kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Ifakara- Taweta- Madeke kwa kiwango cha lami, Dk. Magufuli alisema serikali imepanga kuitekeleza kwa awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2013/2014, serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa sehemu ya barabara kutoka Ifakara-Kihansi yenye urefu wa kilomita 126.

No comments:

Post a Comment