Tuesday, June 4, 2013

BAWACHA watakiwa kudumisha amani

BARAZA la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA (BAWACHA), limetakiwa kudumisha amani, upendo na mshikamano ndani na nje ya chama wawapo katika harakati za ukombozi.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, alipozungumza na wanawake wa baraza hilo wakati wa kufunga semina ya siku nne iliyofanyika mjini hapa.
Alisema kwa sasa kuna watu wengi ambao wanakimezea mate chama hicho ili kiwe na mpasuko na kidhoofike.
“Kina mama msikubali kudhoofisha ukombozi kwa kukubali kuongwa ama kununuliwa na chama kingine cha siasa kwa kupewa kanga, vilemba, T-shirt ama vyakula na kama kuna mtu atafanya hivyo atambue damu na kilio cha maskini ambao wamesababishiwa na CCM vitawaandama,” alisema Selasini.
Mbali na hilo, aliwataka kina mama ambao wamepatiwa elimu ya kukuza chama kupeleka elimu hiyo kwa wanawake wote kuanzia ngazi ya kitongoji hadi taifa na kuwataka wasiwe waoga katika kujikita katika kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama.
Makamu Mwenyekiti wa BAWACHA Tanzania Zanzibar, Mariam Msabaha, aliwataka kina mama kuondokana na tabia ya hofu katika kuwania nafasi za majimbo na badala yake kuvaa ujasiri wa kutafuta uongozi ndani na nje ya chama.

No comments:

Post a Comment