Tuesday, June 4, 2013

Nec yapendekezwa kuvunjwa, iundwe tume huru

Rasimu ya Katiba Mpya iliyozinduliwa jana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, imependekeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ivunjwe na kuunda Tume Huru ya Uchaguzi.
Jaji Warioba alisema Tume Huru ya Uchaguzi itakuwa na wajumbe ambao watateuliwa na Rais na kuthibitishwa na Bunge, baada ya kutuma maombi na kufanyiwa usaili.
Jaji Warioba alisema muundo wa tume hiyo mpya, utahusisha kufutwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo sehemu ya majukumu yake, yatapelekwa kwenye tume hiyo.
Alitaja sifa za wajumbe hiyo kuwa, mwombaji kutokuwa mwanasiasa, mwanaharakati au kutotokana na taasisi yoyote ya kiraia.
“Majina ya waombaji yatachambuliwa na kamati ya uteuzi ambayo mwenyekiti wake atakuwa ni Jaji mkuu na viongozi wengine sita, ambao ni majaji wakuu wa nchi washirika, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, maspika wa Bunge wa nchi washirika na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu,” alisema Jaji Warioba.
Jaji Warioba alisema baada ya kamati hiyo kupendekeza majina matatu yanayofaa, yatawasilishwa kwa Rais ambaye atateua mwenyekiti, makamu na wajumbe wengine, kabla majina hayo hayajapelekwa bungeni kwa ajili ya uthibitisho. Licha ya hilo, Tume Huru ya Uchaguzi itakuwa na mamlaka ya kupokea pingamizi za matokeo ya uchaguzi wa urais ndani ya kipindi ya mwezi mmoja baada ya kutangazwa.
Kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Mwenyekiti wa tume hiyo amekuwa akiteuliwa moja kwa moja na Rais bila kuhojiwa au kujadiliwa na Bunge au kamati yoyote.

1 comment: