MWENYEKITI wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, anayemaliza muda wake, Profesa Issa Shivji, amesema kama rasimu ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ikikubaliwa bila mabadiliko makubwa itasababisha kuvunjika kwa Muungano.
Kauli hiyo aliitoa jana katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati akitoa mhadhara wa kuaga wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Kigoda hicho kwa Wana Kigoda wenzake na Jumuiya ya chuo hicho.
Profesa Shivji aliainisha upungufu uliomo katika rasimu hiyo iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ambapo alisema yanaweza kusababisha kuzuka kwa migogoro mingi na mikubwa itakayovunja Muungano.
Alibainisha rasimu hiyo imekosa maelezo ya wazi na thabiti kuhusu ukuu wa Katiba ya Muungano juu ya katiba nyingine za washirika wa Muungano, hali itakayosababisha migongano na kutoelewana kati ya mamlaka za washirika wa Muungano na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema kuwa Ibara ya nane ya rasimu hiyo inayozungumzia ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayopendekezwa ina kasoro kubwa kwani imeeleza kuwa ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano utakuwa katika mambo ya Muungano tu na si vinginevyo.
“Ukisoma rasimu hii ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 8(1) inasema na hapa nitanukuu: “Bila ya kuathiri masharti ya katiba za washirika wa Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, Katiba hii itakuwa sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano,” mwisho wa kunukuu. Kwa hiyo Ibara hii inaeleza wazi kabisa kuwa katiba inayopendekezwa haitakuwa na nguvu za kisheria juu ya katiba za washirika wa Muungano,” alisema Shivji.
Alifafanua kuwa katiba zote za nchi zinazofuata muundo wa shirikisho kama unaopendekezwa na Tume ya Warioba zikiwemo Katiba za Marekani na Australia, zina vipengele vinavyoeleza wazi kuwa katiba ya shirikisho ni sheria kuu juu ya katiba za washirika, hali aliyosema imeondoa mianya ya kuibuka kwa migongano kati ya mamlaka za shirikisho na washirika wao.
Kwa msingi huo, Profesa Shivji alisema kuwa muundo wa Muungano unaopendekezwa ndani ya rasimu ya Warioba ni tegemezi na dhaifu kwasababu haujawekewa nguvu ya kikatiba ya kuulinda na kuupa mamlaka thabiti.
“Huu muundo ingekuwa sahihi zaidi kama mtu atauita kuwa muundo wa dola tatu badala ya serikali tatu kama rasimu inavyoeleza, kwa sababu tunaona serikali zote tatu zina mihimili mikuu mitatu ya dola; yaani Bunge, Mahakama na Serikali,” alibainisha Shivji.
Akichambua zaidi Profesa Shivji alisema kuwa hata Tume ya Mahusiano ya Muungano inayopendekezwa na rasimu haitaweza kuepusha migogoro baina ya Serikali ya Muungano na washirika wa Muungano kwa sababu si chombo cha kiutendaji.
Alisema kuwa kimsingi rais wa Tanganyika atakuwa na nguvu na sauti kubwa kuliko marais wengine kutokana na kuwa na eneo kubwa la kiutawala, watu wengi, rasilimali nyingi na atakuwa akitoa mchango mkubwa wa kuendesha serikali ya shirikisho.
Mambo mengine aliyosema kuwa yatasababisha migogoro kwa Muungano ni kuruhusu washirika wa Muungano kuwa na majeshi yao, benki kuu zao na uwezo wa kukopa kutoka nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment