Friday, May 24, 2013

Wamemdharau Nyerere na Kuivunja Misingi - Sasa hawana pa Kushikilia!

Kwao Nyerere siyo "Baba wa Taifa" tena; kwao ni "Mzee Nyerere"; kwa watawala wetu hawa walioshindwa wanasema wamefanya mambo mengi sana ya maendeleo kkuliko "Wakati wa Nyerere". Wanajitamba kuwa wao wamekuza sana demokrasia na kuwa hata "Nyerere" hakuweza kufanya waliofanya wao. Katika upotofu wao wanaamini kabisa kuwa wao wanapendwa zaidi; na wanapendwa kwa sababu wamefanya mengi mno na hawaelewi kwanini watu hawaoneshi shukrani! 

Ndio maana kila kukicha hawaachi kubembeleza kwa wananchi kuwa "hamuoni tunayofanya" na kuwa watu wanalaumu tu lakini hawatoi pongezi kwa "mazuri mengi". Imefika mahali Kikwete mwenyewe amedai mahali fulani anataka kukumbukwa kuwa ni "bwana maendeleo"; anasema hivi kwa sababu anapokaa ofisini anaamini kabisa kuwa ameweza kuwapatia Watanzania 'vitu" vingi sana vya maendeleo kuliko wakati wowote wa historia - vitu ambavyo hata Nyerere hakuweza kuwapatia. Kikwete anataka awe juu ya Nyerere kwa kila kipimo kwani kipimo kilichowekwa ni Nyerere. Na bila ya shaka kuna sababu - Nyerere hakuamini kuwa walikuwa tayari kuwaongoza Watanzania - hawa kina Kikwete na Lowassa. 

Sasa katika kumdunisha Nyerere ili wao wakue wameacha propaganda chafu dhidi ya Nyerere na uongozi wake. Leo hii tunashuhudia mambo ambayo - pamoja na 'ubaya' wote wa Nyerere hayakuwahi kutokea chini ya "dhaalim Nyerere"! Matukio yanayotokea leo hii ukiwaambia watu walioshi wakati wa Nyerere, chini ya chama kimoja na uongozi thabiti hawawezi kuelewa yanawezekana vipi kutokea. Watu wa enzi za Mwalimu wanakumbuka vizuri kuwa kiongozi aliyefanya madudu hakuvumuliwa; na bahati mbaya wakati ule hatukuwa na wasomi wengi na watu wengi wenye udhoefu lakini Nyerere hakuwaonea huruma. Wapo ambao hadi leo wana kinyongo na Nyerere kwa sababu hakuwapa nafasi nyingine. 

Lakini katika kumdharaulisha Nyerere na kujaribu kupuuza mafanikio yake makubwa zaidi wamejikuta hawana pa kukimbilia! Tuliokuwa wakati wa Nyerere hatukumbuki jinsi JWTZ likitumiwa kisiasa kama linavyotumika hivi sasa! Fikiria ndege ya jeshi itumwe kumchukua raia kumpeleka Mahakamani!? Kwamba, ati vurugu za uchaguzi zilazimishe JWTZ kuingilia kati! Kwamba vikosi vya kutuliza ghasia vya polisi vizidiwe nguvu na mara moja kuliingiza jeshi kufanya kazi za jeshi la polisi! Unthinkable! Lakini wao wanaamini wako sawa! 

Lakini siyo kwamba wamedharaulisha na kumtupa nje Nyerere ni zaidi ya hivyo; wameitupa misingi ya taifa letu. Wanataka kujenga kwa misingi ya mabua! Waliachiwa misingi ya zege lakini wao wakiamini ni 'magenius" wameamua kutengeneza 'taifa jipya' nje ya misingi iliyounda Tanzania. Leo hii Watanzania kwa mamilioni wananung'unika moyoni kwani hawatambui kama hili ndilo Taifa waliloachiwa kama urithi. Sasa hivi inaonekana Tanzania inazidi kufanana zaidi na mataifa mengine ya Afrika kiasi kwamba linaweza lisitofautike tena mbele ya umma. 

Wameitupa misingi sasa hawana cha kujengea; wamebakia kutumainia vitisho, dharau na matumizi ya nguvu. Wameshindwa kabisa kujenga hoja - kwa mfano kwenye hili suala la gesi. Hawana ushawishi wa hoja na badala yake hata kauli zao wanazotoa zimejaa dharau (contempt) na matokeo yake watu nao wanawadharau! Wanafikiri vitisho na kejeli zinajibu hoja! 

Kushindwa kwa sera zao mbalimbali ni matokeo ya kuachana na misingi ya taifa; wanafikiri wanaweza kutengeneza sera nzuri nje ya misingi ya taifa! Matokeo yake: 

Sera ya Nishati na Madini imeshindwa
Sera yao ya Gesi imeshindwa - hata kabla haijaanza!
Sera yao ya Elimu imeshindwa
Sera yao ya siasa imeshindwa
Sera yao ya Sayansi na Teknolojia imeshindwa 
Sera yao Mazingira imeshindwa 
N.k

Wameshindwa lakini hawaamini wameshindwa na badala yake wanawalaumu wanaowaambia wameshindwa kwa kushindwa kwao! Kana kwamba, wanaowalaumu wakinyamaza basi wao wataweza! Wenyewe wanaambizana kuwa wakipewa nafasi nyingine 2015 basi wataaanza kuweza; na wapo watu wanaamini kuwa hilo linawezekana; kwamba pundamilia anaweza kugeuka na kuwa farasi! Kama wenyewe wameshindwa kuvuana magembe licha ya mbwembwe zote za "kuvuana magamba" kweli kuna uwezekanow wataweza? Na ukweli ni kuwa walipofika sasa hawawezi kurudi kwenye misingi ya Nyerere na Taifa letu; kwa sababu kurudia misingi hiyo ni kujishtaki katika historia.

kuna namna moja ttu ya kuwasaidia... kuendelea kuwakataa.

Maskini CCM!
Maskini Kikwete
Maskini Tanzania chini yao!

No comments:

Post a Comment