Friday, May 24, 2013

Rufaa ya Mahimbo dhidi ya mchumba wa Dk. Slaa yatupwa

Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na aliyekuwa mume wa Josephine Mushumbusi, Mahimbo baada ya kuiona haina msingi wowote kisheria.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Aniseth Wambura, akieleza kwamba  mahakama yake imefikia uamuzi wa kuitupilia mbali rufaa hiyo kwa sababu haina mantiki ya kisheria.

Alisema mahakama imekubaliana na hukumu iliyotolewa Aprili mwaka jana na Mahakama ya  Mwanzo Sinza katika kesi ya madai ya talaka iliyokuwa imefunguliwa na Mushumbusi.

Mahakama hiyo ya chini ilitangaza kuwa hakukuwa na ndoa baina ya watu hao kwasababu Mahimbo alikuwa ni mzinzi, simwaminifu katika ndoa yake na alikuwa akimtesa mkewe.

Hakimu Wambura alisema baada ya mahakama yake kusikiliza hoja za mwomba rufaa na mjibu rufaa, mahakama imefikia uamuzi wa kukubali hoja za Mushumbisi kuwa kwa tabia mbaya ya uzinzi na ukosefu wa uaminifu katika ndoa yake hapakuwapo na ndoa baina yao hivyo inatangaza kuwa hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza ambayo iliivunja ndoa hiyo ilikuwa hukumu sahihi.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili anayemtetea Mshumbuzi, Philemon Mutakyamilwa alisema amefurahishwa na hukumu hiyo kwani mahakama imetenda haki kwasababu kesi hiyo ya madai ya talaka ilikuwa na msukumo wa siasa chafu zilizokuwa na lengo la kumchafulia jina mteja wake (Mshumbusi) ambaye kwa sasa ni mzazi mwenza wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa.

No comments:

Post a Comment