KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuomba hekima kwa Mwenyezi Mungu kutokana na matukio yanayotokea sasa nchini.
Alisema hali inayotokea sasa ni matokeo ya wananchi kupuuzwa na kutokusikilizwa katika suala zima la uwekezaji unaofanyika sehemu mbalimbali za nchi.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana katika kijiji cha Giroda Babati vijijini, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika ziara yake ya siku tisa ya ujenzi wa Chama mkoani Manyara.
Kabla ya kutoa kauli hiyo Dk. Slaa aliwaomba wananchi wasimame kwa muda wa dakika moja, kuomboleza vifo vilivyotokea mkoani Mtwara.
Aliongeza kuwa kuendelea kuwapuuza wananchi wa Mtwara ni kuendelea kucheza na jipu linalopaswa kutumbuliwa na kwamba njia sahihi ni kukaa na kuwasililiza wananchi katika uwekezaji na kufikia muafaka pasipo kutumia nguvu.
Alisema wanachotaka wananchi wa Mtwara ni kujua namna watakavyonufaika kwa kile alichoeleza kuwa katika uwekezaji wowote wanufaikaji wa kwanza wanapaswa kuwa wananchi.
Alisisitiza kuwa katika hali ya Mtwara kulihitajika busara za kawaida za kutatua msingi wa tatizo badala ya wananchi kupigwa mabomu, risasi na kisha kukamatwa.
“Ni jambo la aibu kuwapiga mabomu wananchi wanaodai kunufaika na rasilimali za nchi yao hapa kunahitajika elimu ya kuwafahamisha haki zao ni zipi na siyo mabomu,” alisema Slaa.
No comments:
Post a Comment