BAADHI ya wananchi mkoani Tabora, wameunga mkono kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, kuwa wabunge wa CCM mkoani Tabora ni wasaliti kwa wapiga kura wao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema kauli hiyo ina ukweli kwa kuwa karibu wabunge wote wanaonekana mara chache kwenye majimbo yao.
“Jamani kauli ya Zitto ni ya kweli, hebu angalieni wabunge karibu wote utawaona wanakuja mara chache sana majimboni na wanaweza kuja na wasifanye mikutano yoyote na wananchi,” alisema mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina na Haruna.
Walisema hata kwenye vikao vya DCC na RCC wabunge hao ni nadra kuhudhuria.
“Mara kadhaa ukisoma kwenye muhtasari utaona labda ni mbunge mmoja tu alikuwepo wengine wote ni udhuru,” alisema mmoja wa wananchi hao.
Walisema wamechoshwa na wabunge wanaokwenda na kujifanya wazaliwa wa mkoa huo na baadaye kuhamishia makazi na shughuli zao jijini Dar es Salaam.
“Tunatafakari kwa umakini maneno ya Zitto kuwa Tabora CCM imepafanya ni sehemu ya kuchota kura na kamwe wataendelea kubaki kama tulivyo kwenye kisiwa na hawajui lini tutaokolewa labda pale watakapofanya maamuzi magumu ya kuitosa CCM mwaka 2015,” walisema. Wakati wananchi hao wakitoa kauli hiyo, Rais Jakaya Kikwete kwenye kikao chake na wabunge wa CCM amekea tabia ya wabunge watoro wasiotembelea majimbo yao.
Katika kikao hicho kilichofanyika mjini Dodoma, rais amekaririwa akisema baadhi ya wabunge wameyatelekeza majimbo yao kwa kutorudi kusikiliza kero za wananchi na kutimiza ahadi zao.
No comments:
Post a Comment