Wednesday, May 22, 2013

HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014 (Inatolewa chini ya kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013)


A: UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri wa Nishati na Madini ilianzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 21 cha Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Desemba 2010.
Mheshimiwa Spika, Katika kujadili Mapitio ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2013/2014 naomba tuyatafakari maandiko ya katika muktadha wa uongozi wetu wa leo na hatma ya sekta hizi mbili muhimu za nishati na madini.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE  katika ukurasa wa pili tutafakari  kwamba,  naomba kumnukuu  ‘ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki. Kwake wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa.Ukiniona nataka kulipiga teke jiwe kwa kuwa nafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nitalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi kupuuzwapuuzwa.
Mheshimiwa Spika, Tuendelee kutafakari maandiko ya Nyerere kwamba  Wakati mwingine, mtu tunayempinga huwa anamakosa kweli, lakini hoja tunazozitoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake.Nikisema mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine nifikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha.Ni kweli mbili mara tatu ni sita;lakini mbili na tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali yako kwa kusema kuwa meno yangu ni machafu ,au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana, Huu ni mfano wa upuuzi; lakini mara nyingi hoja tunazozitumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda,au kukubali mawazo yetu, huwa haziuhusiani kabisa na mambo tunayojadili’.
Mheshimiwa Spika, Tutafakari maandiko ya Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA  uk. 50,  nanukuu Rais Mwinyi ni mtu mwema na mpole, lakini ni kiongozi dhaifu; au upole wake na udhaifu wake unatumiwa na watu ambao wala si wema wala wapole kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu, Kipindi chake cha pili kinakaribia kwisha”.

Mheshimiwa Spika, Tutafakari maandiko mengine ya Mwalimu Nyerere kwamba “lakini hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa chama na Serikali. Wala tukiendelea na hali hii, bila kubadili uongozi wa Chama na Serikali, sina hakika kama tutafika huko salama.Masuala muhimu ya nchi yetu hayatashughulikiwa.Viongozi wetu wataendelea na matendo yao ya kuvuruga muungano. Matatizo ya kweli ya muungano hayatashughulikiwa, maana hatuna serikali ya kuyashughulikia.Na masuala mengine muhimu ya uchumi, huduma za umma, rushwa,chuki za uzawa na ukabilana udini yataachwa yajitatue yenyewe.Nasema , katika hili kama hiyo sina hakika kama tutafika salama;na tukifika “salama”,tukiwa na uongozi huu huu wa chama na serikali , mbele yetu kutakuwa ni giza tupu.Majuto ni mjukuu, huja baadaye.Tunaweza tukafikishwa mahali tukilinganisha uongozi wa rais Mwinyi na wa rais wa kesho tukaona kuwa chini ya Ndugu Mwinyi, Pamoja na udhaifu wake wote, tulikuwa peponi”!

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere anaendelea kuandika kwamba  “Waingereza wana msemo  “Nature abhors vacuum”,  “hulka huchukia ombwe” . Hata siasa huchukia ombwe. Kama uongozi ni mbovu, upo kama haupo au upo kwa masilahi ya wenyewe, watatokea watu waujaze uwazi uliopo;hauwezi kuachwa wazi hivi hivi.Lakini uongozi mbovu ni kama mzoga, unatabia ya kukaribisha mafisi na mainzi. Tusidhani kuwa hulka ya siasa yetu ni tofauti na hulka ya siasa ya watu wengine; kwamba sisi tunaweza kuvumilia uongozi mbovu na tusivune matunda ya hulka ya uongozi mbovu”.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere alikuwa akiandika wakati wa awamu ya Rais Mwinyi kuhusu masuala yanayohusu Muungano; sisi tutafakari maandiko haya katika muktadha wa uongozi wa sasa wa taifa letu na mustakabali wa sekta nyeti kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi za nishati na madini.

Bonyeza Read More Kuendelea



B: MASUALA MTAMBUKA
1.0 MAPITIO UJUMLA YA UTEKELEZAJI KWA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2013/2014
Mheshimiwa Spika, tarehe 27 Julai, 2012 niliwasilisha Bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kufuatia maoni hayo, yapo masuala machache ambayo Serikali imeyazingatia kwenye utekelezaji na mengine mengi ambayo Serikali haikuyazingatia pamoja na umuhimu wake kwa maslahi ya nchi na maisha ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka kiwango cha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kuongezwa, miongoni mwa masuala ambayo serikali imetekeleza ni pamoja na kuongeza bajeti ya wizara hii kwa kupanga kutumia kwa mwaka 2013/2014 jumla ya shilingi 1,099,434,031,000/= ikilinganishwa na mwaka 2012/2013 ambako kiasi cha shilingi 641,269,729,000/= kilipangwa kutumika. Aidha napenda kuikumbusha serikali kuzingatia vipaumbele vya miradi ya maendeleo ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza katika Hotuba zake za 2011 na 2012 ili kuweza kuleta maana ya ongezeko hili la bajeti kwa maana ya kuvipatia vipaumbele uzito unaostahili kwa Kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilishauri kuwepo kwa mfumo thabiti wa kuhakikisha maoni na maazimio yanatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu. Lakini serikali imeendelea kupuuza mapendekezo hayo na kutoa ahadi ambazo haikuwa tayari kuzitekeleza, mathalani ahadi ya Mhe Waziri Mkuu aliyotoa wakati akiahirisha bunge la bajeti 2011/2012 ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza pesa wizara ya Nishati na Madini lakini tofauti na ahadi yake, Serikali ikaamua kuja na mpango wa kukopa fedha katika taasisi za fedha ili kulinusuru shirika la umeme Tanzania TANESCO, ambao nao haujatekelezwa kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo ninatambua maoni  machache ambayo yalizingatiwa kuhusu gesi asili, ikiwemo kuendelezwa kwa mchakato wa kuwa na sera na sheria ya gesi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ikaitaka Serikali ieleze hatua ilizochukua juu ya maoni ya kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo hayakuzingatiwa na  mengine yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge na michango ya Wabunge kwa nyakati mbalimbali mwaka 2011 na 2012. 
Aidha, ni Kwa bahati mbaya kabisa serikali haikupenda kufanyia kazi maoni na ushauri iliyopewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,kamati ya Bunge na wabunge mbalimbali kwa nyakati tofauti na ambayo kama yangezingatiwa kikamilifu yangeweza  kuliepusha taifa na matatizo yaliyotokea katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ambayo bado yanaendelea mpaka sasa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 makadirio ya mapato na matumizi ya kawaida yanaombewa jumla ya shilingi 107,221,286,000/= kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi 11,612,542,000/= ni  kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi zilizochini yake na kiasi cha shilingi 95,608,744,000/= ni kwa ajili ya matumizi mengine  (OC). Matumizi haya yanaonekana ni pungufu ya kiasi cha shilingi 2,857,582,000/=  kwenye bajeti ya mwaka jana katika fungu hili la matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, upungufu huu, unaacha maswali, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inaitaka serikali kuwaeleza watanzania sababu za kupungua kwa bajeti ya mishahara ya wizara na taasisi zilizokochini yake, ambayo katika mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara ya Nishati na Madini ilitengewa shilingi 17,292,347,000/= na kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 serikali inaomba kiasi cha shilingi 11,612,542,000/= ikiwa ni pungufu ya  shilingi 5,679,805,000/=  Kambi Rasmi ya Upinzani inataka majibu kwa kuwa wakati wafanya kazi wakitarajia kupandishwa madaraja na ongezeko la mishahara kutokana na kupanda kwa gharama za maisha pamoja na mfumko wa bei, bajeti ya mishahara kwa Wizara na taasisi zilizochini yake inapunguzwa.
Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo iwapo punguzo hilo ni kutokana na kubana matumizi au ni udhaifu katika maandalizi ya bajeti na nini athari zake kwenye ufanisi wa wizara na taasisi zake? Au wizara imebaini mianya ya ufisadi ambayo ilikuwepo katika bajeti zilizopita kuhusiana na fungu la mishahara?
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM inaonekana kuziba masikio katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima pamoja na Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, wananchi na wadau wa maendeleo kulipigia kelele swala hili. Jambo hili limejirudia kwa upande wa matumizi ya kawaida, ambapo serikali iliomba kiasi cha shilingi 92,786,521,000/= katika Bajeti ya mwaka 2012/2013 na mwaka huu wa fedha 2013/2014 serikali inaomba kiasi cha shilingi 95,608,744,000/= ikiwa ni ongezeko la shilingi 2,822,223,000/=.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa wabunge na Bunge kuungana pamoja kabla ya kupitisha matumizi haya makubwa na kuitaka Wizara ya Nishati na madini kubana matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili tupate fedha za kuwekeza kwenye nishati .
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuonyesha udhaifu na uwezo mdogo wa wizara katika kusimamia sheria za nchi, kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya Juni 2012 nchi imepoteza kiasi cha dola za kimarekani 12,634,354.61 sawa na shilingi bilioni 19.71. Hizi ni fedha ambazo hazikukusanywa kutoka kwa makampuni ya madini kwa kufuata sheria mpya ya madini ya mwaka 2010, kifungu cha 87(1) kuwa mrahaba wa 4% utozwe kabla ya makato  na badala yake mrahaba ukawa ni 3% na kutozwa baada ya makato kama sheria ya zamani ilivyokuwa.

Mheshimiwa Spika,katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013, iliathiriwa kwa kiwango kikubwa na mvutano baina ya Watendaji Waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake kwa upande mmoja na baadhi ya wabunge kwa upande mwingine katika mvutano ambao uliambatana na kutuhumiana hadharani kupitia vyombo vya habari juu ya tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. Baadhi yakiwa yamejidhihirisha kufuatia chunguzi na ripoti zilizofanyika na kubaini kasoro kubwa za kiutendaji hususan kupitia ukaguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Shirika la Umeme (TANESCO). 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, inataka Serikali ieleze hatua iliyofikiwa katika uchunguzi juu ya ununuzi wa mafuta mazito kama ambavyo tulipendekeza ufanyike. Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) nayo iliwahi kueleza kwenye vyombo vya habari kuwa imeanza uchunguzi ambao ulipaswa kukamilika mwaka 2012; hivyo tunataka taarifa ya uchunguzi iwekwe hadharani na Serikali ieleze hatua ilizochukua dhidi ya madai ya ufisadi na matumizi ya madaraka kupitia mianya ya dharura ya umeme.
2.0  Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge
2.1 Maazimio kuhusu uhalali wa uchangishaji (‘Sakata la Jairo’).
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2011/2012 Bunge lako lilishuhudia mambo kadhaa yaliyokiuka miiko ya uongozi, ambalo yalilazimu bunge kuunda kamati teule kuchunguza uhalali wa uchangishaji uliofanyika katika Wizara ya Nishati na Madini (‘Sakata la Jairo’) na baadhi ya mapendekezo yake ambayo yalipitishwa kuwa maazimio yalikuwa;

(1). Kamati Teule inapendekeza kwamba Serikali ichukue hatua za kinidhamu kwa Ndugu David Kitundu Jairo kwa matumizi mabaya ya madaraka, kukusanya na kutumia fedha za Serikali kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za Fedha za Umma na kuruhusu matumizi mabaya ya fedha za Umma.
(2)Vile vile Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu, kwa mujibu wa Sheria, watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa kwenye Taarifa hii kushiriki kwa namna mbalimbali katika mchakato wa uchangishaji na matumizi ya fedha hizi za umma. Aidha, kwa kuwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Baraza la Mawaziri Waziri ndiye Msimamizi Mkuu wa Wizara, hivyo suala la uchangishaji halikupaswa kufanyika bila yeye kufahamu,
(3). Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. William Ngeleja, (Mb.)
(4).,……….. Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa upotoshaji huo.. ,
(5). …… Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inahoji ni kwanini hadi sasa Bunge hili limeshindwa kuhakikisha kwamba maazimio haya yametekelezwa na Serikali? Hakika huu ni uzembe wa wazi wa Bunge  kushindwa kutimiza majukumu yake ya kuisimamia serikali kwa mujibu wa katiba .

Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hatua za utekelezaji wa maazimio hayo ya Bunge, kwani baadhi ya wahusika bado wapo ma-ofisini wakiendelea na kazi na wengine wakiendelea kuteuliwa kushika nafasi zingine katika uongozi na utumishi wa umma kama vile hakuna liliowahi kutokea.

2.2 MAAZIMIO YA RICHMOND
Mheshimiwa Spika: Itakumbukwa kwamba taarifa mbili za serikali kuhusu utekelezwaji wa maazimio haya ziliwasilishwa Bungeni na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, tarehe 28 Agosti, 2008 na tarehe 11 Februari, 2009 . Taarifa moja ilikabidhiwa na kujadiliwa na Kamati, ambazo zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa Maazimio 10 kati ya 23 yaliyotolewa na Bunge, yalifanyiwa kazi hadi mwezi Februari, 2009 na Maazimio 13 bado yalikuwa hayajakamilika.
Mheshimiwa Spika; Bunge liliazimia kwamba taarifa za utekelezaji wa maazimio yaliyobaki ziwasilishwe kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo hata hivyo katika mwaka 2011, 2012 na mpaka mabadiliko ya muundo wa Kamati yalipofanyika kamati hiyo haikuwasilisha taarifa yoyote bungeni ya kueleza kukamilika kwa utekelezaji wa maazimio husika hali ambayo inahitaji bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 63 (2) na (3).
Mheshimiwa Spika, katika hali inayozua maswali kuhusu umakini wa Bunge katika kusimamia maazimio yake mwaka 2011, Mbunge wa Monduli Mheshimiwa Edward Lowassa; aliyekuwa Waziri Mkuu na kujiuzulu kufuatia kashfa hiyo ya Richmond alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliyopewa dhamana na Bunge kufuatilia utekelezaji wa maazimio kuhusu mkataba kati ya TANESCO na Richmond. Katika hali hiyo, haishangazi kwamba kwa miaka miwili toka wakati huo, mpaka mabadiliko ya Kamati za Bunge yalipofanyika; Kamati hiyo katika Taarifa zake zote bungeni haijawahi kuisimamia Serikali kuhakikisha maazimio husika ya Bunge yanatekelezwa. Huu ndio uwajibikaji, ndani ya Serikali na uongozi wa Bunge; vyote vikiongozwa na CCM.
Mheshimiwa Spika, sasa inajulikana wazi kuwa Mkataba wa TANESCO na Richmond ulirithishwa kinyemela kwenda kwa Dowans kama inavyoonekana katika nyaraka za mahakama ambapo Dowans na Richmond zilidaiana huko Marekani; na kuwa hilo lilifanyika bila kuitaarifu TANESCO kinyume na kifungu cha 15:12 cha Mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na hukumu ya Dowans ushahidi umepatikana na kuwa mashahidi mbalimbali walioitwa mbele ya Kamati Teule ya Bunge na wakiwa chini ya kiapo walitoa taarifa za uongo kuwa mkataba kati ya Richmond na Tanesco ulihamishwa kwenda Dowans Disemba 23, 2006 na hivyo wahusika hao mbalimbali – wakiwemo wamiliki wa Richmond – walidanganya au kuficha ukweli mbele ya Kamati Teule na hivyo kuonesha dharau dhidi ya Bunge.
Mheshimiwa Spika; Masuala haya ni muhimu yakajadiliwa sasa ili kupata undani wa wahusika wanaopaswa kubeba mzigo wa fidia kwa kampuni ya Dowans badala ya kubebesha mzigo huo TANESCO na umma wa watanzania. Kushindwa kuwashughulikia kwa ukamilifu mafisadi wa Richmond na kukwepa kutumia mianya ya sheria za kimataifa kukana mikataba iliyoingiwa kwenye mazingira ya ufisadi kwa mara nyingine tena kunaelekea kuligharimu taifa hivyo wakati umefika sasa wa Bunge kuingilia kati kwa niaba ya wananchi.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya Nishati na Madini na Serikali kwa ujumla kutoa majibu bungeni juu ya hatma ya maazimio 10 yaliyobaki: Nambari 3,5,7,8,9,10,11,13,14 na 18 ili bunge liweze kuishauri na kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio husika yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka.
Kambi Rasmi ya Upinzani, inataka Taarifa ya utekelezwaji wa Maazimio tajwa yaliyotolewa na Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC badala ya kuwasilishwa kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo kwa sasa haipo, sasa iwasilishwe kwenye Bunge zima ili yaweze kujadiliwa na hatima yake iweze kujulikana.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze kwanini mpaka sasa haijatekeleza maazimio hayo na  bunge liweke muda wa ukomo wa kutekeleza Maazimio yote ya Bunge yaliyokuwa yamesalia katika sakata hili la Richmond ili mara moja na daima sakata hili la Richmond limalizwe na kufungwa baada ya maazimio yote kutekelezwa kwa ukamilifu. Ikiwa maazimio ya mwaka 2008 utekelezaji wake haujakamilika mpaka mwaka 2013 kwa miaka mitano, nini kitalihakikishia taifa kwamba maazimio mengine mapya yaliyopitishwa 2011 na 2012 yatatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu?
Mheshimiwa Spika: Azimio Na. 3, ambalo liliagiza kwamba “Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC (uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na ile kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals, ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo Mikataba ya Madini ilivyopitiwa upya na Serikali”. Iwapo Azimio hili lingetekelezwa kwa ukamilifu wake, gharama za uzalishaji TANESCO na serikali kwa ujumla zinazotokana na matatizo katika mikataba zingepungua.
(1)       Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 5 Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC na sasa Dowans Holdings S.A umesheheni makosa mengi ya kisheria yanayoashiria udhaifu mkubwa wa kitaalamu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au ukosefu wa umakini ama ubinafsi katika kuiwakilisha Serikali. Kwa mfano, kushindwa kutambua ukosefu wa sifa za kikampuni za Richmond Development Company LLC; kushindwa kuishauri Serikali  kuifanyia kampuni hiyo ukaguzi wa awali (due deligence) au ukaguzi baada ya uteuzi (post qualification); kushindwa kutambua tofauti kati ya consortium agreement na proprietary information agreement; kushindwa kuona dosari kisheria za proprietary information agreement; kushindwa kuona tofauti kisheria kati ya Richmond Development Company LLC, RDEVCO,RDVECO na RDC, majina ambayo wamiliki wa Richmond Development Company LLC walikuwa wanayatumia kwa kubadilisha badilisha (interchangerbly) kwa makusudi; kushindwa kuwashauri Wajumbe wa GNT kwamba business card si mbadala wa hati mahsusi kisheria; kushindwa kuishauri Serikali kuhakikisha kuwa muhtasari wa majadiliano kati ya Kamati ya Serikali ya Majadiliano (GNT) na Richmond Development Company LLC ambao ulizingatia baadhi ya maslahi ya nchi, uwe sehemu ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC; kushindwa kuishauri Serikali kutumia fursa iliyokuwepo wazi ya kuvunja Mkataba baada ya Richmond Development Company LLC kushindwa kutekeleza sehemu yake ya Mkataba; kushindwa kuhudhuria idadi kubwa ya vikao muhimu vya majadiliano;n.k. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye katika majadiliano yake na Kamati Teule alionyesha kutokuelewa kabisa kilichokuwa kinatendeka na wasaidizi wake, na mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Wakili wa Serikali Donald Chidowu, ambaye ushiriki wake katika GNT haukuwa na tija yeyote, wawajibishwe na Mamlaka ya juu ya nchi kwa kuchangia kuiingiza nchi katika mkataba wa aibu.
(2)       Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 7 lilikuwa “ Kamati Teule inapendekeza kuwa Wajumbe wote wa GNT ambao ni maafisa waandamizi wa Serikali wawajibishwe mara moja kwa kushindwa kutumia elimu na ujuzi wao kulinda maslahi ya Taifa”.
Aidha,  Azimio namba 9 lilikuwa linataka mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi ya TAKUKURU.
Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 13 “ Kamati Teule inatoa wito kwa Kamati zote za Bunge zihakikishe kuwa zinapitia mikataba mikubwa na ya muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima. Pale ambapo upatikanaji wa mikataba hiyo unakwamishwa kwa urasimu usio wa lazima Kamati zitumie utaratibu uliotumiwa na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara ya kuunda Kamati Teule yenye ufunguo wa mikataba iliyofichika”.
Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 14 “Kamati Teule inapendekeza kwamba Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha (Mb) na Katibu Mkuu Ndugu Arthur Mwakapugi wachukuliwe hatua kali za kinidhamu kwa kuliingiza Taifa kwa makusudi kwenye mkataba na kampuni ya mfukoni ambao umesababisha hasara kubwa kwa nchi. Aidha Kamishna wa Nishati Ndugu Bashir Mrindoko naye achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu mpya wa Wizara kuhusu udhaifu wa Richmond Development Company LLC ambao ulijulikana dhahiri na Wizara toka mwaka 2004 kwenye mkataba wa Bomba la Mafuta. Ndugu Mrindoko ndiye aliyeiandikia barua kampuni hiyo kusitisha mkataba wake na Serikali mwezi mmoja tu kabla ya mchakato wa zabuni ya umeme wa dharura haujaanza”.
2.3 Kamati ya wataalamu wa Ofisi ya Spika.
Mheshimiwa Spika, mbali na maazimio hayo pia kuna uchambuzi uliofanywa na kamati ya wataalam wa Ofisi ya Spika, kuhusiana na makampuni yanayouza umeme kwa TANESCO ambayo mikataba yake haipishani na ule wa RICHMOND, taarifa hiyo iliwasilishwa Bungeni wakati Mhe Harrison Mwakyembe akiwasilisha Taarifa yake ya Kamati Teule ya RICHMOND ili Waziri atoe ufafanuzi ni kwa kiwango gani mapendekezo yake Serikali imeyafanyia kazi;

(a)  Uhalali kisheria wa Kampuni ya Aggreko (legal status)
Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba, Kampuni ya Aggreko International Projects Limited ni Kampuni iliyosajiliwa chini ya Sheria za nchi ya Scotland. Uchambuzi na utafiti wetu haukuweza kuthibitisha kuwa Kampuni hiyo kweli imesajiliwa kisheria huko Scotland ili kubaini kama kulikuwa na udanganyifu kama ule uliofanywa na Kampuni ya RICHMOND, yaani kutoa taarifa za uongo kuhusu uhalali kisheria wa Kampuni.
(b)  Malipo ya Kodi
Kama ilivyo katika Mkataba wa Kampuni ya Richmond, Kifungu cha 3.4 cha Mkataba wa AGGREKO kinatamka kwamba, kodi zote na malipo mengine yanayotokana na uingizaji nchini na utoaji nchi za nje ya nchi wa Mitambo ya uzalishaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na vipuri na vifaa vingine vinavyohusika na uendeshaji wa Mtambo huo italipwa na TANESCO. Aidha, Kifungu hicho kimeweka pia sharti kwamba, pale ambapo bodi au malipo yoyote yatadaiwa na Mamlaka yoyote ya kodi kutoka kwa AGGREKO, Kampuni hiyo italijulisha Shirika la TANESCO ambalo litalipa kodi au malipo hayo kwa mamlaka husika au litairejeshea AGGREKO fedha ambazo itakuwa imelipa kwa Mamlaka hiyo katika kipindi cha siku 14.
(c)  Malipo
Kwa mujibu wa Vifungu vya 4.2 na 4.3 vya Mkataba, Shirika la TANESCO linawajibu wa kuilipa Kampuni ya Aggreko malipo yafuatayo:-
                                          i.    ‘Capacity Charge’ – Dola za Marekani 35.928 kwa Kw kwa mwezi [Tazama Kiambatanisho C cha Mkataba].
                                         ii.    Malipo ya Umeme (energy purchase price) – Dola 4.99 kwa Kwh [Tazama tafsiri ya interim energy purchase price katika uk. wa 3 wa Mkataba]
(d)  Fidia kwa Ucheleweshaji wa Kuzalisha Umeme.
·         Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.4.2 cha Mkataba, Aggreko inawajibika kulipa kwa TANESCO Dola ya Marekani 0.5 kwa Kw kwa siku kwa wiki 4 za kwanza za ucheleweshaji, na baada ya hapo’ kama ucheleweshaji wa uzalishaji umeme utaendelea, anawajibika kulipa Dola ya Kimarekani 1 kwa Kw kwa siku.
·         Hata hivyo, malipo hayo ya fidia (liquidated damages) yamewekewa ukomo chini ya Kifungu cha 10.3 (a) na (c) ambapo hayatazidi Dola za Kimarekani 350,000 na kwamba, malipo hayo kwa ujumla wake chini ya Mkataba huo hayatazidi Dola za Kimarekani 500,000.
·         Aidha, Kifungu cha 8.8 cha Mkataba wa Richmond kinachoiruhusu TANESCO kuendesha Mitambo ya Richmond pale ambapo Kampuni hiyoi itaitelekeza (abandon) Mitambo hiyo, kimeondolewa kwenye mkataba wa AGGREKO.
                                    (c) Nyongeza ya Mkataba
·         Mkataba huo una Nyongeza (Addendum) au (Amendment No.2) ya Januari, 2007 ambayo imebadilisha formula ya kupata ‘capacity payments’, ambapo muda uliopotezwa na TANESCO kutokana na matatizo ya upatikanaji wa gesi na pia kutokana na TANESCO kutoomba kupewa umeme kutoka AGGREKO umepigiwa hesabu kwa ajili ya AGGREKO kulipwa na TANESCO.
·         Nyongeza hiyo pia imebadilisha bei ya Umeme unaotolewa na AGGREKO ambapo, bei mpya sasa ni Dola za Kimarekani 0.0499 x 1000 kwa kila Mwh.

4.1.1              Mkataba Kati ya TANESCO na ALSTOM POWER RENTALS ENERGY LLC
(b)                  Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkatab
Mkataba huo ulisainiwa tarehe 27 Oktoba, 2006
(c)             Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazji wa   umeme wa dharura kutoka kwenye Kinu cha dizeli cha kuzalisha umeme (emergency supply of power from a diesel – based generating plant in Mwanza with a capacity of 40 Mw).                          
(c)             Muundo (form) wa Mkataba
Kama ilivyo kwa Mikataba iliyotangulia, Mkataba huu upo katika muundo wa ‘Standard Power Off-take Agreement’
(d)       Muda wa Mkataba
Muda wa Mkataba huo ni miezi kumi na mbili (12) kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1 cha Mkataba.
(e)       Uhalali Kisheria wa Kampuni ya Alstom Power Rentals Energy LLC
Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba hususan kwenye Kifungu cha 5.1 (a) na (b), Kampuni ya Alstom Power Rentals Energy LLC imesajiliwa chini ya Sheria za Florida, Marekani.
(f)        Malipo ya Kodi
Kifungu cha 3.4 cha Mkataba kinatamka kwamba, TANESCO itatumia juhudi za kibiashara kuhakikisha kwamba Serikali ya Tanzania inatoa msamaha kwa Alstom wa kutolipa ‘import duties’ na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kuhusiana na Mtambo au utekelezaji wa majukumu ya Alstom, chini ya Mkataba huo.
Aidha, Kifungu hicho kinatamka pia kuwa, pale ambapo kodi hizo zitadaiwa, Alstom itaiomba TANESCO ilipe kodi hiyo au kama italipwa na Alstom, TANESCO itarejeshea Alstom malipo hayo ya kodi.
(g)       Kutii Sheria za Mazingira
Kifungu cha 3.9 cha Mkataba huu kinamtaka Alstom kuhakikisha kwamba, hatafanya kitendo chochote ambacho kitasababisha kuwepo kwa hali ya mazingira ambayo inakiuka Sheria za Tanzania.
(h)       Malipo ya Umeme
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.3 cha Mkataba, TANESCO inawajibika kulipa malipo ya ‘capacity charge’ kwa kiasi cha Dola za Marekani 43.8 kwa Kw kwa mwezi.
(i)        Malipo ya Fidia kwa Ucheleweshaji wa Kuzalisha Umeme
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.4 na cha 10.1(a) cha Mkataba, Alstom anawajibika kulipa kwa TANESCO kiasi cha Dola za Kimarekani 400,000 kama kiwango cha mwisho cha malipo ya fidia (damages) kwa ucheleweshaji wa kuzalisha umeme na kiasi cha Dola za Kimarekani 600,000 kama kiwango cha mwisho cha malipo yote ya fidia (damages).
(j)        Dhamana ya Malipo kwa Alstom
Kifungu cha 4.6 cha Mkataba kinaitaka TANESCO kufungua ‘Letter of Credit’ ya kiasi cha Dola za Kimarekani 3,500,000 kwa kipindi chote cha Mkataba, kama dhamana ya malipo kwa Alstom.
Aidha, Kifungu cha 4.7 cha Mkataba kinaitaka TANESCO kufungua ‘Standby Letter of Credit’ ya kiasi cha Dola za Kimarekani 14,000,000 kwa ajili ya malipo ya miezi minane (8) ya Mkataba.
                        (k)       Mafuta (fuel)
Kifungu cha 6 cha Mkataba kinatamka kuwa, TANESCO itawajibika kulipia mafuta ya dizeli yatakayotumika kuendeshea Mtambo wa Alstom wa kuzalisha Umeme.
(l)        Kutolipa Malip ‘Capacity Charges’ Wakati wa Majanga
Kwa mujibu wa Kifungu cha 13.1 cha Mkataba, malipo ya ‘Capacity Charges’ yanayotakiwa kulipwa na TANESCO yatasitishwa kwa siku 30 iwapo litatokea janga lolote ambalo litasababisha Alstom kutelekeza majukumu yake ya kuzalisha na kusambaza umeme.
(m)      Kuhamisha (assign) Majukumu
Kwa mujibu wa Kifungu cha 15.12 cha Mkataba, Alstom au TANESCO inaweza kuhamisha  (assign) sehemu au majukumu yote yaliyomo kwenye Mkataba kwa Kampuni Tanzu, baada ya kutoa taarifa kwa mhusika wa pili uuzaji uhamishaji huo wa majukumu. Hata hivyo, mhusika yeyote anayehamisha majukumu atabaki na wajibu wa kuhakikisha kuwa majukumu hayo yanatekelezwa ipasavyo na yasipotekelezwa, atawajibika.
4.1.2              Mkataba Kati ya TANESCO na WARTSILA FINLAND OY
(a) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
      Mkataba huo ulisainiwa tarehe 20 Juni, 2006.
(b)             Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazaji wa umeme wa dharura kutoka kwenye Kinu cha gesi cha kuzalisha umeme (Energy Purchase Contract for Procurement of Emergency 100 Mw Gas-based Power Generation Plant at Ubungo, Dar es Salaam.)
(c)       Muundo (form) wa Mkataba
Tofauti na Mikataba yote iliyotangulia kufanyiwa uchambuzi hapo juu, Mkataba huo upo katika muundo uliowekwa na Kanuni ya Ununuzi wa Umma [The Public Procurement (Goods, Works, Non-Consultant Services and Disposal of Public Assets by Tender) Rgulations, G.N. No.97 of 15/4/2005] zilizotungwa chini ya Kifungu cha 88 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.21 ya Mwaka 2004 [The Public Procurement Act, 2004 (No.21 of 2004)].
Kanuni ya 115(1) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2005, Taarifa ya Serikali Namba 97 ya Mwaka 2005 inaelekeza kama ifuatavyo:-
“Kwa kadri inavyowezekana, kila jitihada itafanywa kutumia miundo ya rasimu za mikataba iliyotayarishwa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma.” Tafsiri na msisitizo ni wetu.
Ili kuondoa tatizo la tafsiri, Kanuni hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kingereza inasomeka kama ifuatavyo:-
“Every effort shall be made to utilize as for as possible, the sample Standard Contract documents prepared by the Authority.”
                        (d) Muda wa Mkataba
Muda wa Mkataba (contract period) ni miezi 21, kwa mujibu wa Kifungu cha G.C.C 1.1 (aa) na GCC 8.1[Tazama Uk.1 na 2 wa ‘Special Conditions of Contract]
(e)       Uhalali kisheria wa Kampuni ya WARTSILA FINLAND OY
            Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba, Kampuni hiyo imesajiliwa chini ya Sheria za Finland. Hatukuweza kufanya utafiti wa kina kuthibitisha kuwa maelezo hayo ni sahihi, isipokuwa tumefanya hivyo kwa Kampuni moja tu ya RICHMOND.
(f)        Malipo (Contract Price)
            Kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1 cha Mkataba, TANESCO anawajibika kulipa kiasi cha Euro 57,550,000/= kama malipo ya huduma ya kupatiwa umeme wa Megawatt 100 kutoka kwenye Kinu cha kuzalisha umeme cha WARTSILA.
(g)       Utaratibu wa malipo
            Kwa mujibu wa Kifungu cha 2.2 cha Mkataba, TANESCO anawajibika kufanya malipo ya huduma ya umeme kwa kufungua ‘Letter of Credit’ ya kiasi cha Euro 51,795,000/= kwa jina la WARTSILA.
(h)       Dhamana ya Utekelezaji (Performance Bond)
            Chini ya Kifungu cha 3.1 cha Mkataba, WARTSILA anawajibika kutoa dhamana ya utekelezaji wa kazi (Performance security/bond) ya kiasi cha 10%ya malipo anayostahili kulipwa, kabla ya kuanza kazi.
(i)        Malipo ya Kodi
§  Kwa mujibu wa Kifungu cha 14.4 (GCC), uk. wa 3 wa Special Conditions of Contract, kodi zote ambazo WARTSILA anapaswa kulipa zitasamehewa (be exempted) au zitalipwa na TANESCO.
§  Aidha, chini ya Kifungu hicho pia, kodi na malipo yote yanyohusu mishahara ya watumishi wa kigeni wa Kampuni ya WARTSILA zinapaswa kulipwa na TANESCO.
(j)        Taratibu za Usuluhishi
            Chini ya Kifungu cha 6.2.3 taratibu zitakazotumika wakati wa Usuluhishi ni za Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi ya London, chini ya Sheria za Uingereza.
            Tunadhani kifungu hiki si kwa manufaa na maslahi ya TANESCO.
(k)       Malipo ya bonus
            Chini ya Kifungu cha 26.3 cha Mkataba (Taz. Uk. wa 5 wa SCC malipo ya bonus hayaruhusiwi.
(l)        Kipindi cha Matengenezo (Defect liability period)
§  Kwa mujibu wa Kifungu cha 27.2 cha Mkataba (Uk. wa 5 wa SCC), kipindi cha matengenezo ni miaka miwili (2) baada ya kukamilika kwa ufungaji wa Mtambo.
§  Tunadhani kwamba, Kifungu hiki ni kwa manufaa na maslahi ya TANESCO.

4.1.3              Mkataba Kati ya TANESCO na SONGAS LIMITED
(a) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
      Mkataba huo umesainiwa tarehe 11 Oktoba, 2001.
(b) Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazji wa nishati ya umeme kutokana na gesi ya Songosongo (Power purchase relating to the Songosongo gas-to-electricity)
                        (c)       Muundo (form) wa Mkataba
Mkataba huo upo katika muundo wa ‘Standard Power Purchase Agreement’.
                        (d)       Muda wa Mkataba
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.1 cha Mkataba, muda wa Mkataba ni miaka ishirini (20), na unaweza kuongezwa kwa makubaliano kati ya TANESCO na SONGAS.
(e)       Uhalali Kisheria wa Kampuni ya SONGAS LIMITED
            Kampuni ya SONGAS LIMITED ni Kampuni ya kitanzania iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni, Sura 212, Toleo la 2002 [The Companies Ordience (Cap.212) of the Laws of Tanzania, R.E, 2002] (Tazama Kifungu cha 5.1 cha Mkataba)
(f)        Malipo ya Kodi
            Kwa mujibu wa Kifungu cha 15.1 cha Mkataba, SONGAS LIMITED inatakiwa kulipa kodi kulingana na masharti yaliyomo kwenye Mkataba wa Utekelezaji (Implementation Agreement) ulioingiwa kati yake na Serikali ya Tanzania.
(g)       Malipo ya Umeme
            Kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1(a)(i) na (ii) cha Mkataba, kikisomwa pamoja na Vifungu 9.2 na 9.5, TANESCO anawajibika kulipa malipo yafuatayo kwa SONGAS:- ‘Capacity Charge’ – Dola za Kimarekani 6,638,600 ‘Energy Charge’ – kwa kiasi kitakachotokana na ‘formula’ iliyowekwa na Kifungu cha 5 cha Nyongeza F ya Mkataba.
(h)       Usuluhishi
§  Kifungu cha 3.10 cha Mkataba kinatamka kwamba, TANESCO na SONGAS wamekubaliana kutotekeleza masharti na matakwa ya Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Umeme, Sura 131, Toleo la 2002 [Electricity Act, (Cap.131) of the Laws of Tanzania, R.E 2002], na badala yake kusuluhishwa migogoro baina yao kwa kutumia utaratibu uliowekwa na Mkataba.
§  Kwa kuwa kinahusu makubaliano ambayo yanavunja sheria, Kifungu hicho hakina uhalali wowote wa kisheria.
(i)        Kuvunjwa kwa TANESCO
            Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.3(a) cha Mkataba, kikisomwa pamoja na Kifungu cha 17.12, TANESCO haiwezi kuvunjwa kwa Sheria au kuhamisha majukumu yake yaliyoainishwa kwenye Mkataba, isipokuwa tu kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na Kifungu cha 8.7 cha Mkataba wa Utekelezaji (Implementation Agreement).
(j)        Uuzaji Umeme wa SONGAS
            Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.1(b), iwapo TANESCO watakataa kuongeza muda wa Mkataba baada ya muda wa awali wa miaka 20 kumalizika, SONGAS wataruhusiwa kuingia Mkataba na mtu yoyote anayetaka kuuziwa umeme.
(k)       Haki ya Kununua Mradi
            Chini ya Kifungu cha 4.8 cha Mkataba, TANESCO na T.P.D.C wamepewa haki ya kununua Mradi huo wa SONGAS iwapo SONGAS atakiuka masharti ya Mkataba.

Mapendekezo Mengine
Pamoja na mapendekezo ya hapo juu, tunashauri na kupendekeza pia kuwa, kuna ulazima kwa Mikataba mikubwa ambayo inahusu maslahi na manufaa ya Taifa kama vile Mkataba wa IPTL kuwasilishwa Bungeni, kwa utaratibu wa dhana ya demokrasia ya uwajibikaji (accountability in a Parliamentary democracy) kwa ajili ya ushauri wa Bunge.

Tunapendekeza na kushauri vilevile kuwa, pale ambapo kuna ulazima wa kutumia rasimu ya Mkataba ambayo ni tofauti na ile iliyotayarishwa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma, mabadiliko muhimu yafanywe katika rasimu hiyo ili masharti yaliyomo ambayo hayafai yaondolewe na yale ambayo ni kwa manufaa ya Taifa letu yawekwe. Wanasheria watumike katika kuitekeleza jambo hili.
Tunashauri na kupendekeza vilevile kuwa, Mikataba yote ya umma ifanywe kwa kuzingatia misingi ya kibiashara na si vinginevyo, na kwamba, Taasisi na Mashirika yote ya Umma lazima yatekeleze na kufuata utaratibu, masharti na matakwa yaliyowekwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma, Namba 21 ya mwaka 2004, pamoja na Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria hiyo.

Aidha, tunapendekeza na kushauri kwamba utoaji Mikataba utumike kama njia au chombo cha kutekeleza Sera za Taifa na malengo ya jamii, badala ya kutumika kama chombo cha kuchota rasilimali za Taifa na kuongeza umaskini wa wananchi wa nchi hii.

Aidha, tunashuri pia kwamba, pale inapotokea ukiukwaji wa masharti ya Mkataba unaofanywa na Mwekezaji basi hatua mwafaka zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na kudai malipo ya fidia iwapo kuna kifungu cha Mkataba kinachotoa haki hiyo.
Kwa kuzingatia kuwa Mikataba mibovu kati ya TANESCO na Makampuni mbalimbali ambapo Makampuni hayo yanalipiwa kodi yote na TANESCO imekuwa ni chanzo cha bei kubwa za umeme katika nchi yetu, na kwa kuzingatia kuwa Mikataba hiyo inasababisha Sera muhimu za Taifa, kama vile, Sera ya Kupiga vita Umaskini, Sera ya Huduma Bora kwa Jamii, Sera ya Taifa ya Nishati inayolenga kusambaza nishati ya bei nafuu vijijini n.k. kutotekelezeka, tunashauri kuwa Mikataba hiyo ipitiwe upya ili irekebishwe, kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.
Mwisho, kwa kuzingatia ukweli kwamba, Mikataba hiyo mibovu, kwa kiasi kikubwa inadidimiza uchumi wa nchi yetu, tunapendekeza Serikali ichukuwe hatua muafaka zinazofaa ili  kuondoa hali hiyo ambayo inalipeleka Taifa letu ‘shimoni’[1].
Mheshimiwa Spika, hali hiyo ya kuachwa kutekelezwa kwa maazimio ya Bunge la Tisa ya Mwaka 2008, hayahusu tu Richmond bali pia juu ya Kashfa ya Mgodi wa Kiwira aliyomgusa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na baadhi ya mawaziri kama ambavyo hotuba hii itaeleza kwa ufupi wakati wa kutoa maoni kuhusu sekta ya madini. Serikali wakati inaendelea kuchukua hatua kuhusu kashfa hii ni muhimu ikarejea maelezo ya ziada na vielelezo zaidi vilivyotolewa wakati wa kusomwa kwa orodha ya mafisadi (List of Shame) Septemba 15 mwaka 2007 katika uwanja wa Mwembe Yanga.

Mheshimiwa Spika, Aidha, matokeo ya Bunge kuzembea kuisimamia Serikali kukamilisha utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya mwaka 2008 yamesababisha udhaifu wa Serikali katika kutekeleza maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu “Sakata la Jairo” kama nilivyoeleza katika Hotuba hii lakini pia kuhusu uchunguzi juu ya Sekta ndogo ya Gesi Asili na Mpango wa Dharura wa Umeme kama nitakavyoeleza wakati nawasilisha maoni kuhusu sekta ya gesi ya nishati.

C.  NISHATI          

3.0  SEKTA  NDOGO YA GESI ASILIA TANZANIA
Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya gesi asilia ni sekta ambayo kutokana na ukubwa wa hazina iliyokwishapatikana na inayokisiwa kuwepo itakuwa ni kubwa sana katika shughuli za uchumi kwa nchi yetu. Lakini Sekta ya gesi asilia imegubikwa na utata mwingi ambao kwa njia moja au nyingine unatokana na kutokuwepo kwa sera na sheria mahususi ya gesi. Na hivyo kusababisha utendaji wake kutokuwa na mdhibiti (regulator) wa kuhakikisha maslahi ya taifa, mwekezaji na mlaji yanaangaliwa.
Mheshimiwa Spika, Utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi( Upstream); shughuli zote za utafutaji wa mafuta na gesi nchini unatawaliwa na Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji Mafuta ya mwaka 1980 (The Exploration Act,1980). Shughuli ya usafirishaji na uuzaji (down stream) hii hutawaliwa na sheria ya EWURA sura 414 kwa kuwa kwa sasa sheria ya gesi nchini haipo. Hivyo basi, makubaliano katika mkataba baina ya wadau hutakiwa kuwasilishwa EWURA kwa mapitio tu, na baada ya kujiridhisha EWURA hupanga bei za gesi.

Mheshimiwa Spika, mkataba wa ubia ndiyo mwongozo mkuu wa mahusiano yote yanayohusu uzalishaji na ugawanaji wa mapato ya gesi baina ya TPDC na mbia yeyote. Lakini kwa makusudi wabia na TPDC wamekuwa hawafuati matakwa yaliyomo kwenye PSA na mfano mzuri ni Pan African Energy[2].
Mheshimiwa Spika, utakumbuka moja ya mapendekezo ya kamati ndogo iliyoundwa na Bunge lako tukufu toka kwenye iliyokuwa kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ilipendekeza na Bunge kukubali, kuwa nina nukuuu ‘’ipo haja ya kudurusu Sera ya Nishati, kuandaa Muswada wa gesi asili wenye kutoa majibu ya maswali magumu ya Watanzania wa leo na wa miaka 50 ijayo
Majukumu kati ya asasi moja na asasi nyingine yaainishwe bayana na kutenganishwa kwa lengo la kuleta ufanisi na kuongeza tija. Aidha, mipango mkakati na kabambe iandaliwe ili kuibua miradi ya miundombinu na mahitaji ya rasilimali. Taifa likichelewa kuweka nyenzo hizi muhimu, likaruhusu majadiliano na mikataba kuchukuwa nafasi, kipindi si kirefu yatashuhudia manun’guniko kuwa nchi imeuzwa na mivutano kati ya wananchi na wawekezaji na ya wananchi na Serikali yao itajitokeza kwa nguvu sana jambo ambalo ni vyema likaepukwa mapema[3]’’
Mheshimiwa Spika, mapendekezo haja yalitolewa Bungeni Novemba 17, 2011. Sasa ni mwaka mzima na miezi sita, hadi  tunashuhudia maandamano na malalamiko ya wazi toka maeneo ambapo gesi asili imegunduliwa.

Mheshimiwa Spika, Licha ya ukweli kwamba gesi asili ilianza kutafutwa toka mwaka 1952 na iligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini mwaka 1974 na baadae mwaka 1982, wakati wote huo hakuwahi kuwa na sera mahususi ya gesi mpaka mwishoni mwa mwaka 2012 zaidi ya miaka 30 baadae ndipo serikali imeanzisha mchakato wa kutunga sera ya Taifa ya gesi asili.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhihirisha udhaifu mkubwa wa kisera kwa kuzingatia kuwa mikataba kadhaa ya uchimbaji na utafutaji wa gesi imeshatiwa saini kati ya serikali na wawekezaji bila kuwa na sera wala sheria inayotoa mwongozo juu ya namna Taifa linavyopaswa kuthibiti rasilimali hii adhimu. Uwepo wa sera ya gesi asilia ungetoa mwelekeo juu ya namna gani serikali ingeshirikiana na wakazi wa maeneo yaliyogunduliwa gesi, pamoja na wadau wengine katika kutafuta,kugundua na kuvuna, kusafirisha, kununua na kutumia gesi asilia.

Mheshimiwa Spika, Serikali bila uwepo wa sera na sheria hiyo, tayari imefunga mkataba na kampuni ya Statoil, Ophir, British Gas, Artumas, Shell, Texaco, Agip, PetroBras na kadhalika. Ni wazi kwamba mikataba husika imeingiwa bila muongozo wowote wa kisera wala kisheria mahususi. Aidha, licha ya makosa hayo na wakati mchakato wa sera uko karibu kukamilika Serikali imefunga mkataba mwingine kwa Kampuni nyingine kufanya utafutaji  kwenye Ziwa Tanganyika. Jambo hili linazidisha wasiwasi kama kweli Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha sekta hii ya gesi inanufaisha Taifa na watu wake.
Kitendo cha Serikali kuendelea kuingia mikataba na makampuni ya kutafuta gesi asilia bila ya kukamilisha kwanza sera na sheria ni sawa na kuweka mkokoteni mbele ya punda.
Mheshimiwa Spika; Waziri Mkuu akiwa ndiye msimamizi na mdhibiti wa shughuli za kila siku za Serikali ndani na nje ya Bunge, anapaswa kutoa maelezo kuhusu hali inayoendelea hivi sasa katika sekta ndogo (sub sector) muhimu kwa nchi yetu ya gesi asili kuhusu mazungumzo yanayoendelea na makampuni mbalimbali ya kimataifa na mikataba inayozidi kusainiwa huku kukiwa na ombwe la kisera na udhaifu wa kiuongozi katika sekta hizo nyeti hali ambayo itakuwa na athari za muda mrefu sana kwa taifa.
Mheshimiwa Spika, Ucheleweshwaji wa sera na sheria katika sekta ya gesi asilia unachangiwa na wizara yenyewe kwa watendaji wake kuwa na udhaifu katika kuweka mifumo ya kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu na yenye manufaa kwa nchi. Hili linathibitishwa na ukweli kwamba TPDC imeshindwa kusimamia kwa ukamilifu sekta hii ya gesi asilia kwani  hata mikataba iliyopo inayotaka kampuni inayofanya utafiti baada ya muda Fulani kuchimba kisima kipya; lakini hadi sasa kwa mfano tangu Kampuni ya Songas kuchukua visima vilivyochimbwa na TPDC haijawahi kuchimba kisima kipya.
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine ni kampuni ya  Pan African Energy Tanzania (PAT) kukosa sifa za uaminifu ambapo Kamati ilishauri Mkataba wa Pan African Energy Tanzania (PAT) usitishwe. Aidha, utekelezaji wa kuvunja mkataba huu ulipaswa kwenda sambamba na kuhakikisha kuwa taratibu za kisheria na za kimkataba zinazingatiwa, uwepo wa usalama wa visima na mitambo na uwepo wa uhakika wa huduma ya upatikanaji wa gesi nchini. Hili lilikuwa ni pendekezo namba 4 la kamati iliyochunguza uendeshwaji wa sekta ndogo ya gesi asilia hapa nchini na baadae kuwa azimio la Bunge. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwanini mpaka sasa Serikali haijatekeleza azimio hilo? Aidha, ni lini Bunge litachukua hatua ili kuepusha uzembe kwa upande wa chombo hili muhimu?
Mheshimiwa Spika, kuhusu gesi asilia, tarehe 15 Julai, 2011 Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza kuwa, nchi yetu imejaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la umaskini wa wananchi na kwamba Taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na kushindana Kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele uzalendo,upeo, umakini na uadilifu katika sekta ya nishati kuepusha laana ya rasilimali.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012, yalionesha Serikali kutochukua hatua thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi asili.
 Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitaka hatua za haraka kuchukuliwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 ili kuepusha   rasilimali kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi lakini kwa sababu ya udhaifu wa serikali hii kutosikiliza ushauri kitendo hicho kilisababisha vurugu na uharibifu wa mali kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mheshimiwa Spika, ushahidi wa hili unapatikana katika ushauri ambao serikali ilipewa kwa nyakati mbili tofauti lakini ikashindwa kuzuia vurugu za Lindi na Mtwara. Tarehe 27 Julai 2012 nikiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya nishati na madini nilishauri “Mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012, yanaonekana bado serikali haichukui hatua thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi asili hivyo hatua za haraka zisipochukuliwa katika mwaka 2012/2013 na kuendelea rasilimali inaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi”. Lakini pamoja na angalizo hili serikali haikuchukua hatua yeyote na matokeo yake sote tunayafahamu.
Mheshimiwa Spika, wakati wa mchakato wa kutoa maoni juu ya rasimu ya gesi , pamoja na kwamba mchakato huo haukufanyika katika maeneo mengine muhimu kama Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM) ambacho kina kozi mbalimbali za masuala haya na ambako tungepata ushauri mzuri na wa kitaalamu kutokana na wadau hao kutokujua na hivyo kutokujitokeza .
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa wananchi waliojitokeza kutoa maoni ni pamoja na wananchi waliofunga safari kutoka Mtwara hadi Dar es salaam kuja kutoa maoni yao juu ya rasimu ya gesi. Miongoni mwa mapendekezo aliyotoa mwananchi huyo (jina linahifadhiwa) mbele ya  viongozi wa serikali alishauri serikali kujua matatizo yanayotokea katika sekta ya madini ili tuhusianishe na gesi asilia.
Mheshimiwa Spika, Pamoja mwananchi huyo kuwakilisha mikoa ambayo ndiko hasa nishati hiyo inakopatikana, mwananchi huyo alipendekeza kutengwa kwa asilimia kumi (10%) ya mapato yatokanayo na gesi kwa ajili ya kuboresha maeneo rasilimali hiyo inapopatikana. Akapendekeza kijengwe Chuo Kikuu Mtwara kitakachofundisha watanzania elimu ya gesi na pia vijengwe viwanda vitatu kwa faida ya wana mtwara.  Mapendekezo ambayo pia yamewahi kutolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA  kwa mwaka  2011 na 2012, katika hali kama hii ya kushindwa kutimiza wajibu na kusababisha migogoro, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ikiri kuwa imeshindwa kuiongoza sekta hii .

Mheshimiwa Spika, Kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini ilitoa mapendekezo ya kukamilishwa kwa sera na sheria ya gesi kwa haraka na umakini mkubwa. Kamati pia ilishauri serikali kuonyesha katika sera na sheria hiyo ya gesi asilia jinsi ambavyo mapato yanayotokana na gesi asilia yatakavyo simamiwa, mapendekezo hayo ya kamati yalizingatia wingi wa upatikanaji wa nishati hii kwa sasa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kushangaza serikali imeendesha mchakato mzima wa kutengeneza rasimu ya gesi asilia bila kuwa na ushiriki mkubwa wa wananchi kinyume na mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, hakukuwa na uhamasishaji wa kutosha kwa wananchi katika kutoa maoni juu ya rasimu ya kwanza ya gesi iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini na ndio maana mahudhurio katika sehemu ambako mijadala iliendeshwa yalikuwa madogo sana. Kwa mfano katika ukumbi uliopo Makumbusho ya Mwalimu Nyerere waliohudhuria siku ya kwanza hawakufika hata 25 na siku ya pili hawakuzidi watu 30. Pia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), wanafunzi na wadau wa gesi kutoka taasisi hiyo muhimu ya elimu ya juu hawakujitokeza kwa sababu ya uhamasishaji hafifu na hivyo kupelekea kuahirishwa kwa zoezi hilo katika suala la msingi linalohusu uchumi wa watanzania. Lakini pia suala hili kwa wakati huo lilitakiwa liwe ni mjadala wa kitaifa ndani ya vyuo vikuu vingi nchini na jamii kwa ujumla ikihusisha pia mikoa yote ambako kuna uvunaji au utafutaji wa gesi asilia ili kupanua dhana ya kuwashirikisha wananchi katika maswala yanayohusu rasilimali za Taifa kinyume na uhalisia wenyewe.

Mheshimiwa Spika, Kufuatia kasoro zilizoanza kubainishwa na wabunge na wadau mbalimbali katika toleo la tatu la rasimu ya gesi; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo ni kwanini haikuzingatia baadhi ya maoni muhimu ya wadau yaliyotolewa mara baada ya kutolewa kwa rasimu ya kwanza ya Sera hiyo. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inataka mchakato wa kupitia rasimu ya tatu ya sera hiyo upanue wigo wa ushirikishwaji wa wananchi katika mikoa yote ambayo utafutaji wa gesi asilia umeanza au unatarajiwa kuanza pamoja na mikoa yote itakayofikiwa na miradi ya uendelezaji wa gesi asilia.
Ikumbukwe kwamba udhaifu wa Serikali katika kuwezesha ushirikishwaji wa wananchi katika mipango na miradi ya maendeleo na matumizi mabaya ya muda mrefu ya rasilimali za nchi ni kati ya sababu zilizochangia migogoro katika maeneo ambayo uendelezaji wa miradi ya gesi asilia umeanza hususani katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuwashirikisha wananchi na kutoa taarifa za kutosha na kwa wakati juu ya suala hili la gesi asilia na rasilimali nyingine za taifa ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza kwa wananchi juu ya mchakato mzima wa uwekezaji kwenye  rasilimali za Taifa.
Mheshimiwa spika, kwa mujibu wa michango mbalimbali iliyotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini 2012/2013 waheshimiwa wabunge pia walitaka kujua kama taifa mipango ambayo serikali imeweka kufuatia kugundulika kwa kiasi kikubwa cha gesi, kama rasilimali watu kwa maana ya wataalamu waliobobea, idadi ya wataalamu tunaowaandaa kwenda sambamba na uhalisia wa uhitaji wa wataalamu wenyewe katika sekta ya gesi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kuitaka serikali kufanya maandalizi ya kutosha ya kuwekeza  katika suala la rasilimali watu ili kuondoa matatizo yanayoweza kujitokeza hivi karibuni  kutokana na uhaba wa wataalamu katika fani hiyo.
3.1 Ugawaji wa Vitalu vipya vya utafutaji wa gesi na mafuta.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2012/13, baada ya kupokea ushauri wa Kamati kuhusu kusitisha ugawaji wa vitalu vya utafutaji gesi, Serikali iliahidi kwa kusema kuwa “zoezi la kugawa vitalu vipya kwa ajili ya utafutaji wa mafuta  umesitishwa mpaka hapo sera ya Gesi Asilia na sheria ya Gesi Asilia nchini itakapokamilika na kuanza kutumika”
Mheshimiwa Spika, Jambo la kushangaza ni kwamba wakati sera ya Gesi Asilia ipo kwenye rasimu na ndio kwanza wabunge tumeletewa kutoa maoni, Serikali tayari imetangaza kwa mujibu wa vyombo vya habari na tamko la TPDC  tarehe 18.5.2013  kuanza mzunguko mwingine wa leseni za utafutaji Mafuta na Gesi kwenye Bahari kuu na Ziwa Tanganyika Kaskazini. Kutoa leseni kwenye kitalu ya utafutaji ni hatua ya kuelekea kutoa mkataba wa uvunaji.
Zabuni hii mpya ya leseni za vitalu vya utafutaji imetolewa wakati kuna maamuzi ya Bunge kuzuia ugawaji huu mpya mpaka sera ya Gesi Asilia na Sheria ya Gesi vikamilike. Haraka hii ya serikali kugawa vitalu bila sera wala Sheria inatoka wapi.
Mheshimiwa Spika, uharaka huu unaifanya Kambi Rasmi ya Upinzani iwe na mawazo kwamba Wizara iliidanganya Kamati ya Kudumu ya Bunge, je ilifanya hivyo kwa maslahi ya nani? Tunamtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge sababu za kuidanganya kamati inayofanyakazi kwa niaba ya Bunge.
Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikitoa ufafanuzi potofu kwamba tangazo la sasa halina athari kwa kuwa maamuzi ya utoaji wa leseni yatafanyika mwaka 2014 baada ya kuwa na sera na sheria. Hata hivyo, ufafanuzi huu wa Wizara hauzingatii ukweli kuwa, hata zabuni ya maombi ikiwemo vigezo, utaratibu na masuala mengine ilipaswa kutolewa kwa kuzingatia misingi mipya inayopaswa kuwekwa kupitia mchakato wa katiba mpya na maandalizi ya Sera na Sheria ya Gesi Asili.
Katika muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutengua tangazo hilo mpaka baada ya kukamilika kwa mchakato wa katiba mpya na maandalizi ya sera na sheria mpya sio tu kwenye sekta ndogo ya gesi asilia bali katika sekta nzima ya nishati ikiwemo juu ya masuala yanayohusu mafuta.
Vinginevyo, watanzania wataamini kwamba hatua hiyo imefuatia msukumo uliotokea baada ya ziara ya Rais wa China nchini Tanzania; hasa kwa kuzingatia namna ambavyo, pamoja  na vitalu vilivyotangazwa kwenye zabuni ili kutolewa kwa ushindani, vipo vitalu ambavyo vimebakishwa mikononi kwa TPDC ambavyo mazingira ya mchakato wa utolewaji wake yanaacha maswali.
Mheshimiwa spika, Katika hatua ya sasa Wizara ya Nishati na Madini ijielekeze katika kusimamia mikataba ambayo tayari nchi yetu imeingia mpaka sasa kwa maslahi ya nchi na kupitia upya mikataba mibovu. Aidha, katika kutekeleza azma hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Wizara ya Nishati na Madini kutoa kwa Bunge taarifa ya uchunguzi wa mikataba hiyo iliyokamilika toka mwaka 2012 lakini imeendelea kufanywa kuwa siri mpaka hivi sasa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka pia serikali kuweka wazi kwa watanzania wote mikataba hiyo na mingine ambayo serikali imeisaini inayohusu rasilimali za Taifa hili. Aidha inatoa mwito kwa wananchi kuhakikisha kwamba masuala ya uwazi katika mikataba yanapewa kipaumbele katika katiba mpya, sera na sheria.
Mheshimiwa spika, Kitendo ambacho serikali ilikuwa inakifanya kupitia Shirika la Maendeleo ya Petrol (TPDC) cha kugawa vitalu vipya nane vya gesi wakati bado sera na sheria ya gesi haijakamilika ni ushahidi tosha kuwa kuna watu wachache katika serikali wameanza kulichukulia suala hili la gesi asilia kwa manufaa ya watu binafsi.
Mheshimiwa spika, Wizara ya Nishati na Madini katika bajeti yake ya miaka iliyopita imekuwa ikitenga fedha nyingi kwa ajili ya mishahara na posho kitengo cha sheria cha Wizara. Jambo hili la kugawa vitalu vipya nane vya gesi wakati sera na sheria kuhusu gesi havijakamilika linadhihirisha siyo tu udhaifu katika idara hii ya ushauri wa kisheria bali pia mazingira yanayoashiria mianya ya matumizi mabaya ya raslimali za umma katika zoezi hili. Kambi Rasimi ya Upinzani Bungeni inalichukulia jambo hili kuwa ni udhaifu ambao hauwezi kuvumilika hata kidogo na tunaitaka wizara ieleze sababu hasa za kuendesha zoezi hili kinyume na maoni na mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba chama lege lege huzaa serikali legelege; udhaifu huu wa wizara unaweza kutafsiriwa kwamba unachangiwa na ushiriki wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupewa na kukubali hisa toka kwa moja ya makampuni yanayojihusisha na utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini, kampuni ya Ophir energy . Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Bunge za tarehe 08.11.2012 ni kuwa wakati CCM ikipewa hisa wapo pia baadhi ya watanzania ambao waligawiwa sehemu ya hisa hizo kwa ajili ya CCM
Aidha,Katibu Mkuu wa CCM Abdurahaman Kinana anatajwa na vyanzo mbalimbali kwamba amewahaki kuwa Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Artumas ambayo iliingia mkataba na Serikali wa kuzalisha Mega Watt- 300 za umeme Mtwara eneo la Mnazi Bay. Mkataba huo ulikuwa wa misingi ya mabadilishano ya gesi kwa nishati ya umeme (gas for power). Kwamba Artumas ingechimba na kuuza gesi asilia na kuilipa serikali kwa pamoja na mambo mengine kuizalishia umeme wa 300MW. Baadae mwaka 2010 Artumas baada ya kufaidika vya kutosha kutokana na uvunaji na uuzaji  iliacha kuendeleza mradi huo kwa kisingizio cha madai ya mdororo wa Uchumi mwaka 2009 na kuuza hisa zake kwa kampuni ya Wentworth ya Ufaransa.
Mheshimiwa Spika,Ushiriki huu wa viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi na chama hicho kwenye shughuli ambazo zinaitia hasara serikali unazua mazingira ya kwamba CCM inasababisha unyonywaji wa Taifa na wananchi, na hivyo ni dhahiri si mwafaka kuendelea  kuongoza nchi hii. CCM na baadhi ya viongozi wake wamekuwa wakifaidika  kutokana na ombwe la kisera na kisheria katika sekta hii na nyingine muhimu. Katika hali kama hii, maneno ya Mwalimu Nyerere yanapaswa kuongezewa nukuu mpya kwamba “chama cha mafisadi huzaa serikali ya mafisadi”.
3.2 Haki ya Wananchi kumiliki rasilimali asilia
 Mheshimiwa Spika, Wakati Katiba yetu inatambua haki ya kumiliki mali na hifadhi ya mali hiyo na inakataza unyang'anyi wa mali kwa lengo la kuitaifisha au kwa malengo mengine, haki za wananchi kumiliki rasilimali zao za asilia kama ardhi, madini, mafuta, gesi asilia, misitu na wanyama pori, uvuvi, n.k., zimekuwa haziheshimiwi na mamlaka za kiserikali kwa hoja kwamba rasilimali asilia hizo ni mali ya umma.

Mheshimiwa Spika, Dhana ya mali ya umma ni dhana yenye asili yake katika ukoloni. Ni dola ya kikoloni ya Kijerumani ndio ilikuwa ya kwanza kutangaza kwamba mali asilia zote katika koloni lao la Tanganyika ni mali ya Mfalme wa Kijerumani. Baada ya Wajerumani kushindwa Vita ya Kwanza ya Dunia na kunyang'anywa makoloni yao ya Afrika, dola ya kikoloni ya Waingereza iliyokabidhiwa Tanganyika, walitangaza kwamba rasilimali asilia zote ni mali ya umma chini ya mamlaka na udhibiti wa Gavana wa kikoloni. Dhana hii ilipokelewa bila mabadiliko yoyote ya msingi baada ya uhuru na ndio imekuwa msingi mkuu wa sera za rasilimali asilia za nchi yetu kwa muda wote wa uhuru wetu. Jambo hili ni hatari kwani mali ya umma maana yake ni mali isiyokuwa na mwenyewe, na ndio maana wenye nguvu wanatumia mwanya huo kupora wasio na nguvu.

Mheshimiwa Spika, Kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, utekelezaji kivitendo wa dhana ya mali ya umma wakati wote wa uhuru umekuwa ni kuwanyang'anya wananchi rasilimali asilia zilizoko kwenye maeneo yao na kuzimilikisha mamlaka za Serikali (wakati wa miaka ya uchumi-dola), au kuzimilikisha kwa wawekezaji wa kigeni katika zama hizi za soko holela kwa kisingizio cha huria.

Mheshimiwa Spika, Matokeo ya mfumo huu ni kwamba milki na mamlaka ya maamuzi juu ya matumizi ya rasilimali asilia yameondolewa mikononi mwa wananchi na kuhamishiwa kwenye mikono ya warasimu wa Serikali. Sio hio tu, wananchi wamejikuta wakiondolewa kwa nguvu kutoka kwenye maeneo yao ili kuwapisha wamiliki wapya wa rasilimali hizo, yaani wawekezaji wa kigeni au wa ndani. Kwa sababu hiyo, uchumi wa wananchi umeanguka, umaskini umeongezeka na matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yameongezeka.

Mheshimiwa Spika, Dhana ya mali ya umma katika umilikaji wa rasilimali asilia imehakikisha kwamba maeneo yenye rasilimali asilia hayapati faida na manufaa yanayotokana na uwepo wa rasilimali hizo katika maeneo yao. Mrahaba, kodi na tozo nyingine zinazotokana na matumizi au mapato ya rasilimali hizo yanapelekwa kwenye mamlaka za Serikali Kuu. Kwa upande mwingine, madhara yanayotokana na matumizi ya rasilimali hizo Kama vile uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya matumizi ya rasilimali husika, yanawaangukia wananchi wa maeneo ziliko rasilimali hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba nieleze mtazamo na msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA kuhusiana na umiliki pamoja na uendelezaji wa Raslimali zetu asilia,ni  kwamba:
  1. Wananchi hawatanyang'anywa rasilimali zao asilia na mamlaka za Serikali kwa ajili ya matumizi na watu au taasisi nyingine bila kwanza Wananchi watakaoathiriwa na unyang'anyi au matumizi hayo kutoa ridhaa yao baada ya kupatiwa taarifa zote na kamili zinazohusu matumizi yanayotarajiwa ya rasilimali hizo na athari za matumizi hayo kwa mazingira, kiuchumi na kijamii (the right of prior informed consent). Wananchi Kama wamiliki wa msingi wa rasilimali asilia, watakuw
ii.Wananchi wana haki ya kulipwa mrahaba kwa ajili ya matumizi ya watu au taasisi nyingine ya rasilimali asilia za Wananchi, wakati mamlaka za Serikali za mitaa, Majimbo na Serikali Kuu zitakuwa na haki ya kutoza kodi mapato yatakayotokana na matumizi ya rasilimali hizo.

3.4  BOMBA LA GESI TOKA MTWARA HADI DAR ES SALAAM

Mheshimiwa Spika, Pamoja na ushauri wa kambi rasmi ya upinzani bungeni wakati wa kuwasilishwa kwa bajeti ya wizara 2012/2013 kuitaka Serikali kuwasilisha Bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika ili Bunge liweze kuishauri na kuisimamia Serikali kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63; kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya Taifa yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo mkubwa lakini bado serikali haikutilia maanani ushauri huu. Matokeo yake siyo tu kusababisha mkanganyiko kwa wakazi wa Lindi na Mtwara bali pia kuacha maswali mengi kwa watanzania juu ya nini hasa nia ya serikali kwa kuficha mikataba inayohusu rasilimali hizi za Taifa kwa wananchi wake na hata kwa chombo cha kuwakilisha wananchi kama Bunge.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali isiendelee na ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar Es Salaam hadi kwanza; Mosi, iweke wazi kwa Bunge mikataba yote inayohusu uendelezaji wa gesi asilia ikiwemo ya ujenzi wa Bomba hilo. Pili, ikutane na wananchi kuwashirikisha na kuhakikisha manufaa kwa taifa na kwao.

Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA imeshangazwa na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo tangu kuibuka kwa mgogoro huo amejikita zaidi katika kutoa kauli kupitia vyombo vya habari badala ya kwenda kukutana na wananchi hatua kwa hatua na kuwezesha ufumbuzi kupatikana. Aidha, manufaa kwa wananchi wa Lindi na Mtwara ambayo taarifa yake imechapwa kwenye vyombo vya habari yaletwe kama taarifa rasmi bungeni ikiwa na ulinganisho baina ya shughuli za kijamii zilizofanywa na makampuni tajwa pamoja na miradi iliyotekelezwa na Serikali kufuatia mapato katika sekta hii tangu mwaka 2004 na thamani halisi ya mapato ambayo makampuni tajwa na Serikali wamepata.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia kuitaka Serikali kueleza ni miradi ipi  iliyotengewa fedha inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara na imetengewa kiasi gani cha fedha katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 ili kuharakisha msukumo wa maendeleo kwa mikoa hiyo ya Kusini ambayo imesahaulika kwa siku nyingi na hivyo siyo tu kuharakisha maendeleo kwa mikoa ya Kusini bali pia kuhakikisha usalama wa mradi huo mkubwa kwa manufaa mapana ya jamii ya kitanzania.

Mheshimiwa Spika, kuanza kwa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia pamoja na bomba la kusafirisha gesi hiyo hadi Dar es salaam na usambazaji wa umeme katika vijiji 52 vinavyopitiwa na bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Lindi haikidhi wala kujibu kilio cha wananchi wa Mtwara na Lindi cha kutaka ugunduzi wa gesi asilia katika mikoa hiyo uweze kunufaisha mikoa hiyo kimaendeleo kutokana na kuwa nyuma kimaendeleo miaka 52 baada ya uhuru wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, wakati waziri akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2012/2013 ya Wizara ya Nishati na Madini tarehe 27-07-2012 aliliambia bunge hili kuwa, kusainiwa kwa mkataba wa mkopo kati ya Tanzania na China kwa ajili ya kusafirisha Gesi asili na ujenzi wa Bomba la kusafirishia gesi toka Mnazi BAY hadi Dar es saalam na kusainiwa kwa mikataba mingine mitano (5) na mkataba wa uzalishaji na ugawanyaji wa mapato ya mafuta na Gesi asili kuwa ni miongoni mwa jitihada ambazo serikali imechukua katika jitihada za kukabiliana na tatizo sugu la umeme hapa nchini, hata hivyo kama ulivyo utaratibu wa serikali mikataba hii inaendelea kuwa siri.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali na Wizara ya Nishati na Madini kuainisha miradi hiyo na kuitengea fedha ili wananchi wa mikoa ya kusini waweze kunufaika na rasilimali hiyo kwani kwa muda mrefu sana wamekuwa wavumilivu wakisubiria utekelezwaji wa ahadi za kuwapelekea maendeleo kwa miaka mingi bila kuyaona wala kuyapata.
Kambi rasmi ya Upinzani , inaitaka serikali isitishe ujenzi wa Bomba hilo kwanza iende ikajadiliane na wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani na wakubaliane jinsi ya kuendelea na mradi huo ndipo ujenzi wa bomba hilo uweze kuendelea , kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeamua kumaliza tatizo la msingi kwani serikali ikiendelea bila kujali madai ya wananchi hawa na kuamua kutumia mabavu kujenga hakuna atakayekuwa mshindi kati ya serikali na wananchi hawa. Ni rai yetu kuwa serikali itaweza kuiona busara hii ili gesi iweze kuwanufaisha watanzania wote yaani wa Mtwara na wale wa maeneo mengine.
4.0 MAFUTA
4.1 MFUMO WA UAGIZIAJI MAFUTA KWA UFANISI
Mheshimiwa Spika, Marekebisho ya Sheria ya petrol (Petroleum Supply Act 2008) kifungu cha 33(1) kinatamka kuwa uagiziaji wa bidhaa za petroli lazima ufanyike kwa ufanisi na kwa kigezo cha unafuu mkubwa wa gharama na kufafanuliwa zaidi na kifungu cha 33(2) ambacho kinaeleza ufanisi wenyewe ikiwa ni pamoja na :-
a)            Uagiziaji wa pamoja wa kushirikiana (Joint Procurement)
b)            Uagiziaji wa ushindani (Compitative Procurement)
c)             Uagiziaji wa shehena kubwa (Bulk Procurement)
d)            Kwa kutumia fursa ya viwango vya kiuchumi (Taking advantage of economic Scale). Pia Sheria imetoa fursa ya kubadili kwenye aina nyingine za uagiziaji utakao onekana unatija zaidi.
Mheshimiwa Spika, sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA) sura ya 414 pamoja na Petroleum Conservation Act (cap 392) zimeongeza majukumu ya kudhibiti na kuratibu uagiziaji mafuta kutoka nje. Pia mfumo wa  ununuzi na usafirishaji wa mafuta kwa pamoja umependekeza kuwa na mratibu (Petroleum Importation Co-ordinator  - PIC) wa kukusanya taarifa za mahitaji na kutayarisha zabuni.
Mheshimiwa Spika, Kampuni hii , iliratibiwa na EWURA lakini ilisajiliwa kwa masharti ya sheria ya makampuni na hivyo kuifanya kuwa kampuni binafsi inayomilikiwa na Umoja wa Makampuni yanayoagiza na kusafirisha mafuta nchini (TAOMAC). Uendeshwaji wa Kampuni hiyo upo chini ya bodi na Mwenyekiti wa bodi uteuliwa na mkutano wa wanahisa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikieleza jinsi gani Wizara inavyoshindwa kusimamia mambo ya msingi kwa mujibu wa sheria na kanuni za uwepo wake. Mfano dhahiri ni kitendo cha Mhe Waziri kuteua Mwenyekiti wa Bodi ya PIC kwa kutumia Nafasi yake na mbaya zaidi kumteua Ndugu James Andindile ambaye ni Kamishna msaidizi-Wizara ya Nishati ni dhahiri kuwa Wizara itashindwa kufanyakazi yake ya usimamizi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe.Waziri alieleze Bunge ni kwa vipi ana uwezo wa kuingilia utendaji wa Kampuni Binafsi kwa kuteua Mwenyekiti wa Bodi?  Ni mfumo gani umewekwa wa kuhakikisha Wizara inafanya usimamizi?
Mheshimiwa Spika, ili kuepusha watanzania kubebeshwa mzigo wa gharama kubwa ya mafuta katika Kikao cha Arobaini na Mbili – Tarehe 9 Agosti, 2011,kulitolewa hoja ya dharura kuhusu uhaba wa mafuta baada ya michango kadhaa ya waheshimiwa wabunge na hatimae Serikali ilitoa kauli yake. Baada ya mjadala huo Bunge lilifanya uamuzi. Hata hivyo hakukuwa na ufuatiliaji wa karibu baada ya maazimio. Hali hii ni moja katika kasoro kubwa ambayo kuanzia mwaka huu Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA ilitaka irekebishwe. Katika Kamati zote zilizopo za sekta hakuna Kamati ambayo inafuatilia maazimio yote  ya Bunge ili Serikali kusimamiwa kwa zile ahadi au maazimio  tuliyoyapitisha hapa Bungeni.
 Mheshimiwa Spika, Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge la Tisa iliweza kupendekeza kwa Serikali mara nyingi sana kuhusu suala la TPDC kupitia kampuni tanzu ya COPEC kuanzisha biashara ya mafuta. Kamati ya Nishati ya Bunge la Tisa ikazungumzia pia Bulk Procurement pia Strategic Reserve. Masuala yote haya yamehojiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani mwaka 2011 na 2012
Mheshimiwa Spika, baada ya kushindwa kuchukua hatua hatimaye Serikali ikaleta ahadi nyingine, nanukuu “leo hii tarehe 9 Agosti, 2011, Serikali kupitia EWURA imeipa leseni Kampuni ya COPEC ambayo ni Kampuni Tanzu ya Serikali kupitia TPDC kuanza kufanya biashara ya mafuta mara moja.
Naomba kurudia. Leo hii tarehe 9 Agosti, 2011 Serikali kupitia EWURA imeipa leseni COPEC ambayo ni Kampuni Tanzu ya Serikali kupitia TPDC kuanza kufanya biashara ya mafuta mara moja”.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2011/2012 wa fedha Wizara ya Nishati na Madini, COPEC ilikuwa imepangiwa shilingi milioni 20 tu kwa ajili ya kampuni hiyo kuanza kufanya biashara. Ukweli ni kwamba kampuni hiyo haikuwa na miundombinu yoyote ya kuiwezesha kufanyabiashara kama Serikali ilivyoagiza.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge toka ilipopatiwa leseni ya biashara hadi sasa COPEC imeongeza tija ipi katika biashara ya mafuta kwa watanzania?
Mheshimiwa Spika, Waziri aliahidi mbele ya bunge kuanza kwa mpango wa utekelezaji uingizaji wa mafuta wa pamoja (Bulk procurement) mwezi January 2012. Wizara ieleze kuanza kwa utaratibu huu umeokoa kiasi gani cha pesa kilichokuwa kinapotea kabla ya kuanza kutumika kwa utaratibu huu mpya na sababu za mpango huo kushindwa kushusha bei ya mafuta kinyume na ahadi za Serikali.

5.0 UMEME
Mheshimiwa Spika, Bado kunaendelea kuwepo na utata kuhusu mgawo wa umeme katika maeneo mengine ya nchi huku serikali ikikanusha kuhusu mgawo wakati watanzania wakiendelea kupewa nishati hiyo kwa mgawo. Aidha Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini akiwasilisha makadirio ya Bajeti ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka  2012/1013 aliliambia bunge lako tukufu kuwa “hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2012 lengo la kuondoa mgao wa umeme lilifikiwa kwa asilimia 100”. Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni  inalitaka shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini kuwaambia ukweli watanzania kuhusu mgawo wa umeme kwa kuzingatia hali mbaya ya shirika hilo kifedha ambayo imeripotiwa na vyombo vya habari hivi karibuni. 
Mheshimiwa Spika, kitendo cha kutowaambia wananchi ukweli kuhusu mgawo wa umeme wakati wananchi wakipata nishati hiyo kwa mgawo huku wakipewa sababu ambazo zinaonekana hazina ukweli kinazidi siyo tu kushusha heshima na hadhi ya serikali kwa wananchi wake bali pia kinadhihirisha udhaifu uliopo katika mfumo wa kiutendaji wa serikali pamoja na mashirika yake likiwemo shirika la umeme Tanzania (TANESCO).
Mhesimiwa Spika, mradi wa kuboresha mifumo ya umeme katika jiji la Dar es salaam ambayo imekuwa ndio kisingizio kikubwa cha mgawo wa umeme hali ambayo inazua maswali mengi kwa watanzania. Hii ni kutokana na ukweli kwamba  kazi hiyo ilianza katika bajeti ya 2011/2012  na mpaka sasa tatizo la kukatika kwa umeme bado linaendelea kitendo ambacho kinatafisiriwa kuwa kazi hiyo bado haijakamilika  miaka miwili tangu kuanza kwa kazi hiyo iliyogharimu shilingi billion 120. Watanzania wanapenda kujua ni lini hasa kazi hii itakamilika ili kupunguza kero ya mgawo wa umeme kwa Dar es salaam na Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha serikali kutoa ahadi hewa zisizo tekelezeka na kutochukua hatua stahiki dhidi ya watumishi wa serikali wanaoihujumu TANESCO imekuwa ndio chanzo cha kuzorotesha ufanisi wa shirika hili na kufanya liendelee kuendeshwa kwa hasara. Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni imekuwa ikishauri mara kadhaa juu ya kufikishwa mahakamani kwa watumishi wote wa serikali na mafisadi wote wanaohujumu uchumi wakiwemo wale wa TANESCO, Kiwira, Meremeta, Richmond n.k  lakini inaonekana kuwa ni utaratibu wa serikali hii au udhaifu wa serikali katika kushughulikia watuhumiwa hao wa  uhujumu uchumi. 
Mheshimiwa Spika, kutokana na udhaifu wa Serikali ya CCM katika kuchukua hatua, kama ilivyokuwa katika kusamehe naadhi ya wezi wa EPA
na kuzimwa kwa sakata la Richmond lililosababisha hasara ya mabilioni ya fedha. Hali hiyo imechangia kuzaliwa kwa sakata jipya la DOWANS linalopelekea TANESCO kutakiwa kuilipa kampuni hii ya DOWANS ambayo ilirithi mkataba wa kampuni hewa ya Richmond zaidi ya shilingi 97,000,000,000 kuna zidi kulipatia taifa mzigo mkubwa. Hii ni kwa sababu kodi za wananchi  na malipo ya wateja zinazotumika katika kashfa zote hizo na kuwasababishia wavuja jasho wa taifa hili kuwa na  ugumu wa maisha pamoja na kwamba waliahidiwa maisha bora kwa kila mtanzania.

Mheshimiwa spika,Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kutoa taarifa kwa Bunge lako tukufu ikieleza sababu zinazowafanya wasimfikishe Mahakamani aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco Eng. William Mhando, siyo tu kwa matumizi mabaya ya ofisi yaliyosababisha TANESCO hasara ya zaidi ya bilioni 6,000,000,000 kwa kila mwezi baada ya kukatisha mkataba wa ununuzi wa mafuta kwa ajili ya IPTL kutoka kwa BP waliokuwa wakiuza kwa bei nafuu na kuanza kununua kwa kampuni za Oryx na Camel oil ambayo gharama yake ilikuwa juu bali pia kwa kukiuka miiko ya maadili ya viongozi wa umma?

Mheshimiwa spika, katika mjadala wa bajeti ya mwaka 2012/2013 kulijitokeza pia wasiwasi wa namna TANESCO inavyojiendesha. Bunge liliiomba Wizara ya Nishati na Madini ichunguze kwa kina suala la mapato ya TANESCO na jinsi yanavyotumika. Ilionekana TANESCO kwa mwezi inapata takribani Billion 60 au Billion 70. Mishahara ya wafanyakazi wa TANESCO peke yake ni takribani Billion kumi na moja. TANESCO inatumia fedha nyingi sana kununua umeme kutoka makampuni yanayotumia umeme hususan wa dharura su kukodisha mitambo ya kufua umeme wa dharura. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia wizara ya Nishati na Madini itoe majibu juu ya uchunguzi unaohusu uendeshaji wa shirika hili.
Mheshimiwa spika, Mnamo tarehe 18 Julai, 2011 serikali kupitia Waziri Mkuu Mizingo Pinda iliahidi kupunguza matumizi yasiyo ya msingi ya serikali ilikupata fedha ambazo zilitegemewa kuliongezea Shirika la Umeme la TANESCO ili liweze kutekeleza mpango wa umeme wa dharura na kuliongezea shirika hilo uwezo wa kujiendesha. Hata hivyo ahadi hiyo ilichukua sura mpya baada ya serikali kushindwa kutekeleza tamko lake la kwanza na kutoa ahadi nyingine tena ya kupata fedha kwa kukopa ambayo mpaka sasa utekelezaji wake bado unasuasua.

Mheshimiwa spika, Mnamo 13 Agosti, 2011 serikali ilitoa ahadi ya kuisaidia TANESCO kuweza kukopa bilioni 408 kutoka kwenye mabenki, lakini mpaka sasa ni jumla ya dola za marekani milioni 65 ambazo ni sawa na billion 104 tu ndizo TANESCO imeweza kukopa tena kwa kuchelewa. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali kama ilivyoainishwa na Wizara katika ripoti yake ya utekelezaji kwa Kamati ya Nishati na Madini TANESCO ilipokea fedha hiyo mwezi Januari mwaka huu (2013). Ahadi hizi zisizotekelezeka zimekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya sekta hii muhimu ya umeme ndiyo maana mpaka sasa ni sehemu ndogo sana ya Watanzania wameunganishwa na huduma hii muhimu ya umeme.

Mheshimiwa spika,katika mwaka wa fedha 2012/13 kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini ilitoa mapendekezo kazaa kwa lengo la kuboresha sekta ya umeme, mapendekezo hayo ya kamati pamoja na yale yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  mengi hayajafanyiwa kazi na serikali na hata yale ambayo yamefanyiwa kazi utekelezaji wake ni kwa kiwango kidogo. Aidha mapendekezo ambayo hayajafanyiwa kazi ni kama ifuatavyo:
(i)     kuanzishwa kwa mfuko wa kuendeleza nishati ya umeme nchini kwa lengo la kutumia mfuko huo kama mtaji (Equity) ili fedha zake zitumike katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa umeme nchini na pia kukopa kutoka vyombo vingine vya fedha.
(ii). Kamati pia ilishauri wizara kutenga fedha za kutosha katika uzalishaji, usambazaji na usafirishaji wa umeme kwani vinategemeana. Cha kushangaza katika bajeti ya serikali ya mwaka 2013/2014 haijatengwa fedha yoyote ile kwa ajili ya kuboresha njia za usafirishaji umeme mbali ya kuwepo kwa asilimia 22.5 ya upotevu wa umeme unaozalishwa inayosababishwa na miundombinu chakavu ya umeme.

(iii). Kamati baada ya kuona ugumu na gharama ambayo TANESCO itapata katika kusafirisha mafuta toka bandarini kwenda Nyakato Mwanza ilishauri tangu kwenye bageti ya mwaka 2011/2012 na kurudia ushauri huo katika bajeti 2012/2013 kwamba mradi huu uhamishiwe sehemu ambayo yatapatikana mafuta ya uhakika na mitambo hiyo itumie mafuta ya dizeli ili kuweza kunusuru gharama  ambazo nchi itaingia baadaye na kupelekea ufanisi wa mitambo hiyo kuwa mdogo.

(iv)                        Pia Kamati iliitaka serikali kuiwezesha TANESCO kumiliki mitambo yake badala ya kutegemea mitambo ya kukodi ambayo inaligharimu shirika hilo fedha nyingi linazolipa kwa makampuni yanayomiliki kama capacity charge.

Mheshimiwa Spika, Katika hoja hii Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaamini kwamba kamati ilifanya uchunguzi wa swala hili kabla ya kutoa ushauri kwa serikali. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa mchanganuo wa gharama ambazo TANESCO itazipata katika kusafirisha mafuta mazito ya mitambo ya kufua umeme inayo jengwa Nyakato Mwanza.
Mheshimiwa spika, katika hoja hii serikali imejaribu kueleza jitihada yake ya kujenga mitambo mbalimbali ya kufua umeme wa gesi ikiwemo ile ya Kinyerezi, Ubungo na Mwanza.
Mheshimiwa spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kueleza bayana namna mitambo hii inayojengwa itakavyokuwa mbadala wa mitambo ya kukodi kuliko kuendelea kijisifia inajenga mitambo wakati kuna baadhi ya mitambo imekamilika lakini bado mitambo ya kukodi haipungui na TANESCO inazidi kulipa capacity charge.
Mheshimiwa spika, umeme vijijini, zaidi ya bilioni50 ambazo REA imetengewa, kiasi hiki ni kikubwa,  hivyo kitendo cha Wizara kutenga fedha kwa ajili ya kupeleka umeme vijijIni bila kutaja idadi na majina ya vijiji vitakavyonufaika na miradi ya fedha hizo linatoa mwanya wa kutumia vibaya fedha za serikali. Hali hii imejitokeza pia katika Taarifa za Serikali za mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo hakuna vijiji vya kutosha vilivyooneshwa kunufaika na hivyo kuleta mkanganyiko mkubwa katika utekelezaji wa miradi hii vijijini.
Mheshimiwa Spika, pia tunamtaka Waziri aelezee juu ya mradi uliotengewa fedha na Serikali katika bajeti mwaka wa fedha 2011/2012 mradi uliohusu taa za mwanga bora vijijini ambao ulitakiwa kutekelezwa Bukombe, Kahama, Biharamulo na Chato. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe majibu kwa nini mradi huo haukutekelezwa wakati fedha za mradi huo zilitengwa? Pamoja na majibu hayo Kambi Rasmi Bungeni pia inaitaka Wizara kueleza juu ya mradi mwingine ambao ulifahamika kwa jina la “TANZANIA AFFORDABLE RURAL ELECTRIFICATION PLAN” ambao ulitakiwa utekelezwe Bukombe na Kibondo, hasa juu ya hatua iliyofikiwa hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, TANESCO imefika hapo ilipo sasa kutokana na kutokuwa makini katika uingiaji wa mikataba mbalimbali na makampuni yanayoiuzia umeme. Kamati ya wataalam wa sheria ya Bunge wakati wa sakata la RICHMOND ilishauri yafuatayo kuhusiana na mikataba: “kuna ulazima kwa Mikataba mikubwa ambayo inahusu maslahi na manufaa ya Taifa kama vile Mkataba wa IPTL kuwasilishwa Bungeni, kwa utaratibu wa dhana ya demokrasia ya uwajibikaji (accountability in a Parliamentary democracy) kwa ajili ya ushauri wa Bunge kuwasilishwa Bungeni….. Aidha, Kwa kuzingatia kuwa Mikataba mibovu kati ya TANESCO na Makampuni mbalimbali ambapo Makampuni hayo yanalipiwa kodi yote na TANESCO imekuwa ni chanzo cha bei kubwa za umeme katika nchi yetu, na kwa kuzingatia kuwa Mikataba hiyo inasababisha Sera muhimu za Taifa, kama vile, Sera ya Kupiga vita Umaskini, Sera ya Huduma Bora kwa Jamii, Sera ya Taifa ya Nishati inayolenga kusambaza nishati ya bei nafuu vijijini n.k. kutotekelezeka, tunashauri kuwa Mikataba hiyo ipitiwe upya ili irekebishwe, kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu”.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge katika ufanyaji kazi wake ni mikataba mingapi ya uzalishaji wa umeme na kuiuzia TANESCO, Madini au Gesi imefungwa bila ya kuzingatia ushauri au mapendekezo yaliyokwishatolewa Bungeni? Kama imefanyika je jukumu la Bunge kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63 ina maana gani?
Mheshimiwa Spika, matumizi mabaya ya raslimali za umma hayako katika mikataba ya kukodi mitambo ya umeme tu, bali katika ununuzi wa huduma za kisheria. Hivyo, narudia kutoa mwito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aeleze ni kiasi cha fedha kilichotumika kwenye kuendesha kesi za Dowans na IPTL mpaka sasa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya mawakili wa TANESCO na makampuni binafsi yanayotuhumiwa kusababisha mzigo mkubwa wa gharama za kesi ambazo serikali inashindwa kwa nyakati mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Izingatiwe  kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012 pekee jumla ya shilingi bilioni 10 zimetumika kwa ajili ya gharama za kuendesha kesi hizo kwa kuilipa kampuni ya Rex Attorneys na Makampuni mengine ambayo kwa nyakati mbalimbali yamekuwa yakiiwakilisha serikali na TANESCO na kushindwa katika mahakama za kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa Spika, kufuatia mfululizo wa TANESCO kushindwa mahakamani huku mabilioni ya walipa kodi na wateja wake yakitumika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inapendekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za  Serikali (NAO) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wachunguze tuhuma za ufisadi na ubadhirifu kwa Shirika la Umeme (TANESCO) kwenye matumizi ya  mabilioni katika idara ya sheria na ununuzi wa huduma za kisheria kutoka makampuni binafsi unaofanywa na TANESCO.
Ukaguzi na uchunguzi huo ufanywe kuhusu matumizi na ufanisi wa huduma za kisheria ambazo TANESCO imekuwa ikizipata kutoka kwenye makampuni binafsi katika kesi kubwa za kimataifa ikiwemo ya Dowans na IPTL kwa kurejea pia maoni niliyoyawasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Kambi Rasmi bungeni mwaka jana ilitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu matumizi ya kifungu cha 1005 cha Kitengo cha Sheria ambacho kina kasma ya 229900 ambayo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kimetengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 4  kama  gharama za utetezi wa Serikali katika kesi ya IPTL ikiwemo kwa ajili ya kuilipa kampuni ya Mkono & Co. Advocates.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka Serikali kueleza jumla ya fedha zilizotumiwa na Wizara kati ya mwaka 1995 mpaka 2011 kwa ajili ya kulipa makampuni binafsi ya uwakili kwenye kesi kubwa za kitaifa na za kimataifa pamoja na kutaja orodha ya makampuni hayo.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali ilitakiwa ieleze mkakati wa kudhibiti ongezeko la gharama za kisheria ambazo ni mzigo mkubwa kwa mashirika ya umma na wananchi walipa kodi kwa kuwa yamekuwepo mazingira ya kesi kuendelezwa kwa muda mrefu na kugeuzwa kuwa vitega uchumi vya watu wachache. Nilitaja Mifano ya kesi zilizodumu kwa muda mrefu ni ya IPTL ambayo Serikali inawakilishwa na Mkono and Co. Advocates na ile ya Dowans ambayo Serikali imekuwa ikiwakilishwa kwa nyakati mbalimbali na Rex Attorneys.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanapaswa kulieza Bunge sababu za kuacha kutoa majibu kuhusu suala hilo mpaka hivi sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua hatua ambazo Serikali imechukua juu ya matumizi hayo.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo ni mdeni mkuu katika sakata la IPTL ilifungua kesi ya madai katika mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSID case Na. ARB/10/20) inayodai kiasi cha dola za Kimarekani milioni 225, pamoja na riba katika kuendesha kesi hiyo. Kampuni ya uwakili ya Mkono (inayomilikiwa na Nimrod Mkono Mbunge wa CCM) ilipewa zabuni ya kuitetea Serikali katika shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa kesi hiyo tutashinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni kinzani kuhusu suala hilo.  Kampuni ya Mkono imekuwa ikiishauri Serikali isifanye usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai kupitia kwa Mfilisi wa Mali na Madeni za IPTL (RITA) wanakubali kusuluhishwa nje ya mahakama. Je, mpaka lini Serikali itaendelea kuingia gharama hizo na ni kiasi gani Serikali imelipa kwa kampuni hiyo na zingine  mpaka hivi sasa?

5.1 MPANGO WA UMEME WA DHARURA
Mheshimiwa spika, itakumbukwa kuwa Bunge lako tukufu lilipitisha mpango wa umeme katika mkutano wake wa nne. Serikali ililiambia Bunge hili usafirishaji wa gesi kutoka Songosongo hadi, Somanga hadi Dar es salaam ungeongezwa ndani ya miezi kumi na mbili ili majenereta yaliyokuwa yamenunuliwa kutumika katika mfumo wa gesi yafanye kazi ndani ya miezi kumi na mbili. Aidha ilikusudiwa pia kuwa mpango huo ulilenga kushusha gharama za uzalishaji wa umeme hapa nchini. Ikiwa sasa ni mwaka mmoja na zaidi umepita fedha zinazidi kutengwa kwa ajili ya kununulia mafuta mazito ya kuendeshea majenerata, kwa sehemu kubwa ikiwa ni kwa ajili ya mitambo ya kufua umeme.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa kauli kuhusu sababu za ucheleweshaji katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme  na kushindwa  kubadilisha mfumo wa majenereta kutumia gesi badala ya mafuta, na kama kweli dharura iliyokuwepo bado ipo au imekwisha?
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa miradi ya dharura iliyotakiwa kuwa imekamilika ni pamoja na mradi wa Jacobsen awamu ya pili ambao ulitakiwa kutekelezwa kuanzia mwezi Januari hadi disemba 2012 ambao ungezalisha mega-watt 150 na kuendeshwa na fedha za mkopo. Tunapenda kupata ufafanuzi kuhusu miradi hii ya umeme wa dharura miradi mingapi imekamilika, kiasi gani cha pesa kimetumika na kama taifa tunadaiwa kiasi gani cha fedha ambazo hadi sasa zimekopwa kwa ajili ya miradi ya umeme kwa vile ni miongoni mwa maeneo ambayo nchi hii imekuwa ikiingia gharama kubwa lakini ikishindwa kumaliza tatizo hili na kuchangia katika deni la Taifa ambalo sasa linafika trilioni 22.
Aidha Mheshimiwa Spika, moja ya mambo ambayo serikali iliahidi kuyafanyia kazi katika mpango wa umeme wa dharura ni kununua mitambo yake, napenda kunukuu maneno ya mheshimiwa waziri mkuu “Mheshimiwa spika ushauri mlioutoa ni wa msingi sana, moja mumesema serikali nunueni mitambo, ”Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kuliambia bunge hadi sasa tangia kupitishwa kwa mpango wa umeme wa dharura ni mitambo mingapi ya kuzalisha umeme ambayo inenunuliwa na tayari imeshaanza kuzalisha umeme. Pia serikali iliambie bunge lako tukufu ina mpango gani kuhusu mitambo ambayo tumekuwa tunakodi kwa maana ya mitambo ya Symbion miaka miwili, na mitambo ya Aggreko ambayo yote tumekuwa tunalipa capacity charge, je serikali imeandaa njia gani mbadala zaidi ya ambayo tumekuwa tukitumia?
Mheshimiwa Spika katika mpango wa umeme wa dharura, mashirika ya mifuko ya jamii  kama NSSF nayo yaliruhusiwa kuwekeza katika sekta hii ya umeme, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata ufafanuzi kuhusu mipango inayoendelea juu ya nia hiyo ya mifuko ya jamii kuwekeza katika sekta ya umeme hapa nchini.
5.2  SYMBION POWER AFRICA LLC, TANESCO NA KUANZISHA KAMPUNI MPYA YA UMEME KUSINI MWA TANZANIA (SECO).
Mheshimiwa Spika, kutokana na andiko la kinadharia ‘conceptual proposal’ la kujenga mtambo wa kufua umeme katika mji wa Mtwara na usambazaji wake  lililoandikwa na  kuwasilishwa Wizara ya Nishati na Madini ,TANESCO na TPDC mnamo tarehe 07 Septemba 2012 na baada ya andiko hilo kupitiwa kwa kina na TANESCO kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 12 Februari 2013 Symbion Power Africa LLC waliandaa /waliwasilisha MOU baina yao na Tanesco ili iweze kusainiwa kwa ajili ya kuanzisha kampuni ya kuzalisha umeme chini ya kinachoitwa  ‘Special Purpose Company’ (SPC), Kampuni hiyo itajulikana kama “Southern Electric Company” (SECO) ambayo inaanzishwa chini ya utaratibu wa PPP .Kwa mujibu wa MOU ni kuwa Kampuni hii itakuwa ni kwa ajili ya kujenga ,kumiliki na kuendesha  mitambo inayotumia gesi  kuzalisha umeme 600 MW katika miji ya Mtwara na Dar Es Salaam.
Aidha ,kampuni hiyo ‘mpya’ ya SECO itajenga ,kumiliki na kuendesha mtandao wa usafirishaji na usambazaji wa umeme kutoka kusini mwa Tanzania kwenda kwenye Gridi ya Taifa , Kaskazini mwa Msumbiji na Malawi  ( ….AND to build,own and operate transimission and distribution networks that will link power plants in the south to the Tanzania grid, northern Mozambique and Malawi (“the project”))
Mheshimiwa Spika, MOU hii iliingiwa baada ya Symbion kufanya mazungumzo na Shirika la umeme la Msumbiji ‘Electricite de Mozambique’ (EDM) kwa ajili ya kuwauzia umeme eneo la kaskazini mwa Msumbiji katika maeneo ya Pemba na Nacala, hii ni baada ya EDM kuonyesha kuwa watakuwa tayari kununua umeme kutoka Symbion Tanzania.
Aidha kwa mujibu wa MOU hiyo ni kuwa tayari Symbion wameshasaini makubaliano na Wizara ya Nishati ya Malawi kwa ajili ya kuanzisha uchunguzi kuhusiana na mradi huo wa umeme kutoka nje , kipengele E cha MOU kinasomeka hivi, nanukuu “Symbion has signed an agreement with the Ministry of Energy in Malawi that provides for the investigation of a cross border project”
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa MOU kipengele cha 2.1 ni kuwa Symbion ndio watakuwa na jukumu la kufanya upembuzi yakinifu kwa gharama zao wenyewe na kuwasilishwa TIC kupitia kampuni ya ‘Special Purpose Company’ (SPC) kwa ajili ya kupatiwa hati ya PPP. Aidha, kampuni ya Special Purpose Company (SPC) itapewa hadhi ya kuwa ‘mwekezaji wa kimkakati’ ‘strategic Investor’ .
Aidha , kwa mujibu wa kipengele cha 2.2 cha MOU ni kuwa umpembuzi yakinifu huo utahusisha pia kuhusiana na mtaji unaohitajika kuwekezwa na SPC kwa ajili ya mtambo wa kuzalisha 300MW kwa kutumia gesi pamoja na mtambo wa kuzalisha 300MW Kinyerezi DSM kwa kutumia gesi.
Mheshimiwa Spika, kipengele cha 2.4 cha MOU kinasema kuwa upembuzi yakinifu huo utahusisha pia uwezekano wa kuhamisha mara moja baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme kutoka mtambo wa kuzalisha umeme wa Symbion Ubungo na kupelekwa Mtwara,lengo likiwa ni kuongeza ufanisi kwa muda mfupi huko Mtwara.
Kwa mujibu wa kifungu cha 2.5 ni kuwa upembuzi yakinifu huo pia utahusisha utoaji wa mafunzo ya kina kuhusiana na uendeshaji wa mitambo ya kisasa ya uzalishaji,usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini Marekani kwa ajili ya utawala wa baadae wa SPC .
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani inasikitishwa sana na tabia ya Serikali hii ya CCM kutokana na tabia yake ya kuendelea kupuuza maazimio ya Bunge hili ,kwani itakumbukwa kuwa Moja ya maazimio ya Bunge kuhusiana na Richmond ilikuwa ni kuhusisha Kamati za Bunge katika kuingia mikataba na makampuni ya kuzalisha umeme , sasa hapa sio kuzalisha tu bali ni kuanzisha kampuni nyingine .
Aidha, tunataka kujua ni kwanini serikali hii ya CCM imeamua kusaini MOU ya aina hii bila kuishirikisha kamati ya Bunge au Bunge, tena huu ni mkataba wa kwenda kuuza umeme nje ya nchi wakati sisi tuna shida kubwa ya umeme. Je, hii haiwezi kwenda kuwa Richmond nyingine?

5.3          MIRADI MIKUBWA YA UMEME NCHINI 2013/2014
5.3.1 Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mheshimiwa Spika, wakala huyu alianzishwa kwa sheria Na 8 ya mwaka 2005 na alianza kazi rasmi oktoba mwaka 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2003. Lengo likiwa ni kuwapatia wananchi waishio vijijini nishati bora. Pamoja na umuhimu wa wakala huyu bado serikali haijaonyesha kwa vitendo kuwa ina nia ya kusaidia wakala huyu ili aweze kutimiza majukumu yake kikamilifu na hasa linapokuja suala la kuupatia fedha kama zinavyoombwa na zinavyopitishwa na Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, Takwimu zinaonyesha kuwa serikali imekuwa haitimizi wajibu wake wa kuipatia REA fedha kama zinavyotengwa na kuidhinishwa na Bunge hili , kwa mfano mwaka 2008/2009 zilipitishwa shilingi bilioni 20.00 ila zilitolewa shilingi bilioni 12.06 sawa na asilimia 60. Mwaka 2009/2010 zilipitishwa shilingi bilioni 39.55, zilizotolewa ni bilioni 22.14 sawa na asilimia 56. Mwaka 2010/2011 zilipitishwa bilioni 58.883, zilizotolewa zilikuwa bilioni 14.652 sawa na asilimia 25. Mwaka 2011/2012 zilipitishwa bilioni 71.044,zilitolewa bilioni 56.748 sawa na asilimia 80 na mwaka 2012 /2013 zilipitishwa bilioni 53.158, zilitolewa bilioni 6.757 sawa na asilimia 13.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 wakala unahitaji kiasi cha shilingi bilioni 366.9  kwa ajili ya kutekeleza miradi sita ya nishati vijijini ambayo ni pamoja na awamu ya pili ya kusambaza umeme vijijini bilioni 200, mradi wa kupunguza gharama za miundombinu  na usambazaji wa umeme vijijini bilioni 10, kupeleka umeme katika makao makuu ya wilaya mpya 13 bilioni 70, mradi wa kusambaza umeme kwenye maeneo yaliyopitiwa na njia kuu bilioni 75, mradi wa Global Village Energy Partinership bilioni 10.4 na mradi wa kuhamasisha na kuongeza matumizi ya nishati jadidifu bilioni 1.5.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaitaka serikali kutenga fedha kama zilivyoombwa na wakala yaani bilioni 366.9 kwa mwaka huu wa fedha na sio kutenga kiasi cha shilingi bilioni 91 za ndani na bilioni 62 za nje, kama Kifungu 3001, kasma 3113 zinavyoonyesha, kwani wakala huyu asipopewa fedha kulingana na mipango ilivyo atashindwa kufikia lengo la kusambaza umeme kwa asilimia 30 Vijijini
Aidha, Kambi rasmi ya Upinzani, inataka kujua fedha zilizotengwa kwa ajili ya REA 2012/2013 asilimia 87 zimeenda wapi ? Mbona hazikupelekewa REA kama Bunge lilivyokuwa limeamua? 
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, haikubaliani na pendekezo la Waziri aliloliwasilisha mbele ya kamati ya Bunge (randama uk 22) la kuongeza tozo ya shilingi 100 kwenye kila lita moja ya mafuta ya petrol kwa ajili ya nishati Vijijini kwani huku ni kumwongezea mwananchi mzigo wa gharama za maisha, badala yake tunaendelea kusisitiza kuwa fedha zilizoongezwa kwenye kila lita moja ya mafuta ya taa mwaka 2011/2012 kwa hoja kwamba ni kuzuia uchakachuaji shilingi bilioni 600 kwa mwaka zipelekwe zote REA kwani watumiaji wakuu wa mafuta ya taa wapo vijijini na nusu zipelekwe TANESCO. Aidha makampuni ya madini yalipe kodi na tozo za mafuta wanayosafirisha na wanayotumia.
5.3.2               Thermal Power Operation Bilioni 273.207
Mheshimiwa Spika,mradi huu ni kwa ajili ya kuhudumia vituo vya uzalishaji umeme ambavyo vimeungwa kwenye Gridi ya Taifa na kununua vipuri vyake wakati kina cha maji kwenye mabwawa ya kufua umeme kitakapopungua kutokana na ukame. Kwa mwaka huu fedha zilizotengwa ni kwa ajili ya kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya dharura ya kufua umeme na kununua umeme kutoka kwa wazalishaji hao binafsi.
Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 28.07.2012 Naibu Waziri wa Nishati na Madini (nishati) Mhe.Simbachawene wakati akiwasilisha maoni juu ya hotuba ya bajeti alisema kuwa tatizo la mgao wa umeme nchini ni la kupangwa mezani, nanukuu (hansard uk.488) ‘………..lakini kila unapokaa siku mbili unaombwa kukubaliana na mgawo wa umeme na mkizungumza mezani mgawo unatoweka .Kumbe umeme wa Tanzania ni suala la kuzungumza mezani halafu mnakubaliana kuwa unakuwepo mgao au haupo;hii haikubaliki’
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani inaona kuwa hata suala la kutenga fedha nyingi kiasi hiki kwa ajili ya mafuta ya kuendeshea mitambo binafsi ya kuzalisha umeme wa mafuta nalo ni jambo la kupangwa mezani, kwani kama tukiamua kuwekeza kwenye vyanzo vingine vya umeme hakika tusingekuwa tunatumia fedha nyingi namna hii kwa ajili ya umeme wa mafuta nchini tena kutoka kwa wazalishaji binafsi. 
Mwenendo wa wizara hii ni kutenga mabilioni ya fedha kila mwaka , Kwa mfano mwaka 2011/2012 zilitengwa bilioni 204.643, mwaka jana 2012/2013 tulitenga bilioni 51.3 (lakini serikali ikatumia kiasi cha shilingi bilioni 242.96 randama uk.4) na mwaka huu wa fedha tunatenga bilioni 273.207 kwa ajili ya kununulia mafuta ya mitambo ya kuzalishia umeme. Yaani kwa miaka 3 tu  taifa limeunguza fedha kiasi cha shilingi bilioni 720.81.kwa ajili ya kulipa makampuni binafsi, hivi Mchuchuma,Liganga, Stiglersgorge, inahitaji uwekezaji wa kiasi gani? 
5.3.3 MRADI WA UMEME IGUNGA
Mheshimiwa Spika, kutokana na mradi wa umeme ambao unaendelea katika Wilaya ya Igunga kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa vijiji vya Mbutu, Mwamakona, Bukama, Igunga na vijiji vingine ambavyo mradi huu unapita kutokana na kutokuridhishwa na kiwango cha fidia ambacho walilipwa ili kuweza kupisha na kuachia ardhi yao, nyumba zao na mazao yao kwa manufaa ya mradi huo .Wapo waliolipwa shilingi laki sita, milioni moja nk
Kambi rasmi ya upinzani, imepokea malalamiko ya wananchi juu ya viwango vidogo vya fidia kwani  na madai yao ya kutoona tathimini iliyofanywa kulingana na mali zao na pia hawakulipwa kwa njia ya hundi pamoja na kutakiwa kufungua akaunti bali walilipwa kwa fedha taslimu. Hivyo, tunataka kujua juu ya yafuatayo;
i.              Ni lini wananchi hawa watalipwa kiasi halisi kulingana na ardhi na mali zao?
ii.             Ni kwanini wananchi hawa walilipwa fedha taslimu na sio kwa njia ya hundi kama ulivyo utaratibu wa malipo wa serikali?

5.3.4 SERIKALI NA MADENI YA SHIRIKA LA UMEME TANZANIA (TANESCO)
Mheshimiwa Spika kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaishangaa serikaLi hii ya CCM kwa kukosa dira ya kuongoza nchi hii, hali hii inatokana na serikali yenyewe kuwa sehemu ya kudhoofisha Shirika lake yenyewe huku ikitaka kuwaaminisha watanzania kwamba inashughulikia matatizo ya kupatatikana kwa umeme nchini.

Mheshimiwa Spika miongoni mwa matatizo yanayokwamisha shirika la umeme Tanzania kujiendesha ni pamoja na madeni ambayo yamekuwa sugu kutoka kwa makampuni mbalimbali, watu binafsi , mashirika , katika hali ya kushangaza idara za serikali zikiwemo pia  Wizara za Serikali ambayo inajinadi kuweka mpango wa kumaliza tatizo la umeme wakati ikishindwa kulipia hata bili zake za umeme.
Taasisi za serikali ambazo zinaonekana kuwa ni wadaiwa sugu hadi kufikia mwazi Januari 2013 ni pamoja na Zanzibar State Fuel inayo daiwa kiasi cha shilingi 46,136,823,543/=, Jeshi la wananchi wa Tanzania (TPDF) linadaiwa shilingi 13,839,849,487/=, Jeshi la Polisi linalodaiwa shilingi 8,994,752,654/= Wizara ya maji inadaiwa shilingi 4,997,245,027/= DAWASA inadaiwa shilingi 4,114,828,175/= na Jeshi  la  MAGEREZA  linalodaiwa shilingi 3,530,850,068/=  pamoja na mifano hii michache wadai wengine ni pamoja na Regional Water Engineers, Muhimbili Medical Centre, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Hospitali za serikali, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Radio Tanzania.
Kwa mjibu wa taarifa rasmi za TANESCO zilizopo ni kuwa shirika linadai jumla ya Tsh 83,773,824,632/= hadi mwezi januari 2013 kutoka kwa wadaiwa ambao ni wizara na taasisi za Serikali hii ya CCM .

Kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaitaka serikali kueleza sababu za kulihujumu shirika la umeme Tanzania kwa kutolipa bili za umeme, lakini pia ikumbukwe kuwa kila mwaka bunge hili Tukufu linapitisha bajeti kwa Wizara husika zenye vifungu vya matumizi mengine (0C) ambayo hutumika kufanyia shughuli nyingine zikiwemo kulipia bill za umeme na gharama za wizara husika , tunataka wakati wa majumuisho serikali itoe maelezo kwanini imeshindwa kulipa hadi sasa, fedha hizo zinafanya kazi gani na lini serikali italilipa shirika la umeme Tanzania ili kuepukana na matatizo ambayo serikali inayasababisha yenyewe.
6.0          MADINI
Mheshimiwa Spika, sekta ya madini ni miongoni mwa sekta ambazo, kama serikali ikiamua kutumia vizuri rasilimali hii ni miongoni mwa rasilimali ambazo kama zikitumika kwa masilahi ya Taifa zinaweza kulitoa taifa katika lindi hili la umasikini. Hata hivyo inaonekana kuwa bado sekta hii kama ilivyo kilio cha watanzania walio wengi na wenye mapenzi mema na taifa hili bado haijaweza kuchangia pato la Taifa kwa kiwango kinachotakiwa.
Mheshimiwa Spika,  Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali hazina ya madini iliyothibitika hadi sasa ni pamoja na Dhahabu tani 222, Nikel tani milioni 209, shaba tani milioni13.65, chuma tani milioni 103, Almasi tani milioni 50.9, Limestone tani milioni 313,  magadi soda tani milioni109, chuma tani milioni 103,  jasi tani milioni 3, phosipahate tani milioni 577, na makaa ya mawe tani milioni 911. Lakini pamoja na kuwepo kwa hazina hii mchango wa sekta hii katika uchumi wa Taifa na maendeleo ya jamii haukidhi matarajio ya wananchi. Aidha miongoni mwa vitu vinavyofanya sekta hii kutochangia vyema ukuaji wa uchumi ni pamoja na misamaha katika  ulipaji wa kodi ya madini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishangaa serikali hii ya CCM kwa kushindwa kufuta misamaha inayotoa kwa makampuni ya uchimbaji wa madini hapa nchini licha ya kwamba jambo hili limekuwa linapigiwa kelele na wadau walio wengi. Kama taifa tunajiuliza na kutaka majibu toka kwa serikali ni nini nia hasa siri ya serikali katika kuendelea kutoa misamaha hii ya kodi.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ripoti ya kodi katika madini iliyotolewa na shirika la International Centre for Tax and Development (ICTD) iliyotolewa mwezi April 2013 inaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinapata pato dogo la mapato ya ndani yanayotokana na madini kwa wastani wa 1:1.3 ikilinganishwa na nchi ya Botswana ambayo inawastani wa 1.32:1 ikifuatiwa na nchi ya Chile. Aidha ripoti hiyo inaonesha kuwa Tanzania ingeweza kufikia kiwango cha nchi ya Chile kama ingekuwa na viwango vya kutoza kodi kama nchi ya Chile kwa sekta ya madini na kuchangia kukua kwa pato la Taifa  endapo ongezeko ya kodi ya thamani, kodi ya kusafirisha na kodi ya mapato zinazotokana na madini zingechangia kupanda kwa pato la Taifa (GDP).
Mheshimiwa Spika, Swala la mrahaba limeonekana kutopatiwa jawabu halisi kwani kiwango cha asilimia 4% kinachotozwa  kwa sasa baada ya kufanyika marekebisho bado ni kidogo. Pamoja na kwamba kamati ya Jaji Mark Bomani kupendekeza kuwa tozo la mrahaba lizingatie ukokotoaji kwa kigezo cha gross value badala ya net back value pendelezo hilo halitekelezwi kwa ukamilifu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuboresha mazingira ya utoaji wa mrahaba pamoja na kodi, ikizingatiwa kuwa baadhi ya makampuni hayafuati sheria ya mpya ya madini ya mwaka 2010 inayotaja kiwango kipya cha mrahaba (Royalty), na kuchukua hatua nyingine za ziada kwa kuzingatia mapendekezo tuliyotoa  2011 na 2012 hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ieleze kwanza ni makampuni gani ambayo hayajaanza kutumia sheria hii mpya, pili ni hatua gani imechukuliwa dhidi ya suala hili lakini pia viwango vya kodi na mrahaba vinavyotozwa vilingane na viwango vinavyotozwa katika nchi nyingine kama Botswana.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mchango wa sekta ya madini katika maendeleo na huduma za jamii (Corporate social responsibility); Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kuwa sekta ya madini inayo kazi ya kuhakikisha maendeleo na huduma za jamii. Katika kufanikisha adhima hii ripoti ya Jaji Mark Bomani ilipendekeza miongoni mwa mambo mengine ni pamoja na wawekezaji kutoa huduma za jamii ili kuimarisha uhusiano na jamii zinazozunguka migodi, wawekezaji washiriki katika mashauriano ya mashauri ili wajue vipaumbele na mirahaba inayokwenda halmashauri itumike katika kuboresha huduma za jamii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mapendekezo hayo lakini hali ya halmashauri ambako makampuni ya uchimbaji wa madini yanakopatikana bado ni wilaya maskini sana. Halmashauri za Kahama, Geita, Tarime hazifanani na thamani ya madini yanayopatikana katika maeneo yao. Pamoja na hayo kuna mkanganyiko katika sheria ya Local Authority Finance Act dhidi ya mikataba na kusababisha halmashauri kukosa haki zake.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kueleza hatua zaidi za makusudi ambazo inachukua kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo na watanzania kwa ujumla wananufaika na rasilimali za nchi hii kwa maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kushughulikia mkanganyiko huo wa kisheria.
Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu tulichokisema mwaka 2011/2012 kuhusiana na ujanja wa makampuni makubwa ya madini “Mheshimiwa Naibu Spika, Ili kuongeza kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi kutokana na uchimbaji wa madini; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutekeleza mikakati ya kupenya kuta za umiliki na mitaji (capital and ownership structures) zilizojengwa kwa muda mrefu na makampuni ya kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria na ushawishi wa kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya madini nchini. Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza bayana hatua ambazo imechukua kufuatia Ripoti ya Tume/Kamati mbalimbali ambazo ziliundwa na Serikali kwa nyakati mbalimbali kwa kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini mapendekezo yake bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake. Mathalani ripoti za karibuni za Kamati ya Masha na ile ya Bomani (2008) zilieleza bayana namna ambavyo makampuni makubwa ya madini yamekuwa yakitumia sehemu kubwa ya uwekazaji wao kama mkopo (debt financing). Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba makampuni hayo yamekuwa yakitumia mianya hiyo ya kisheria na kimikataba kuwezesha wamiliki na wanahisa kupata faida mapema kuliko kuweka mtaji kwa kuwa riba ya mikopo huondolewa katika kukokotoa kodi. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali iwaeleze Watanzania ni trilioni ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995
mpaka 2010 katika kipindi cha miaka 15 ya kuachia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuruhusu asilimia kubwa ya mikopo kuwa mitaji. Aidha, ni hatua gani zimechukuliwa kwa waliohusika kuliingiza Taifa katika mikataba mibovu iliyoruhusu makampuni hayo kujitangazia hasara kila mwaka huku yakipata faida kubwa”.

Mheshimiwa Spika, matatizo ya wachimbaji wadogowadogo wa madini, kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa taifa hili. Kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati ya Jaji Bomani kuhusu namna ya kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogowadogo wa madini, kamati ilishauri muda wa leseni kuongezwa kufikia miaka 10 ili kuwawezesha wachimbaji hao waweze kupata mikopo kutoka taasisi za fedha. Wachimbaji kusaidiwa mbinu kwa ajili ya kupata mtaji wa kufanya shughuli za uchimbaji, kuchangia katika mfuko wa wachimabji wadogowadogo, kuwekwa kwa utaratibu wa kisheria kwa ajili ya kuwakatia bima wafanyakazi wao na kuanzisha taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo kupitia SACCOS zao.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012  pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013, kamati ilithibitisha matatizo ya wachimbaji wadogowadogo kuwa ni pamoja bajeti ndogo inayotengwa kwa wachimbaji, elimu kutotolewa kwa wachimbaji, uhaba wa maeneo ya uchimbaji kwa vile maeneo yao yamechukuliwa na wawekezaji wakubwa, ukosefu wa masoko ya kuuzia bishaa zao na kodi kubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kueleza hatua ilizofanya katika kutekeleza mpango mkakati wake hususan katika matatizo yafuatayo;
(a)           Serikali imeongeza kiasi gani cha fedha kwenye bajeti ya wachimbaji wadogowadogo,  ni utaratibu gani umewekwa ili fedha hizo ziwafikie walengwa?
(b)           Kuna mkakati gani wa kuhakikisha wachimbaji hao wanapata mafunzo ya uchimbaji na masuala yanayolenga kuongeza thamani ya madini yao?
(c)               Maeneo gani na kanda zipi ambapo wachimbaji hawa wametengewa maeneo kutokana na maeneo yao kuchukuliwa na wawekezaji wakubwa?
(d)           Serikali imeweka mfumo gani katika kuhakikisha mchango wa uchimbaji mdogo unajulikana kwenye pato la Taifa?
(e)           Ili kuongeza thamani ya madini, kuna mkakati gani wa wa kuhakikisha kazi hii inafanyika hapa nchini na kuongeza siyo tu thamani bali ajira kwa watanzania?
(f)                Hatua gani zimefanywa na serikali kuhakikisha soko na bei ya madini inakuwa imara na mikakati gani imewekwa ili kuhakikisha umeme unapatikana katika maeneo ya wachimbaji wadogowadogo?

Mheshimiwa Spika, sasa ni takriban miaka sita toka  kuwasilishwa  kwa ripoti ya Mheshimiwa Jaji Mark Bomani kwa Rais. Baada ya kuwasilishwa pia hapa Bungeni na Kamati husika na Bunge likaijadili na mapendekezo yake yakawa ni maazimio ya Bunge. Lakini hadi sasa maazimio ya Bunge bado hayatekelezwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Katika mapendekezo ya tume ya Jaji Bomani ambayo pia yaliridhiwa na Bunge lako tukufu na kupitishwa kama Azimio la Bunge ni pamoja na kufutwa misamaha ya kodi, kwa badiliko alilotoa Waziri wa Fedha la kufuta utekelezaji wa GN  99 kuanzia Julai 2009 kwa makampuni. Marekebisho haya yanahusu kampuni za madini zilizoingia mkataba na Serikali kuanzia July 2009.  Kwa nini ufutaji wa misamaha hii usiyaguse makampuni yaliyokuwepo kabla ya kamati ya Jaji Bomani haijaanza kazi?
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba msamaha ambao unaendelea kutolewa hadi sasa kwa makampuni hayo ya mafuta unaukosesha mfuko wa barabara mabilioni ya fedha na huko makampuni hayo ndiyo yanaharibu kwa kiasi kikubwa barabara zetu. Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Waziri alieleze Bunge ni kwanini maazimio ya Bunge hadi leo hii hayajatekelezwa kikamilifu?
Aidha, Mheshimiwa Spika, mapendekezo mengine ya kamati ya Mheshimiwa Jaji Bomani yalikuwa ni:
1.     Serikali kumiliki hisa ndogo kama kwa kampuni ya Williamson Diamonds Limited ambapo Serikali ina hisa 25%, hali ambayo si sawa kwa umiliki wa kigeni. Upo umuhimu wa ushiriki wa kutosha wa watanzania katika umiliki wa hisa za kampuni za uchimbaji mkubwa.
2.      Shughuli zote za uchimbaji wa vito, na Kampuni za uchimbaji wa kati wa madini mengine, zimilikiwe ama kwa 100% au kwa kiasi kisichopungua 50% na wananchi wa Tanzania.
3.    Shughuli zote za wachimbaji wadogo zimilikiwe na kuendeshwa na watanzania tu.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Serikali itawaeleza watanzania utekelezwaji wa maazimio hayo ya Kamati ya Mhe.Jaji Bomani ambayo yaliridhiwa na Bunge yametekelezwa kwa kiwango.
Mheshimiwa Spika, Utaratibu unaotumika katika kuingia mikataba ya uchimbaji wa madini umewekwa wazi katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Sehemu ya 23 ya Sheria hiyo inaelezea kuhusu kuanzishwa kwa bodi itakayojulikana kama Bodi ya Ushauri ya Sekta ya Madini. Bodi hii inamshauri Waziri anayesimamia madini kuhusu masuala ambayo yako chini ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo yanatakiwa kufikishwa kwenye Bodi.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini imeonyesha udhaifu wa kumnyima hata Mkuguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikia mikataba ambayo Serikali imefunga na wachimbaji ili “kubainisha taratibu ambazo zinafuatwa na Wizara katika kutekeleza matakwa ya sheria hii kwa vile mikataba hii ya Uchimbaji ni ya watu binafsi na ni siri kwa watu wengine wasiokuwa sehemu ya mikataba hiyo. Kutokana na usiri huo, sikupewa haki ya kuipitia mikataba hiyo na hivyo kuzuia wigo wa ukaguzi wangu[4].

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaliomba Bunge katika mjadala huu utakaoendelea kupitisha azimio mahususi kuilazimisha Wizara kuwajibika kwa kuendelea na utekelezaji wa mikataba yote ambayo, kwa njia moja au nyingine imekiuka sheria na pia imekiuka maazimio na ushauri unaotolewa na Bunge. Kwa njia hii tutakuwa tumetimiza wajibu wetu wa Kikatiba wa Kuisimamia na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa spika, mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa bado ni mdogo mno ukilinganisha na jinsi nchi yetu ilivyojaliwa rasilimali hii na uchimbaji unaoendelea sehemu mbalimbali katika nchi yetu. Kwa ujumla madini tuliyojaliwa hayawafaidishi watanzania kwa kiwango kilichotegemewa zaidi ya kuwaingiza kwenye matatizo ya uchafuzi wa kimazingira ugumu wa maisha.

6.1 STAMICO
Mheshimiwa Spika, Shirika la Madini (STAMICO) linaimarishwa upya na serikali baada ya kuondolewa kutoka kwenye orodha ya mashirika ya umma yanayotakiwa kufutwa mwezi Machi, 2009. Hivyo lilipewa majukumu makuu manne, ambayo ni:
a.     Kuwekeza katika utafutaji,uendelezaji na uchimbaji wa madini
b.     Kusimamia hisa za serikali katika migodi
c.     Kuratibu uendelezaji wa wachimbaji wadogo nchini, na
d.     Kutoa huduma za kibiashara katika sekta ya madini, huduma hizo ni uchorongaji wa miamba, utafutaji wa madini na utoaji ushauri katika masuala ya madini.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya shirika liyowasilishwa kwenye kamati ya madini na nishati, inaeleza kuwa Bodi ilimaliza muda wake  mwezi Juni, 2012. Hivyo basi shirika hilo halina bodi hai. Kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti ameongelea kitendo cha Mwenyekiti wa Bodi kuingilia moja kwa moja utendaji wa shirika hilo kiasi kwamba, shirika limekuwa likimlipa posho ya mafuta Mwenyekiti huyo sawa na lita 100 za mafuta kila wiki, asilimia 40 ya posho ya mafuta kama fedha za matengenezo kila wiki na shilingi 500,000/= kwa mwezi kama fedha za mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, msuguano huu wa kiutendaji kati ya mkurugenzi mtendaji na Mwenyekiti wa bodi kwa kiasi kikubwa inadumaza utendaji wa shirika. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwachukuliwa hatua za kinidhamu Wenyeviti wenye tabia kama hii kwani malipo hayo ni aina nyingine ya matumizi mabaya ya raslimali za umma ambayo yanapaswa kudhibitiwa.

Mheshimiwa Spika, STAMICO ndiyo yenye dhamana ya uendelezaji wa Mgodi wa Buhemba, kwani tangu mwezi Julai, 2011 shirika lilipewa leseni ya utafutaji wa madini juu ya eneo la mgodi wa zamani wa dhahabu wa Buhemba, mkoani Mara kwa kumiliki asilimia 40 za mgodi huo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli kwamba mgodi huu wa Buhemba ndio uliokuwa ukimilikiwa na kampuni ya MEREMETA kampuni ambayo mbali ya kuiingiza nchi kwenye kashfa bali pia iliwaacha wananchi/ wachimbaji wadogo wa eneo la Buhemba wakiwa na malalamiko ya kutokulipwa fidia kwa kutwaliwa maeneo yao. Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuelewa je STAMICO inamkakati gani wa kwanza kuchukua mali zilizokuwa zinamilikiwa na MEREMETA? Na pili madai ya wananchi wanayalipa vipi kwa pamoja na mbia wake?

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ushauri ulipotolewa na Mkaguzi kuhusu ushiriki wa Sekta ya Umma na Sekta binafsi kugubikwa na mapungufu makubwa ambapo faida inakuwa kwenye upande wa pili zaidi na Serikali. Mfano ni ubia wa SONGAS Ltd, IPTL ltd, Kiwira Coal Mines (TANPOWER LTD), TICTS na kadhalika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwahakikishie watanzania ni kwa kiwango gani ubia huo wa STAMICO na MANJARO RESOURCES Pty Ltd kutoka Australia  utakuwa na tija kwa taifa?

6.2 WAKALA WA UKAGUZI WA MADINI-TMAA

Mheshimiwa Spika, wizara ya nishati na madini 08 desemba, 2011 ilitoa  taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya sekta ya madini.
Mrabaha uliolipwa na migodi mikubwa ya dhahabu katika kipindi hicho cha kuanzia mwaka 1998 hadi 2010 ilikuwa ni Shilingi Bilioni 341.57, wakati hadi kufikia mwaka 2010 kulikuwa na Watanzania 6,129 walioajiriwa rasmi kwenye migodi mikubwa 6 ya dhahabu. PAYE wanayolipwa ya kati ya asilimia 14 mpaka 30 kutegemea kiwango cha malipo.

Mheshimiwa Spika, ili kufanya ulinganisho ulio sahihi wa kama kweli mchango wa sekta ya madini kwenye kodi unatokana na mrahaba au kodi ya PAYE wanayolipa waajiriwa hao 6,129 ilitakiwa tuambiwe ni kiasi gani, kwani kuna uwezekano mkubwa PAYE inazidi kwa mbali fedha inayoingia itokanayo na mrahaba.

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ndiye mwenye dhamana katika kudhibiti uzalishaji wa madini na ukusanyaji maduhuli yatokanayo na mrahaba kwa kampuni za uchimbaji madini. Hata hivyo, TMAA haina udhibiti wowote katika uzalishaji na uthamanishaji wa madini kwa wachimbaji wadogo na wa kati ambao wameachwa kueleza wenyewe kiasi cha madini wanachozalisha.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli huo, ni kwa vipi Wizara inataka kuliaminisha Bunge kuwa takwimu za madini hasa dhahabu  zilizozalishwa hapa nchini kuwa ni sahihi?

Mheshimiwa Spika, mapungufu haya kwa kiasi kikubwa yanatokana na ukweli kwamba “control mechanism” kwa wachimbaji wadogo wakati wa kutoa leseni umegubikwa na matumizi mabaya na udanganyifu ambapo watu wachache  wamehodhi maeneo mengi na kuajiri wachimbaji wadogo na kinachopatikana kutokana na machimbo hayo Serikali inanyimwa taarifa. Pia kushindikana kwa udhibiti ni viwanja vidogo vya ndege vilivyotapakaa hapa nchini ambavyo TMAA haina udhibiti navyo.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba Serikali imechukua hatua zingine za kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini ni pamoja na:
1. Kutenga maeneo maalum ya wachimbaji wadogo;
2. TANSORT kuhamishia rasmi shughuli zake hapa nchini kutoka Uingereza mwezi Agosti, 2010;
3. Upigaji marufuku wa usafirishaji nje ya nchi madini ghafi ya Tanzanite yenye ukubwa unaoanzia gramu moja na kuendelea mwezi Aprili, 2010;
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge tangu kitengo hicho cha kuchambua almasi kirudishwe hapa nchini toka Uingereza ni kiasi gani cha fedha kimepatikana kutokana na kazi zake hizo?
Mheshimiwa Spika, yamekuwepo madai ya wachimbaji wadogo wadogo ambao ndiyo wazawa kunyimwa leseni katika maeneo yao ya uchimbaji na maenea yao kugawiwa kwa wanaojiita wawekezaji na wao wakihamishwa hamishwa pasipo kupatiwa maeneo mbadala.
Mheshimiwa Spika, Kuna matatizo mengi ya wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo ya Kalalani Tanga, Mgusu, Nyarugusu, Mtakuja Geita, Winza Mtakanini Mpwapwa, Simangulu Chamwino, North Mara, Rwamgasa, Kasema,Kilindi Nyamongo na kadhalika. Hivi karibu ni wachimbaji wapatao 400 wa kijiji cha Nkongilangi wanaochimba eneo la Machimbo ya Sekenke-Iramba Magharibi, ambao toka mwaka 1982 wamekuwa wakiomba leseni lakini hawapatiwi majibu ya maombi yao. Mwaka 2007 waliomba tena na kuambiwa leseni imetolewa kwa kampuni ya WASEKE, kwa mshangao mkubwa mwaka 2011 alikuja mtu anayedai kuwa ndiye mmiliki wa eneo hilo la uchimbaji mdogo la kijiji cha Nkongilangi aitwaye “JOHN BINA”. Na hapo ndipo matatizo na unyanyasaji ulipoanzia na kusababisha uporaji na vifo kutokea[5].
Mheshimiwa Spika, katika mazingira kama hayo, wachimbaji wadogo wapatao 3000 kwa ushirika wao wilayani Maswa baada ya kulipia ada ya maombi yao imechukua takriban miezi minne baadae wakajibiwa kuwa eneo hilo tayari lilikuwa na mmiliki toka mwaka 2002.  Lakini baada ya kuangalia coordinates zilizosemwa kwenye barua na zile zilizoko kwenye ramani, ni kwamba leseni PL 4233/2007 ambayo mmiliki wake ni SAVANNAH EXPL. Ltd iliyotolewa tarehe 02/05.2007 na eneo lake liko Luguru na Luguru ni kijiji kilicho ndani ya wilaya ya Bariadi na sio Maswa. Huu ni mkakati unaotumiwa na watendaji Idara ya Madini kwa kushirikiana na wenye dhamana katika Serikali kuwanyima haki wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza wachimbaji fedha zilizotengwa kiasi cha shilingi bilioni moja kama kianzio cha Mfuko wa kuendeleza Wachimbaji wadogo nchini, kama hotuba ya Waziri Mkuu Mhe. Mazengo Pinda alivyosema Bungeni wakati akiwasilisha mapitio na makadirio ya matumizi ya fedha yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2010/2011 zilipewa wachimbaji wadogo wa wapi?
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa mujibu wa maneno ya Mhe Naibu Waziri Madini  wakati akijibu swali tarehe 22 April 2013 alisema “SERIKALI inatarajia kukamilisha taratibu za Mfuko rasmi wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini, ili kuwawezesha kupata mikopo, ikiwa ni pamoja na kuwapatia mikopo ya vifaa vya kuchimbia kwa kanda zote nane zinazochimba madini nchini”.
 Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza mfuko huo ambao umekwisha tengewa fedha na hapa Naibu Waziri anasema inatarajia kukamilisha taratibu  rasmi za mfuko huo, hii maana yake nini? Na mfuko huo utaendeleza wachimbaji gani wakati ambapo maeneo mengi wana malalamiko ya leseni na wanafukuzwa ovyo kama mifano ambayo tumeitoa hapo juu.
Mheshimiwa Spika, Kwa wale walio na maeneo ya kuchimba madini wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kuwa na mtaji mdogo unaowafanya washindwe kupata zana bora kwa ajili ya uchimbaji. Aidha, watoto wa walalahoi wamekuwa wakiajiriwa katika migodi mbalimbali nchini mbali ya kuwa na sheria inayopinga ajira kwa watoto hususan katika maeneo ya migodini.
Mheshimiwa spika, Kitendo cha serikali kupandisha kodi mara kawa mara kwa wachimbaji au wawekezaji wadogo wadogo ni kufanya wawekezaji wadogo wasimudu kushiriki kikamilifu katika kuwekeza ndani ya sekta ya Madini wakati serikali inajigamba kuwasaidia wawekezaji hao huku serikali ikipandisha kodi kutoka 80,000/= hadi 1,000,000/= kwa wachimbaji hao.
Mheshimiwa spika, Jambo hili ambalo pia lililalamikiwa na wabunge wengi limeonekana limetafsiriwa kuwa ni mkakati wa makusudi wa kuwafukuza wawekezaji wadogo wadogo katika sekta hii na kutoa mianya kwa wawekezaji wenye pesa zao kuendelea kuwekeza katika sekta hii ya madini.  Kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali kieleze kwa kina ni kwa jinsi kani itawasaidia wachimbaji wadogo kama gharama za uendeshaji wa migodi hiyo zinapanda bila kuzingatia hali halisi ya wachimbaji hao. Hii ni hatari sana kwani tunafanya wazawa washindwe kunufaika na sekta hii moja kwa moja.
Mheshmiwa spika, Katika kuboresha sekta hii ya madini kamati ilishauri mambo yafuatayo yafanyike:
Ø  Serikali kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kushiriki katika shughuli za kutoa huduma(supply)mbalimbali migodini
Ø       Sheria ya ajira kwa watoto isimamiwe  ipasavyo
Ø  Migodi mikongwe ilipe kodi(corporate tax)
Ø  Kuwepo kwa soko la pamoja la madini
Ø  Kutenga  maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika kila kanda na kusimamia vizuri zoezi la ugawaji wa leseni
Ø  Serikali iwasaidie wachimbaji wadogo iliwaweze kapata mikopo ya kuwawezesha kuanzisha viwanda vidogo vitakavyowasaidia kuongeza thamani ya madini yao
Ø  Serikali kukomesha biashara haramu ya madini
Hata hivyo serikali haijayafanyia kazi kwa ukamilifu mapendekezo hayo ya kamati katika mwaka wa fedha 2012/2013 na bado sekta hii inakumbwa na hali ileile na kuifanya iendelee kutokuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Mheshimiwa spika, Taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za serikali  ulioishia 30 Juni, 2012 inaonesha kuwa Wizara ya Nishati na Madini imeliingizia taifa hasara ya zaidi ya shilingi 20,000,000,000 katika sekta ya madini. Hasara hiyo kama ilivyooneshwa kwenye taarifa ya CAG ilisababishwa na malimbikizo ya maduhuli ambayo hayakuonyeshwa Sh.1,645,582,899.Taarifa za fedha zilizowasilishwa na Wizara hazikuonyesha malimbikizo ya maduhuli yenye jumla ya Sh. 1,645,582,899/- kama ilivyotakiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
Mheshimiwa spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inashangaa ni kwa sababu gani hasa bado sheria ya zamani inaendelea kutumika wakati tayari sheria ya mwaka 2010 imeshaanza kufanya kazi. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka Wizara ieleze kwanini hali hiyo imejitokeza na hatua gani inachukua dhidi ya watendaji waliohusika katika kulipatia hasara hiyo?

Kambi Rasmi ya Upinzani pia inaitaka serikali kutumia sheria mpya ya kukusanya mrahaba katika kampuni za madini na hivyo makampuni yote yaliyolipa mrahaba huo kwa kutumia sheria ya zamani yalipe sehemu iliyobakia kwa mujibu wa sheria mpya.
Pamoja na hayo tunaitaka serikali ilitaarifu bunge lako tukufu kuhusu malimbikizo ya maduhuli ambayo hayakuoneshwa kwenye taarifa za mahesabu ya wizara hii, tunataka tujue serikali inampango gani na fedha hizi ambazo ni zaidi ya 1,000,000,000/=.

Mheshimiwa spika, mambo mengine yanayo sababisha hasara katika sekta ya madini ni pamoja na kutokuwa na udhibiti wa mapato ya wachimbaji wadogo wa madini na kutokuwa na udhibiti katika viwanja vya ndege. Udhibiti mdogo katika sekta hii ya madini kumesababisha kupotea kwa mapato mengi ambayo nchi ingeyapata kutokana na madini yanayosafirisha bila kulipa kodi na biashara haramu ya madini inayoendelea nchini.
Mheshimiwa Spika, Pia kwa mujibu wa taarifa ya CAG hukuna ushirikianao kati ya wizara na TRA na hivyo kodi nyingi zinashindwa kukusanywa kutokana na TRA kukosa taarifa sahihi juu ya vyanzo vya mapato vya wizara hiyo.
Mheshimiwa spika, utekelezaji wa ahadi nyingine  za Waziri wa Nishati na Madini  katika bajeti ya 2012/2013; Waziri wa Nishati na Madini katika majumuisho yake aliahidi Bunge kuwa kuna madini ya VANADIUN na PGE yanayopatikana katika madini ya Copper na Nickel. Hilo atalifanyia kazi suala la wawekezaji wanaochukua leseni ya Copper na Nickel kwani kuna upatikanaji wa madini ya VANADIUM na PGE ambayo inasemekana kuwa yanathamani kubwa kuliko Copper na Nickel. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kueleza juu ya utekelezaji wa suala hili kama waziri alivyoahidi bungeni wakati wa kuhitimisha hotuba ya  bajeti ya wizara yake ya mwaka wa fedha 2012/2013
 Mheshimiwa spika, katika suala la mkopo wa billion 8.9 kwa wachimbaji wadogo kwamba ni kwa vipi wachimbaji wadogo wangepewa mikopo hiyo wakati kwa wakati huo leseni nyingi na maeneo yote wamepewa wawekezaji wakubwa, Mh. Waziri aliliambia bunge kuwa lesini hizo zinaisha muda wake, na zikiisha muda wake wawekezaji wakubwa wanaacha nusu ya eneo walilokuwa wanamiliki na hivyo maeneo haya wanapewa wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa spika, katika suala hilohilo la wachimbaji wadogo wadogo ilijitokeza pia hoja kutoka kwa wabunge, waliomuuliza Waziri wa Nishati na Madini jinsi gani mkopo wa billion 8.9 uliopangwa kuwanufaisha wachimbaji wadogo wadogo nchini utagawiwa kwa wachimbaji husika. Waziri alijibu wanatakiwa waunde vyama vyao kila mkoa na wawe na chama chao kitaifa ambako ndiko mkopo huu utaelekezwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali itupe takwimu sahihi mpaka sasa tathmini ikoje juu ya leseni za wawekezaji wakubwa kuisha muda wake na wawekezaji wadogo kupewa maeneo husika na je mkopo wa billion 8.9 umewanufaisha wachimbaji wadogo wadogo wangapi mpaka sasa? Na Kama wachimbaji wadogo hawajanufaika na mkopo huu serikali itueleze fedha hizi zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili ya kazi hii zimefanyiwa nini?
Mheshimiwa spika, kuhusu madeni ambayo wawekezaji katika sekta ya madini wanadaiwa na serikali, Naibu Waziri Wa Nishati na Madini wakati wa mjadala wa bageti ya mwaka 2012/2013 alipokuwa anajibu hoja ya madeni ambayo wawekezaji katika sekta ya madini walikuwa wanadaiwa tangu mwaka 1997 hadi mwaka 2005 aliliahidi bunge kwamba kampuni ya BARRICK ambayo ndiyo kampuni pekee iliyokuwa inakataa kulipa deni lake atalifanyia kazi swala hilo na kuhakikisha wanalipa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali ieleze kama madeni yote yamelipwa kwa kuzingatia sheria mpya ya madini ambayo pamoja na mambo mengine inataka mirahaba kulipwa kwa asilimia nne [4%] kabla ya makato ya makato ya Kodi.  Na kama kuna makampuni hayataki kutii sheria hii mpya ya madini kwa nini serikali isiyafutie leseni ya kufanya kazi za uchimbaji wa madini nchini ? Kwa sababu nchi haiwezi ikavumilia wawekezaji ambao hawatii sheria za nchi.
Mheshimiwa spika, Pia Naibu Waziri alikiri mbele ya bunge lako tukufu kuwa mgodi wa BUZWAGI haujalipa kodi ya kampuni yaani (Corporate tax), na kuahidi kuwa mgodi wowote mpya utaoanza kuanzia wakati huo serikali itaanza kuwa na share ya 15% kama hisa za kubeba (free carried interest).
Tunaitaka serikali ilieleze bunge lako tukufu na umma wa watanzania kwa ujumla wake kama mgodi huo umelipa kodi hiyo na serikali imejipangaje kumiliki hisa kwenye migodi inayotegemewa kuanzishwa na hii ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kuwa na udhibiti wakati  kwa kuzingatia masharti ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inatoa haki hiyo ya Serikali kuwa na hisa.
6.3 UCHIMBAJI MADINI AINA YA URANI
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa swala la uchimbaji na utafutaji wa madini ya aina yeyote lipo chini ya wizara ya nishati na madini , na kwa kuwa swala la uchimbaji wa madini ya aina ya urani kama taifa tunahitaji kuwa na angalizo kubwa ikiwa ni pamoja na kutochimba madini hayo ya aina ya urani kutokana na uhatari wake kwa maisha ya binadamu, na kwa kuwa kambi rasmi ya upinzani kwa mara kadhaa ndani ya bunge hili imekuwa ikitoa maoni yenye nia njema na maisha ya watanzania na viumbe vingine na kwa kuwa tatizo la serikali kutokubali kufanya maamuzi ya kubadili mtazamo wa kutegemea uchumi wa urani na kujikita katika uchumi wa rasilimali mbadala ambazo taifa letu limebarikiwa kuwa nazo.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la mbarang’andu katika wilaya ya Namtumbo ambapo kampuni ya Game Frontiers iliyojipatia kitalu hicho kwa ajili ya uwindaji kwa mujibu wa sheria imeamua kufanya biashara ya kuruhusu utafiti wa uchimbaji madini aina ya urani kinyume na taratibu za uendesahji wa vitalu vya uwindaji.
Mheshimiwa Spika,katika bunge hili mnamo Tar 28/07/2012 zilitolewa taarifa hapa ndani ya bunge hili kwa vielelezo kutoka kwa msemaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu maswala ya ardhi Mhe. Halima Mdee juu ya kampuni ya Game Frontiers kukodisha kitalu chake cha uwindaji kwa ajili ya utafutaji wa madini ya urani katika eneo la mbarang’andu katika wilaya ya Namtumbo.
Mheshimiwa Spika, lakini pia msemaji wa kambi rasmi ya upinzani alitaka kupata ufafanuzi kwa Waziri juu ya maagizo yaliyotolewa na Naibu Spika wakati wa majumuisho ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, maagizo husika yalitaka Wizara ya Nishati na Madini, wakati wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi itoe maelezo juu ya mkataba ulioingiwa tarehe 23 Machi, 2007 kati ya Uranium Resources PLC na Western Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited. Mkataba ambao, pamoja na mambo mengine una ihalalishia Game Frontiers Limited kupata malipo toka kwa makampuni yanayofanya utafiti katika kitalu cha uwindaji katika kijiji cha Mbarang‘andu.

Mheshimiwa Spika, majibu ya waziri yalikua kama ifuatavyo nanukuu …..“Mheshimiwa Spika, lingine lililoulizwa na Kambi ya Upinzani hasa Mheshimiwa Mdee, huu mkataba wa siri, kweli tumeufuatilia mkataba wa siri, ule wa uchimbaji wa uranium”…. Kuonesha waziri alikiri mbele ya bunge na kuahidi kulitafutia ufumbuzi swala hilo, na kuwa ataleta taarifa kwa mtoa hoja.
Mheshimiwa Spika,kwa mara nyingine tena kambi rasmi ya upinzani bungeni inataka kujua ni vipi wizara ya nishati na madini imeshughulikia swala la kampuni ya uwindaji ya Game Frontiers kukodisha kitalu chake cha uwindaji kwa ajili ya utafutaji wa madini ya urani katika eneo la Mbarang’andu wialayani Namtumbo, lakini pia serikali iwaambie watanzania kwa hatua ilizochukua za kuchimba urani ni vipi itaweza kuwalinda dhidi ya madhara ya uchimbaji wa madini hayo?

6.4 MGODI WA KIWIRA
Mheshimiwa Spika, kati ya kashfa ambazo ziliikumba serikali ya awamu ya tatu ya Rais Mkapa ilikuwa ni pamoja na kubinafsishwa kwa mgodi huu wa Kiwira  
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu za bunge lako tukufu, bunge lilipitisha maazimio yake juu ya taarifa ya kamati ya Nishati na Madini kuhusu ubinafisishaji wa mgodi wa kiwira kufuatia mapendekezo yaliyokuwa yameelekezwa serikalini kwa ajili ya hatua stahiki, miongoni mwa maazimio ya bunge ambayo hayakufanyiwa kazi na serikali yalikuwa ni pamoja na;
i.      Urejeshwaji wa vifaa na mali ambavyo vimeibiwa au kuhamishwa kutoka kwenye miundombinu ya mgodi wa kiwira
ii.     Bilioni 17 zilizotolewa na serikali  kwa ajili ya ukarabati wa miundomninu ya mgodi, serikali ilitakiwa kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha hizo kupitia kwa Mthibiti na Mkaguzi wa Hesabu za serikali ili kujua matumizi halisi na halali ya fedha za umma
iii.    Serikali kufuatilia uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU wa shilingi milioni 50 zilizotolewa kutoka mfuko wa Consolidated Holdings Corporation
iv.    Kuwalipa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira  mafao yao na stahiki zao kwa wafanyakazi ambao CAG alithibitisha kuwa hawakulipwa
v.     Serikali kukamilisha haraka zoezi la kukabidhiana mgodi huo
vi.    Serikali kueleza kigezo kilichotumika kuwalipa viongozi waandamizi  kiasi cha shilingi milioni 80 wakati wafanya kazi wa kati walilipwa  kati ya shiligi milioni 8 na wafanya kazi wa chini  wakilipwa shilingi milioni moja na nusu.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo halijafanyiwa kazi lilikuwa ni hili la malipo yaliyolipwa mara mbili, kwa mjibu wa hansard za bunge , maoni ya wabunge yalikuwa ni … “niligusie hili la dola milioni nne na laki nane na sitini na tano ambazo ni sawa na bilioni tano na laki sita, serikali imekiri…imefanya double payment jambo ambalo ni kosa la jinai, … mwenzangu anadai tuachane nayo, haiwezekani” lakini katika hali ya kustaajabisha hadi hivi leo haijulikanai hatima ya fedha hizo zilizolipwa mara mbili. Ni maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuwa serikali ihakikishe maoni yote yanafanyiwa kazi , fedha za walipa kodi haziwezi kupotea hivihivi kwa wajanja wachache.
Kambi rasmi ya Upinzani, inataka maelezo ya kina kuhusiana na mambo yafuatayo;
i.              Fedha za mwaka jana zilitengwa Bilioni 40 na zilitumika Bilioni 28 kulipa fidia, je fedha hizo alilipwa nani na zilikuwa ni kwa ajili gani?
ii.             Mwaka huu tumetenga tena bilioni 20 je, ni kwa ajili ya kuendelea kufidia ufisadi huu ? au ni kwa ajili ya kazi gani?

7.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Maoni yetu juu ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2012/2013 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 yanaonyesha kwamba chanzo cha hali tuliyonayo hivi sasa ni cha muda mrefu. Bunge la tisa likiongozwa na Spika Samuel Sitta halikuweza kukamilisha kurekebisha hali hiyo, ikiwemo kukwepa kukamilisha kwa wakati maazimio ya Bunge ya mwaka 2010. Bunge la kumi, likiongozwa na Spika Anna Makinda katika kipindi chake cha kwanza cha miaka miwili na nusu, halijaweza kukamilisha utekelezaji wa maazimio ya mwaka 2008 na maazimio yake ya mwaka 2011 na 2012. Bunge hili, bado linalo nafasi ya kurekebisha hali hii kuanzia sasa katika kipindi chake cha miaka miwili na nusu iliyobaki.

Mheshimiwa Spika, mwalimu nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE ukurasa wa pili (2) aya ya 4 kinasema nanukuu “Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa,au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga pia ni unafsi. Pengine twaweza kuwa hatuna cheo cochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tama yoyote ya kupata cheo Fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila bindamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tama hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana. Ni kweli kwamba demokrasia haiwezi kudumu ikiwa wachache hawatakubali matakwa ya wengi, lakini matakwa ya wengi hujulikana katika majadiliano au mazungumzo ya wazi wazi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika ukurasa wa tatu (3) aya ya pili anasema nanukuu “Kadhalika, matakwa ya wachache hujulikana katika majadiliano na na mazungumzo. Bila wale wachache kusema wazi wazi matakwa yao, majadiliano hayana maana. Wakati mwingine, hata baada ya majadiliano, wachache japo wamekubali kutii uamuzi wa wengi wanaweza kuendelea kuamini kwamba mawazo yao ni sawa, na ya walio wengi yamepotoka. Democrasi inawapa haki, na ukweli unawapa wajibu wa kuendeleza mawazo yao mpaka wengi waone kuwa ni ya kweli.Bila hivyo maendeleo katika mawazo hayawezekani, kwani mara nyingi wazo zuri hutokana na mtu mmoja tu. Mwanzo laweza likapigwa, pengine kwa nguvu kabisa,na walio wengi, lakini hatimaye wengi hulikubali. Huu ndio msingi wa maendeleo katika mawazo ya binadamu”.

Mheshimiwa Spika,  Katika sekta za Nishati na Madini, kama ilivyo katika sekta nyingi nchini; tumefika hapa tulipo kwa sababu ya udhaifu wa Serikali inayoongozwa na Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na ulegelege wa CCM. Kambi Rasmi ya upinzani inayoongozwa na CHADEMA inataka kama taifa; TUBADILIKE, TUWAJIBIKE, TUJISAHIHISHE.

Mshimiwa Spika,  Naomba kuwasilisha.

John John Mnyika (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Nishati na Madini
22.05.2013




1 comment:

  1. shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa wema wake na wema juu ya maisha yangu nini i wamefanya kama si kwa Bibi Kate Lisa ambaye i daima kuona kama Mungu alimtuma mwanamke ambaye Mungu wamechagua kuwasaidia watu walio katika haja ya fedha kama mimi maskini mjane ambaye alikuwa short waliotajwa, na short wa fedha mwanamke ambao wana watoto wawili na ana majukumu mengi mwanamke ambaye alipoteza mume wake na ina kulipa bili yenye kodi ya nyumba na umeme bili zote mbili na ilikuwa scammed Jumla ya $ 4,000 uSD i kamwe kuamini kwamba bado kuna legit mkopo kampuni online ambao bado wanaamini kwamba watu ni katika tatizo la kifedha na tayari kusaidia baada ya kuwa scammed $ 450,000 uSD i kamwe kuamini kwamba bado kuna legit mkopo kampuni ya mpaka i alimkuta baada ya kuwa alikuwa posted na moja Bibi Luis juu ya jukwaa hiyo yeye alielezea jinsi yeye alipata mkopo wake kutoka Bibi Kate Lisa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Bibi Kate Lisa nyumbani mkopo na kisha i mara baada ya hakuna chaguo zaidi kuliko kujaribu bahati yangu kwa wakati wa tatu ili kuepuka kupoteza nyumba yangu (malazi ) ili i kufikiri juu yake i alikuja na hitimisho kwamba i unapaswa kujaribu tena hivyo i kuwasiliana Bibi Kate Lisa kupitia barua pepe wao walihudhuria kwangu katika chini ya 10mins i kutumika kwa ajili ya mkopo jumla ya $ 95,000,00 dola mkopo kupitishwa na ya chini kiwango cha riba na baada ya usindikaji i got mkopo wangu katika akaunti ya benki yangu jana hivyo i unataka haraka kutumia kati ya ushauri yoyote mtafuta mkopo huko nje kuwasiliana na Bibi Kate Lisa email mrskatelisaloanhome1@gmail.com yeye dhahiri kukupa mkopo unahitaji bila matatizo yoyote kwa mara nyingine tena , shukrani kwa Mungu kwa huruma yake juu ya maisha yangu. i itakuwa kuangalia mbele na kusikia ushuhuda wako mwenyewe tu kama yangu.

    Bibi Sarah .

    ReplyDelete