Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuwa waangalifu na kuchukua hatua kwa kujilinda dhidi ya watu wasiowatakia mema ambao wanaweza kuwashambulia kutokana na kazi zao za kila siku wanazozifanya ndani ya jamii.
Kadhalika, imeelezwa kuwa idadi kubwa ya waandishi wa habari ni waadilifu, ingawa wapo wachache wasio na uadilifu ambao wanatumiwa na watu kuwaangamiza wenzao. Ushauri huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Nchini (MOAT), Dk. Reginald Mengi, alipofungua mkutano wa siku moja uliowashirikisha watetezi wa haki za binadamu, walimiki wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari nchini.
Dk. Mengi alisema waandishi wa habari wanakumbana na matatizo mengi kupitia kazi wanazozifanya kila siku katika jamii na kuongeza kuwa wanatakiwa kujilinda wao wenyewe na kuachana na tabia zinazoweza kuwatumbukiza kwenye hatari.
Bonyeza Read More Kuendelea
Alitaja baadhi ya maeneo ambayo yanaweza kumtumbukiza katika hatari mwaandishi kuwa ni pamoja kukaa baa mpaka nyakati za usiku bila kujua anafikaje nyumbani kwake ama watu gani anaweza kukutana nao wakamdhuru.
Alisema hakuna kazi yoyote kubwa na ya thamani kuzidi uhai wa mwandishi na kwamba anatakiwa kujilinda kwanza kabla ya kufanya kitu chochote kilicho mbele yake wakati akitekeleza majukumu yake. Akizungumzia uadilifu wa waandishi wa habari, Dk. Mengi alisema idadi yao kubwa wanafanya kazi vizuri isipokuwa wapo wachache wanaotumiwa na watu wasiokuwa waadilifu kufanya mambo mabaya.
Alisisitiza ndani ya vyombo vya habari kuna waandishi wananunuliwa na watu wenye fedha ili watoe siri mbalimbali zinazohusu chombo husika na kwamba tabia hiyo inahatarisha maisha ya wenzao.
“Inakuja stori kubwa ndani ya chombo cha habari na stori kubwa inayohusu mtu fulani, chombo cha habari kinaamua kuficha jina la mwandishi, lakini mwandishi asiye mwadilifu anatoa siri nani aliyeandika hiyo stori,” alisema Dk. Mengi.
Aidha, Dk. Mengi alisema ndani ya Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa taifa pia kuna watu waadilifu ambao ndiyo wengi, lakini pia kuna wachache wasiokuwa waadilifu. Kutokana na hali hiyo, Dk. Mengi alivitaka vyombo vya habari na watetezi wa haki za binadamu nchini kuwatumia watumishi hao waadilifu kufichua maovu yanayotendeka.
“Kuna polisi ambao hawachukui rushwa, wasiotesa watu na hawa wasiwekwe kwenye kundi moja la watu wabaya kwani wakiwekwa hivyo wananchi wanaweza wasituamini,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Mengi, kuna watu hapa nchini wanatumia fedha zao kuwatesa watu wanaopinga vitendo vya rushwa na kuwasisitiza waandishi kuandikia ukweli ambao utawaepusha na lawama. Aidha, Dk, Mengi alisema ukweli utawaweka huru waandishi na kutawataka wafuatilie stori walizoanza kuziandika badala ya kuziacha ziishie njiani.
Mwenyekiti wa mtandao huo wa utetezi wa haki za binadamu, Martina Kabisama, aliwakumbusha waandishi wa habari wanaopata nafasi za uteuzi wa Rais kutobadilika na kusahau mambo ya msingi waliyokuwa wakiyafanya na kuyapigania wakati wakiwa waandishi wa habari.
Alisema uzoefu unaonyesha hata wanaharakati mbalimbali walio mbele kutetea haki za wengine wakipewa ubunge wanabadilika na kusahau waliyokuwa wakiyasema kabla.
Aliwataka kuacha kugeuka na badala yake waendelee kufanya yale waliyokuwa wanayafanya kabla ya kuchaguliwa ama kuteuliwa kushika nafasi mbalimbali ndani ya serikali au kuwakilisha wananchi.
Katika mkutano huo waandishi wa habari walipata fursa ya kuchangia mawazo yao ili kupata njia sahihi za kujilinda kupitia kazi wanazofanya katika jamii. Kwa mujibu wa mtandao wa kutetea haki za binadamu duniani, kila siku waandishi wa habari 30 duniani wanauawa katika matukio mbalimbali yanayohusiana na kazi wanazozifanya.
No comments:
Post a Comment