KAMBI ya Upinzani bungeni imeibua ufisadi wa mabilioni ya fedha unaolihusisha Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Shirika hilo linadaiwa kuingia ubia na kampuni binafsi ya Power Pool East Afrika Ltd na hivyo kuwezesha kumpuni hiyo kupatiwa mkopo wa zaidi ya Sh bilioni 217 kutoka Benki ya Exim ya China kwa dhamana ya Serikali.
Mkopo huo uliombwa kwa ajili ya kampuni hiyo kuendesha mradi wa kuzalisha umeme wa upepo mkoani Singida.
Taarifa hiyo ilitolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani bungeni, Highness Kiwia, wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Katika taarifa hiyo, kambi hiyo ilihoji uhalali wa NDC kuingia ubia na kampuni hiyo, huku wamiliki wa kampuni hiyo wakitajwa kuwa na uhusiano na vigogo wa CCM (majina tunayo).
“Kwa mujibu wa randama ya wizara uk. 55 na nukuu. Wizara inaendelea kushughulikia upatikanaji wa fedha Dola za Marekani milioni 136 kutoka Exim Bank ya China, ambayo imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu na tayari ridhaa ya Serikali imewasilishwa Exim Bank na wizara ya fedha.
“Kambi ya upinzani bungeni, inataka kujua Kampuni ya Power Pool EA iliwezaje kupata ubia huu na NDC na ni kwa nini NDC kwa kushirikiana na Serikali ndiyo imeenda kutafuta fedha za mradi huu kwa kutumia guarantee ya Serikali?
“Waziri aweke wazi wamiliki wa Power Pool EA, maana habari za kuaminika zinaonyesha kuwa wamiliki wa mradi huu ni ndugu na jamaa wa wabunge na mawaziri wa CCM,” alisema.
Mradi huo uliopo kilomita 12 mashariki mwa Halmashauri ya Singida, unatarajiwa kuzalisha megawati 300, lakini utaanza kuzalisha megawati 50.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda, aliwasilisha bajeti ya Sh bilioni 108 kwa ajili ya kuendeleza sekta ya viwanda, biashara na viwanda vidogo vidogo.
Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 29 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni 78 zimeombwa kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo.
Dk. Kigoda alisema katika fedha za matumizi ya kawaida Sh bilioni 22 zimetengwa kwa ajili ya mishahara (PE) na Sh bilioni zimetengwa kwa matumizi mengineyo (OC).
Kiwanda cha General Tyre
Katika hotuba hiyo, Dk. Kigoda alisema wizara yake ipo katika hatua za kufufua kiwanda cha General Tyre, kifanye uzalishaji wa matairi.
Bonyeza Read More Kuendelea
Dk Kigoda alisema mpango wa ufufuaji wa kiwanda hicho upo katika hatua nzuri na kwamba jitihada hizo zinafanywa na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).
“Wizara kupitia shirika la NDC imekamilisha ukarabati wa baadhi ya majengo ya kiwanda pamoja na kuandaa mpango wa biashara (Business Plan).
Dk. Kigoda alisema mhandisi mshauri wa kiwanda amekamilisha uhakiki na ukaguzi wa mitambo iliyopo katika kiwanda hicho.
Ujenzi wa viwanda
Akizungumzia uwekezaji katika maeneo maalumu ya kuzalisha bidhaa za kuuza nje (EPZA), Dk. Kigoda alisema makampuni 29 yamepewa leseni za kujenga viwanda chini ya EPZA.
Alisema tayari makampuni matano yamekwisha kuanza uzalishaji na yatawekeza mtaji wa Dola za Marekani milioni 113 na kuajiri watu 9,254.
Alisema idadi hiyo itafanya makampuni yanayozalisha chini ya EPZA kufikia 70 na mtaji uliowekwa kufikia Dola za Marekani bilioni moja na ajira za moja kwa moja kufikia 23,000.
Akizungumzia vipimo, Waziri Kigoda alisema wizara, kupitia wakala wa vipimo imefanya ukaguzi wa vipimo mbalimbali vitumikavyo katika biashara, ikiwamo mizani itumikayo katika ununuzi wa mazao ya wakulima.
Wafanyabiashara 10 walifikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali yanayohusu vipimo, alisema.
Alisema hata hivyo ukamilishaji wa sheria mpya ya vipimo unaendelea na waraka wa Baraza la Mawaziri ulijadiliwa na kutolewa ushauri wa kuboresha waraka huo.
Wabunge
Wakichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina (CCM) alitaka Serikali iweke utaratibu maalumu wa kuisaidia SIDO.
Alisema njia pekee ambayo itasaidia kuleta ajira nyingi nchini ni pamoja na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo.
Alisema pamoja na kuisaidia SIDO pia ni vyema serikali ihakikisha kiwanda cha UFI ambacho kwa sasa kimebadilishwa matumizi kinarejeshwa.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alisema taifa limekuwa na idadi kubwa ya watu wasiokuwa na ajira na kuitaka Serikali kuacha kuwanyanysa wamachinga.
Alisema tatizo hilo limechangiwa na hatua ya Serikali kujitoa katika kusimamia viwanda, hali iliyofanya baadhi ya wanunuzi kubadili matumizi ya viwanda hivyo.
“Nchi hii ni matatizo, wamachinga wanapigwa, watu wakiandamana kudai haki zao kipigo, ukifanya hivi kipigo. Jamani siyo wakati wote mnatumia nyundo,” alisema.
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM) alisema kuna haja ya kuvunjwa kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni na Utoaji wa Leseni (BRELA) akidai kuwa kimeshindwa kazi.
Mkono alisema kitengo hicho kimejaa urasimu kwani kazi ya muda wa miezi mitatu inaweza kufanywa kwa miaka miwili hadi mitatu.
Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Asaa Othman Hamad (CUF) alisema hali ya viwanda ilivyo hivi sasa inatisha.
Alisema hali hiyo ingemstaajabisha zaidi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere endapo angerudi duniani hivi sasa ambapo angejionea sekta ya viwanda ilivyo taabani.
kila mwaka wa general tire itafunguliwa hizo ni kelele 2 hamna kinacho fanyika apo
ReplyDelete