Thursday, May 16, 2013

NEC yatupa mapendekezo ya vyama vya siasa

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekataa mapendekezo ya vyama vya siasa ya kutaka uchaguzi mdogo Jimbo la Chambani, kisiwani Pemba na ule wa udiwani katika kata 26 kwenye halmashauri 21 za Tanzania Bara uahirishwe, kwa madai kwamba, unawanyima wananchi waliotimiza umri wa kisheria haki ya kupiga kura.

Pia imekataa pendekezo la vyama vya siasa ya kutaka jukumu la kuwalipa mawakala posho za kazi ya kulinda kura za wagombea wa vyama hivyo kwenye uchaguzi.

Mapendekezo hayo yalitolewa na viongozi wa vyama hivyo, katika mkutano uliotishwa na NEC kwa lengo la kujadili na kupeana taarifa za maandalizi ya chaguzi hizo, jijini Dar es Salaam jana. 

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na NEC, chaguzi hizo mbili ndogo zitafanyika Juni 16, mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa NEC, Hamid Mahmoud Hamid, alisema iwapo chaguzi hizo hazitafanyika watakuwa wanavunja sheria.

Alisema kwa mujibu wa sheria, katika uchaguzi mkuu mmoja na mwingine, uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura (DKWK), unatakiwa ufanyike mara mbili tu, hivyo akasema kuitishwa kwa chaguzi hizo ndogo, hakujakiuka sheria.

Kamishna wa NEC, Profesa Amon Chaligha, alisema Tume itakuwa na uwezo wa kuboresha DKWK mara kwa mara tofauti na sasa iwapo tu sheria husika itabadilika.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha NRA, Rashid Mtuta, akichangia mada ya maandalizi ya chaguzi hizo ndogo iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Mallaba, katika mkutano huo jana, aliitaka NEC kueleza jitihada ilizofanya kuhakikisha wananchi, ambao baada ya mwaka 2010 walitimiza umri wa kisheria, wanapata haki ya kupiga kura katika chaguzi hizo.

Rais wa Chama cha Tadea, John Chipaka, alisema vyama vya siasa vinao ushahidi kwamba, NEC haijaboresha DKWK tangu mwaka 2010, hali ambayo inawanyima wananchi wengi wenye sifa ya kisheria haki ya kupiga kura.

Kutokana na hali hiyo, Chipaka alipendekeza chaguzi hizo ndogo mbili ziahirishwe kwa madai kwamba, DKWK halijawaingiza wapigakura hao hivyo, zinafanyika kinyume cha sheria.

“Tusibabaishane hapa. Kubabaishana kumeshapita miaka 19 kwa mwenyekiti aliyepita. Kwa hiyo, uchaguzi hakuna,” alisema Chipaka.

Pendekezo hilo liliungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha DP, Abdul Mluya, Mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahami Dovutwa na Katibu Mkuu wa Chama cha AFP, Rashid Rai.

Kuhusu pendekezo la vyama hivyo kutaka NEC ichukue jukumu la kulipa mawakala posho hizo, Profesa Chaligha, alisema suala hilo liliwahi kufanywa na serikali kwa kukivipa vyama katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, lakini likabadilishwa na sheria kufuatia mivutano iliyojitokeza baadaye baina ya mawakala na vyama iliyosababisha kufikishana mahakamani.

No comments:

Post a Comment