Friday, May 17, 2013

Upinzani wataka ufafanuzi Bandari ya Bagamoyo

Kambi rasmi ya upinzani bungeni imeitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu mkataba wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unaosemekana kuwa sehemu ya bandari hiyo itatumiwa na Wachina kwa ajili ya matumizi ya kijeshi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Aidha, pia umetaka ufafanuzu kuhusu madai kuwa baadhi ya vipengele vya mkataba huo vinakataza uendelezwaji wa bandari nyingine zilizoko karibu na Bagamoyo kwa miaka 50 ijayo.

Akisoma maoni ya upinzani kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Wizara ya Uchukuzi, Pauline Gekul, alisema wakati wa ziara ya Rais wa China nchini, miongoni mwa mikataba iliyosainiwa baina ya serikali na ile ya China ni makubaliano ya jumla ya ushirikiano wa kimkakati kuhusu uendelezaji wa Kanda Maalumu ya Kiuchumi ya Bagamoyo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya China Merchant Holding International (CMHI).

“Pamoja na kusainiwa kwa mkataba huo mkubwa wa kihistoria katika ujenzi wa bandari hii pamekuwepo na usiri mkubwa kuhusiana na mkataba wenye na hali hiyo imefanya uwepo wa maneno mengi sana kuhusiana na vipengele vya mkataba huu,” alisema Gekul.

Aidha, kambi hiyo ilitaka kujua uendeshaji na usimamizi wa bandari
hiyo utafanywa na Watanzania ama Wachina.

Ikizungumzia Shirika la Ndege nchini (ATCL), ilitaka lifilisiwe na kuanza upya badala ya kuendelea kutenga fedha kila mwaka kwa shirika ambalo halina tija.

Kambi hiyo ilisema kuna taasisi zingine zilizo chini ya wizara hiyo
ambazo ni muhimu kiutendaji lakini zinaonekana kutokuwa na umuhimu kwa sababu ya kutotengewa fedha za kutosha kutekeleza mipango.

Ilitaja taasisi hizo kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Chuo cha Usafirishaji, Chuo cha Ubohari, Chuo cha Usafiri wa Anga, Chuo cha Hali ya Hewa na Chuo cha Bandari.

No comments:

Post a Comment