Friday, May 17, 2013

Cuf yaungana na wanaokosoa mchakato wa Katiba mpya

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kinaungana na Watanzania walioonyesha shaka juu ya mchakato wa kupata Katiba mpya kwani hakioni nia njema na utayari wa Tume kuwa na Katiba inayotokana na maoni ya wananchi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha baraza kuu la chama hicho kitaifa.

Alitaka  Rasimu ya Katiba inayoandaliwa iwekwe hadharani kwa wakati ili wananchi waweze kutoa maoni yao kabla haijapelekwa katika Bunge la Katiba na kupigiwa kuwa na wananchi.

Alisema Cuf hakitakuwa tayari kuiunga mkono Katiba ambayo haitakuwa na misingi imara ya kidemokrasia na isiyotokana na maoni ya Watanzania na kitakuwa tayari kuwahamasisha kuikataa katiba hiyo.

Profesa Lipumba ameitaka tume ya kuratibu ukusanyaji wa maoni kuweka mpango wa kuyafikia makundi yenye mahitaji maalumu ikiwa ni wanawake, walemavu, vijana na asasi za kiraia zinazoshughulika na malezi ya watoto ili yaweze kutoa maoni yao.

Alisema pamoja na mchakato wa uandikaji wa katiba kupangiwa miezi 18 muda huo  hautoshi  kwani kuna chaguzi mbalimbali ambazo zinatarajiwa kufanyika mwakani hivyo hakuna sababu za msingi za kuharakisha zoezi hilo na kupata katiba mbovu isiyokidhi matakwa ya wananchi na badala yake kupata katiba ya matakwa ya kikundi kidogo cha watu wenye dhamana.


Kuendelea Bonyeza Read More








Mchakato wa Katiba kufikishwa mahakamani Jumatatu


Jukwaa la Katiba Tanzania, limesema limekamilisha mchakato wa kwenda mahakama Kuu na Mei 20, mwaka huu watatinga mahakamani.

Jukwaa hilo linakwenda Mahakamani kuweka zuio dhidi ya Tume ya Marekebisho ya Katiba, kusitisha mchakato wa Katiba mpya hadi watakaporekebisha kasoro zilizojitokeza.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, akizungumza na NIPASHE jana, Deus Kibamba, alisema wamefanya vikao kadhaa na jopo la mawakili 10 ambao wanaendelea kuandaa hoja za msingi.

“Tumeshafanya vikao kadhaa na jopo la Mawakili wakiongozwa na Mwanasheria wa masuala ya Haki za Binadamu, Dk. Rugemeleza Nshala, wamefika pazuri na Jumatatu tutakuwa mahakamani,” alisema Kibamba.

Kibamba alisema uamuzi wakwenda mahakamani unatokana na Jukwaa hilo kupuuzwa na mihimili ya Bunge na Serikali na wasaidizi wa Rais kuwakataza kuonana na Rais, Jakaya Kikwete, kwa ajili ya kuwasilisha maoni yao na kuona njia pekee ya kutafuta haki ya Watanzania ni kwenda mahakamani.

“Tunaenda mahakamani kuomba isimamishe mchakato wa Katiba mpya hadi watakaoona umuhimu wa kuheshimu na kufuata ratiba waliojiwekea, kuheshimu misingi ya uandikaji na iamuru kusimama kwa mchakato huo,” alisema.

 Alianisha kasoro ni mchakato huo kupelekwa kwa kasi inayoathiri misingi mikuu ya ujenzi wa Katiba mpya kwenye  uelewa na hamasa, ushiriki, umiliki wa wananchi na hivyo mchakato huo unaweza kuzaa Katiba isiyo na sauti na maoni ya Watanzania wote.

Alisema wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya walichaguliwa kwa mizengwe, rushwa na ushabiki wa kiitikadi za vyama, dini na wengi hawana sifa muhimu za kuchambua, kutafsiri na kujadili rasimu ya katiba mpya.

Alisema nyingine ni Bunge Maalum la Katiba, kutokuwa na sifa kwa kuwa ni wa kuchaguliwa na kuweka watu huru, kwa kuwa wabunge waliopo Dodoma na Zanzibar hawakuchaguliwa kwenda kutunga Katiba Mpya bali sheria za kawaida za nchi ikiwamo marekebisho ya Katiba.

No comments:

Post a Comment