Friday, May 17, 2013

Mdee ahoji ujenzi barabara Kawe


MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), ameihoji serikali kuhusiana na ujenzi wa barabara za Kawe katika bajeti ya mwaka huu, ambazo hazikutekelezwa katika bajeti ya mwaka jana.
Mdee alitoa kauli hiyo bungeni hapa jana alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.
“Katika bajeti ya mwaka jana tulitenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ‘Ring Roads’ lakini Kawe hakukuwa na matengenezo yoyote, je, serikali inasemaje kuhusiana na bajeti ya mwaka huu, itatengeneza kilomita ngapi katika barabara zote za Kawe?” alihoji Mdee.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua mpango mpana wa serikali wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara za ndani.
Katika swali jingine la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya, aliihoji serikali kuhusiana na ukarabati wa kipande cha barabara ya Kunduchi Mtongani ambacho kimeharibika na kimekuwa kikisababisha ajali za mara kwa mara.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Greson Lwenge, alisema serikali imetenga sh bilioni 28 katika bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa barabara mbalimbali nchini.
Alisema fedha hizo zinatosha kuanza kujenga barabara hizo na nia ya serikali ni kutekeleza miradi yote iliyoanzisha.
Akijibu swali la msingi, Lwenge alisema serikali ina mpango wa ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam hadi Kibaha kuwa ya njia sita kupitia mradi wa Dar es Salaam Chalinze kwa utaratibu wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi au utaratibu mwingine utakaoonekana unafaa.
“Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), imeshatangaza zabuni za ujenzi wa Dar es Salaam Chalinze na kampuni 19 zimewasilisha nyaraka kuonesha nia ya kufanya ujenzi wa barabara hiyo,” alisema Lwenge.
Aidha, alisema serikali inaendelea na ujenzi wa ‘Ring Roads’ kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.
Alisema miradi ambayo ujenzi unaendelea ni Ubungo Bus Terminal - Kawawa Road Roundabout kilomita 6.4, Kawawa Roundabout-Msimbazi Valley-Jangwani/Twiga Junction kilomita 2.7 na Jet Corner – Vituka - Devis Corner kilimota 10.4.
Lwenge alisema miradi ambayo zabuni kwa ajili ya ujenzi zimetangazwa katika mwaka 2012/13 ni Mbezi-Malamba Mawili-Kinyerezi-Banana kilomita 14, Tegeta Kibaoni-Wazo Hill-Goba-Mbezi Mwisho (Morogoro Road) kilomita 20, Kimara Baruti – Msewe - Changanyikeni kilomita 2.6, Ubungo Maziwa - External na Tabata Dampo - Kigogo kilomita 2.25, Kimara-Kilungule-Excternal kilomita tisa na Tangi Bovu-Goba kilomita tisa.
Alisema serikali imekamilisha upembezi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa ‘Outer Ring Roads’ ya Bunju- Victoria (Morogoro Roads) - Pugu kilomita 54 kwa kiwango cha lami barabara hiyo itakuwa ya njia nne (mbili kwa kila kipande).
Akijibu swali la Bulaya, Lwenge alikiri kuwepo kwa tatizo hilo katika kipande cha barabara ya Kunduchi-Mtongani.
Alisema kazi ya ujenzi wa barabara hiyo haijakamilika, lakini kipande hicho kimeanza kuharibika, hivyo watahakikisha mkandarasi anarudia kazi hiyo kwa gharama zake kabla hajakabidhi kazi.

No comments:

Post a Comment