KATIBU Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amesema viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ni wanafiki ndiyo maana amani na utulivu vinaanza kupotea.
Alisema serikali ya chama hicho ni mtuhumiwa mkubwa wa uvunjifu wa haki mbalimbali za wananchi lakini imekuwa kinara wa kuzungumzia amani ambayo ni tunda la haki.
Kauli hiyo aliitoa juzi mkoani Manyara alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kukijenga chama ambapo alisema viongozi wa CCM wamekuwa wakihubiri amani bila kuzungumzia haki ambayo ni msingi wa amani na utulivu imara.
“Kama watawala wangekuwa na dhamira ya dhati na amani ya nchi hii, wangetenda haki, amani haihubiriwi majukwaani ni tunda la haki na matumaini ya wananchi kwa viongozi wao,” alisema.
Alisisitiza kuwa ni vigumu kwa viongozi kueleweka kuwa wana nia ya dhati kuona nchi ikitawalika kwa amani na utulivu, wakati wananchi wengi wanaendelea kutaabika kwa kunyimwa haki zao na kunyanyaswa ndani ya maeneo yao.
“Nani hajui uvunjifu wa haki za wananchi unaofanyika katika ardhi, elimu, ajira na usalama wa raia?...haya yanafanywa chini ya serikali ya CCM ambayo inahubiri amani inaacha haki, hawa ni wanafiki ndiyo maana nchi inawashinda,” alisema.
Dk. Slaa pia alisema CHADEMA inajisikia fahari kuona serikali ya sasa inatekeleza sera za chama hicho kikuu cha upinzani nchini chenye utajiri wa mawazo mbadala mbalimbali namna ya kuwatumikia Watanzania.
Alisema wamefurahi kusikia serikali ina mpango wa kuongeza miaka ya wanafunzi kusoma elimu ya msingi kutoka miaka saba ya sasa hadi 10, ambayo ilikuwa sera ya CHADEMA siku nyingi na waliinadi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, akadai kuwa kutokana na mawazo mgando ya chama kilichoko madarakani na viongozi serikalini, walimbeza.
“Tunashukuru wameanza kutekeleza sera zetu. Sisi hatuna kinyongo kama wanatumia sera zetu kuongoza nchi hii, kwa sababu hatimaye anayenufaika ni mwananchi na hiyo ndiyo furaha yetu. Lengo letu ni Watanzania hawa kunufaika na nchi yao,” alisema.
Alibainisha kuwa mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu waliposema kuwa wakiichukua nchi wangetoa elimu bure walijua wangefanya nini lakini CCM kwa mawazo mgando walibeza kwa madai haiwezekani.
Aliongeza kuwa CHADEMA ilisema ikichukua nchi itaangalia na kurekebisha mfumo wa kodi na kushusha bei ya vifaa vya ujenzi ikiwemo mfuko wa saruji uwe sh 5,000.
Alisema chama chake kilitoa kauli hizo kwa kuwa kinaamini bati, nondo na vinginevyo kadhalika, vingeshuka bei. Alisisitiza kuwa ni suala la formula na mfumo wa ulipaji kodi na uzalishaji viwandani, hilo nalo walibeza na wakasema haiwezekani lakini sasa wanatekeleza.
No comments:
Post a Comment