HATIMA ya dhamana ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph, inatarajia kujulikana leo watakapopandishwa katika mahakama ya Kisutu.
Wakati watuhumiwa hao waliofutiwa makosa ya ugaidi wakipandishwa kizimbani leo, Tanzania Daima, imedokezwa kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinafanya mbinu za kukwamisha dhamana hiyo.
Chanzo cha Tanzania Daima, kimedokeza kuwa lengo la CCM kutia mkono kwenye kesi hiyo ni kutaka kumnusuru Naibu Katibu Mkuu wake, Mwigulu Nchemba, aliyesema anao ushahidi wa ugaidi na yuko tayari kuutoa popote.
Wakati Mwigulu akijinasibu kuwa tayari kutoa ushahidi wa ugaidi wa Lwakatare, Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka ya Ugaidi Lwakatare na Ludovick.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania Daima, zinabainisha kuwa kabla ya mkutano wa siku mbili wa Rais, Katibu Mkuu wa CCM na wabunge wa chama hicho uliofanyika Dodoma wiki iliyopita, Kamati Kuu ilikutana na kujadili masuala mbalimbali likiwemo la Lwakatare.
Inadaiwa suala la kesi ya Lwakatare lilionekana kuwakera baadhi ya wajumbe walioweka wazi kuwa badala ya kuiumiza CHADEMA imekuwa tofauti na kumuweka katika mazingira mabaya Nchemba na CCM.
Bonyeza Read More Kuendelea
Chanzo chetu kinathibitisha kuwa katika kikao cha Kamati Kuu kilichoketi Dodoma baada ya Rais kukutana na wabunge wa CCM tarehe 18 na 19 mwezi huu, Mwigulu Nchemba aliwalalamikia wajumbe kwa kumtelekeza kuhusu suala la kesi ya Lwakatare.
“Mwigulu alisimama mara kwa mara kuomba kwa nini suala hilo ameachiwa yeye binafsi limwangamize wakati ni suala la chama, na kadiri linavyomwathiri yeye ndivyo linavyokiathiri chama, hivyo mwisho aibu itakuwa ya wote,” alisema mtoa habari wetu.
Inasadikika katika kikao hicho ndipo lilitolewa shinikizo la kumtaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Eliezer Feleshi, akate rufaa haraka dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu kumzuia Lwakatare kupata dhamana.
Tanzania Daima, iliwahi kudokezwa kuwa Mwigulu ndiye aliyepanga namna ya kupata mkanda wa video unaodaiwa kumwonyesha Lwakatare na Ludovic wakipanga kumdhuru Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi Denis Msacky.
Mei 8 mwaka huu, Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu alikubaliana na hoja za mawakili wa Lwakatare kuwa mashtaka ya ugaidi hayana maelezo ya kutosha kuonyesha kuwa ni ya ugaidi akisema yalipaswa yawe na maelezo yanayoelezea uhalisia wa ugaidi.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya mawakili wa watuhumiwa hao kupinga uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa kuwafutia kesi na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi yenye mashtaka hayo hayo kwenye Mahakama ya Kisutu, Machi 20, mwaka huu.
Mei 13, mwaka huu, katika Mahakama ya Kisutu jopo la Mawakili wa Lwakatare waliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, impatie dhamana, Lwakatare baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kumfutia, mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili yeye na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura, ambayo hayana dhamana.
Mmoja wa mawakili hao, Peter Kibatala, aliliambia gazeti hili kuwa walikuwa wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa wangeweza kumtoa kwa dhamana kwa kuwa walikuwa tayari wamekamilisha masharti ya dhamana.
Hata hivyo, jitihada zao ziligonga mwamba kufuatia kitendo cha hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Aloyce Katemana, kutokuwapo mahakamani na hivyo kusababisha kesi hiyo kuahirishwa hadi leo ambapo mawakili na wafuasi wa chama hicho wanatarajia Lwakatare apate dhamana.
Tanzania Daima ilimtafuta Naibu Katibu Mkuu huyo kuzungumzia suala hili bila mafanikio kwani simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani muda wote.
No comments:
Post a Comment