MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), ameitaka serikali kuzishirikisha halmashauri zote nchini ili ziweze kusaidia kutatua tatizo la makazi ya polisi.
“Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiofichika kwamba vijana wetu wa polisi wanadhalilika kwa kukosa makazi na hivyo kufanyakazi zao katika mazingira magumu sana na tumekuwa tukisikia serikali ikisema kwamba ina mpango wa kujenga nyumba.
“Kwa nini serikali isishirikishe halmashauri zote nchini zikasaidia katika kutatua tatizo hili la makazi wa askari wetu?” alihoji.
Akijibu swali hilo la nyongeza, Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alisema halmashauri si ya kuhusishwa isipokuwa inahusika moja kwa moja.
“Na zipo halmashauri ambazo zimeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha zinatoa huduma na baadhi ya askari wanapata makazi katika maeneo yao. Napenda kusisitiza kuwa juhudi hizi zipo na mtu yeyote mwenye macho ya kawaida lazima ataona kwamba kuna mabadiliko,” alisema.
Awali, katika swali la msingi Mbunge wa Viti Maalum, Maryam Salum Msabaha (CHADEMA), alihoji kama serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kuongeza mitaala ya Mafunzo ya polisi.
Pia, alitaka kujua ni lini serikali itaboresha na kujenga Kambi za Jeshi la Polisi za kutosha ili maaskari wanaohitimu mafunzo waishi humo.
Naibu Waziri alisema ajira kwa Jeshi la Polisi huzingatia Taratibu na Kanuni za Jeshi la Polisi na zile za Utumishi wa Umma.
“Ajira hizi hutolewa kwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 25. Vijana hao hupaswa kuhudhuria mafunzo ya awali kwa muda wa miezi 9 hadi mwaka mmoja kuhitimu,” alisema.
No comments:
Post a Comment