VIONGOZI wa vyama vya siasa na serikali nchini wametakiwa kuacha ugomvi wa itikadi za kisiasa bali kujikita katika mustakabali na maslahi ya taifa kwa kuwa taifa lilikuwepo kabla ya vyama na litaendelea kuwepo hata baada ya vyama vilivyopo kufa.
Rai hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Taifa, Freeman Mbowe, kwenye mkutano uliofanyika katika kata ya Matarawe ambao ulitanguliwa na mafunzo kwa viongozi wa Kanda ya Kusini inayoundwa na mikoa mitatu ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Alisema si busara kwa kiongozi yeyote wa serikali au chama chochote cha siasa kuhamasisha chuki baina ya wananchi wa taifa moja ambalo limejengwa katika misingi ya ushirikiano, bali kila mmoja anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia ustawi wa taifa.
Alieleza kuwa kilio kikubwa cha CHADEMA ni juu ya ustawi wa taifa na kwamba rasilimali zilizopo zinapaswa kuwanufaisha wananchi eneo zilizopo na kisha kwenda kwa wengine.
Aidha, Mbowe aliwataka wananchi kuvipenda na kuvisaidia vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo nchini kwa sababu vipo kwa ajili ya wananchi na kuvitaka vyombo hivyo kufanya kazi kwa uadilifu.
No comments:
Post a Comment