Tuesday, May 28, 2013

Lwakatare akwamishwa tena

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana iliahirisha tena kesi ya kula njama na kutaka kumuua kwa sumu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky, inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.
Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, alisema anaiahirisha kesi hiyo hadi Juni 10 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa kwa kuwa Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Aloyce Katemana bado hajarejea kazini.
Alisema Hakimu Katemana akirejea kazini anatakiwa kupata muda wa kuzipitia hoja za kuomba na kupinga dhamana ziliwasilishwa mawakili wa utetezi na mashataka ndipo atoe uamuzi wake.
Awali, wakili wa utetezi, Peter Kibatara, Profesa Abdala Safari na Nyaronyo Kichere waliiomba mahakama kupanga tarehe za karibu za kesi hiyo.
Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, baadhi ya wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wamevalia sare za chama hicho walisikika wakiwatuhumu viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuingiza mkono kwenye suala hilo.
“Huu ni mchezo mchafu unaofanywa na CCM na mahakama kupiga chenga kumpatia dhamana Lwakatare…kamanda wetu amesota gerezani muda mrefu na leo ni mara ya pili tunakuja kesi inaahirishwa kwa kisingizio cha hakimu kutokuwapo.
Mei 8, mwaka huu Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lawrance Kaduri alimfutia mashtaka matatu ya ugaidi Lwakatare na Ludovick.
Wakati huohuo, Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema ametoa hati ya kukamtwa kwa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi, Theophil Makunga, anayekabiliwa na kesi ya kuchapisha makala ya uchochezi baada ya kushindwa kufika mahakamani.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda, na mwandishi wa makala hiyo, Samson Mwigamba. Kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya kutajwa kwa kuwa Kibanda yupo Afrika Kusini kwa matibabu.
Kutokana kutokuwapo mahakamani kwa Makunga bila taarifa zozote, Wakili wa serikali, Lilian Itemba, aliiomba mahakama itoe amri ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 20 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment