Wednesday, May 22, 2013

Profesa Jay atua CHADEMA


MSANII maarufu wa hip hop nchini, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay, au Jay wa Mitulinga, pamoja na msanii wa kundi la Mapacha, Levison Kasulwa wamekabidhiwa rasmi kadi za kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mjini Dodoma jana.
Zoezi hilo lilifanyika katika hoteli ya Desert Palm, ambako walikabidhiwa kadi hizo na Mbunge wa Mbeya Mjini, ambaye pia ni Waziri Kivuli, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
Akizungumza baada ya kukabidhi kadi hizo, Sugu alisema wasanii hao wameamua uamuzi wa busara, kwani CHADEMA ni chama cha kutetea haki za wanyonge na wasanii kwa ujumla.
Sugu alisema yeye alipofikia uamuzi wa kujiunga na CHADEMA, alipokelewa na kupewa ushirikiano mkubwa na makamanda wote ambao sio wasanii, hali inayoonesha kuwa chama hicho hakina ubaguzi kwa mtu yeyote.
“Naamini kamanda licha ya kujiunga huku, lakini utaendeleza muziki na utashirikiana kwa hali na mali kupeleka mbele gurudumu la chama na Watanzania kwa ujumla,” alisema Sugu.
Waziri kivuli huyo aliongeza kuwa kama angeambiwa amshauri Profesa Jay, angemwambia arudi nyumbani Mikumi akawatumikie wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, akizungumza katika hafla hiyo, alisema yeye ni mmoja kati ya watu waliowashawishi wasanii hao wawili, Profesa Jay na Sugu kujiunga na CHADEMA.
Alisema baada ya kuwashawishi, Mbilinyi ilimchukua miaka mitano kufikia uamuzi wa kuwa mwanachama, wakati Profesa Jay imemchukua miaka sita hadi jana alipoamua kufikia uamuzi huo, kitendo ambacho kinaonesha dhahiri kuwa kuchukua kwao muda mrefu ni kwa dhati na wala hakutetereki.
“Mtu yeyote anayefanya uamuzi kwa muda mrefu, anakuwa amefanya uamuzi sahihi na wa uhakika na anakuwa anajiamini katika uamuzi huo,” alisema Mnyika.
Naye Profesa Jay, alisema atailinda kwa gharama yoyote CHADEMA na atakuwa tayari kushirikiana na wapiganaji wenzake ambao ni makamanda ndani ya chama hicho, katika kuhakikisha inasonga mbele na kuendelea kutetea haki za Watanzania.
“Mimi Profesa Jay ni kama daraja, nawahamisha watu wa upande huu na kuwapeleka upande mwingine wa sarafu,” alisema.
Kaselwa wa Mapacha, alisema ameamua kwa moyo wake mwenyewe na wala hajashinikizwa na yeyote kujiunga na chama hicho.

ILI TUENDELEE TUNAHITAJI VITU VINNE, KWANZA WATU, PILI ARDHI, TATU SIASA SAFI, NNE UONGOZI BORA - PROF J





No comments:

Post a Comment