Wednesday, May 22, 2013

Mdee ahoji matumizi ya fedha za shule


MBUNGE wa Kawe Halima Mdee (CHADEMA), ameihoji serikali kuhusiana na mabilioni ya fedha za uendeshaji shule (Capitation Grant) ambazo zimekuwa zikitengwa, lakini hazifikishwi shuleni na kuwasababishia wazazi kulipa michango.
“Mabilioni ya Fedha za Capitation Grant ambazo Naibu Waziri anazungumzia anajua kama hayafiki chini, mwaka 2011/2012 tulitenga sh bilioni 50 zilizofika zilikuwa bilioni 10, hii ni changamoto kubwa na imekuwa ikiwasababishia wazazi mzigo mkubwa wa kutoa michango lukuki isiyokuwa na maana,” alisema.
Mdee alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu Moza Saidi (CUF), alitaka kujua mpango wa serikali wa kunusuru elimu kwa kuboresha fedha na vifaa vya kufundishia.
Pia mbunge huyo alihoji kama serikali haioni haja ya kutoa elimu kwa walimu na watendaji wa elimu juu ya maboresho katika sekta ya elimu nchini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kassim Majaliwa alisema kwa maelekezo ya serikali shule hizo ni za wananchi wenyewe na maendeleo ya shule hizo yanaratibiwa na wananchi wenyewe.
Aidha, aliwasihi wabunge kusaidiana na serikali kusimamia shule hizo ili kuhakikisha wazazi na wananchi hawachangishwi michango mingi ambayo haina tija na badala yake fedha hizo zinapotea.
Awali, Mbunge wa Viti Maalumu, Moza Saidy (CUF) alihoji kwamba serikali haioni haja ya kutoa elimu kwa walimu na watendaji wa elimu juu ya maboresho katika sekta ya elimu pamoja na mazingira ya kufundishia.
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema serikali imekuwa na mipango mbalimbali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Majaliwa alisema kupitia awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES -II) ujenzi wa ukamilishaji wa shule za sekondari 264 wa sh bilioni 56.3 umeanza ili kuzifanya kuwa na miundombinu yote muhimu ikiwemo maabara, maktaba, vyoo, umeme na maji.
Aidha, alisema serikali kupitia Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi na Sekondari (MMEM na MMES) inaendelea kutoa mafunzo ya kujenga uwezo wa kusimamia elimu katika nyanja ya kamati na bodi za shule, walimu wakuu, halmashauri, mikoa na wizara kupitia vyuo vya ualimu na ADEM Bagamoyo.

No comments:

Post a Comment