Tuesday, May 7, 2013

‘Polisi ivunjwe’


 YADAIWA KUTUMIWA VIBAYA NA CCM
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetaka Jeshi la Polisi nchini livunjwe na ligeuzwe kitengo ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Msimamo huo umetolewa jana bungeni na baadhi ya wabunge wa chama hicho walipokuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyowasilishwa na Waziri Emmanuel Nchimbi.
Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde, alisema Jeshi la Polisi limeoza, kwa sababu limeshindwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu, ikiwamo kuwakamata wahalifu mbalimbali wanaoshiriki kwenye matukio ya kihalifu.
“Napendekeza Jeshi la Polisi livunjwe na liingizwe ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liwe sehemu ya kitengo katika jeshi hilo.
“Naamini kwa kufanya hivyo tutaboresha utendaji wake, silaha kubwa iliyobaki kulinusuru taifa hili kwa sasa ni kusema ukweli, kwani bila kufanya hivyo miaka sita ijayo hali itakuwa mbaya,” alisema.
Aliongeza kuwa lazima Watanzania wakubali kuwa nchi imegubikwa na matukio ya udini na ukabila, ingawa serikali ama kwa kufanya makusudi au rais na Waziri Nchimbi kudanganywa wamekuwa wakishindwa kuchukua hatua.
Silinde alisema kuwa kama ilivyoandikwa kwenye maandiko matakatifu kuwa itafika wakati wenye macho hawataona na wenye masikio kutosikia, na kuifananisha hali hiyo na CCM ya sasa.
Mbunge huyo aligusia tukio la Arusha akisema huo ni mwendelezo wa kile walichokipanda CCM kwa kutochukua hatua kwa watu wanaochochea vurugu hizo za udini.
“Serikali ya CCM haioni tena, haisikii wala haiwezi kunusa tena, hili ndilo anguko la serikali hii,” alisema.
Hata hivyo alimshangaa Waziri Nchimbi kwa kumtaja mtuhumiwa mmoja kwa jina na kuwaacha wengine watano aliodai ni raia wa kigeni, akisema huo ni mwendelezo wa kuficha maovu.
“Kama huyu mmoja katajwa, kwanini hao wengine wasitajwe? Tunaficha nini? Ama ndio mwendelezo huo huo wa kutaka kupindisha ukweli wa tatizo na kuibua mambo mengine?
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu ‘Sugu’ alisema serikali imekosa mikakati ya kutuliza vurugu hizo na badala yake inakuja na maneno ya kisiasa yasiyo na ufumbuzi wa tatizo.

Bonyeza Read More Kuendelea


Sugu alishauri Jeshi la Polisi livunjwe kwa kushindwa kazi na kisha liundwe upya kwa kuwapa kazi vijana wasomi ambao wana uwezo mkubwa badala ya kung’ang’ania kuwaongeza wastaafu mikataba.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), alisema vitendo vya vurugu za kidini vinavyoendelea nchini ni matunda ya serikali ya CCM.
Lissu alianza kujenga hoja yake akitumia usemi wa mwanafalsafa mmoja kuwa hakuna uchochezi mkubwa kama kukaa kimya.
Alisema kile kilichotokea Arusha juzi pamoja na matukio ya kuvamiwa kwa viongozi wa kidini visiwani Zanzibar ni ukimya wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwa ni pamoja na kuchochea matendo hayo.
“Nchi hii imeshuhudia baadhi ya watu wakifanya mihadhara ya kidini na kuhamasisha uchochezi, magazeti yanaandika kuchochea udini, zipo radio zinatangaza kashfa mbalimbali dhidi ya dini nyingine, lakini serikali hii iko kimya.
“IGP Omar Mahita, alitangaza mchana kweupe kuwa Chama cha Wananchi (CUF) ni cha kigaidi, akaonesha na visu kwenye vyombo vya habari, lakini serikali hadi leo haijasema kitu juu ya hilo,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, CCM iliweka kwenye ilani yake kuwa itawapatia Waislamu Mahakama ya Kadhi na ilipoona haiwezi kufanya hivyo ikawasingizia maaskofu kuwa ndio hawataki mahakama hiyo iwepo.
Lissu alifafanua kuwa hali imekuwa mbaya kutokana na uchochezi huo ulioasisiwa na serikali ya CCM halafu sasa inageuka na kuanza kutaka kujinasua.
“Tumeambiwa tusimlaumu mtu katika tukio hili la Arusha, nami nakubali ila ninachosema ni kwamba huu ni wakati wa Waziri Nchimbi kuachia ngazi mwenywewe kutokana na kushindwa kazi ama awajibishwe.
“Huu ni wakati wa IGP Said Mwema kujiuzulu na akishindwa awajibishwe kwa kushindwa kazi,” alisema.
Lissu alisema kuwa serikali ya CCM ndiyo imepalilia uchochezi wa udini na ukabila nchini kama kinga ya kujilinda na kasi ya vyama vya upinzani.
“Serikali hii ndiyo ilisema CHADEMA ni chama cha Wachaga, serikali hii ndiyo ilisema CHADEMA ni chama cha Wakristo, ni chama cha Wakatoliki. Leo wanajigeuza na kuanza kujifanya wanachukia vitendo hivi.
“Mheshimiwa Spika lazima tuambiwe kwanza CUF imeacha lini kuwa chama cha kigaidi na Uislamu wenye itikadi kali, CHADEMA kimeacha lini kuwa chama cha Wachaga, Wakristo na Wakatoliki?” alihoji Lissu.
Nchimbi atoa kauli
Mapema akisoma kauli ya serikali bungeni kueleza mlipuko huo wa Arusha, Waziri Nchimbi alisema idadi ya watu waliokufa ni wawili baada ya mmoja kuongezeka usiku wa kuamkia jana.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Regina Kurusei (45) aliyefariki juzi akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru na James Gabriel (16) aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana huku watu wengine 59 wakiachwa majeruhi, ambapo miongoni mwao watatu ni mahututi.
Dk. Nchimbi alisema kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mlipuko huo ni bomu na kwamba uchunguzi wa kubaini aina ya bomu lililotumika unaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na wataalamu wa JWTZ.
“Hadi sasa watuhumiwa sita wanashikiliwa na polisi. Miongoni mwao ni Victor Ambrose (20) dereva wa bodaboda, mkazi wa Kwa Mrombo, Arusha ambaye anatuhumiwa kurusha bomu hilo. Watuhumiwa wengine watano waliokamatwa ni raia wanne wa kigeni na Mtanzania mmoja, ambao wanashikiliwa kwa mahojiano,” alisema.
CCM yanena
Nacho Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, kimeeleza kusikitishwa na kitendo hicho cha kulipuliwa kwa kanisa mjini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Kinana alisema kuwa CCM imeguswa na tukio hilo na kwamba wanalilaani kwa nguvu zote pamoja na kuitaka serikali kufanya kila mbinu kuwakamata wahusika na kuwachukulia hatua.
Kinana alitoa pole kwa waathirika wa tukio hilo wakiwamo wafiwa, majeruhi pamoja na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, akisema kuwa wanaamini kuwa serikali itachukua kwa karibu kila taarifa kuhusiana na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment