Tuesday, May 7, 2013

CHADEMA yamshukia Tendwa


YADAI ANAANDA SHERIA YA KUUA UPINZANI
KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imemshtumu Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa, kwa kuandaa mapendekezo yatakayopiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa wakati ambao si wa kampeni za uchaguzi.
Kwa mujibu wa kambi hiyo mapendekezo hayo yameonekana yana dhamira ya kuua upinzani na kukipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimetishiwa na ukuaji wa harakati za vyama vya upinzani.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na msemaji mkuu wa kambi hiyo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Josephat Nyerere, wakati akisoma maoni ya upinzani bungeni jana ambapo alisema mapendekezo hayo yakifanikiwa kuwa sheria haki ya vyama vya siasa kufanya shughuli za kisiasa itakuwa imeuawa na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Nyerere alisema mapendekezo hayo ya Tendwa ambayo lengo lake ni kufanya marekebisho kwenye sheria ya vyama vya siasa ambayo yakikubaliwa yatapelekea kupiga marufuku mikutano ya siasa yanatokana na shinikizo la CCM na kwamba yana lengo la kuidhibiti CHADEMA.
“Kwa miaka mingi CCM, na viongozi wake, imekuwa ikivikejeli vyama vya upinzani kwa kuviita vyama vya msimu. Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, CHADEMA imethibitisha kuwa si chama cha msimu kwa kufanya mikutano na maandamano kwa wingi kuliko chama kingine cha siasa. Matokeo yake sasa CCM na serikali yake wanakula njama ya kuzuia vyama vya upinzani kufanya mikutano ya siasa,” alisema.
Alisema kuwa hiyo ni kwa sababu taarifa ya Kamati ya Jaji Ihema iliyoundwa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Nchimbi, inasema: “Kasi ya CHADEMA kuendesha mikutano katika sehemu mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya kujiimarisha kichama imepokewa kwa hisia tofauti na vyama vingine vya siasa. Wakati kuna makundi ya watu katika jamii yakidhani kuwa hiyo ni haki yao kama chama cha siasa kinachotaka kukua na kukubalika kisiasa, wengine wanaona mikutano hiyo ya hadhara ya 
CHADEMA kama ni kuwapunguzia muda wa kufanya shughuli zao za maendeleo hasa baada ya kipindi cha uchaguzi kumalizika.”

Bonyeza Read More Kuendelea
Nyerere aliongeza kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alishauri kufanyiwa marekebisho sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 itakayoweka wazi shughuli za vyama vya siasa baada ya Uchaguzi Mkuu.
Alisisitiza kuwa shughuli za siasa baada ya Uchaguzi Mkuu zihamie Bungeni kwa wanasiasa kuhoji mipango wa maendeleo ya serikali na matumizi ya rasilimali za nchi na wananchi waachwe wachape kazi zao za maendeleo.
“Ushauri wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM ndio uliochukuliwa na kufanyiwa kazi na Msajili wa Vyama vya Siasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili juu ya hatua zozote kama zipo, za kutekeleza mapendekezo haya ya Kamati ya Jaji Ihema,” alihoji.
Nyerere alisema kuwa haki ya kufanya mikutano ya siasa na mikutano mingine yoyote na kwa wakati wowote, inatambuliwa na kulindwa na Katiba ya nchi Ibara ya 20(1).
Alisema kuwa uhuru huu haujawekewa masharti ya muda au wakati wa kukutana au kuchanganyika na watu kwa wakati au kipindi fulani. Mapendekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya kupiga marufuku mikutano ya siasa kwa nyakati zisizokuwa za kampeni za uchaguzi yanaenda kinyume na Katiba na hayakubaliki.
“Ni ajabu iliyoje kwamba wakati nchi nyingine jirani zetu zinapanua demokrasia kwa kupanua haki ya kufanya mikutano na maandamano, serikali hii ya CCM inapendekeza kuminya demokrasia kwa kudhibiti na kufifisha haki hizo. Na hii inafanyika wakati taifa likiwa kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya,” alisema.
Akizungumzia maslahi ya askari polisi, Nyerere alisema mara zote Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikitetea maslahi bora na mazingira mazuri ya kazi kwa watumishi wa serikali na hata wa sekta binafsi ili kuwapa motisha watumishi jambo ambalo huongeza tija katika uzalishaji na hatimaye kukuza uchumi.
Alisema kuwa katika maboresho ya maslahi na stahili mbalimbali kwa watumishi wa serikali, askari polisi wamekuwa wakiachwa nyuma sana; kwamba wameshuhudia posho zikipanda mara dufu kwa kada nyingine za watumishi selikalini huku fedha za kujikimu kwa askari polisi na magereza zikiwa palepale licha ya gharama za maisha kupanda kila kukicha.
“Ikumbukwe kwamba kitendo cha gharama za maisha kupanda huku mishahara na stahili nyingine za askari kubaki katika kiwango kilekile cha zamani ndicho kinachofanya askari wetu kuingia tamaa ya kupokea rushwa na kutoa vitisho kwa raia ili kujipatia kipato cha ziada kunusuru maisha yao na wategemezi wao,” alisema.
Nyerere pia aligusia utaratibu wa kujiendeleza kimasomo nje ya kituo cha kazi kwa maofisa polisi na magereza umekuwa na utata kwani kwa mujibu wa ‘general service order (GSO)’ na sheria nyingine za kazi, mtu akiajiriwa kwa mara ya kwanza na akataka kujiendeleza kimasomo nje ya kituo chake cha kazi anatakiwa kukaa kazini kwa muda wa miaka miwili au mitatu ndipo aweze kuomba ruhusa ya kwenda masomoni.
Alisema kuwa jeshi la magereza limechakachua sheria na kujiwekea utaratibu wake kwamba ili askari aweze kupata kibali cha kwenda masomoni ni mpaka akae miaka sita, yaani aende likizo mbili ndipo aombe kibali cha kwenda masomoni.
“Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuliagiza jeshi la magereza kufuta haraka sana masharti hayo ya kukaa kazini miaka sita ndipo askari apate fursa ya kujiendeleza kimasomo kwani hauna tija hata kidogo,” alisema.
Kuhusu msongamano gerezani alisema licha ya uwezo wa magereza ni kuhifadhi wafungwa na mahabusu 22,669 lakini kwa sasa inatunza zaidi ya wafungwa na mahabusu 45,000 kiwango ambacho kimezidi kwa zaidi ya asilimia 100.
Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama katika maoni yake yaliyowasilishwa na Augustine Maselle mbunge wa Mbogwe (CCM) ilishauri serikali kuhakikisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inawezeshwa kifedha ili ikamilishe kazi yake kwa wakati.
Alisema kuwa vitambulisho hivyo vitaisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwatambua Watanzania wanaostahili kupiga kura; kwamba ili lengo litimie mamlaka inahitaji vifaa 5000 aina ya “mobile enrollment unit” (biometric) dhidi ya 200 ilivyonavyo kwa sasa.
Alisema mamlaka hiyo imetengewa sh 151,200,000,000 ikilinganishwa na mahitaji halisi ya sh 270,000,000,000 ili kukamilisha zoezi muhimu la utoaji wa vitambulisho vya taifa kabla ya uchaguzi mkuu 2015.
Nao baadhi ya wabunge waliochangia hotuba ya Waziri Emmanuel Nchimbi licha ya kulipongeza jeshi la polisi kwa kasi kubwa lakini walilitaka likomeshe vitendo vya rushwa ndani yake na kubambikiza raia kesi.
Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, aliipongeza polisi kwa kazi yake ya kudhibiti wapinzani na kudai kuwa Rais Jakaya Kikwete amekuwa mpole mno kwani amekuwa akitukanwa mara kwa mara na wanasiasa hao.
Pia aliitaka serikali kuweka utaratibu wa kupiga marufuku uagizaji wa samani kwenye ofisi za serikali kutoka nje badala yake fedha hizo ziokolewe ili zibaki nchini kwa kununua samani hizo kutoka jeshi la magereza.
Esther Matiko (Viti Maalumu) na Mustapher Akonay (Mbulu-CHADEMA) waliitaka serikali kuzingatia haki za binadamu ikiwa ni jeshi la polisi kuacha vitendo vya kuua raia na washtakiwa wa makosa ya kawaida kupewa haki yao ya dhamana.
Naye Salehe Kidawa wa Viti Maalum CCM alilitaka jeshi la polisi kujenga utamaduni wa kuchukua hatua mapema katika kudhibiti matukio ambayo viashiria vyake vinajionyesha mapema.
Aligusia matukio ya Zanzibar ya kuvamiwa na kuuawa kwa baadhi ya viongozi wa dini akisema kuwa baada ya hali kuwa tete kwenye tukio la awali, polisi walipaswa kuchukua hatua zaidi za mapema ili kuepusha matukio mengine.

No comments:

Post a Comment