MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ametuma salaam za pole na rambirambi kwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini na Watanzania wote kwa ujumla kutokana na mlipuko uliotokea katika Kanisa la Olasiti, Jijini Arusha, uliosababisha vifo na majeruhi, huku wengine wakipatwa na mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo.TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mwenyekiti Mbowe
ametoa salaam hizo alipozungumza kwa njia ya simu na Katibu wa Baraza la
Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Antony Makundi, jioni ya Jumapili, baada ya
kupata taarifa za tukio la mlipuko huo unaodhaniwa kuwa ni bomu.
"Tumepokea habari
za tukio la mlipuko uliotokea leo (jana) katika Kanisa la Olasiti huko Arusha
kwa mshtuko na masikitiko makubwa. Kupitia kwako tunapenda kutoa pole kwa
familia, ndugu, jamaa na waumini wa Kanisa la Olasiti waliopatwa na msiba,
waliojeruhiwa na wengine waliopatwa na mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo
lisilokuwa la kawaida.
"Tunapenda pia
kupitia salaam hizi, kuwapatia pole waumini wote wa Kanisa Katoliki nchini na
Watanzania wote walioguswa na tukio hili la leo (jana). Mwenyezi Mungu awajaze
imani, nguvu na kuwapatia moyo wa subira nyote, wakati huu mgumu wa majonzi
mazito na kutafakari tukio hilo.
"Tumuombe
awajalie uponyaji wa haraka na ahueni na afya njema wale wote waliojeruhiwa na
waliopatwa na mshtuko kutokana na tukio hilo. Kupitia kwako pia naomba utufikishie
salaam zetu za pole za uongozi kwa Rais wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalemkutwa
kwa niaba ya uongozi wa Kanisa Katoliki nchini," alisema Mwenyekiti Mbowe.
Mwenyekiti Mbowe,
ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB) aliwataka Watanzania
wote kuwa watulivu wakati huu, wakati ambapo serikali kupitia vyombo vya dola
inafanya uchunguzi wa tukio hilo. Alisema serikali haina budi kuchunguza na
kutoa taarifa za matukio mengine yote ya namna hiyo ili kuwahakikishia
Watanzania wote haki na matumaini ya kuendelea kuishi kwa utulivu katika nchi
yao.
Imetolewa leo Mei 6,
2013,Dar es Salaam na;
Kurugenzi ya Habari na
Uenezi
Makao Makuu ya
CHADEMA.
No comments:
Post a Comment