Uamuzi wa Spika wa Bunge, Anne Makinda, Jumamosi kuunda kamati ya Bunge kwenda kuchunguza chanzo cha vurugu Mtwara umepingwa na Mbunge wa Ubungo, (Chadema), John Mnyika.
Mnyika anasema Bunge lilipaswa kuunda kamati teule badala yake Spika ameunda kamati yake maalum ambayo haitazingatia kwa ukamilifu matakwa ya sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge katika kuwahoji mashahidi na kuitisha ushahidi.
Anasema kamati teule inaundwa na Bunge lenyewe kwa mujibu wa kanuni ya 120 kipengele cha kwanza, lakini alichofanya Spika Makinda ni tofauti kabisa na kilichokusudiwa kufanyika kwa ajili ya sakata la Mtwara.
“Bunge halikuhojiwa kufanya uamuzi wa kuridhia ili iwe ni kamati ya Bunge…. Kipengele cha nne cha kanuni hiyo kinaeleza kwamba wajumbe wa kamati wateule watateuliwa na Spika na watamchagua mwenyekiti wa kamati kutoka miongoni mwao”
“Alichofanya Spika si utaratibu, yeye aliteua wajumbe na akateua mwenyekiti jambo ambalo ni kinyume cha kanuni, hivyo kamati ile haiwezi kuitwa kamati teule kwa kuwa haikukidhi kanuni za uundwaji wa kamati teule,”
Alisema kwa kutambua hilo ndiyo maana hata Spika mwenyewe hakuiita kamati teule bali alisema ameunda kamati maalum na kwamba kimsingi Spika ameunda kamati ndogo wakati suala la Mtwara ni kubwa ambalo lilihitaji kushughulikiwa na kamati teule.
Alisema kamati teule inamamlaka makubwa zaidi kwa mujibu wa kanuni za Bunge na Sheria ya Kinga, haki na madaraka ya Bunge.
Anasema Kamati ya Makinda inaweza kufunika kombe mwanaharamu apite kwani mgogoro wa Mtwara ni matokeo ya maazimio ya Bunge yaliyohusu miradi ya maendeleo, rasilimali za taifa na mapambano dhidi ya ufisadi katika sekta za nishati na madini ya Richmond, Kiwira, kamati ya Bomani, Jairo, Mafuta, mpango wa umeme wa dharura na na gesi asilia.
No comments:
Post a Comment