Monday, May 27, 2013

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/14

 I.   UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, hakuna ubishi kwamba ardhi ndio msingi mkuu wa uchumu wa taifa lolote, na kwa maana hiyo ardhi ni msingi maisha ya mwanadamu.  Ardhi ni miongoni mwa vitu vikuu vine vinavyohitajika ili taifa liendelee.  Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwashi kusema “Ili taifa liendelee linahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikijiuliza kuhusu chimbuko la umasikini uliokithiri Tanzania kwa kuzingatia vigezo vya maendeleo alivyotoa Hayati Mwalimu Nyerere.  Baada ya kufanya marejeo ya machapisho mbalimbali lakini pia baada yakupata uzoefu wa uongozi kama Mbunge wa Wananchi na hasa kama Waziri Kivuli kwa Arhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na kwa kuzingatia mwenendo halisi wa watawala hapa Tanzania nimegundua kuwa kiwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchi yetu sio watu (watu wapo wengi sana takribani milioni 45), tatizo sio ardhi (hiyo ipo ya kutosha na ziada takribani hekta milioni 94.3[1]).

Mheshimiwa Spika, tatizo ni “siasa safi na uongozi bora”. Tofauti na Kauli Mbiu mkakati za kisiasa enzi za Mwalimu, kwamba Sisa ni kilimo,  Uhuru na Kazi, Kilimo cha Kufa na Kupona, sasa hivi tunashuhudia siasa za watawala za kuongeza umasikini wan chi hii “kwa ari na kasi zaidi, tunashuhudia watawala wakijigamba kwamba wamethubutu na wameweza” kuwa mafisadi wa rasilimali za nchi hii.
Mheshimiwa Spika, maneno niliyoyatumia hivi punde hayanifurahishi hata kidogo, lakini nimelazimika kuyasema kwa kuwa sioni watawala wa nchi hii wakifikiri namna ya kumkomboa mtanzania kutoka kwenye wimbi la umasikini, bali kila mmoja anajitahidi kujilimbikizia mali hasa kwa hofu ya kuondolewa madarakani (akakosa namna ya kuishi) kutokana na kuenea kwa kasi na kuungwa mkono kwa wingi na wananchi kwa chama kikuu cha upinzani nchini cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mheshimiwa Spika, nasikitika sana kwamba badala ya Serikali ya CCM kutumia muda na rasilimali ilizo nazo kutatua matatizo sugu ya kiuchumi ya taifa hili (hususan uporaji wa ardhi ya wananchi), inatumia fedha nyingi za umma kupambana na CHADEMA ambayo inatetea maslahi ya wananchi.

Mheshimiwa Spika,  Nchii hii ina rasilimali nyingi sana ikiwemo ardhi  ambazo zingeweza kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za ulimwengu wa pili kiuchumi,  lakini tuna tatizo la uhaba wa  viongozi wenye “ufahamu, maadili  na busara” ya kutumia rasilimali hizi kwa maslahi ya taifa.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ombwe la uongozi katika taifa hili, na kutokana na “ubinafsi, ulafi na ufisadi” wa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za nchi yetu, leo taifa hili ni masikini, miaka hamsini na mbili baada ya uhuru.

Mhshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA imekuwa ikibainisha mapungufu na kasoro nyingi katika masuala ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tangu mwaka 2011 hadi leo, lakini Serikali hii ya CCM imeendelea kuwa na shingo ngumu kuyafanyia kazi mapendekezo ya Kambi ya Upinzani jambo ambalo linaendelea kusababisha migogoro mingi na ufisadi katika umiliki na matumizi ya ardhi hapa nchini

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya msemaji mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika bajeti ya wizara hii kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilianisha matatizo makubwa ya  ardhi nyumba na maendeleo ya makazi na kuitaka Serikali kutafuta ufumbuzi kwa kuchukua hatua za haraka. Matatizo hayo yalikuwa kama ifuatavyo:-

1.      Uporaji wa ardhi ya Tanzania unaofanywa chini ya usimamizi wa Serikali kwa mbinu au hila ya uwekezaji,
2.      Ufisadi wa ardhi unaofanywa na viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi  kwa kuuziana ardhi kwa bei ya kutupwa,
3.      Ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria namba 5 ya ardhi ya vijiji ambapo viongozi wa Serikali walikuwa wakigawa ardhiki holela bila kuzingatia matakwa ya sheria hizo,
4.      Migogoro mikubwa ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji ambayo kwa nyakati tofauti imepelekea umwagaji wa damu miongoni mwa wananchi,
5.      Matatizo makubwa katika tathmini ya malipo ya fidia kwa wananchi wanaotakiwa kuondoka katika maeneo yao kupisha matumizi mapya ya ardhi,
6.      Kuendelea kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi jambo ambalo limesababisha wananchi kuendelea kuishi katika makazi duni na hivyo kuhatarisha usalama wao na kutweza utu wao,
7.       Serikali na taasisi zake kutolipa kodi za pango kwa wakati kwa Shrika la Nyumba la Taifa na hivyo kulirudhisha nyuma kimaendeleo, na
8.      Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba bora na Vifaa vya Ujenzi kushindwa  kuleta mabadiliko kutokana na kuongezeka kwa nyumba zisizo bora ( kama vile nyumba za tembe, tope na nyasi) na kuongezeka kwa bei ya vifaa vya ujenzi

Bonyeza Read More Kuendelea


Mheshimiwa Spika, Aidha, katika bajeti ya wizara hii kwa mwaka 2012/2013, Kambi Rasmi ya Upinzani iliendelea kuipigania ardhi ya watanzania inayoporwa kwa kuitaka Serikali kufanya yafuatayo:-

1.      Kuyarejesha kwa wananchi, mashamba yote yaliyobinafsishwa ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza,
2.      Kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na vijiji vya Gijedabung,  Ayamango[2] na Gedamar[3] katika Wilaya ya Babati Mkoani Manyara ambapo mamlaka ya hifadhi ilitoa amri kwa wananchi wa vijiji hivyo kuondoka kwa kuwa walikuwa wako ndani ya hifadhi,
3.      Kutatua migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima hasa katika Wilaya ya Karagwa na Biharamulo  Mkoani Kagera ambapo wananchi walifukuzwa kwenye maeneo yao ya kilimo na maeneo hayo kugawiwa kwa wafugaji matajiri bila wananchi kuhusishwa,
4.      Kulipa fidia stahiki kwa wananchi wanaotakiwa kuondoka katika maeneo yao kupisha matumizi mapya ya ardhi hasa katika maeneo ya Kibamba –Luguruni, Kwembe Kati na Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam,
5.      Kuandaa mpango mkakati na endelevu wa kukomesha uvamizi wa ardhi (hasa katika Manispaa ya Kinondoni ) unaofanywa na magenge ya watu wenye silaha  wanaovamia maeneo ya watu, kuharibu mali na kuyakalia maeneo hayo kwa nguvu jambo linalosababisha uvunjifu wa amani na hatimaye vifo,
6.      Kubatilisha mkataba wa kifisadi kati Kampuni ya Uwindaji ya Game Frontiers of Tanzania Limited na Kampuni mbili za nje za uchimbaji madini za Uranium Resourses PLC na Western Metals, kufanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya Uranium kwenye kitalu cha uwindaji katika kijiji cha Mbarang’andu kinyume cha sheria.
7.      Kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Kodi za Nyumba (Real Estate Regulatory Authority) ili kuratibu, kuweka viwango na miongozo ya kodi za nyumba ili kuwaondolea wananchi wapangaji wa nyumba adha kubwa ya gharama kubwa za pango zisizo na viwango.
Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali hii ya CCM kuoneka kutojali maslahi ya wananchi katika kumiliki na kutumia ardhi yao, na baada ya kuongezeka kwa kasi ya kugawa ardhi kwa wageni kwa hila ya uwekezaji, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA iliendelea kupambana kuitetea ardhi ya Tanzania ili wananchi wawe wanufaika wa kwanza wa rasilimali ardhi.

Mheshimiwa Spika, Safari hii, Kambi Rasmi ya Upinzani ilileta hoja binafsi bungeni tarehe 8 Novemba, 2012 kwa ajili ya hatua za kibunge baada ya Serikali kuoneka kutojali uporaji wa ardhi ya wananchi unaofanywa kwa kisingizio cha uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, katika hoja hiyo, Bunge liliazimia kwamba :
  1. Zoezi la ugawaji ardhi kwa wawekezaji wa nje na ndani lisitishwe hadi hapo tathmini ya kina itakapofanyika kubaini ni kiasi gani cha ardhi kipo mikononi mwa wawekezaji na wasio wawekezaji.
  2. Tathmini ya kina ifanyike kuweza kubaini raia wa kigeni na wa ndani waliojipatia ardhi kinyemela kupitia serikali za vijiji kinyume na matakwa ya sheria ya ardhi Na. 5 ya mwaka 1999.

Mheshimiwa Spika, baada ya mvutano mkali kati ya wabunge wa CCM wakiisaidia Serikali yao dhidi ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hatimaye Serikali ilikubali kwa shingo upande kufanya tathimini ya ardhi iliyoko mikononi mwa wageni  lakini ilikataa kusitisha uwagaji wa ardhi kwa wageni. Hata hivyo, Serikali ilitakiwa kuleta ripoti ya tathmini hiyo bungeni mwezi Aprili, 2013,  lakini mpaka sasa Serikali haijafanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, kabla sijajielekeza katika mambo mahsusi yanayohusu wiza hii kwa mwaka wa fedha 2013/2014 napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuitaka Serikali ilieleze Bunge hili na wananchi wote, kwamba imetatua kwa kiasi gani matatizo yaliyoainishwa hapo juu na imetekeleza kwa kiasi gani mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani yaliyoorodheshwa hapo juu (moja baada ya jingine) ya tangu mwaka 2011 hadi leo?. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili imetekeleza vipi maazimio ya bunge ya tarehe 8 Novemba, 2012 yaliyoitaka Serikali kufanya tathmini ya ardhi iliyopo chini ya umiliki wa wageni (wawekezaji) na kuleta taarifa ya tathmini hiyo bungeni mwezi Aprili, 2013?[
Mheshimiwa Spika, ni masikitiko yangu kwamba mpaka nawasilisha bajeti hii, licha ya kupeleka taarifa ya maandishi kwenye ofisi yako nikikutaka uielekeze serikali kuwasilisha ripoti husika mbele ya Bunge hili tukufu ,ili kuliwezesha Bunge kufanya maamuzi ya msingi/muhimu katika sekta ya ardhi sioni jitihada zozote za kuleta ripoti hiyo katika mkutano huu wa bunge.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  imezipata,  ambazo tunaamini ndicho chanzo cha serikali kushindwa kuleta ripoti kwa wakati ni kushindwa kwa timu iliyopewa jukumu la kuzunguka nchi nzima kufanya tathmini  kushindwa kumaliza kazi ndani ya muda iliyopewa, sambamba na kukumbana na upinzani mkubwa wa kupata taarifa kutoka kwenye mashamba ambayo yanamilikiwa na viongozi na vigogo wakubwa serikalini!


II. UWEKEZAJI KATIKA ARDHI YA TANZANIA 
Mheshimiwa Spika, Tanzania  ina ukubwa wa Zaidi ya Km2 940,000. Kwa mujibu wa sheria  za ardhi  na 4 na 5  za 1999 ardhi ya Tanzania imegawanyika  katika makundi 3 ambayo ni ardhi ya Jumla, ardhi ya kijiji na ardhi ya hifadhi. Hadi sasa ardhi ya hifadhi  inaelezewa kufikia zaidi ya 30% ya ardhi yote. Ardhi yenye rutuba  na inayofaa  kwa kilimo  cha aina mbali mbali  inakadiriwa kufikia hekta milioni 80, eneo linalotumika kwa sasa  linakadiriwa kufika 10% tu.

Mheshimiwa Spika, shughuli za uwekezaji huongozwa  na sheria ya uwekezaji ya mwaka namba 26 ya  1997. Hata hivyo sheria ya ardhi inatamka  wazi kuwa  wasio raia  wa Tanzania hawaruhusiwi kumiliki ardhi isipokuwa kwa matumizi ya uwekezaji  ambapo hupewa hati hafifu kupitia kituo cha uwekezaji  (TIC)

Mheshimiwa Spika, pamoja na katazo hili la kisheria,  tumeshuhudia  mara nyingi  wawekezaj wasio watanzania wakimiliki ardhi,wakiwaondoa  wamiliki wa asili katika maeneo yao na kuharibu kabisa mifumo yao ya maisha.Hii mara nyingi imetokea kwa sababu ya kukiuka kwa makusudi sheria na taratibu zilizopo , udhaifu wa mifumo ya utekelezaji  wa sheria  na dharau kwa vyombo vya ngazi za chini za utawala  na wananchi wao kwa kuwa  maamuzi hufanywa na ngazi za juu.

Mheshimiwa Spika, ingawa karibu kila eneo limevutia wawekezaji wa aina fulani katika ardhi, lakini maeneo ya uchimbaji madini, shughuli za wanyhama pori (kama vile uwindaji, mahoteli, na utalii) pamoja na kilimo yameonekana kuwavutia zaidi wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, katika Kilimo, ambako kuna wazalishaji wadogo, shabaha ya hivi karibuni imekuwa ni kuwekeza  kwenye kilimo cha “nishati uoto” kwa ajili ya mafuta ya magari na mitambo. Jambo la kutilia shaka ni kwamba; wawekezaji wengi sasa wanaenda vijijini kutafuta ardhi wenyewe badala ya kupewa na kituo cha uwekezaji kama sheria inavyotaka. Kutokana na wanavijiji kutokuwa  na uwezo wa kimaarifa na ujuzi wa kujadiliana na wawekezaji kwa mizania sawa, wamekuwa wakitoa ardhi kiholela  bila kufuata taratibu za  kisheria .Pale ambapo wanavijiji  wamethubutu kuhoji, sheria imetafsiriwa  vibaya kuwapora ardhi  na haki yao. Kwa mfano; sheria ya ardhi namba 4 ya 1999 inaeleza kwamba:   ardhi ya kijiji isiyotumika, wala kukaliwa, ni ardhi ya jumla na hivyo inaweza kuchukuliwa na serikali kuu wakati wowote ingawa ukweli unabaki pale pale kuwa ni ardhi ya kijiji.

III. UKADIRIFU NA TATHMINI YA WAMILIKI WA MASHAMBA  TANZANIA BARA 2013[4]

Mheshimiwa Spika, kikosi kazi kilichopewa kazi na Wizara ya Ardhi , kilipewa jukumu la kufanya tahmini nchi nzima ya watu wanaomiliki mashamba makubwa .Mashamba yaliyofanyiwa tathmini ni yale tu yenye ukubwa zaidi ya ekari 50 (Hekta 20).

Malengo ya Tathmini:
i)                    Kufanya uchunguzi wa  mashamba ya wawekezaji wa ndani na wa nje  yaliyopatikana kwa njia halali  na ambazo sio halali,
ii)                  Utaratibu uliotumiwa na wawekezaji kupata mashamba
iii)                Kuangalia uhalali wa umiliki  (kwa wenye hatimiliki)au ukodishaji wa mashamba,
iv)                Kutambua tozo mbali mbali (land rent,fees,levies) za ardhi  au malipo mengine yeyote  yananayotakiwa kulipwa kutoka katika mashamba husika,
v)                  Kutambua matumizi ya ardhi, kama yanaendana na matakwa ya Mkataba,
vi)                Kutambua maendelezo yaliyofanywa katika mashamba husika, kama yapo!
vii)              Kutambua migogoro ya ardhi (kama ipo) kati ya wamiliki wa mashamba na wanavijiji na hatua ambazo zimeshachukuliwa/zinazochukuliwa kutatua migogoro husika
viii)            Kutambua faida iliyotokana na uwekezaji na kwa namna vijiji vinavyowazunguka wawekezaji  vimenufaika kutokana na uwekezaji huo!

Mheshimiwa  Spika, tathmini hii ilikuwa muhimu kutokana na ukweli kwamba  ongezeko  la mahitaji ya chakula duniani, nishati mbadala, mali ghafi,  mbao na uhifadhi wa misitu imesababisha ongezeko kubwa la uhitaji wa ardhi duniani . Uhitaji huu[5] ndio unazisukuma kwa kasi kubwa  nchi zilizoendelea kuja Afrika kutafuta ardhi.[6]

Mheshimiwa Spika, watafiti hawakutembelea nchi nzima, walitembelea wilaya 79 tu! na  kukagua  mashamba 763 tu (sampling). Licha uchache wa maeneo yaliyotembelewa ripoti hii sio ya kupuuzwa kwa kuwa inatoa sura ambayo,yawezekana ikawa ndio hali halisi ya maeneo mengine ya nchi.
Utafiti umegundua yafuatayo:
1) Umiliki.
Imegundulika kwamba katika mashamba makubwa  763 yaliyotembelewa, mashamba 455 sawa na 65.8% yalikuwa yanamilikiwa na watanzania wenyewe  (individual ownership), ikilinganishwa na 14 (2%) yaliyokuwa chini ya umiliki wa raia wa kigeni . Mashamba yaliyokuwa yanamilikiwa kwa ubia   kati ya watanzania na wageni yalikuwa 31 (4.4%).
Hata hivyo, licha ya raia wa kigeni kuwa na mashamba machache kiidadi walikuwa wanamiliki  maeneo makubwa ya ardhi ukilinganisha na watanzania. Timu ya uchunguzi imebainisha kwamba hali hii inatakiwa iangaliwe kwa jicho pana!
Kielelezo Na. 1
Aina ya umiliki
Wastan wa ukubwa wa shamba
Idadi ya Mashamba
Jumla (Ekari)
% ya  eneo lote



Kampuni zinazomilikiwa na watanzania
2,972.03
72
213,986.38
23.71



Kampuni zinazomilikiwa kwa ubia kati ya watanzania na wageni
3,091.66
31
95,841.37
10.62



Kampuni za Kigeni
6,301.55
31
195,348.04
21.65



Mashamba yanayomilikiwa na watanzania (individuals)
280.59
455
127,669.61
14.15



Mashamba yanayomilikiwa na wageni (individual)
2,547.18
14
35,660.50
3.95



Mashamba yanayomilikiwa na Taasisi
2,049
63
129,108.09
14.31



 Mashamba ambayo hayajulikani ya nani
4,191.58
25
104,789.39
11.61



Jumla
1,305
691
902,403.38
100




Mheshimiwa Spika, utafiti umeonyesha kwamba kuna tofauti kubwa sana ya umiliki wa mashamba makubwa kati ya raia wa kigeni na watanzania. Wakati watanzania (mmoja mmoja) wanaonekana kumiliki 60% ya ‘mashamba’ yote yaliyotembelewa, mgao wao katika jumla kuu ni ekari  127,670  ambayo ni sawa na  14% ya eneo lililofanyiwa utafiti. Wakati huo huo, makampuni yanayomilikiwa na  wageni, ambayo wana miliki asilimia 4% tu ya idadi ya mashamba yaliyotembelewa, lakini wanahodhi/miliki eneo lenye ukubwa wa Zaidi ya   21% (ekari 195,348 ) ya ardhi yote iliyofanyiwa utafiti. Mashamba   yanayomilikiwa na makampuni ya kitanzania ni ekari 213, 986 tu.
 Mheshimiwa Spika, kwa wastani makampuni ya kigeni  wana maeneo makubwa ya mashamba , yakifuatiwa na makampuni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya watanzania na raia wa kigeni. Ni muhimu hapa ikaeleweka kwamba, katika makampuni ambayo watanzania inasemekana wana ubia, hisa zao ni finyu sana kati  ya (1%-10%)..ya hisa zote.
Mheshimiwa Spika,  utafiti umeonyesha pia  kwamba;  wakati raia wa kigeni  kwa wastani wanamiliki shamba lenye ukubwa  wa ekari 6,302, raia wa kitanzania kwa wastani wanamiliki shamba lenye ukubwa wa ekari  280 tu! Aidha, mashamba mengi ya raia wa kigeni yalikuwa  na ukubwa  unaokaribia ekari  1,526, ambao ni mara 18 zaidi ya mashamba yanayomilikiwa na watanzania. Wataalam hao wanazidi kusisitiza kwamba:   ni ukweli usiofichika kwamba:  umiliki wa mashamba makubwa umetawaliwa na raia wa kigeni.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu wabunge na wananchi  wakaelewa kwamba;   kinachozungumziwa hapa  ni mashamba ambayo tayari  yana hati miliki (miaka 33, 66 au 99) na sio ardhi za vijiji ambazo ( kisheria ziko chini ya vijiji)lakini  zinaweza kubadilishwa wakati wowote na kupangiwa matumizi mengine pasipo kijiji kuwa na mamlaka ya kuzuia. Hii inashabihiana kabisa na utafiti uliofanywa  na Oxfarm uliobainisha kwamba katika nchi zinazoendelea kuna  zaidi  ya ekari 203 milioni  ambazo ziko chini /zimechukuliwa na raia/wawekezaji wa kigeni.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya mashamba  yaligundulika kwamba yanamilikiwa  na maafisa waandamizi  wa serikali, ambao taarifa za  mashamba yao zilishindwa  kupatikana katika utafiti huu wa serikali, chini ya usimamizi wa wizara ya ardhi  kwa sababu  wamiliki husika  hawakuwepo kwenye mashamba yao na walinzi wao hawakuwa tayari kutoa taarifa  za mashamba husika zaidi ya kutaja majina ya wamiliki wa mashamba!hii ilitokea Dakawa, na ilihusisha mashamba 28!  Ni azma ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwataja wamiliki wa mashamba hayo, kama serikali itagoma kufanya hivyo!

Mheshimiwa Spika, katika kile ambacho hakikutarajiwa uchunguzi umebaini kwamba kuna makampuni ya kigeni na raia wa kigeni wanaomiliki ardhi kimila (customary land right) ambayo kwa mujibu wa sheria za nchi,   ni maalum/ mahsusi kwa raia wa Tanzania pekee mpaka pale ambapo ardhi husika itahuilishwa (transferred from one category to another).  Huu ni uvunjwaji mkubwa sana wa sheria ya umiliki ardhi kimila… Aidha, utafiti umegundua pia kwamba; wageni wanamiliki ardhi ambayo haijulikani iko kwenye kundi gani (‘the unspecified category’) la ardhi ambayo ina ukubwa wa ekari 94,360 (10%ya ardhi iliyofanyiwa utafiti).
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha na kushtua sana kama ardhi yenye ukubwa kiasi hicho iko mikononi mwa wawekeaji wa  kigeni. Aidha, ni jambo la kushangaza sana kama Wizara haifahamu kiasi kikubwa hivyo cha ardhi kiko katika himaya ya nani? Kama wizara au mamlaka zilizo chini yake hazijui jambo hili , ni nani atakaye jua?

IV.  MUDA WA UMILIKI WA MASHAMBA

Mheshimiwa Spika, utafiti umeonyesha sehemu kubwa ya makampuni ya kigeni au raia wa kigeni wanaomiliki ardhi  ndio wanaoongoza kwa kuwa na mikataba ya muda mrefu ya umiliki  wa ardhi, yaani  miaka 99! (ekari 500,135 kati ya 902,403 zilizofanyiwa utafiti). Halika dhalika utafiti umegundua pia kuna wawekezaji ambao wana umiliki wa ardhi wa kimila (Customary Right of Occupancy). Kitu aambacho ni kinyume kabisa na sheria za nchi , ambazo zinampa fursa Mtanzania tu kuwa na umiliki wa aina hiyo!

 V. UPORAJI WA ARDHI

Mheshimiwa Spika,  imebainika pia kwamba watu wenye fedha na watu wenye ushawishi wa kisiasa wamekuwa  wakitumia nguvu zao kushawishi  na kupoka ardhi za vijiji , katika mazingira ambayo hakuna ushirikishwaji wa wanakijiji (55.11% ya maeneo yaliyotembelewa, wanakijiji waliohojiwa walikiri hakukuwa na  ushirikishwaji wakati ardhi yao inapochukuliwa). Ushawishi husika ni pamoja na kutoa ahadi za uongo na hongo kwa viongozi wa serikali za vijiji kama ilivyotokea kwa makampuni  ya Bioshape (Wilaya ya Kilwa  na Sun Biofuels- Wilaya ya Kisarawe). [7]

Mheshimiwa Spika, utafiti pia iligundua kwamba fidia kwa wananchi wanaoondolewa kwenye maeneo yao ili kupisha uwekezaji kama  ilivyoelekezwa na  kifungu 34(3)b   cha  sheria ya ardhi, namba 4 ya 1999 hailipwi.

VI. TOZO ZA ARDHI ( LAND RENT , FEES,LEVIES  AND OTHER PAYMENTS)
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 33  cha Sheria ya Ardhi (Sheria na 4,ya mwaka 1999) kinatamka kwamba , mwenye hati miliki  anatakiwa, pamoja na masharti ya vifungu vingine vya sharia,  kulipa kodi ya  mwaka  kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Fedha za Umma (Public Finance Act). Utafiti umegundua kwamba kati ya mashamba 763 yaliyotembelewa, ni mashamba 278 (36.4%) tu ndio yaliyolipa kodi ya ardhi (2012) kama sheria inavyotaka. Wamiliki wa mashamba 432 (56.6%) waliohojiwa walikiri kwamba hawajalipa kodi husika.  Halikadhalika utafiti umegundua kwamba 43.47% ya wenye mashamba waliohojiwa  walikiri kwamba hawajawahi kulipa kodi ya ardhi toka  walipomilikishwa mashamba hayo!. Hii inaonyesha kwamba , hata wale watu ambao wanamiliki ardhi kihalali,  uhalali wa umiliki wao una mashaka  kutokana na kutokidhi takwa muhimu la kumiliki ardhi husika ambalo ni ulipaji wa kodi ya ardhi. Zaidi ya hayo, utafiti umeonyesha pia kwamba;   mashamba 643 kati  ya 763 yaliyotembelewa yalishindwa kutoa ushahidi (risiti) kuonyesha kama ni kweli walikuwa wanalipa kodi za ardhi kama matakwa ya kisheria yanavyoelekeza.


VII. UWEKEZAJI KATIKA NISHATI UOTO (BIOFUELS) NA MUSTAKABALI WA ARDHI YA WATANZANIA

Mheshimiwa Spika, kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia  na mabadiliko hasi ya hali ya hewa  duniani vimechangia kwa kiasi kikubwa  wimbi la utafutaji  nishati mbadala ili kukabiliana  na uchafuzi wa hali ya hewa na pia kuleta uhuru  katika matumizi ya nishati. Kuanzia miaka ya 2000, matumizi ya nishati yalianza kushika kasi sana katika maeneo mbali mbali duniani. Kwa Tanzania, tangu nishati hiyo ianze kuchukua  mkondo wake  ikiwahusisha  wawekezaji wakubwa na wadogo , ujio wake umeshuhudia kiasi kikubwa cha ardhi kikichukuliwa  kwa ajili ya mashamba ya kuzalisha nishati hiyo.

Mheshimiwa Spika, watetezi wa Nishati Uoto, wamekuwa wakiipigia chapuo aina hiyo ya nishati kwa kutaja faida zake ambazo ni pamoja na kuzalisha na kukuza ajira kwa wananchi waishio maeneo yalipo mashamba au viwanda vinavyozalisha aina mbalimbali za nishati hiyo, kuongeza mapato kwa wakulima wadogo na  kupambana na gesi zijulikanazo kama Green house gases (GHG). (Wizara ya Nishati na Madini, 2006)[8]

Mheshimiwa Spika, maeneo kadhaa nchini yamekuwa katika utekelezaji wa miradi ya mashamba ya kuzalisha Nishati Uoto kama vile Kilwa, Kisarawe, Bagamoyo, Arusha, Manyara, Shinyanga, Singida na Mwanza. Tokea makampuni haya ya kigeni,yalipokabidhiwa ardhi ya watanzania kama njugu, na katika mazingira mengine chini ya ukuwadi wa Kituo cha uwekezaji nchini hakuna faida “endelevu” iliyopatikana zaidi ya kuongezeka kwa migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wanavijiji na kutamalaki kwa rushwa, udanganyifu, hadaa na mizengwe  miongoni mwa watendaji wa vyombo vinavyosimamia masuala ya ardhi, wananchi na  wawekezaji. 

Mheshimiwa Spika, taratibu nyingi za ugawaji na uhawilishaji wa ardhi zilikiukwa makusudi kwa lengo la kuwapendelea wawekezaji hasa wa kigeni. Katika maeneo ya uwekezaji, mifumo ya maisha ya wananchi imehatarishwa kwa kunyang’anywa ardhi walizokuwa wakitumia kwa shughuli za kilimo, malisho na shughuli nyinginezo za uzalishaji na za kijamii. Wale waliobahatika kupata ajira katika kampuni za wawekezaji nao wameachwa njiani hawajui kesho yao baada ya wawekezaji kuwaachisha kazi na wengine  kususa miradi yao,  kuwatelekeza wafanyakazi na kutokomea kusikojulikana. 

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa  taratibu za kisera na kisheria nchini ni dhaifu katika usimamizi wa Nishati Uoto, uanzishwaji wa miradi ya nishati hii nchini kwa kiwango fulani  umesababisha kuwapo kwa unyonyaji wa rasilimali muhimu za taifa ambazo ni ardhi, maji,misitu na nguvu kazi ya  watanzania. 

VIII. HALI YA MASHAMBA WALIYOPORWA WANANCHI NA KUKABIDHIWA WAWEKEZAJI KWA KILIMO CHA MAZAO YA NISHATI UOTO (BIOFUEL)

Mheshimiwa Spika,  uchunguzi umebaini kuwa katika wilaya ya Kilwa,mwekezaji alikuwa kampuni iitwayo Bioshape kutoka  nchini Uholanzi. Kampuni hii ilipewa ardhi yenye ukubwa wa hekta 80,000 kwalengo la kulima zao la mbono kaburi.Ardhi hiyo ilihusisha  vijiji vine ambavyo ni Mavuji, Migelegele,Liwiti na Inokwe.  Mwekezaji hakuwahi kulima eneo lote bali alilima hekta 800 ambazo ni shamba la mfano lililopo katika kijiji cha Mavuji.

Mheshimiwa Spika, dhana ya uwekezaji  ni jitihada  za kugeuza mali asili  za nchi kuwa  katika rasilimali kwa kutumia nyenzo  kama mtaji , teknolojia na nguvu kazi. Ziada inayotokana na uzalishaji hurejeshwa  katika kuimarisha miundombinu , mitaji, teknolojia  na rasilimali watu ( watu, fedha, malighafi ) ili faida iweze  kupatikana na pale inapopatikana  faida ndipo  matunda ya maendeleo huonekana!

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tulifanya makosa ya kutokulinda maslahi ya watanzania katika uvunaji wa madini mbali mbali yanayopatikana nchini, na kama ambavyo tunaelekea kufanya makosa katika uvunaji na nishati muhimu ya gesi , ama kutokana kuwa na viongozi wasio na upeo/wabinafsi/wanaoendekeza njaa/waliokosa uzalendo kutokana na nchi yetu kutokuwa na intelijensia ya kiuchumi, nchi yetu imejikuta ikikaribisha wawekezaji wa hovyo,wasio na mitaji, teknolojia wala nguvu kazi!

Mheshimiwa Spika, serikali ilikaribisha makampuni ya kigeni  pasipo hata kuandaa sera kwa ajili ya nishati uoto. Sote tunafahamu fika kwamba  sera ndio dira, na  mwongozo utakaoelekeza nini kifanyike,kwa namna gani na malengo yapi. Uzembe huu umelisababishia Taifa na vijiji vilivyoporwa mashamba yao hasara kubwa. Ikumbukwe kwamba katika maeneo mengi kama sio yote wananchi walipoteza ardhi yao pasipo kulipwa fidia,waliolipwa fidia walilipwa kidogo sana,ajira zilizopatikana katika mashamba hazikuwa endelevu. Maeneo yaliyokuwa mapori huku yakiwanufaisha  wananchi kwa kufanya  shughuli  za kijamii kama kupata miti ya dawa ,kuchota maji,kukata kuni na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi, hivi sasa  yamegeuka kuwa majangwa ). Na katika mazingira mengine vijiji vilikumbwa na njaa kwa sababu ardhi  waliyokuwa wakiitumia kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo,  walipewa wawekezaji ambao walijikita  katika uzalishaji wa mibono!

Mheshimiwa Spika, kutokana na uzembe wa serikali, wawekezaji waliokuja kwa ahadi kemkem waliiishia kutelekeza mashamba. Mheshimiwa Spika, kwa ufupi naomba Bunge lako tukufu lipate taarifa juu ya hali ya maelfu ya hekta ya ardhi zilizoporwa kwa wanakijiji, kwa mabavu kulikoenda sambamba na kuvunjwa kwa sheria kwa makusudi : Naamini taarifa hii itapelekea Bunge lako tukufu, kutoa au kufanya maamuzi yenye busara kwa manufaa ya taifa  na wananchi wake:

 1. Sun Biofuel  (Mwekezaji toka Uingereza) alipewa eneo la  – Kisarawe  ardhi ya  vijiji 11  ( hekta 8200-9000) kwa miaka  99, akiahidi kutengeneza ajira  5000 [9]. Walianza kusafisa eneo kwa ajili ya kupanda mazao mwezi Juini, 2009,na kufanikiwa kupanda  hekta 600 ilipofika Novemba, 2009. Waliahidi kusaidia wakulima wadogo wadogo wa pembezoni, ahadi ambayo haikutimia mpaka walipositisha shughuli za uwekezaji (HAKIARDHI). Mwaka 2011 eneo husika liliuzwa  kwa mwekezaji mpya 30 Degree ( ubia kati ya Raia wa Mauritania 90% na Mtanzania 10%. Mwaka 2012 kampuni ilifilisika .Imeachisha kazi ghafla wafanyakazi 750..ahadi zake zote za kiuchumi na kijamii zilizoahidiwa zikaishia hapo…

2. Africa Biofuel & Emmission Reduction Co. (Tanzania Ltd).[10]Ardhi waliyopewa   hekta 60,000 ,  wilaya ya Biharamulo (Biofuel)[11] Taarifa za serikali zinaonyesha ,kampuni ilisimamishwa  na ofisi ya makamu wa Rais  kutokama na masuala yanayohusiana na masuala ya ardhi  ( locher 2010)/wako kwenye hatua za mwisho za  kumilikiswa eneo na walitaraji ingia mkataba 2010.

3. Agrisol energy Tanzania ( ubia kati ya   Serengeti Adivisors ltd na Agrisol Energy  LLC / group (IOWA based ) . Mshirika: Pharos Global Agricultures Fund, chini ya usimamizi wa Pharos  Financial Group (Dubai), wilaya ya Mpanda –Rukwa na Kigoma (Oakland Institute) Mchakato wa kupata eneo la Rukwa bado unaendelea  ( 325117 ha). Eneo ambalo limeshakabidhiwa kwa mwekezaji  hekta10,000( Lugufu) na 3250 (Basansa)- kigoma .Agrisol Energy Tz inamiliki  25% ya hisa za kampuni. Kampuni hii imeungana na Kampuni ya Kitanzania the Serengeti  Advisors (Inayoundwa na vigogo/viongozi wastaafu wa serikali wenye ushawishi mkubwa sana kwenye serikali ya CCM)  ili kuhakikisha kampuni inapata ardhi  kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mpanda ( Baha 2011).

4. Agro Forest Plantation ( Misri), Rufiji  ,(kilimo cha sukari kwa soko la Misri na la ndani) ardhi waliyoomba  ni hekta 10,000  iliyopo ni hekta  8,000  (RUBADA) ,  Ilikuwa ardhi ya Kijiji (Mojoro,Chumbi A,B,C na Ruma Villages ,imeasjiliwa na TIC   Desemba,  2011, na inatarajiwa kuanza kazi  Desemba 2014 

5. Arkadia  Ltd (Italia), imesajiliwa Brela Septembe 2007 , Wilaya ya Mkinga( jatropha ),  Wilaya iliidhinisha hekta 500,  wizara ya adhi  imesajili/register hekta 25,000 ( Project bado ina utata  ,maofisa wa wilaya  hawaelewi ni vigezo gani na  kwa utaratibu upi kampuni iliweza kupewa na wizara ya ardhi   hekta 25,000  (Sulle 2012)

6.Bagamoyo Eco Energy Ltd. (Eco Energy Tanzania Ltd). Kampuni hii ina mchanganyiko wa wamiliki toka mwaka 2009. Eco Energy Bagamoyo[12] inamilikiwa kwa 100% na Agro EcoEnergy Tanzania (ambayo nayo inamilikiwa  93.5% na EcoEnergy Africa  AB, na 5%  Tanzania Petroleum   Development Co Ltd.(TPDC ) na 1.5% Community Finance  Corporation Ltd(CFC).

EcoEnergy Africa nayo inamilikiwa na  Eco Development Europe AB , mwanahisa mdogo wa SEKAB (SEKAB ndiye alikuwa mmiliki wa awali ,kabla ya kushindwa kuendelea na uwekezaji kisha kuikabidhi ardhi kwa kampuni nyingine ya Sweden  EcoEnergy  October 2009  , mwaka 2010 Eco Energy inaunda Kampuni nnyingine, Bagamoyo EcoEnergy Ltd-Kampuni tajwa hapo juu!).

TPDC inamilikiwa kwa 100% na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na CFC ina milikiwa  na watanzania watatu. Kampuni inamiliki  hekta 8000. Kwa makubaliano ya sasa Eco Energy  watapata mkataba wa miaka 99 na fursa ya kutumia ardhi kwa uhuru kwa kuipatia serikali 25% ya hisa za Kampuni na ujumbe wa Bodi.


7. Bio shape  Tanzania  ltd (Dutch)- Kilwa-Lindi (Jatropha),  hekta 81, 000. Kampuni imefilisika  mwishoni mwa mwaka 2009, imefanikiwa kusafisha eneo lenye ukubwa wa hekta 70 (Simeye 2011). Kampuni ilianza kufanya biashara ya Magogo badala ya kulima. Baada ya shughuli zenye utata na hatimaye kufilisika kwa kampuni hii, inasemekana kuwa wawekezaji wapya  toka Netherlands, Uingereza, Marekani na Italia  wanataka kuuziwa eneo husika na BIOSHAPE (Valentino 2011).

8.Bio Energy Tanzania ( Mtanzania na Mcanada), amepewa hekta 4500[13]. Kilimo cha Jatropha , ardhi ya vijiji (Vigwaza  na Kidogozero). Bado haijaanza uzalishaji kicha ya kukabidhiwa ardhi,pia kuna mgogoro mkubwa wa ardhi baada kijiji cha awali kugawanywa mara mbili ,kijiji kipya hakikuhali eneo lake kuchukuliwa na mwekezaji (Sulle 2012)

9. CAMS Agrienergy Tanzania Ltd.[14] Inamiliki hekta 45000 .Katika maeneo ya Handeni na Bagamoyo . Mpango ukia ni kuzalisha  lita 250 milioni za Ethanol na umeme wa 120MW (Oakland Institute 2011a) .Kutokana na mgogoro  wa fedha  mpango ulipunguzwa  kukiwa na malengo ya kuzalisha lita milioni 20 kwenye hekta 18,000. Kampuni iko kwenye mipango wa kuanza uzalishaji. Kwa sasa nguvu wamezielekeza miradi yao huko  Uganda na Kenya!

10. Eco Carbon (French)  - Zamani ikiitwa (Diligent Tanzania Ltd)- Bagamoyo kilimo cha  Jatropha .Waliomba hekta 75000, bado hawajakabidhiwa ardhi.

11.Euro Tech ( ya Korea). Ina mpango ya  kulima  hekta 100,000 za Jatropha na Castor Oil  for biodiesel , wanaanza na hekta 10,000 na wana mpango wa kuwekeza dola za kimarekani milioni 20[15]

12. Eurovista Trading Co. Ltd ( ya India), Kampuni hii imepewa hekta 6,000 za ardhi ya Kijiji[16], kwa ajili ya kilimo cha mahindi. (Inasemekana kwamba alikuwa kwa madhumuni ya kulima  pamba,  lakini amekuwa akilima mahindi toka 2006).

13. FELISA (Farming for energy for better Livelihoods in Southern Africa) Kampuni hii ni ubia kati ya Tanzania na Ubeligiji. Hawa walipewa hekta 4,258 huko Kigoma kwa ajili ya kilimo cha nishati joto   kwa soko la ndani. Wananchi hawakushirikishwa ipasavyo katika suala hili na matokeo yake ni kwamba vyanzo vya maji  vimezuiwa na mwkezaji (LEAT 2011).

14. FJS  African Starch Development  Ltd. ( ya Kimarekani), Hawa waliomba hekta 5,000 za ardhi ya vijiji vya Nyambili na Nyambunda huko Rufiji kwa ajili ya  Kilimo cha Mihongo. (Rubada 2012).

15.Green Resourses  Ltd ( Subsidiary of  Green Resources SA       (ya  Norway),  mwekezaji huyu anamiliki hekta 20,434 zikiwa ni ardhi ya kijiji huko Mufindi, kwa ajili ya  upandaji wa misitu, uzalishaji wa nishati , na uuzaji wa mbao.

16. Green Resources Ltd. (ya Norway), hawa wanamiliki shamba kubwa la Kilombero Forest Plantation, lenye ukubwa wa hekta 12,121. Wamepeleka maombi ya ziada hekta 10,000, na maombi hayo yamepata Baraka za Halmashauri ya Wilaya, ila kibali cha Kamishna wa ardhi kinasubiriwa (Sulle 2012)

17.Kagera Sugar Plantation (Mhindi na Mtanzania), hawa wamepewa hekta 7,000 huko  Misenyi kwa ajili ya  kuzalisha sukari, hata hivyo kiasi cha ardhi kinachotumika ni hekta 300 tu

18. KYC Mpanga Co. Ltd (Kilimo cha Yesu) ya Switzerland, Kampuni hii ilipewa hekta 3,000 za ardhi ya kijiji huko Kilombero kwa ajili ya Kilimo cha Mpunga. Baada ya kupata hasara mwaka 2004, kampuni hii ilianza kukodisha mashamba kwa wakulima wadogowadogo kwa shilingi   170,000/= kwa heka moja.

19. Kilimanjaro Aloe Vera Plantation Ltd (Mwingereza), huyu alipewa hekta 400 kwa ajili ya kulima jatropha lakini baadaye alibadili mpango na kuanza kulima Aloe Vera. (Mwamila et al. and  Bengesi et.al  2009)

20.Kilombero Plantations Ltd (KPL), subsidiary fo AGRICA Ltd. Kampuni hizi zilipewa hekta 8,000 katika bonde la Mto Rufiji kwa ajili ya kilimo cha Mpunga (Chachage 2010).  Mwaka 2010, AGRICA ilipewa tuzo ya Mwekezaji wa Kimkakati wa Kitaifa na Serikali. Ni kampuni inaoongoza Afrika Mashariki kwa uzalishaji wa mchele.

21.Kilombero Sugar Company  Ltd. (Afrika Kusini hisa 55% - Ilovo Sugar Plantation , mwingereza hisa 20% ED &F Man, na Serkali ya Jamhuri ya Muungazo –Tanzania, hisa 25%). Hawa wana hekta 8,000 za ardhi ya vijiji vya Msolwa Station, Hifadhi ya Selous, Gombala na Nyange.

22. Kilomero Valley Teak Co. (Finland), hekta 4,748  - Kilombero –Ulanga [17].

23. Korean Rural Community Cooperation (KRC) ( Korea Kusini na RUBADA). Hawa wana hekta 15, 000 za ardhi kwa ajili ya kilimo cha Mpunga huko Rufiji (Oakland Institute 2011a;Daily News & RUBADA 2012).  Mwaka 2010, kampuni hii  ilipanga kuwekeza Dola za Kimarekani  50 milioni.

24. Lindi Forests LTD (Subsidiary of Green Resources SA(Norwegian). Kampuni hii inamiliki hekta 13,000 za ardhi huko Lindi. Kiasi cha hekta 600 tu zilikwa zimelimwa na kupandwa mazai mpaka 2009.

25. Lukulilo Farm Holdings (ya Uingereza) ina jumla ya hekta 5,000 za ardhi ya vijiji vya Ndundunyikanza, Nyaminywili na Kipo – Rufiji. Kampuni  imesajiliwa na TIC, 10/11/2011 na Itaanza kazi Novemba 2014.

26.Mufindi Paper Mills  (Mhindi), huya amepewa kibali cha kumiliki  hekta 10,000  na Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya Kilimo cha Mbao laini huko Kilombero,


 27.Nava Bharat Africa Resources PVT Ltd. (NBAR) (Mhindi), huya  ameomba hekta 10,000 za ardhi ya kijiji huko kwa ajili ya kilimo cha Michikichi ili kuzalisha mafuta ya Mawese,( RUBADA 2012- Sulle).

28. Pharos Financial Group ( Kampuni binafsi UAE)-Pharos  Miro Agriculture Fund – hawa wamepewa hekta 50,000 kwa ajili ya kilimo cha Mpunga ila Kampuni hii haijasajiliwa Brela (Bakr 2010- Reuters article )

29.Rufiji Sugar Plant (mwekezaji wa nje, asili yake haifahamiki, (RUBADA 2012),  hawa wana hekta 12,132 ikiwa ni ardhi ya vijiji vya Tawi, Nyamwange na Utunge – Rufiji. Wanatumia ardhi hii kwa kilimo cha sukari, Kampuni imesajiliwa na TIC 9/5/2012. Itaanza ifikapo shughuli zake Mei, 2015 (DAO 2012- Sulle2012)

30.SAP Agriculture Ltd.(Uturuki), Kampuni hii ina hekta 5,000 za ardhi ya kijiji (Nyamwange na Ikwiriri) – Rufiji. Wananchi wamelalamikia sana utarajibu wa utwaaji wa ardhi husika uliotawaliwa na ubabe na vurugu( Sulle 2009 field visit: Kweka 2012).  Mpaka mwaka 2006, kampuni ilifanikiwa kuendeleza   hekta 500-600 tu. Kwa mujibu wa Uongozi wa Halmashauri ya kijiji, ardhi husika amepewa mwekezaji mwingine  anayetambulika kwa jina la Majani ya Chai  (Mwami & Kamata 2011), Kampuni haijasajiliwa Brela.

31. Shanta Estate Ltd. (Mkenya na Mhindi) Hawa wa jumla ya hekta 14,500 huko Bagamoyo kwa ajili ya Kilimo cha Jatropha  Eneo hili limetolewa kwa  makubaliano baina ya mwekezaji na wanavijiji wa Kibindu,Mkange na  Miyono, (Mwamila et.al).  TIC haina taarifa kususiana na huyu mwekezaji (Locher 2010). Sehemu ya eneo ambalo mwekezaji huyu   analimiliki hekta 2000 , mwekezaji mwingine Eco Energy  naye anadai analimiliki kutokana na makubaliano waliyoingia na wizara  ya Ardhi (Sulle 2012).

32.Sun BioFuels  ( huyu alibadilisha jina  na sasa inaitwa 30 Degree East). Shamba lipo  Kisarawe kwa kilimo cha Jatropha.

33.SyEnergy – hekta 30,000 za ardhi ya kijiji kwa ajili ya kilimo cha mpunga – Kilombero (sulle 2012 interview  with District land Officer).

34. The New Forest company (NFC)(Uingereza na Afrika ya Kusini). Hawa wana hekta 6,000 za ardhi huko  Kilolo -  Iringa  kwa ajili ya  upandaji miti kwa ajili ya mbao kupunguza hewa ukaa (Chachage & Baha 2010) . Mchakato huu ulivihusisha vjiji 11, hata hivyo mchakato wa kuhamisha ardhi kwa mwekezaji ulifanikiwa katika vijiji sita ( hekta 4800, mchakato ulifanyika 2009 ukihusisha vijiji vya  Isele, Ukwega,Ipalamwa na Magome na hekta  1,175  ukihusisha  vijiji vya Kisang’a  na Iselemwaka mwaka 2010 (Locher 2011). Mwekezaji anaendelea kupora ardhi ya wananchi, hali iliyopelekea kuibuka kwa mgogoro mkubwa katika  kijiji  cha Kidabaga na Kilawamo  ambacho kinapinga ardhi yao kuchukuliwa kimabavu  pasipo wananchi kushirikishwa wala kutoa ruksa!. Wananchi wamelazimishwa kutia sahihi nyaraka za fidia kuonyesha kwamba wamehalalisha uporaji huo! Mwekezaji huyu anaendelea kuhodhi ardhi kwa kununua rdhi kutoka kwa mwananchi mmoja mmoja katika vijiji husika(Locher 2010/2011).

35. TPC Ltd (CUEL Agro – Industry, Mauritius & Group Quartier –France), - Kampuni hii inahodhi hekta 15,000 za ardhi ya vijiji huko Moshi vijijini kwa ajili ya kilimo cha miwa (uzalishaji wa sukari).Hata hivyo ni hekta 7,700 tu zilizolimwa.

36.Vita Grain Ltd/GK Farm Ltd (RUBADA 2012- Sulle 2012 ) Kampuni hizi zina hati ya Makubaliano (Memorandum Of Understanding) na  RUBADA  na mchakato ulikuwa katika hatua za mwisho, mwaka 2012 (RUBADA 2012).

IX. MASHAMBA AMBAYO TAARIFA ZA WAWEKEZAJI HAZIKO WAZI/HAZIELEWEKI

1.CHAWAGWA – hekta 200 za ardhi ya Kijiji[18], lipo Kisarawe. Lilikuwa ni kwa ajili ya kilimo cha Jatropha lakini  halijaendelezwa

2 . Euro Mine Export  Ltd – Kampuni hii ina shamba Mikese- Morogoro kwa ajili ya kilimo cha Jatropha. Hali ya sasa ya kampuni haijulikani  (Sulle 2012)

3. Oxman Tanzania Ltd – Shamba lipo Rufiji, ni kwa ajili ya Kilimo cha Mpunga. Halijaendelezwa[19]

4. RUBANA  - Shamba lipo Mwanza, ni kwa ajili ya kilimco cha Jatropha, ila  halijulikani kwa maafisa kilimo wa  ardhi wa Wilaya[20]
 5.SYNERGY  Tanzania Ltd -  Kampuni hii ina shamba la hekta 20,000 huko Rufiji kwa ajili ya kilimo cha Mpunga [21]

 6. Tanzania Biodiesel Plant –  hekta 16,000 za shamb, lipo  Bagamoyo, ( Halmashauri ya wilaya iliidhinisha     mwaka 2008[22] Mpaka Novemba 2012  Rais bado alikuwa hajaibadilisha toka ardhi ya kijiji (village lands) kwenda general lands[23].

X. BAADHI YA MAKAMPUNI AMBAYO YAMETELEKEZA MASHAMBA/YAMEACHA KUFANYA KAZI
1. African Green Oils Ltd  Kampuni hii imetelekeza hekta            5,000ha[24] huko Rufiji.  Kwa sasa kampuni haifanyi kazi [25]

2.Bio diesel East Africa  Ltd - Bahi, hekta  10000ha [26]zimetelekezwa.

3. Bio Massive – hekta  7500 zimetelekezwa huko Lindi Vijijini.  Kampuni ilisitisha shughuli zake kutokana na mtikisiko wa kiuchumi  na mgomo wa wanakijiji  kutoa ardhi yao kwa mwekezaji.[27]

4.Boleyn International (T) Ltd.  Ilisajiliwa na Brela 2012 ila haifanyi kazi kwa sasa.

 5.CAMS AGRI-Energy Tanzania -  Rufiji
6. Clean Power Tanzania - Bagamoyo
7.Donester  -  Bagamoyo
8.J &J group -  Tabora Kaliua
9.JCJ  Co. Ltd-  Mwanza, Mara, Shinyanga ,Tabora
10.Kitomondo Ltd  - Bagamoyo  (Shamba la Makurange)
11.Safe Production  Ltd - Rufiji.
12.Savannah Biofuels Ltd - Handeni
13.Savannah  Biofuels Ltd. - Kongwa
14.Sekab Bioenergy  Tanzania -  Rufiji
15.Tanga Forest(s) - Handeni
16. Tanga Forest(s) - Mkinga
17.Tanga Forest(s) - Pangani

XI. NTELIGENSIA MBOVU YA KIUCHUMI

Mheshimiwa Spika, kama ilivyojidhihirisha hapo juu  wanaojiita au kutambulishwa kama wawekezaji, ambao wametawaliwa la lugha tamu ,zilizojaa hadaa na matumaini makubwa, wengi wao  hawana mitaji au wamefilisika  huko waliko toka,wakitarajia kutumia mtaji wa ardhi ya Tanzania kwenda kutafuta/kukopa fedha nje. Na mbaya Zaidi , baadhi yao badala ya kutumia mikopo kwa manufaa ya kuendeleza kilimo, wamekuwa na mtindo wa kuzihamishia fedha  kwenye miradi yao mingine. Hali iliyopelekea miradi mingi kushindwa kuanza wakati tayari miliki ya ardhi imeshapokwa toka kwa wanakijiji.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya upinzani inaitaka serikali, kurejesha mashamba yote ambayo hayajaendelezwa/yametelekezwa chini ya miliki ya vijiji vilivyoathirika .



Mheshimiwa Spika, wakati taarifa za kiuchunguzi naonyesha kwamba hakuna  uwiano wa miliki za mashamba makubwa kati ya wawekezaji wa nje na raia ya watanzania,  ripoti ya hivi karibuni ya Kaimu Mkurugenzi  wa kituo cha uwekezaji  Tanzania (TIC) Raymond Mbilinyi wakati akitoa taarifa ya uwekezaji nchini,  alisema kuwa Tanzania  ina hazina kubwa ya ardhi kwa shughuli  za uwekezaji kwa kuwa mpaka sasa ni wawekezaji 52 pekee ndio waliopewa hati ya kumiliki ardhi nchini,  akiwataka watanzania kuondokana na dhana kwamba ardhi yao inaporwa!  Alibainisha  hayo alipozungumza  katika kikao  cha kikundi kazi kilichojadili umuhimu  wa kuwa na Bank ya ardhi nchini. Alisisitiza kuwa kampuni za uwekezaji zinazokuja kuwekeza  nchini zinahitaji ardhi hivyo ni lazima Tanzania kuweka mazingira  kulingana na hali ilivyo na kwenda na wakati[28].

Mheshimiwa Spika, hawa ndio watendaji wa serikali ambao kutokana na kuzoea kufanyia kazi makaratasi hawana uelewa wa kile kinachoendelea DUNIANI! Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa TIC kabla haijaendelea na utaratibu wake wa kupiga mnada ardhi ya Tanzania, wafanye tathmini ya uendelezaji  wa ardhi ambayo mpaka sasa wamewapa wawekezaji. Inakadiriwa kwamba zaidi ya hekta 640,000 zilitolewa kwa kilimo cha mazao ya nishati pekee...ardhi ambayo ilipatikana  kwa kuhawilisha  ardhi ya vijiji . Mengi ya mashmba hayo yameendelezwa kidogo au hayajaendelezwa kabisa!



XII. SHERIA NO. 5  NA MUSTAKABALI  WA TAIFA

Mheshimiwa Spika, katika hotuba yetu ya Bajeti ya mwaka mwaka 2011/12, pamoja na mambo mengine tuliieleza Serikali juu ya haja ya kuifanyia marekebisho sheria ya Sheria ya Ardhi ya Kijiji ambayo inatoa mamlaka kwa Halmashauri  ya kijiji kusimamia  ardhi yote ya kijiji, na imepewa mamlaka ya kugawa ardhi isiyozidi heka 50 baada ya kuruhusiwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji. Kambi ya upinzani ilitoa mapendekezo hayo kutokana na uchunguzi wa kitaalam iliyoufanya na kugundua kwamba kutokana na kutokuwa na ufahamu mpana wa sheria, watu wenye fedha  wamekuwa wakitumia fursa hii ya kisheria  vibaya  kwa kuwarubuni viongozi wa vijiji, na hatimaye kugawa maeneo ya kijiji kwa watu wachache wenye fedha /ushawishi wa kisiasa, huku ikiwaacha  wanakijiji bila ardhi kinyume na matakwa ya kisheria.

Mheshimiwa Spika,hali inakuwa mbaya zaidi pale ambapo watu ambao sio watanzania wanatumia upenyo huu wa kisheria ,na kumilikishwa maeneo makubwa ya kijiji kinyemela! Hakuna ubishi kwamba kuna wageni wengi  waliopata maeneo ya vijiji kinyemela kwa kutumia upenyo huo ,wakati sheria ya Ardhi No.4 , kifungu na 20 kinakataza wageni kumiliki ardhi nchini isipokuwa kwa malengo ya uwekezaji tu, na ambao umiliki wake lazima upitie Kituo cha uwekezaji Tanzania na si vinginevyo.

Mhesimiwa Spika,kama ilivyo kawaida,maoni ya Kambi ya Upinzani yalipuuzwa...miaka mitatu baadae utafiti wa chombo kilichopewa kazi na serikali kufanya tathmini ya ardhi nchini, pamoja na watafiti wengine wamethibitisha kile ambacho Kambi ya Upinzani ilikisema, kwa vielelezo zaidi ya miaka mitatu iliyopita!

Kambi Rasmi  Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA  inaitaka serikali  ilieleze Bunge hili tukufu...ni lini sheria hii itafanyiwa mabadiliko? Aidha, ni lini serikali itawanyang’anya ardhi watu wote (watanzania na wageni) ambao wamemilikishwa ardhi za vijiji kinyume na sheria ya ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999?.

XIII. UKOMO WA ARDHI KWA WAWEKEZAJI WA KILIMO- MKANGANYIKO NA KAULI ZA SERIKALI .

Mheshimiwa Spika, tarehe 28/11/2012 (Kufuatia hoja binafsi ya Ardhi Bungeni  tarehe 8/11/2012) Serikali ilitangaza ukomo wa ardhi kwa wawekezaji kwenye sekta ya kilimo nchini, ambao utakuwa kati ya hekta 5,000 hadi 10,000 ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wengi na kuongeza ushindani katika sekta hiyo.
Serikali pia  imeweka masharti kwa kila mwekezaji anayekuja nchini, kulazimika kumsaidia mkulima mdogo katika uwekezaji, ili kumwinua kiuchumi na kumfanya awe sehemu ya uwekezaji huo.

Mheshimiwa Spika, kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano maalumu wa wadau wenye ari ya kuwekeza katika sekta ya kilimo kupitia Mpango wa Ukuzaji wa Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Waziri Mkuu alisisitiza kwamba  si busara kwa Serikali kutoa eneo kubwa la zaidi ya hekta 60,000 au 100,000 kwa mwekezaji na badala yake, uwepo ukomo wa ardhi.
“Moja ya mambo ambayo ni ya msingi ni hili la kupunguza ukubwa wa eneo kwa mwekezaji, kwa mfano kama mwekezaji wa mpunga, tumeona hekta 5,000 ni nyingi kuzimaliza mapema, zinamtosha hivyo tunaanza na kiasi hicho,”

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu  alisema uchunguzi wa Serikali umebaini kuwa wawekezaji wenye maeneo makubwa hawajayafanyia kazi na hivyo kuwanyima nafasi wengine na kuongeza kuwa kwa upande wa mashamba ya sukari, hekta 10,000 zinatosha kuanzia.

Mheshimiwa Spika, wakati Waziri Mkuu akitoa  taarifa juu ya ukomo wa ardhi kwa wawekezaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais , Mahusiano na Uratibu, Mheshimiwa Stephen Wassira (Mb) akiwasilisha  katika Kamati ya Bunge Mapendekezo  ya mpango  wa maendeleo ya Taifa  kwa mwaka 2013/14 (Ofisi ya rais Tume ya Mipango, Machi 2013[29] alisema katika kuendeleza kilimo cha ‘miwa’  kwa mwaka 2012/13 , mashamba  kwa ajili ya uwekezaji  katika mabonde  ya Wami, Ruvu,Kagera,kilombero na Malagarasi kiasi cha Hekta 277,000 yametambuliwa na uhakiki wake  unaendelea  kwa ajili  ya kuwezesha uwekezaji . Wawekezaji walioonesha nia ni:- Kampuni ya Ecoenergy[30] (Bonde la Ruvu- hekta  20,000); Agroforestry (Muhoro  Rufiji- hekta  20,000). Wawekezaji hawa wanatarajia kushirikiana na ‘wakulima wadogo’ (rejea taarifa ya tathmini ya ardhi juu ya nafasi ya wazawa katika kuhodhi ardhi). Aidha shamba  la ukubwa wa hekta 50,000 katika eneo la Mkulazi (Morogoro) limepatikana  na utafiti wa maji unaendelea!



Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya  Upinzani Bungeni  inaitaka serikali kupitia waziri wa ardhi ,ilieleze Bunge lako tukufu, utekelezaji wa kauli ya Waziri Mkuu juu ya ukomo wa ukomo wa ardhi ya kilimo kwa wawekezaji unaanza lini? Mipango na kauli za waziri Mkuu zina uhusiano na Mpango wa Taifa wa  Taifa wa miaka mitano kama ulivyowasilishwa na Mhe. Wassira au kila mtu ana jipangia mipango yake kwa kadiri atakavyoona inafaa? Kauli ipi hasa ni msimamo wa serikali: Kauli ya Waziri Mkuu au kauli ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mahusiano na Uratibu?

XIV. UPANGAJI WA MATUMIZI YA ARDHI

Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia migogoro ya ardhi isiyokwisha. Migogoro ikiwahusisha wakulima na wafugani, vijiji na vijiji , wawekezaji na wananchi wenyeji n.k . Migogoro hii mara nyingi inachangiwa na serikali ya CCM kutokuwa na mipango thabiti ya matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Spika,  miaka 52  baada ya uhuru,  Wizara  imeandaa  mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji takriban 1,300 tu (sawa na asilimia 11 ya vijiji vyote nchini) kati ya vijiji 12,000. Hadi mwaka 2011 kwa upande  wa mijini, miji mikuu ya mkoa , yenye mipango ya uendelezaji (master plans) iliyo hai ilikuwa 10 tu kati ya miji 25. Miji mikuu   ya wilaya yenye mipango ya matumizi ya ardhi ni 20 kati ya miji zaidi ya 110, na miji midogo  yenye mipango  ni 25 tui kati ya  miji 95 !Mwisho lakini nsio kwa umuhimu....miaka 52 baada ya uhuru  viwanja vilivyopimwa  ni laki tisa na tisini na tano elfu tu ( 995,000).


Mheshimiwa Spika, kwa kasi hii , hatutaweza kumaliza squatters, hatutaweza kumaliza  migogoro ya ardhi ambayo imekuwa donda ndugu katika Taifa hili...donda ambalo halina dalili yoyote ya kupata tiba !!! Kwa kuonyesha ni kwa kiwango gani serikali haina mpango kabisa wa kuhakikisha vijiji vinakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi ,sambamba na kuhakikisha kwamba kasi ya upimaji wa ardhi inaongezeka, serikali imekuwa na mkono wa birika katika kutenga fedha mahsusi  kwa ajili ya upimaji wa viwanja hususan kuwezesha ujenzi wa kituo cha satelite ambacho kingekuwa mhimili  wa kupima viwanja haraka na kwa njia ya kisasa!

Mheshimiwa Spika, kwa miaka miwili mfululizo (mwaka 2010/11 (bilioni 3), 2011/12 (bilioni 4)) Bunge lako tukufu limekuwa likitenga fedha  imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo husika, lakini ama kwa dharau ama kwa  kutokuona umuhimu wizara ya fedha (hazina) wamekuwa wagumu kutoa fedha....na kwa taarifa iliyonayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mwaka huu hakuna fedha iliyotengwa  kwa ajili ya kupima viwanja !

Mheshimiwa Spika,taarifa za kitaalam zinaonyesha kwamba kama wizara wangepewa shilingi bilioni 12 tu, wangeweza  kupima   viwanja visivyopungua milioni  5. Ni rai yangu kwa wabunge, tunaokabiliwa na changamoto ya migogoro ya ardhi inayotishia amani na ustawi wa nchi yetu,tuungane kwa pamoja kuhakikisha kwamba kwa mwaka huu wa fedha zinapatikana fedha kwa ajili ya maandalizi ujenzi wa kituo cha satelite, na fedha kwa ajili ya upimaji viwanja.



XV. VIONGOZI WA CCM  NA UJAMBAZI WA ARDHI

Mheshimiwa Spika, dhuluma hii inalihusisha shamba  namba 24 Lorkisalie ( OLDUPAI SEED CO. LTD) ,lililopo Wilayani Simanjiro, Jimbo la Simanjiro , Kitongoji cha Lemooti, Kijiji cha  Loiborsoit A.
Kwa mujibu  wa barua ya ofisi  ya Msajili  wa Hati Kanda  ya  Kaskazini- Moshi  ya tarehe 1/3/2010 yenye kumbukumbu namba LR/MS/T/1127 4/15 inaonyesha kwamba  shamba husika lilisajiliwa  tarehe 28/11/1994 na kupewa hati namba 11274.

Mheshimiwa Spika, mhusika mkuu katika mgogoro huu ni  bwana  Brown Mathew Oleseya, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, ambaye amejimilikisha kiujanja-ujanja  hekta za kijiji 3,425 ambazo ni sawa na ekari 8,562.5.  Licha ya kujipatia eneo husika kimizengwe, Mheshimiwa huyu wa Chama Tawala  amefungia wananchi  njia zote za chemchem za maji na  malisho ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, barua yake ya maombi ya shamba  ya tarehe 14/4/1978 , yenye kumb Na:PF/MI/40  inaonyesha kwamba   aliomba eneo  tofauti  na analolitumia kwa sasa. Barua inaonyesha aliomba eneo la LESHUTA, ambayo ipo katika kijiji cha Engonongoi Kata ya Terat na  Shamba  ’analolimiliki’  kwa sasa lipo eneo la  LEMOOTI kijiji cha Loiborsait A.

Mheshimiwa Spika, muhtasari wa kikao cha kamati ya maendeleo ya Kata kilichoketi tarehe 26/4/1978. kilichohudhuriwa na wajumbe 19 kinachosemekana kilimpatia Mwenyekiti huyu wa CCM Ardhi (ekari 5000, ekari 2000 za kulima na 3000 kwa ajili ya mifugo ), haujaidhinishwa na mamlaka yoyote  na hakuna  muhuri wala sahihi  ya Mwenyekiti , Katibu wala wajumbe.  Barua pekee yenye sahihi, bila muhuri wowote  ni ya Katibu Kata ya tarehe 26/4/1978 ikimtaarifu kwamba amepewa shamba husika.

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Ushauri wa ardhi ya  Wilaya ya Kiteto Ilioketi tarehe  16 Januari 1979 iliyohudhuriwa pia na na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya kipindi hicho , Ndugu Ole Kone  na katibu wa CCM (W) ,ndugu P.Bura , pamoja na mambo mengine  walijadili maombi ya mashamba , yaliyopitishwa na ngazi ya Kata pamoja na shamba la Bwana Brown Mathew Ole Suya. Kikao husika  kiliamua kwamba katika ekari 5000 zilizoombwa , eka 2000 za kilimo atazitumia kwa miaka 5 kisha zirejeshwe kijijini, na ekari 3,000 apewe lease ya miaka 33. Lakini asiingilie  Hifadhi , sehemu ya jeshi na wilaya ya Monduli. Kama ilivyo nyaraka zilizotangulia Muhtasari wa kikao husika,hakikuwa na sahihi ya Mwenyekiti wala Katibu!

Mheshimiwa Spika, licha ya kwamba nyaraka husika (anazozitumia kiongozi huyu kama ushahidi wa kupewa shamba) hazina uhalali wowote kisheria , kwa mujibu wa makabidhiano ya ardhi husika,kama ilivyoamauliwa na kamati ya ardhi ya Wilaya, Bwana Brown alitakiwa arejeshe ardhi ya kijiji( ekari 2000 za kilimo) mwaka  1985, na ardhi ya mifugo (ekari 3000 kwa ajili ya malisho ) mwaka 2011! Mwaka  1985, shamba la kijiji halikurudishwa  (ekari 2000), mwaka 1991 kada huyu aliendelea kupora ardhi  ya kijiji  kwa kuongeza ukubwa wa eneo lake kutoka! Hekta 2000 za awali mpaka hekta 3,425 (Ekari 8,000)!, ambayo ni hekta 1425 zaidi ya kiasi ’alichopewa’. Eneo hilo jipya liliingia kwenye kijiji cha Lolksale  wilaya ya Monduli !

Mheshimiwa Spika, kada huyu wa CCM, licha ya kutokuwa mmiliki halali wa eneo husika ,tarehe 31/8/ 2009  kwa kushirikiana na watumishi wa serikali wasio waaminifu walibadilisha  matumizi ya shamba  kutoka kilimo  na ufugaji  na kuwa Hifadhi ya kitalii.[31]

Uhalali wa Kubadilisha Matumizi ya Ardhi na Mwenye Mamlaka ya Kubadilisha Matumizi

Mheshimiwa Spika, Kanuni na  na taratibu  za kubadilisha matumizi hazikufuatwa:
i)      Bango kwa lengo la kukusanya maoni  ya wananchi majirani kuhusu nia ya mmiliki kutaka  kuongeza matumizi  kama inavyotakiwa kwenye waraka  wa kitaalam Na.1  wa mwaka 2006
ii)    Kibali cha Mkurugenzi wa mipango Miji na vijiji  kama inavyotakiwa  kwenye Sheria ya Mipango miji  Na.8  ya mwaka  2007 kifungu 32(1) na 6(3)

iii)   Kibali cha nyongeza ya matumizi katika Miliki ( Land Form na. 28) kimetolewa  na kusainiwa  Paulo E .Kibona ambaye hana mamlaka  kisheria kusaini Fomu hiyo. Fomu hiyo husainiwa na Kamishna wa ardhi kwa mujibu wa sheria ya ardhi na.4 ,1999 kifungu 35(4)

Nyaraka ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani inazo zinaonyesha kwamba  Wizara ya Ardhi, kupitia kwa Kamishna Msaidizi Kanda ya Kaskazini kwa barua yenye kumbukumbu Na. LD /NZ/6014/22/DW ya tarehe 22/09/2010  ilimtaka arejeshe hati iliyoofanyiwa mabadiliko ya matumizi....lakini alipuuza amri ya mamlaka halali! Hali iliyoilazimu  Kamishna  msaidizi kuandaa hati ya marekebisho  ya mabadiliko ya matumizi (deed of rectification) na kuiwasilisha  kwa Msajili wa hati  msaidizi kanda ya Moshi ili afanye  marekebisho kwenye daftari lake . Marekebisho  yalifanyika tarehe  26/01/2011 na kusajiliwa  kwenye FD. No. 29828 ambapo matumizi kwenye hati yalitakiwa yabaki yale ya awali (japokuwa hakuwa na uhalali wowote wa umiliki)

Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa na uelewa wa mgogoro husika  bado Kada huyu wa CCM  aliuza eneo husika (ardhi ya kijiji) kwa raia wa kigeni , mmiliki wa Kampuni   Maasai  steppe Conservancy limited  mnamo tarehe 14/12/2010.
Kwa mujibu wa Taarifa za BRELLA , kampuni ya Maasai Steppe  Conservancy  limited ina jumla  ya hisa 10,000, kama ilivyoainishwa  hapa chini:
i)                    BCZV Holdings limited  ni kampuni inayomilikiwa na  Baastian  bruins  9Mdachi) na Jerome Bruins  (Mdachi) wana hisa 9700
ii)                  John warren (Mwingereza ) ana hisa 100
iii)                Brown Mathew Ole suya  ( Mtanzania)  ana hisa 200.
Kutokana na hisa nyingi ( 9800) za kampuni ya Maasai Steppe Conservancy kumilikiwa na wageni  ni dhahiri  kwamba kampuni  hiyo ni ya kigeni.

Kwa mujibu wa sheria ya ardhi Na. 4  ya mwaka 1999, fungu la 20 : Kampuni /raia wa kigeni  kabla ya kumiliki ardhi  wanatakiwa wapate  kibali  ( Cerificate of incentives) kutoka TIC. Utaratibu huu haukufuatwa! Wakati nchi inakabiliwa na changamoto kubwa ya ardhi kumilikiwa na wageni! Kada/kiongozi  wa chama cha mapinduzi amegeuka kuwadi namba moja wa kuuza nchi  kwa wageni! Waziri wa ardhi ana taarifa zote kuhusiana na uvunjwaji huu wa sharia kuanzia na uporaji wa wa eneo la kijiji, kubadilishwa kwa matumizi ya ardhi pasipo kufuata sharia na taratibu na kuuza ardhi kwa raia wa kigeni kinyume na sharia za nchi! Waziri aliahiidi kwenda kulishughulikia  toka mwaka 2011 mpaka sasa hajatia mguu.

Kambi ya upinzani inataka kupata majibu ya maswali yafuatayo:
I)                   Wizara ya ardhi ilitumia vigezo gani kumpatia hati?
II)                Wizara ilitoaje uhalali wa kubadilisha matumizi  ya ardhi
III)             Wizara imeafiki vipi  wa umiliki wa ardhi kwa  raia wa kigeni (Mdachi)
IV)             Hatua gani zitachukuliwa kwa kada huyu wa CCM kwa  kukiibia kijiji  na watanzania ardhi yao na kwa kuvunja sheria?

XVI. UVAMIZI WA MAENEO YA WAZI MKOA WA DAR ES SALAAM

Mheshimiwa Spika, Rais, Mheshimiwa  Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete  wakati akifanya  majumuisho  ya ukaguzi wa hali ya maji  katika mkoa wa Dar es salaam  tarehe 24 Mei,  2010 alitoa hoja ya kuvamiwa kwa maeneo mengi ya wazi  katika Mkoa wa Dar es salaam,ambapo alilalamikia baadhi ya Madiwani kuhusika  na uvamizi huo.

Halikadhalika aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es  salaam Mhe. William Lukuvi, alipotembelea  Manispaa ya Kinondoni  tarehe 15 Juni 2010  alibaini mapungufu husika hali iliyopelekea  kuunda  kamati  maalum ya kuchunguza  maeneo yote ya wazi  yaliyovamiwa  katika Mkoa wa Dar es salaam. Kamati ambayo iliundwa  tarehe 18 Juni, 2010  lengo la kazi  likiwa ni kuchunguza  maeneo ya wazi  yaliyomo katika  Jiji la Dar es salaam, ambayo yamevamiwa, kuendelezwa  au kuuzwa  kinyume na taratibu za mipango miji. Kamati ambayo ilikamilisha kazi yake tarehe  13/7/2010 (taarifa ya Kamati husika,pamoja na mapendekezo tunayo).

Mheshimiwa Spika,Kambi  ya upinzani inaitaka serikali itueleze, baada ya miaka 4  kupita tokea Kamati husika imalize kazi yake; 
1)       Ni hatua gani zimeshachukuliwa ili kuyarudisha maeneo husika?
2)       Ni maeneo mangapi kati ya yaliyobainishwa yamesharudishwa?
3)       Ni Hatua gani zimechukuliwa dhidi ya maafisa waliohusika na ubadhirifu huu na kwa kiwango gani?
4)       Ni  lini serikali inatarajia kukamilisha utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati husika?
5)      Je serikali itakuwa tayari kuvunja majumba makubwa makubwa ya watu wenye fedha waliouziwa maeneo ya wazi kinyume na utaratibu  na kupewa hati na maafisa wasio waaminifu ?
6)      Serikali inatoa tamko  gani juu  ya Kiwanja namba 856 Msasani beach,  ambacho kwa mujibu  wa Ramani ya  upimaji  iliyosajiliwa namba 29331 ilikuwa ni kwa matumzi ya wazi, lakini baadae  kilimilikishwa kwa mtu binafsi. Matokeo yake njia ya mkondo wa maji  kuelekea baharini imezibwa,na mvua ikinyesha maeneo ya kwa Warioba, mpaka njia panda ya kuelekea Clouds FM yanajaa maji.

7)      Mheshimiwa Spika,  Kambi Rasmi  ya Upinzani inaitaka serikali itoe  maelezo kuhusiana na  viwanja namba 9 & 10 Kitalu ’S’ Tabata Segerea. Mgogoro huu ni wa muda mrefu sana, Waziri wa Ardhi anayo taarifa. Barua ya mwisho kwa waziri iliandikwa  tarehe 2/5/2013 ,ilikuwa na viambatanisho kumi. Viwanja husika vilivyotengwa mahsusi kwa matumizi ya Umma (soko). Tume  ya Ardhi iliyoundwa  tarehe 23/9/2008 kuchunguza mgogoro husika  ilibaini kwamba viwanja husika vilimilikishwa kimakosa  kwa  Walter Camilius  na Rose Samwel Binagi.

8)      Kambi  Rasmi ya Upinzani bungeni, inataka  Serikali itoe maelezo juu eneo la wazi la Kitalu D, Registered Plan  namba  8750, mtaa wa Mikumi  na Makongoro, Magomeni , lango la JIJI , ambalo licha wa maelekezo na kauli mbali mbali za serikali,bado linaendelea kuendelezwa!


XVII. SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
SERIKALI  NA TAASISI ZAKE KUTOLIPA  KODI ZA PANGO  KWA WAKATI

Mheshimiwa Spika, ’Katika kipindi cha  Julai 2011  shirika lilikusanya  kodi  za pango pamoja  na malimbikizo kiasi  cha shilingi  bilioni 31.Pamoja na  na jitihada za  kukusanya kodi na malimbikizo na hasa  yale yanayodaiwa  serikali na taasisi zake, malimbikizo bado ni makubwa . Hadi machi  2011,  Serikali  na taasisi zake  ilikuwa ikidaiwa  kiasi cha shilingi  bilioni  1.543, baada ya  kupunguza  malimbikizo  kwa kiasi  cha shilingi  milioni 115 ,sawa na  asilimia 8 tu!’ hii ilikuwa hotuba yetu ya mwaka 2011...miaka mitatu baadae taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya wizara katika mwaka 2012/13 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/14 kwa kamati ya kudumu ya Bunge ardhi , maliasili na mazingira  inaonyesha kwamba madeni[32] ya serikali na taasisi zake yaliongezeka  kutoka shilingi bilioni 2.8 mwaka 2011/12  mpaka bilioni 3.4 mwezi Februari 2013!

Kambi ya upinzani inataka serikali ieleze  ni kwa nini imekuwa  ni mdaiwa sugu , na kwa nini hailipi madeni ya shirika la nyumba?

XVIII. MIKOPO YA UNUNUZI NA UJENZI  WA NYUMBA

Mheshimiwa Spika,Pamoja na kuwepo kwa sheria ya Mikopo ya nyumba  (Mortgage  Financing Act) ya mwaka 2008  na sheria  ya umiliki wa  sehemu ya majengo ( Unit Titles  Act) ya mwaka  2008, masharti ya mikopo hii bado ni magumu. Mfano, kwa sasa  benki zanazotoa mikopo ya nyumba  masharti yake  ni pamoja na muda wa marejesho  ya kati  ya miaka  6 mpaka 15 na riba  kati ya asilimia 17  mpaka 22 kwa mwaka .

Mheshimiwa Spika, Iwapo  hali hii haitabadilika , itakuwa vigumu kwa wananchi , halikadhalika  shirika letu la nyumba  kujenga nyumba  za gharama  nafuu  na kwa wananchi walio wengi  kuweza kumudu  mikopo  ya ununuzi wa nyumba.

XIX. SERIKALI KUVUNJA AHADI YA KUWAUZIA NYUMBA (KWA BEI NAFUU) WAPANAGAJI WA SHIRIKA LA NYUMBA KINYEMELA.

Mheshimiwa Spika,  Serikali, tangu mwaka 1996, ilpitisha maamuzi ya kuliruhusu Shirika la Nyumba kuwauzia wapangaji wake nyumba za gharama ndogo na gharama ya kati zilizojengwa na Shrika lenyewe. Hata hivyo, nyumba zilizotaifishwa hazihusiki na uamuzi huu.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2008, Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa Ziarani Manispaa ya Iringa kuzindua majengo ya SNT/NHC (Agosti, 07 2008) alikazia uamuzi wa Serikali kwa kusema   ”Sheria ya Mikopo ya Nyumba inatarajiwa kuwasilishwa Bungeni Oktoba mwaka huu, ambapo ikipitishwa, itawezesha Watanzania wanaoishi kwenye nyumba za Shirika la Taifa, kununua nyumba hizo” Rais aliongeza kuwa ”MTU HAWEZI KUISHI NDANI YA NYUMBA ZA NHC KWA MIAKA 30 BILA KUFAIDIKA”.

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, Sheria ilitungwa lakini Serikali imeamua kubadili mwelekeo kimyakimya. Serikali imesema kwamba jukumu la msingi la Shirika la Nyumba litakuwa ni kufanya bishara ya kujenga na kuuza nyumba badala ya jukumu la sasa la kupangisha nyumba na kukusanya kodi kwa mwezi. Hata hivyo, bei ya nyumba inazingatia bei ya soko la sasa hivi ambapo gharama ni kubwa sana na kihalisia hakuna mtanzania masikini anayeweza kununua nyumba hizo.

Kwa mfano: UNUNUZI WA NYUMBA UBUNGO KN 242/1-242/12
BEI YA UNUNUZI BILA VAT                   TSHS 67,946,567.86
VAT 18%                                                TSHS 12, 230,382.21
BEI YA UNUNUZI PAMOJA NA VAT    TSHS. 80,176,950.07
RIBA YA BENKI 18%                              TSHS. 144,318,510.234

MUDA WA KULIPA NI MIAKA 15
TSHS 800,000 KWA MWEZI XMIAKA 15 = 144,000,0000

MAJI TAKA 3000X48 DEPARTMENT BLOC 1 =TSHS. 144,000
BLOCK 9X 144,000             BLOCK 9= MWEZI TSHS. 1,296,000
                                                  KWA MWAKA TSHS. 15,552,000
PARKING – HAKUNA
VIWANJA VYA MICHEZO – HAKUNA

Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo, ni mtanzania gani ataweza kununua nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa? Hakika huu ni ubaguzi mkubwa kwa kuwa sasa hivi wenye uwezo ambao wengi ni wageni (wahindi, wachina na wazungu) ndio wameanza kujaa katika nyumba hizo. Haki ya Mtanzania iko wapi?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli mbele ya bunge hili leo hii kama bado ina mpango wa kuwauzia nyummba za bei nafuu wapangaji wa shirika la nyumba la taifa. Aidha,  Kambi ya upinzani , inaitaka Serikali itueleze ni kwa namna  gani imejipanga kuweza  kutatua tatizo hili ! Lazima Serikali  iweke Mazingira  ya kuziwezesha Benki kutoa mikopo  yenye masharti nafuu  kwa wawekezaji  na wanunuzi wa nyumba.!!!!



XX. KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI  (VAT) NA ONGEZEKO  LA MTAJI (CAPITAL GAIN TAX)  KWENYE  MAUZO YA NYUMBA ZINAZOJENGWA NA SHIRIKA

Mheshimiwa Spika, Shirika la Nyumba la Taifa, lilipoanzishwa  mwaka 1962 , moja kati malengo yake  ilikuwa ni kujenga nyumba nafuu kwa ajili ya watanzania  wafanyao  kazi mijini . Hata hivyo kwa kadiri  siku zilivyosonga  mbele, Shirika hili liligeuka kutoka kuwahudumia masikini na watu wenye kipato cha kati na badala yake kuwahudumia watu wa kipato cha juu.



Mheshimiwa Spika,  kodi ambazo Shirika  hulipa  pale linapouza  nyumba: Uwepo wa kodi hizi huzifanya nyumba zinazojengwa na shirika kuwa ghali  na hivyo  zisiweze kushindana  kwenye soko na kuwa mzigo mkubwa sana kwa wananchi wanaotaka kununua nyumba .  Mfano dhahiri, kwa mwaka wa fedha  2010/11 shirika  lilitarajia kujenga nyumba  49 , zenye jumla ya thamani  ya shilingi  bilioni 4.08. Kwa gharama iliyotumika, wastani  wa nyumba moja ililigharimu shirika shilingi milioni 83.4,

Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa Taarifa ya utekelezaji wa Kazi za Shirika la Nyumba la Taifa kuanzia  Julai 2010 hadi Mei 2011 wanatarajia kupata  shilingi bilioni  6.3  kutokana na mauzo  ya nyumba hizo , yaani faida ya shilingi  bilioni 1.9  Kwa tafsiri nyingine nyumba moja itauzwa na shirika la nyumba kwa shilingi milioni 129.2, wakati gharama halisi za ujenzi ni shilingi  milioni 83. Kwa kila nyumba iliyounzwa shirika limepata faida ya  shilingi  milioni 46.

Mheshimiwa Spika, Kwa hali hii, inawezekana kweli Shirika hili kujenga nyumba kwa ajili ya wananchi wa kawaida  ,kuweza kumudu? Kama kweli tatizo ni kodi la ongezeko la thamani  na kodi ya ongezeko la mtaji, serikali haioni kwamba  ina wajibu wa kuondoa hizi kero ili shirika lifanye kazi kwa maslahi ya wengi, na sio kwa maslahi ya wachache?


XXI. KODI KWA VIFAA VYA UJENZI

Mheshiwa Spika,gharama  za  vifaa vya ujenzi imekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi wengi,  tumekuwa tukilizungumzia hili kwa kipindi kirefu sasa na serikali imekuwa ikiahidi kulitafutia ufumbuzi ili kuwapungumzia  raia wake mzigo katika ujenzi wa nyumba..ili hatimaye makazi na nyumba  za wananchi wetu ziakisi  maendeleo na mafanikio  yanayotokea nchini  na kuondokana kabisa na nyumba za matope, fito na nyasi ifikapo 2020.

 Mheshimiwa Spika ,Kambi ya upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge lako tukufu ni lini  kodi katika vifaa vya ujenzi wa nyumba kama saruji, mabati, nondo nk. itaondolewa ili kuweza kufanikisha dhamira hii?

XXII. KODI ZA PANGO
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ni kero ,ni  kodi za nyumba. Kila mwenye nyumba katika nchi hii amekuwa akijipangia kodi , kwa kadiri atakavyoona inafaa. Ni kwa bahati mbaya sana wamiliki wa nyumba  licha ya kupata mapato (ya kibiashara),hawalipi kodi serikalini. Kambi ya upinzani imelizungumza hili kwa kipindi kirefu sana, hivyo tunaitaka Serikali ianzishe Taasisi itakayosimamia na kudhibiti kodi za pango la nyumba ambazo hivi sasa ni kubwa mno!  zinatozwa kwa mwaka mzima, hivyo kuwatesa wapangaji husan wa kipato cha chini.

XXIII. UENDELEZAJI   MAJENGO MIJINI

Mheshimiwa spika, yamekuwepo matukio  ya kujirudia ya  kuanguka kwa majengo ya maghorofa yaliyokamilika na yanayoendelea kujengwa  katika  jiji la Dar es salaam, na tukio la hivi karibuni  jengo lililokuwa  linaendelea kujengwa  katikati ya jiji  la Dar es salaam, mtaa wa Indira Ghandi,kiwanja namba 2032/73  na kupoteza maisha ya watanzania wasiopungua 36. Kambi ya upinzani inasikitishwa  kwa tukio hilo  ambalo lingeweza  kuzuilika  iwapo mkandarasi  angezikatia  kanuni za usalama, halikadhalika kama mamlaka zenye jukumu ya kusimamia sekta hii ya ujenzi zingetekeleza wajibu wao ipasavyo!

Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kawaida yetu , pale ambapo panatokea tatizo watu wenye dhamana ya kutafuta mbinu za kutatua matatizo wamekuwa ni mabingwa ya kujificha kwenye vivuli vyao!

Mheshimiwa spika, hakuna ubisihi kwamba Waziri pekee aliyeonekana japo kuguswa kilichotokea na hata kutoa maelekezo ya kiutendaji kwa mamlaka za chini kwa utekelezaji ni waziri wa ArdhiM(japokuwa mpaka sasa kauli yake haijafanyiwa kazi) mawaziri wengine walidiriki, kukana mbele ya Bunge lako tukufu ( akiwemo waziri wa Ujenzi, Mhe.John Pombe Magufuli wakati akijibu hoja za wabunge ,wakati wa wa mawasilisho ya Bajeti ya wizara ya Ujenzi na wengine walikuja kuchungulia kwenye kamati ya ardhi na maliasili,walipopewa maelekezo ya nini wanatakiwa walete kwenye kamati,waliingia mitini – Mhe Aggrey  Mwanri, naibu waziri TAMISEMI) huku  kiti cha  Spika kikiwalinda kwamba hawahusiki kwa namna yoyote,na hoja zote za wabunge zikatupiwa kapuni!

Mheshimiwa Spika, ni muhimu Bunge lako tukufu likaelewa kwamba kuna mamlaka zaidi ya moja katika suala zima la uendelezaji wa majengo mjini. Ni muhimu mamlaka zote hizi zielewe wajibu wake,na ziwajibike ipasavyo kwa mema na mabaya!Katika sakata hili,wizara zifuatazo haziwezi kukwepa uwajibikaji:
1)      Wizara ya Ardhi
2)      Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI)
3)      Wizara ya Ujenzi na
4)      Wiza ya Kazi na Ajira

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa sheria ya mipango miji , No.8  ya mwaka 2007,Wizara ya ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi  ina jukumu  la kusimamia upangaji na uendelezaji wa maeneo ya mjini(Kisera).

Mheshimiwa Spika, Mamlaka zinazohusika na kutekeleza sheria ya Mipango Miji , namba 8 ya mwaka  2007 ni Halmashauri za Jiji, Miji na Wilaya pamoja  na kampuni au taasisi yeyote itakayopewa hadhi ya kuwa mpangaji . Sheria ya serikali za mitaa( Local government Act number 3 of 1982)inazipa  mamlaka halmashauri zote  nchini kuandaa mipango ya uendelezaji  maeneo yaliyomo kwenye eneo lililotangazwa  kuwa la upangaji kisheria (kulingana na sheria ya mipango miji  namba 8 ya 2007).

Mheshimiwa spika, kimsingi usimamizi wa uendelezaji  wa majengo mijini  uapaswa kusimamiwa chini ya wizara ya Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI).Maeneo muhimu yanayosimamiwa na Halmashauri ili kuhakikisha majengo yanayopjengwa yanakuwa katika ubora stahiki  ni  pamoja na:
i)                    kukagua ramani zinazowasilishwa kwao kutumia wataalam mbali mbali,
ii)                  kutoa vibali  kwa waombaji ambao ramani zao zimebuniwa na kampuni zilizosajiliwa ,
iii)                kufanya ukaguzi wa majengo kwa kutumia  timu ya wakaguzi wa majengo  ili kubaini kama majengo yanayojengwa  kwa kufuata sheria,
iv)                Kukagua  na kujiridhisha kama wajenzi wanaojenga  ndani ya Halmashauri wamesajiliwa na Bodi husika !

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi inawajibIka kwa kupitia vyombo mbali mbali ambavyo viko chini yake, ambavyo kisheria vinawajibuka katikasuala zima la usimamizi wa majengo: Bodi ya wabunifu wa majengo na wakadiriaji Majenzi  ni mamlaka iliyoanzishwa  na sheria Na. 16/1997 ( the Architects and Quality  Surveyors (Registration) Act { Cap. 269 R.E  2002) na mwaka 2010. Fungu la 4  la sheria hii linaweka majukumu  kuwa ni pamoja na :
i)                    Kusimamia shughuli na utendaji  kazi wa wabunifu  majengo na wakadiriaji majenzi , pamoja na kampuni zinazofanya kazi ya utaalam ushauri katika kusimamia miradi ya ujenzi
ii)                  Kuingia na kukagua  shughuli zote za ujenzi unaofanyika hapa nchini kwa madhumuni ya kujiridhisha na kuhakikisha kama kazi ya ujenzi inayofanyika inafanywa na mtu ambaye amesajiliwa na Bodi na anazingatia taratibu, kanuni na sheria zote zinazosimamia ujenzi mijini
iii)                Kuhakikisha kuwa maeneo yote ambako ujenzi unafanyika kumewekwa mabango yenye kuonyesha  jina na anwani ya mradi,jina la mmiliki ,wataalam wahsauri  kwa maana  wabunifu majengo ,wakadiriaji majenzi ,wahandisi pamoja na mkandarasi endapo atakuwa hakufanya hayo atachukuliwa hatu za kisheria

Mheshimiwa Spika,Chombo kingine ambacho kiko chini ya wizara ya ujenzi  ni Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB). Bodi hii ilianzishwa  chini ya Fungu la 4 la sheria  Na .15 ya mwaka 1997 (The Engineers  registration Act [Cap . 63  R.E 2002]. Sheria hii imeainisha  wajibu na  majukumu  ya Bodi mbali mbali kama ifuatavyo:
i)                    Kufuatilia na kusimamia shughuli za utendaji kazi wa wahandisi ikiwa ni pamoja na kampuni zinazofanya kazi ya utaalam ushauri wa usimamizi wa miradi ya majenzi mijini,
ii)                  Kuingia na Kukagua  shughuli zote za ujenzi  unaofanyika hapa nchini kwa madhumuni ya kujiridhisha na kuhakikisha kama kazi ya ujenzi inafanyika /inafanywa na mtu ambaye amesajiliwa na bodi na anazingatia  taratibu, kanuni na sheria zote zinazosimamia ujenzi nchini,
iii)                Kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo ujenzi unafanyika kumewekwa  mabango yenye kuonyesha  jina na anwani ya mradi ,jina la mmiliki ,wataalam washauri  kwa maana wabunifu majengo , wakadiriaji majenzi ,wahandisi  pamoja na mkandarasi  endapo atakuwa hajafanya hivyo,atachukuliwa hatua za kisheria.

Mheshimiwa Spika, Chombo kingine ni bodi  ya wakandarasi (CRB) ,imeanzishwa  na sheria Na. 17/ 1997 (The Contractors Registration Act [ Cap. 234 R.E 2002.Fungu la 4 la sheria  hii imekipa chombo hichi majukumu  yafuatayo:
i)                    Kusimamia  shughuli za utendaji kazi wa wakandarasi katika kujenga majengo imara yenye kufuata viwango kwa mujibu wa michoro ya majengo hayo
ii)                  Kuingia na kukagua shughuli zote za ujenzi unaofanyika hapa nchini  kwa madhumuni  ya kujiridhisha na kuhakikisha  kama kazi ya ujenzi inayofanyika inafanywa na mtu ambaye amesajiliwa na bodi  na anaingatia taratibu ,kanuni na sheria zote  zinazosimamia ujenzi mijini,
Wizara ya Kazi na ajira , inabeba dhamana kwa kupitia  chombo chake cha wakala wa afya  na usalama kazini (OCCUPATIONAL,SAFETY AND HEALTH AGENCY –OSHA). Chombo hiki kinasimamia usalama mahali pa kazi ,pia kinashiriki kusimamia miradi ya ujenzi mijini. Mamlaka hii hutoa kibali na kusajili mradi kama ambavyo mamlaka nyingine zinafanya kwa kutoa sticker.

Mheshimiwa Spika, Wizara zote hizi zinawajibika kwa namna moja au nyingine kwa maisha ya watanzania 36 yaliyoteketea kutokana tu na uzembe! Ni TAMISEMI kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala iliyohusika moja kwa moja na kubadilisha  kibali cha awali cha ghorofa tisa ( 10 storeys) ilichokitoa 4/12/2007[33] na kutoa kibali kingine  cha kuongeza sakafu saba ,kufikia ghorofa 16!Kinyume na matakwa ya Mpango wa Uendelezaji upya wa eneo la Kati la jiji la Dar es salaam  wa mwaka 2000. Mpango ambapo  unaainisha kuwa  ujenzi kwenye  viwanja vilivyoko eneo hilo  uwe  wa uwiano wa jengo 2.0, ujazo wa kiwanja  wa asilimia 60 hadi 70 na sakafu  kati  ya 7 na 10 . Na kama kuna nyongeza yotote inayotaka kufanyika, lazima kibali kitolewa na Wizara yenye dhamana, suala ambalo halikufanyika. Halikadhalika wizara ya ujenzi na wizara ya kazi na ajira kwa vyombo vilivyo chini ya wizara husika, kama ilivyoainishwa hapo juu  vyenye mamlaka ya kisheria ya usimamizi kushindwa kufanya hivyo!



Mheshimiwa Spika, licha ya uthubutu ulioonyeshwa na waziri wa ardhi , kulishughulikia suala hili, Shirika la nyumba la Taifa haliwezi kukwepa wajibu kama mbia. Mbali na kwamba Sera  ya Ubia ya NHC na Mkataba wa Ubia  baina ya pande mbili(NHC na M/S LADHA CONSTRUCTION LTD),inabainisha kwamba NHC itatoa Kiwanja na mbia atagharamia mradi husika kwa 100%. Na kwamba Mbia ana wajibu wa kuteua  wakandarasi na washauriwa ujenzi  na kulipia gharama zao zote, Ni ukweli usiopingika kwamba  baad ya jengo kukamilika, NHC angekuwa na umiliki wa 50% ya Jengo lote. Jengo ambalo ( kama yalivyo majengo mengine ya NHC) ni kwa ajili ya makazi au biashara!

Mheshimiwa Spika, kwa namna yeyote ile , shirika la nyumba lilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba linafuatilia kwa ukaribu(kama ambavyo taasisi nyingine za serikali zinazoingia ubia na zinavyofanya) ili kuwa na uhakika na usalama wa majengo kwa watumiaji! Shirika lina wajibu wa kufuatilia  kila hatua ya ujenzi. Ni muhimu ikaeleweka kwamba  miradi ya ubia ni mhimili muhimu sana wa shirika, ikumbukwe kuwa hadi Februari ,2013  miradi na majengo 11 ilikamilika  na miradi ya majengo 19 iliendelea na mradi wa jengo 1 ulianza! Hii ni miradi inayogharimu si tu mabilioni ya shilingi ,bali yanahusisha maelfu ya watanzania ambao wanatarajia kuishi au kufanya biashara katika nyumba husika!

XXIV. KIWANJA NAMBA 1662 INDIRA GHANDI /ASIA  

Mheshimiwa Spika,kufuatia kuporomoka kwa jengo kiwanja namba 2032/75 tarehe 29/ March 2013  ilibainika kwamba jengo lililoko mkabala na eneo hilo  lenye kiwanja na 1662/75  chenye mita za mraba 150 nalo limejengwa kwa viwango visivyokidhi  kanuni za upangaji miji kama zilivyoainishwa  kwenye Mpango wa Uendelezaji  Upya eneo la Kati  la jiji la Dar es salaam ! ( Rejea Mpango unasemaje katika maelezo ya kiwanja 2032/75).

Mheshimiwa Spika, TAMISEMI- kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, iliendelea na mtindo ule ule wa kukiuka sheria baada ya kupokea  maombi ya kibali cha ujenzi wa michoro ya ghorofa  kumi na nne (15 Storeys yenye sakafu ya wazi (Terrace) tarehe 21 Mei ,2009 kwa ajili ya biashara na makazi  yaliyosajiliwa  kwa plan na. ILA  /213/2009, maombi ammbayo yalipishwa na kamati ya vibali vya ujenzi  iliyoketi tarehe 20/07/2009 na kuthibitishwa  kwenye kikao cha tarehe 24/08/2009. Na kupewa kibali Na.0398 cha tarehe 12/08/2009.[34]

Mheshimiwa Spika,licha ya Mamlaka husika kutakiwa kuvunja jengo husika ili kuepuka madhara mengine kutokea, kwa barua ya 5/04/2013,kutoka kwa Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji , Bibi albina Bura ...katika muktadha ule ule wa baadhi ya watendaji  kujificha katika vivuli vyao..mpaka leo jengo husika bado halijavunjwa. Taarifa zilizopo ni kwamba imebidi wakazi wa eneo hilo kwa gharma zao watelekeze nyumba zao na kutafuta makazi mapya,nyumba ya ibada iliyokuwa inahudumia waumini imefungwa, kituo cha afya nk..

Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inatambua juhudi kubwa inayofanywa na kamati ya Bunge ya ardhi na mazingira katika kushughulikia hili suala, licha ya kutokupata ushirikiano kutoka kwa baadhi ya mawaziri!Kambi ya upinzani haitarajii kwamba Mhe. Waziri mkuu, ambaye,wizara ambayo iko chini yake inahusika moja kwa moja na akiwa kama   kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni ataruhusu uzembe huu uendelee: Tunaitaka serikali ichukue hatua zifuatazo :
i)                    Hatua  stahiki za kinidhamu  za kisheria  zichukuliwe kwa wahusika wa maafa haya
ii)                  Itoe Bungeni Taarifa ya uchunguzi ya kuanguka  kwa magorofa Dar es salaam ya mwaka 2006 na hatua zilizochukuliwa na baada ya ukaguzi nyumba ngapi zilitakiwa kuvunjwa .Taarifa tulizonazo ile taarifa iko kwenye makabati,imejaa vumbi!
iii)                Bodi zote zilizotajwa hapo juu ziwajibike ipasavyo kila moja  katika eneo lake  iliyotakiwa kuwajibika kisheria
iv)                Ukaguzi ufanyike kwenye majengo yote yaliyojengwa na Ladha Construction LTD, taarifa ambazo kambi ya upinzani inazo mbia amekuwa na mahusiano ya kikazi ya muda mrefu na NHC na kuna nyumba alizozijenga ambazo kuna wapangaji ndani yake
v)                  Takukuru ichunguze mchakato mzima wa utoaji wa vibali uliotawaliwa na ukiukwaji wa sheria ili kujiridhisha kama hakukuna na harufu ya rushwa katika mchakato mzima. Kamati zilizohusika na utoaji vibali zinahusika hapa.
vi)                Sheria ziangaliwe upya na ikiwezekana  tuwe na chombo mamlaka mahsusi ya ukaguzi (Inspection Authority ) inayosimamia  majengo  hususan maghotofa ambayo itakuwa na wataalam wa fani zote kwa miji na majiji yetu badala  ya halmashauri  zinazotoa vibali na kushindwa kusimamia kutokana na ukosefu  wa wataalamu.
vii)               Serikali iongeze idadi ya wataalam katika Halmashauri zetu ili waweze kukidhi mahitaji na ukuaji wa kasi wa mji.
XXV. MSISITIZO KUHUSU MIGOGORO YA ARDHI

  • FIDIA ZA ARDHI

Mheshimiwa Spika; Mfano mwingine wa mgogoro na madai ya muda mrefu ya fidia ni ya wananchi wa Kata ya Kwembe hususan wanaoishi katika maeneo ya Mloganzila. Tarehe 1 Julai 2011 wakati Bunge lilipokaa kama Kamati kupitia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali iliulizwa kuhusu fidia ya wananchi wa eneo la Kwembe Mlonganzila wanaopaswa kuhama kupisha ujenzi wa majengo ya Chuo cha Afya Muhimbili (MUHAS). Serikali ilitoa majibu siku hiyo kuhusu wananchi ambao walibaki baada ya wananchi 1919 kupewa fidia ya maendeleo na mimea. Hata hivyo Serikali haikutoa majibu yoyote juu ya madai ya fidia ya ardhi ambao wananchi hao walipewa.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaikumbusha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi izingatie kwamba izingatie kwamba Rais Jakaya Kikwete aliahidi Julai, 2008 kuwa wananchi wa eneo hilo wangelipwa fidia stahiki pamoja na kupewa viwanja mbadala (rejea Daily News – 22 Julai, 2008). Aidha, Waziri Mkuu aliwahi kuandika barua kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya  tarehe 21 Aprili, 2010 yenye Kumb. Na. PM/P/1/569/29 ya kuelekeza mgogoro wa fidia ya ardhi umalizwe.

Mheshimiwa Spika; Ikumbukwe pia kwamba Tarehe 22 Novemba, 2010 katika kikao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Serikali iliahidi kulipa fidia zote stahiki ikiwemo fidia ya ardhi. Hii ni baada ya Wizara kuzingatia historia ya eneo husika tangu wakati wa uhuru na uwepo wa hati ya kijiji cha Kwembe kilichosajiliwa na kupewa hati No.DSM VC 40 ya tarehe 22 Februari, 1980.  Maeneo mengine yote yanayozunguka eneo hili yalipotwaliwa na mamlaka mbalimbali  yalilipwa fidia ya ardhi, mfano viwanja 600 Kwembe, Dampo Kisopwa, ekari 200 za wasioona, na mji wa mdogo Luguruni.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali hii inayojiita sikivu ya CCM; ni sababu zipi zinazofanya mpaka sasa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba na Afya (MUHAS) pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokulipa wananchi hao fidia ya ardhi mpaka hivi sasa kama Serikali ilivyoahidi? Je, serikali hii inayojiita inajali inaona fahari gani kuwa na wakimbizi wa ndani (internally displaced persons) wanaoishi baadhi katika mahema katika eneo hilo na wengine wengi wakitangatanga katika maeneo mengine baada ya kukosa walau kupewa viwanja mbadala kama Serikali ilivyowaahidi?


  • VIWANJA VYA WAZI

Mheshimiwa Spika; Kwa nyakati mbalimbali kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikihoji juu ya hatua zilizochukuliwa kurejesha viwanja vya umma (public spaces) vilivyouzwa au kubadilishwa matumizi kinyume cha sheria. Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kueleza ni lini hasa itakamilisha kuchukua hatua na ni kwanini Serikali inashindwa kusimamia utawala wa sheria na hivyo kuachia viwanja vingine zaidi kuvamiwa?

Mheshimiwa Spika; Itakumbukwa kwamba Tarehe 1 Julai 2011 katika mkutano wa nne wa Bunge kikao cha kumi na saba, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati akijibu maswali bungeni aliahidi kuweka wazi kupitia kwa Manispaa za Dar Es Salaam taarifa ya kamati ya uchunguzi ya mwaka 2010 iliyoundwa na aliyekuwa mkuu wa mkoa wakati sasa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi. Aidha, Waziri aliahidi kupitia kada ya askari wa ardhi (land rangers) kuhakikisha maeneo hayo yanarejeswa na pia maeneo mengine mapya hayavamiwi. Tangu wakati huo mpaka hivi mabango yamesimikwa katika baadhi ya maeneo mapya yaliyovamiwa na wahusika kupewa notisi bila kuvunjika huku maeneo mengine mapya yakiendelea kuvamiwa.

XXVIMUHSTASARI WA MATUMIZI YA FEDHA  ZA KAWAIDA NA MAENDELEO
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13 wizara iliidhinishiwa  jumla  ya shilingi 101,731,722,000 , kati ya fedha hizo  shilingi 10,422,891,000 zilitengwa kwa ajili ya mishahara shilingi  20,308,831,000 kwa ajili  ya matumizi mengineyo na shilingi 71,000,000,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo… hadi  februari 2013  wizara ilipokea  jumla ya shilingi 30,991,919,144. Kati ya fedha hizo  shilingi  15,505,928,393 ni fedha za  matumizi mengineyo, shilingi 6,773,240,751 ni  fedha za mishahara  na shilingi 8,712,750,000 kwa ajili ya maendeleo..
Hata hivyo ,mpaka Februari 2013  ni shilingi 2,465,731,973 kwa ajili ya miradi ya maendeleo !

Mheshimiwa Spika, niliwahi kusema hapa Bungeni, na ninarudia kusema; kama kuna eneo ambalo linaweza kutuletea uvunjifu wa Amani,kama lisipofanyiwa kazi kwa umakini mkubwa ni ardhi . Migogoro ya ardhi inachangiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu hakuna mipango utekelezaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi!Wizara hii licha ya unyeti wake ,ni kati ya wizara ambazo kwa miaka 5 mfululizo,mbali na kutengewa fedha kidogo sana za miradi maendeleo,pamoja na ufinyu wa fedha husika zimekuwa zikitolewa kidogo sana…wakati mwingine chini ya 20% ya fedha zote . Ni jukumu letu wabunge kulisimamia hili.


Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inayoongozwa na CHADEMA, naomba kuwasilisha.









______________________________________
Halima James Mdee (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA
WAZIRI KIVULI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI

Imesomwa leo, tarehe 27 Mei, 2013



1 comment: