Friday, May 17, 2013

Selasini aishukia serikali


MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini, (CHADEMA), amesema serikali imeshindwa kutekeleza ujenzi wa barabara ya Ndundu-Somanga kwa muda mrefu kutokana na kudaiwa mabilioni ya fedha.
Selasini alitoa kauli hiyo bungeni jana alipouliza swali la nyongeza ambapo alitaka kujua ni kwanini serikali inaendelea kumlea mkandarasi anayejenga barabara hiyo bila kumtoza tozo licha ya kufanya uzembe huo.
“Serikali imekuwa ikitozwa fedha nyingi kama tozo mara kwa mara kutokana na kuchelewa kuwalipa makandarasi lakini yenyewe haifanyi hivyo na badala yake imekuwa ikiwalea makandarasi ambao wanachelewesha kazi,” alisema mbunge huyo.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM), alitaka kujua sababu zinazochangia ujenzi wa barabara ya Ndundu- Somanga baina ya serikali na Kharafi & Sons Ltd kutokamilika.
Pia alitaka kujua hatua ambazo serikali imezichukua dhidi ya mkandarasi huyo kutokana na kutokamilika kwa barabara hiyo.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujjenzi, Injinia Gerson Lwenge, alisema serikali haiwezi kumtoza kodi mkandarasi wakati anaendelea na kazi.
Alisema mkataba unasema mkandarasi atatozwa tozo baada ya kumaliza kazi hiyo.
Akijibu swali la msingi, alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya Ndundu-Somanga yenye urefu wa kilomita 60 kwa kiwango cha lami ulitarajiwa kukamilika Januari 14, mwaka 2011.
Alikiri kuwa kazi haikuweza kukamilika kama ilivyopangwa kutokana na sababu mbalimbali na kuongeza kuwa hiyo ilitokana na mvua nyingi zilizonyesha kuliko kiwango kilichotarajiwa katika kipindi cha Desemba, 2009 hadi Mei 2010.
“Udhaifu wa menejimenti ya mkandarasi na kuongezeka kwa kiwango cha kazi zaidi ya zile zilizoainishwa kwenye mkataba navyo vilichangia,” alisema Injinia Lwenge.
Alisema kutokana na matatizo hayo na kulingana na matakwa ya mkataba mkandarasi aliomba na kupewa muda wa nyongeza wa siku 607 hadi Septemba 12, mwaka 2012.
Aidha, alisema serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuongeza kazi ya utekelezaji wa mradi ambazo ni kuimarisha usimamizi wa kazi, kumwelekeza mkandarasi kuongeza mitambo yenye uwezo mkubwa, kumtaka mkandarasi kuongeza saa za kufanya kazi na kumwelekeza kuongeza uwezo wake kifedha kuendelea na kazi wakati wote.
Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ya Ujenzi imetenga sh bilioni 5.288 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa barabara hiyo.

No comments:

Post a Comment