1.0. UTANGULIZI
Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba Sura ya 83 (kifungu cha 18 (3)) imetoa wajibu kwa tume wa kuunda
Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba
iliyoandaliwa na Tume.
Kifungu cha 17 (8)
kinaeleza kuwa, isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, Tume itabuni
utaratibu unaofanana ambao utatumika kila upande wa Muungano.
Kifungu cha 18 (6)
kinaeleza aina nyingine ya Mabaraza ya Katiba kwa kueleza kuwa Tume inaweza
kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya Watu kuwasilisha maoni yao kuhusu Rasimu
ya Katiba.
Ikumbukwe
kwamba Kamati Maalum ya CHADEMA ilikutana
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 7 Januari 2013 kuwasilisha maoni ya
CHADEMA kuhusu katiba mpya kama ilivyoalikwa lakini pia kutumia fursa hiyo
kuwasilisha mapendekezo ya CHADEMA kuhusu marekebisho na maboresho
yanayohitajika kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kupata katiba bora.
Tarehe 31 Januari 2013
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa kwamba imeamua kuwa Mabaraza ya
Katiba yatakuwa katika makundi mawili yafuatayo: Mabaraza ambayo Tume
itayasimamia na kukusanya Maoni (Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa) na Mabaraza
ambayo Tume haitayasimamia. Mabaraza hayo yatajisimamia yenyewe na kukusanya
maoni yatakayowasilishwa kwenye Tume kwa mujibu wa maelekezo. (Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na
Makundi ya Watu).
CHADEMA
baada ya kupitia muongozo huo na kwa kuzingatia kuwa tayari tume ilishafanya
uamuzi kuwa mabaraza ya katiba yatakuwa ya wilaya, tarehe 14 Februari 2013
kiliwasilisha maoni na mapendekezo yake kuhusu uteuzi wa wajumbe ambayo kwa sehemu kubwa hayakuzingatiwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kusababisha matatizo makubwa katika
mchakato mzima wa uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya.
Kufuatia
hali hiyo katika Maoni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu
hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa ushiriki wake
katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi
hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2013:
“Mosi; Kufutwa kwa uchaguzi wa
wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za
Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja
kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;
Pili: Serikali ilete mbele ya Bunge
hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho.”
Bonyeza Read More kuendelea
2.0
MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU MWONGOZO WA MABARAZA YA ASASI, TAASISI NA MAKUNDI
YENYE MALENGO YANAYOFANANA:
Bila kujali upungufu uliokuwepo
katika uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imetoa rasimu ya Mwongozo kuhusu Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na
Makundi yenye malengo yanayofanana; hivyo, CHADEMA kinatoa maoni kuhusu rasimu
hiyo kama ifuatavyo:
1.
Uendeshaji
(2.2) ; makundi yaliyotajwa ni yale
yanayoanzia chini mpaka taifa na taifa: wakati ambapo kuna makundi ya ngazi ya
chini pekee mathalani taasisi za jumuiya (CBOs), au taasisi iliyosajiliwa
kwenye ngazi ya wilaya au hata mitandao ambayo haijasajiliwa, hivyo wigo
upanuliwe kuruhusu makundi yote.
2.
Utaratibu
wa kutambua makundi (3.0); kipengele cha kutaka
kuwasilishwe ‘taarifa ya kusudio’
kiondolewe, kinaongeza urasimu hasa kwa kuzingatia kwamba taarifa hizo
zinawasilishwa tume makao makuu. Tume ikishatoa muongozo maana yake ni kwamba
tayari imefungua mlango kwa makundi kujadili rasimu, hivyo ngazi pekee
itayobaki iwe ni 4.0 ya kuwasilisha maoni. Hatua hii itachelewesha makundi ya
kijamii kutumia haki na uhuru wako wa kikatiba wa kujumuika na kuwasilisha
maoni.
3.
Utaratibu
wa kuwasilisha (4.0), maneno “Tarehe
zitazoelekezwa na tume ya mabadiliko ya katiba” katika sentensi ya kwanza, kwa
sababu inaweza kuleta tafsiri ya kwamba tume itayapangia tarehe za kukutana
mabaraza hayo ya makundi ya kijamii ambayo kimsingi ni kuyaingilia. Tume ipange
tu tarehe ya mwanzo wa kupokea maoni na mwisho wa kupokea maoni kwa awamu ya
mabaraza. Tarehe ya kuanza uendeshaji imeshatajwa kwenye 2.2 “wakati wowote
kuanzia tarehe itayotangazwa na tume”, tarehe ya mwisho wa kuwasilisha maoni
imewekewa utaratibu kwenye 4.0 “ maoni yatawasilishwa kwa tarehe zitazoelekezwa
na Tume”; hivyo sentensi hiyo ya kwanza haina haja ya kuwepo.
4.
Uzito
wa maoni (6.0), maelezo ya kwamba ‘maoni yatakuwa
na uzito ulio sawa’, yanapaswa kufafanuliwa; kwa mantiki ya sentensi hii ni
kwamba makundi yenye malengo yanayofanana hata yawe mengi kiasi gani yatakuwa
na uzito sawa na mabaraza yatayosimamiwa na tume ambayo tayari
yameshalalamikiwa kwamba yana hodhi ya chama kimoja na hayana uwakilishi wa
moja kwa moja wa wananchi. Hivyo, tafsiri itolewe ambayo itahakikisha kwamba
maoni ya wengi na matakwa ya umma yatatamalaki.
5.
Tume
kualikwa kusikiliza; Pamoja na kwa mujibu
wa kipengele 2.2 mabaraza ya makundi yenye malengo yanayofanana ‘yatajisimamia
na kujiendesha yenyewe’, pawepo na kipengele kwamba iwapo asasi, taasisi au
kundi husika linaweza kuomba tume itume maafisa wake kuangalia/kusikiliza moja
kwa moja ziada/zaidi ya utaratibu uliotajwa kwenye 4.0
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO JUU YA MASUALA MENGINE
KUHUSU UENDESHAJI WA MABARAZA NA UTOAJI MAONI JUU YA RASIMU:
Aidha,
pamoja na maoni kuhusu muongozo; CHADEMA kinatoa maoni ya ziada kwa Tume
kuzingatia yafuatayo:
·
Muongozo wa kwanza uliotolewa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulihusu “Muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa
mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji
wake”. Hata hivyo, muongozo uliotolewa ulijikita katika muundo wa mabaraza na
mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa mabaraza hayo, lakini haujatoa maelezo na
maelekezo ya kutosha kuhusu namna mikutano ya mabaraza ya katiba ya wilaya
itavyoendeshwa na utaratibu mzima utakaotumika kujadili rasimu ya katiba mpya
katika mabaraza hayo. Aidha, CHADEMA kinapendekeza kwa mara nyingine kwamba
tume itoe muongozo mwingine mahususi kuhusu uendeshaji wa mabaraza ya katiba
ikiwemo utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili rasimu katika mabaraza; aidha
kabla ya muongozo huo kuanza kutumika wananchi wapewe nafasi ya kutoa maoni na
mapendekezo kama ilivyokuwa kwa muongozo huu kuhusu uteuzi wa wajumbe.
·
Kwa kuwa mpaka awamu ya
nne ya ukusanyaji maoni ya wananchi binafsi ilipokamilika wananchi waliotoa
maoni kwa njia ya simu walikuwa 16,261 tu kati ya idadi ya wateja wa makampuni
ya simu za mkononi ambao watajwa kuwa zaidi ya milioni 20 (mobile phone
subscribers); Tume ya Mabadiliko ya Katiba iweke mfumo wa wananchi binafsi
kuweza kutoa maoni kuhusu rasimu ya katiba kupitia simu za mkononi. CHADEMA
kinarudia kutoa mwito kwa tume kushirikiana na makampuni ya simu
kuwezesha ujumbe wa simu ya mkononi kutumwa kwenye kila mtanzania mwenye simu
kumpa dondoo juu ya rasimu ya katiba na kumpa namba anazoweza kutuma maoni kwa
njia ya simu na pia maelekezo ya namna ya kutuma ujumbe wa bure wa maoni yake.
Hii itafanya wananchi wengi kuweza kushiriki kutoa maoni. Aidha, pawepo na
uwazi katika mfumo mzima wa maoni yanayokusanywa kwa njia ya simu na mitandao
mingine ili kusiwe na uwezekano wa ‘kuchakachua’.
4.0 HITIMISHO:
Pamoja
na kuwasilisha maoni na mapendekezo haya izingatiwe kuwa madai ya Kambi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA kuhusu kufutwa kwa chaguzi za mabaraza na
kuwasilishwa bungeni kwa muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya
mabadiliko ya katiba katika mkutano wa kumi na moja wa Bunge unaoendelea
hayajatimizwa.
Waziri
Mkuu aliahidi (wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri ) kwamba Serikali
italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya
mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti.
CHADEMA
kinasubiri ahadi hiyo kutekelezwa katika kipindi hiki ambacho kitaenda sambamba
na Tume kutoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya kwa ajili ya kuanza kujadiliwa na
Watanzania.
Endapo
hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada wa
marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya
kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya; basi CHADEMA itawaalika
wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima, pamoja na taasisi za
kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania wote wenye nia njema na
taifa hili kuhamasisha umma kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni
itakayofanyika kwa ajili ya kuihalalisha Katiba hiyo mbovu.
Naomba
kuwasilisha,
John
Mnyika (Mb)
Kny.
Katibu Mkuu
19/05/2012
No comments:
Post a Comment