Tuesday, May 21, 2013

Sugu atibua Bunge


Hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu Makadirio na Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, jana ilisababisha shughuli za Bunge kusitishwa kwa muda, kwa kile kilichoelezwa kuwa imejaa maneno ya uchochezi.

Hotuba hiyo iliyokuwa ikisomwa na Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, maarufu kama Mr. Sugu, ilisitishwa mara baada ya Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Erasto Zambi, kuomba mwongozo.

Zambi aliomba mwongozo kupitia kifungu cha 68 (1) na Kanuni ya Bunge ya 6 (a), akisema kuwa Mbunge aliyekuwa akiendelea kutoa hotuba anatoa maneno ya uchochezi ambayo hayawezi kuvumiliwa.

Zambi alisema kuwa katika ukurasa wa kwanza hadi wa 14 wa hotuba hiyo kumejaa maneno ya uchochezi yanayosema kuwa serikali ya CCM inafanya vitendo vya kiharamia vya kuwateka na kuwatesa waandishi wa habari kwa kuwango’a meno, macho na kuwatoa kucha.

Baada ya Zambi kuomba mwongozo huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema analazimika kuahirisha kikao hicho cha Bunge ili hotuba hiyo ya kambi ya upinzani ikafanyiwe marekebisho kabla ya kusomwa tena.

“Sisi wenyewe juzi hapa tumepitisha azimio la kukataa mambo ya uchochezi humu, sasa nasitisha kikao cha Bunge hadi jioni ili kamati ya kanuni ya Bunge ikae na kufanyia marekebisho hotuba hii,” alisema Makinda.


Bonyeza Read More Kuendelea




Kwenye hotuba yake, Sugu alisema Tanzania imeingia rasmi katika orodha ya fedheha ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni taaluma ya hatari kwa wale wote wanaoitumikia kama sehemu ya wajibu wao kwa taifa na kama ajira kwao.

Katika hotuba yake, Sugu alisema kuna ushahidi kwamba serikali ya CCM na Jeshi la Polisi wamekuwa wakihusika na kuwaua na kuwaumiza waandishi wa habari wanaoandika habari zisizowapendeza  viongozi  wa serikali na Jeshi la Polisi.

Alisema miezi sita baada ya kuuawa kwa Daudi Mwangosi, mwandishi mwingine mwandamizi, Absalom Kibanda, alitekwa nyara na kuteswa vibaya nje ya nyumba yake.

Sugu alisema Kibanda alitekwa na kuteswa baada ya nyendo zake kufuatiliwa na polisi na watu wengine wanaodhaniwa kuwa ni watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS).

Alisema badala ya kuchukua hatua za dhati na kuwachukulia hatua waliohusika na tukio hilo la kigaidi, Jeshi la Polisi likishirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa, maofisa wandamizi katika Ofisi ya Rais Ikulu na viongozi wandamizi wa CCM walianzisha kampeni ya kuichafua Chadema.

Sugu alisema CCM iliamua kuanza kumsingizia Mkurugenzi wa Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare kwa madai ya kuhusika na ugaidi kutokana ushahidi wa kutunga tunga.

Sugu alisema kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari Ulimwenguni (CPJ), iliyotolewa mwaka huu 2013, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa CPJ mwaka 1992, Tanzania imeingizwa kwenye orodha ya nchi 20 ambazo ni hatari kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao kutokana na hatari ya kuuawa kwa mwaka 2012.

Alisema kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania ilishikilia nafasi ya saba ulimwenguni kati ya nchi 20 zinazoongoza kwa kuhatarisha maisha ya waandishi wa habari. Mbunge huyo alisema kwa mujibu wa taarifa ya CPJ, tishio kubwa kwa waandishi wa habari duniani ni kuuawa kwa kutekwa na kuteswa au kutishiwa maisha.

Aidha, alidai kwamba serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni washiriki wakubwa wa mauaji ya waandishi wa habari na kwa  mujibu wa takwimu za CPJ, kati ya waandishi waliouawa mwaka 2012, karibu asilimia 20 waliuawa ama na maafisa wa serikali au na majeshi yake.

Alisema karibu idadi hiyo hiyo ya waandishi wa habari waliuawa kwa sababu ya kufuatilia taarifa za kiuchunguzi na za hatari na taarifa hiyo inaonyesha kwamba hadi kufikia Aprili 2013, waandishi wa habari wapatao 30 tayari wamekwishauawa ulimwenguni wakati wakitimiza wajibu wao wakati mwaka 2012 waandishi wa habari 103 waliuawa ulimwenguni kote.

Baada ya Bunge kurejea jioni, Spika Makinda alitoa maelekezo kwa Kambi ya Upinzani kutosoma ukurasa wa kwanza hadi wa 14, lakini Sugu alisoma hotuba yake kuanzia ukurasa wa 12 na kuzimiwa kipaza sauti.

Baada ya kuimaliza, Zambi alisimama kuomba mwongozo wa Spika akitaka aelezwe ni jambo gani lilisababisha maelekezo ya Spika ya kubadilisha hotuba hiyo yasitekelezwe huku akilalamikia hatua ya Sugu kuisoma bila kufanyiwa marekebisho.

Hata hivyo, Spika alisema kuwa hotuba hiyo haitakuwa katika kumbukumbu za hansard.

DK. SLAA AJA JUU
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, amesema ikibidi Bunge livunjike au wabunge wa chama hicho wafukuzwe bungeni, lakini hawako tayari kuzibwa mdomo kuzungumzia masuala yanayohusu maisha ya Watanzania.

Amesema chama hicho hakitakubali wabunge wake wapangiwe mambo ya kuzungumza kwa kutegemea busara za Spika au Naibu Spika, bali wataangalia na kufuata maelekezo ya kanuni za Bunge, akisema ndiyo msingi wa uendeshaji wa chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi.

Akizungumza katika mikutano ya hadhara jana katika maeneo ya Ngalangala, Basotu, wilayani Hanang na Haydom, wilayani Mbulu, kuhusiana na  hotuba ya Sugu kuahirisha Bunge, Dk. Slaa alisema wabunge wa chama hicho daima wataendelea kuwasemea Watanzania wanyonge ndani na nje ya Bunge.

“Moja ni tukio lililotokea leo (jana) bungeni. Kwa wale mliofuatilia mkutano wa Bunge mliona kilichotokea. Ninachotaka kumwambia Spika na wasaidizi wake bungeni ni kwamba Bunge linaongozwa kwa kanuni za bunge, si vinginevyo.

Uamuzi aliofanya wa kuagiza hotuba ya wabunge wetu ipelekwe kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge ni kinyume na kanuni ambazo ndizo msingi wa utendaji kazi wa bunge. Hakuna sehemu yoyote katika kanuni inampatia mamlaka Spika ya kupeleka hotuba ile kwenye kamati hiyo, ili waelekeze nini kisemwe. Hakuna,” alisema Dk. Slaa.

Alisema kuwa baada ya mawasiliano ya viongozi wa juu wa chama hicho na uongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, walikubaliana kuwa kwa sababu hotuba hiyo haikuvunja kanuni yoyote ile ya Bunge, hawatakubali kuondoa au kupunguza neno hata moja.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

  1. Chadema ni chama cha Mungu. Kinatuletea ukombozi wa Kisiasa, Kiuchumu na Kiutamaduni. Mungu Ibariki Chadema

    ReplyDelete