Thursday, May 23, 2013

Kambi ya Upinzani yamwibua Jairo, Richmond

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeibua upya sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo na Richmond, huku ikilishutumu Bunge kwamba, limeshindwa kusimamia utekelezwaji wa maazimio yake.

Imesema tatizo hilo ni uzembe wa wazi wa Bunge kushindwa kutimiza majukumu yake ya kuisimamia serikali kwa mujibu wa Katiba ya nchi. 

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, aliibua hayo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2012/13 na makadirio na matumizi ya bajeti ya mwaka 2013/14.

Aliitaka serikali kulieleza Bunge hatua za utekelezaji wa maazimio ya Bunge, kwani baadhi ya wahusika bado wapo maofisini wakiendelea na kazi na wengine wakiendelea kuteuliwa kushika nafasi nyingine katika uongozi na utumishi wa umma, kama vile hakuna liliowahi kutokea.

Alisema Bunge liliazimia kwamba, taarifa za utekelezaji wa maazimio yaliyobaki ya Richmond ziwasilishwe kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ambayo hata hivyo katika mwaka 2011, 2012 na mpaka mabadiliko ya muundo wa kamati yalipofanyika, kamati hiyo haikuwasilisha taarifa yoyote bungeni ya kueleza kukamilika kwa utekelezaji wa maazimio husika.

Alisema hali hiyo inahitaji Bunge kuingilia kati kuisimamia serikali kwa mujibu wa Katiba ya nchi Ibara ya 63 (2) na (3).

Alisema kutokana na hukumu ya Dowans, ushahidi umepatikana kuwa mashahidi walioitwa mbele ya Kamati Teule ya Bunge na wakiwa chini ya kiapo, walitoa taarifa za uwongo kuwa mkataba kati ya Richmond na Tanesco ulihamishwa kwenda Dowans Desemba 23, 2006.

Mnyika alisema wahusika hao, wakiwamo wamiliki wa Richmond, walidanganya au kuficha ukweli mbele ya Kamati Teule na hivyo kuonyesha dharau dhidi ya Bunge.

Alisema masuala hayo ni muhimu yakajadiliwa sasa ili kupata undani wa wahusika wanaopaswa kubeba mzigo wa fidia kwa kampuni ya Dowans badala ya kubebesha mzigo huo Tanesco na umma wa Watanzania. 

Aliitaka serikali kutoa kauli kuhusu sababu za ucheleweshaji katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme  na kushindwa  kubadilisha mfumo wa majenereta kutumia gesi badala ya mafuta, na kama kweli dharura iliyokuwepo bado ipo au imekwisha.

Mnyika alisema taifa linahitaji kuwa na angalizo kubwa ikiwa ni pamoja na kutochimba madini hayo ya aina ya urani kutokana na uhatari wake kwa maisha ya binadamu.

No comments:

Post a Comment