VURUGU za kupinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam jana zilimlazimisha Spika wa Bunge, Anne Makinda, kusitisha kikao cha Bunge.
Lengo la uamuzi huo ni kutoa fursa kwa serikali kupeleka taarifa rasmi bungeni leo kuhusu tukio hilo.
Hatua hiyo ilikuwa baada ya wabunge kurejea kutoka katika mapumziko ya mchana ili kuendelea na mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Hata hivyo, kabla ya kikao hicho kuanza baadhi ya wabunge walionekana katika makundi wakijadiliana kuhusu vurugu hizo huku wengine wakizungumza na ndugu zao kwa simu ili kujua hali inavyoendelea mkoani Mtwara.
Baada ya kikao kuanza baadhi ya wabunge walisimama kwa ajili ya kuomba mwongozo lakini Spika aliwaomba wakae chini na kisha akatoa taarifa fupi ya kile kilichokuwa kikiendelea.
“Kuanzia wiki ile taarifa zilipotolewa kuwa wizara itajadiliwa, naambiwa watu wa Mtwara walijiandaa kufanya vurugu. Na kweli tangu tumeanza kufanya shughuli hii huko vurugu zinaendelea.
“Sasa najua wengi mnataka tujadili jambo hilo…nakubali, lakini tutajadili yale tuliyoyaona kwenye vyombo vya habari. Naiagiza serikali kesho (leo) ilete taarifa kuhusu hali halisi iliyopo Mtwara,” alisema.
Kabla ya Spika Makinda kuliahirisha Bunge aliitisha kikao cha Kamati ya Uongozi wa Bunge kupanga utaratibu wa shughuli zao pamoja na kuangalia vurugu za Mtwara.
“Mtakumbuka suala hili tulikuwa hatujalimaliza wakati ule niliivunja Kamati ya Nishati na Madini, sasa itabidi tukutane,” alisema Spika.
Bonyeza Read More Kuendelea
Mjadala bungeni
Muda mfupi baada ya Bunge kuahirishwa, wabunge walijikusanya katika makundi madogo madogo wakiwa wanajadili hali ya Mtwara na kuitaka serikali ichukue hatua za makusudi kufuatilia mgogoro huo.
Baadhi ya wabunge walisikika wakitofautiana kuhusu vurugu hizo ambapo wengine walisema zinachochewa na wanasiasa huku wenzao wakidai kampuni za mataifa za Magharibi ndizo zipo nyuma, kutokana na kuipiga vita Serikali ya China ambayo kampuni zake ndizo zitawekeza kwenye mradi huo kwa asilimia kubwa.
Rais Kikwete aonya
Rais Jakaya Kikwete alisema waliohusika na vurugu zilizotokea Mtwara watashughulikiwa hata kama watakuwa na pembe zitakatwa.
Kikwete alitoa kauli hiyo mkoani Dodoma alikokuwa kwa ajili ya uzinduzi na uwekaji wa jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya Dodoma-Fufu yenye urefu wa kilometa 70.9.
Kabla ya kutoa kauli hiyo, Rais Kikwete ambaye aliwasili jana jioni alilazimika kuacha jukwaa kwa muda wa dakika zaidi ya 15 na kwenda kando kwa ajili ya kuzungumza na simu.
Licha ya gazeti hili kutonasa moja kwa moja mazungumzo hayo ambayo yalifanyika huku akiwa amezungukwa na maofisa kadhaa wa Usalama wa Taifa, chanzo chetu kilisema kuwa alikuwa akiwasiliana na viongozi wenzake kuhusu vurugu hizo.
Hata hivyo baadaye kiongozi huyo alisema vurugu hizo hazivumiliki na serikali itawashughulikia wote waliohusika.
Mjadala bungeni
Wakati Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ikiitaka serikali isiendelee na ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, alisema ni lazima gesi hiyo itoke huko, huku akibainisha faida za kiuchumi zitakazopatika.
Msigano huo ulitokea jana bungeni wakati waziri huyo alipowasilisha hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2013/2014 na kuelezea mipango mbalimbali ikiwamo sekta ya gesi.
Waziri Muhongo alisema kuwa umeme ni uchumi, hivyo hawawezi kukuza uchumi kama wananchi hawana nishati hiyo, hasa wale wa vijijini.
Alisema bomba hilo lina uwezo wa kusafirisha futi za ujazo wa gesi asilia milioni 784 kwa siku na kwamba mradi huo utagharimu sh bilioni 1,960.
“Kazi za usanifu wa mradi na ulipaji fidia kwa wananchi wapatao 3,092 waliopisha maeneo ya mradi zimekamilika. Aidha, hatua za awali za ujenzi wa mitambo ya kusafirisha gesi asilia zimeanza,” alisema.
Waziri alifafanua kuwa ujenzi wa miundombinu hii utaleta manufaa makubwa kwa taifa, na kwamba hadi sasa mikoa ya Lindi na Mtwara imepata manufaa mbalimbali yatokanayo na miradi ya gesi asilia, ikiwa ni pamoja na tozo ya asilimia 0.3 ya mauzo ya gesi hiyo.
Pia alitaja faida nyingine kuwa ni huduma za jamii kama zahanati, shule, umeme, maji na ufadhili wa mafunzo katika vyuo vya ufundi (VETA) na sekondari.
Aliongeza kuwa pia kutakuwa na ujenzi wa viwanda mbalimbali, kikiwamo kiwanda cha saruji cha Kampuni ya Dangote ambacho ujenzi wake umeanza, kiwanda cha mbolea na mtambo wa kufua umeme wa MW 400.
Kuhusu utafutaji wa gesi asilia na mafuta, Waziri Muhongo alisema kuwa kwa mwaka 2013/2014 serikali imeamua kwamba zabuni ya awamu ya nne ya kunadi maeneo mapya ya uwekezaji katika kina kirefu cha bahari ifanyike hapa nchini Oktoba 25, mwaka huu.
Wapinzani wapinga
Hata hivyo kambi ya upinzani imepinga mikakati hiyo miwili ya kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na ugawaji wa vitalu vya utafutaji wa gesi na mafuta huku ikibainisha hatua zinazopaswa kufanyiwa marekebisho.
Akisoma maoni ya kambi hiyo, msemaji mkuu kwa wizara hiyo, John Mnyika (CHADEMA), alisema kuwa ili bomba la kusafirishia gesi asilia liweze kujengwa ni lazima kwanza serikali iweke wazi kwa Bunge mikataba yote inayohusu uendelezaji wa gesi asilia ikiwamo ya ujenzi wa bomba hilo.
Pili, Mnyika alisema kuwa serikali ikutane na wananchi kuwashirikisha na kuhakikisha manufaa kwa taifa na kwao.
Alisema kuwa pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asilia Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kuitaka serikali kueleza ni miradi ipi iliyotengewa fedha inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Jitahidini kuepuka mtego wa kutaja neno CCM wakati wabunge wenu wanachangia kwenye hoja mbalimbali bungeni kwani kwa kufanya hivyo mnakosa support ya wabune wa CCM kwani mnawaprovoke kwa kutaja neno CCM.Mfano hoja ya gesi Mtwara wabunge wa CCM wanapingana na serikali yao, lakini mnaposema serikali ya CCM dhahiri wanakuwaprovoked, then hawezi kukusupport ingawa anaintrest sawa nayenu!
ReplyDeletejaman penye ukwel uongo ujitenga achana na masilai ya chama utasemaje kunufaika kwa wanamtwara kwa kutajataja mirad watakayo nufaikanayo bila kutaja kias kilichotengwa kwa kufanikisha mirad hyo achen ujinga wakua mnashabkiashabkia bila kujua mambo ujinga utawaisha lin?
ReplyDelete