MWANASIASA mkongwe, Dk. Salim Ahmed Salim, amesema kuporomoka kwa maadili ya uongozi na maadili ya utaifa yamechangia umoja, usawa, amani na utulivu kumomonyoka.
Kauli hiyo aliitoa visiwani Zanzibar mwishoni mwa wiki mara baada ya uzinduzi wa tawi jipya la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Dk. Ali Mohamed Shein, eneo la Bububu, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Dk. Salim alisema Watanzania wanapaswa kuzingatia maadili ya uongozi na kuzingatia maadili ya utaifa aliyoyaacha Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere.
Alibainisha kuwa jambo muhimu kwa Watanzania ni kuzienzi tunu za taifa ambazo ni umoja, usawa, amani na utulivu vilivyojengwa kwa muda mrefu hapa nchini.
“Tuna matatizo makubwa kwenye eneo la maadili ya uongozi na maadili ya utaifa,..…ninawashauri Watanzania wenzangu tujikumbushe maadili yaliyofundishwa na Mwalimu Nyerere,” alisema.
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, alisema viongozi wengi hivi sasa hawafuati misingi ya uongozi aliyoiacha Mwalimu Nyerere.
Alisema malumbano ya kidini yanayotokea hivi sasa hapa nchini ni uthibitisho wa kupotea kwa misingi ya umoja, usawa, amani na utulivu.
Mkuu wa Chuo cha Mwalimu Nyerere, Dk. Chinuno Magoti, alisema kwa kutambua umuhimu wa falsafa ya Mwalimu Nyerere kuhusu usawa, umoja, amani na utulivu, chuo hicho kinatoa mafunzo kwa kumuenzi Mwalimu kwa vitendo.
No comments:
Post a Comment