Wednesday, May 8, 2013

CHADEMA YABUNI MKAKATI WA KUJIIMARISHA UCHAGUZI MKUU UJAO


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema watakipa pigo takatifu Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa serikali na mitaa na mkuu utakaofanyika mwaka 2015.
Dk. Slaa anasema wanazijua mbinu zote za CCM zinazofanywa kuiua CHADEMA zinazolenga chaguzi zijazo lakini kamwe hazitofanikiwa na badala yake wataambulia pigo zito.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Slaa alisema CCM sasa itarajie pigo zito zaidi kutoka CHADEMA kuliko lile ililolipata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ilipopoteza viti vingi vya ubunge na udiwani.
“CHADEMA tumejifunza mbinu zote za CCM, ndio maana tunaenda sasa zaidi ya msingi (balozi wa nyumba kumi) ambako ndiko CCM ilikokuwa inapatia ushindi.
“Sisi tutawafikia mabalozi (misingi) 250,000 kila mtaa nchini, mahali ambapo kila mara CCM imekuwa ikijidai kuwa ndio mitaji ya kura zao inapatikana, tutakuwa na mabalozi katika misingi ambayo CCM huita nyumba kumi, kwa hiyo tutakabana kuanzia ngazi ya nyumba kumi.”
Aliongeza kuwa ili kutekeleza mkakati huo CHADEMA kina mpango wa kuwapeleka katika mafunzo viongozi 36,000 hadi kufikia mwishoni mwa Juni mwaka huu katika ngazi mbalimbali kuanzia kanda, mikoa, wilaya hadi kata.
“Tutafanya mazoezi kujifua, kujipatia mafunzo ya sera zetu, na hili sio jambo la siri ambalo hata watu wa usalama wa taifa wanaweza kuanza kuhangaishwa nalo.”
Akizungumzia kuhusu viongozi kununuliwa katika mchakato na wengine kuhama Dk. Slaa alisema mamluki watakuwa na wakati mgumu sana kwani CHADEMA itatoa tangazo kwenye vyombo vya habari wenye kutaka kugombea watangaze nia.
Aliongeza kuwa wagombea hao watachujwa kwa vigezo vya uadilifu, uaminifu wao kwa jamii na kwa chama sambamba na kufanya mithani mbalimbali kabla ya kuteuliwa kuwa wagombea.
“Huwezi kumwambia mtu aliyeingia kwa pesa kwenye uongozi mkajenge nchi, tunataka watu waadilifu…, CHADEMA zamu hii tumejipanga zaidi kubaini hata mbinu za kutengeneza vituo hewa ambavyo huwa vinatoa fursa ya kura kuongezwa bila utaratibu.”
Dk. Slaa aliongeza kuwa sasa Watanzania wako tayari kwa mabadiliko huku akibanisha kuwa zama za kuwanunua kwa kofia, fulana, vitenge umepitwa na wakati.
Alisema hawako tayari kununuliwa kwa vitu hivyo vidogo kwa sababu watoto wao wanaishi maisha magumu, hawana elimu bora, hawana madawati shuleni, na mfumko wa bei unaosababisha maisha kuwa magumu.
“CCM ilizoea kununua wananchi; zamu hii itakuwa na wakati mgumu, ilizoea kuiibia 
CHADEMA sasa mambo ni magumu ijiandae kwa pigo kuu,” alisema.
Wakati Dk. Slaa akiweka mikakati ya CHADEMA, Tanzania Daima Jumatano, limedokezwa na baadhi ya vigogo wa CCM kuwa kuimarika kwa chama hicho kikuu cha upinzani kunahatarisha mustakbali wa chama hicho tawala.
Uchuguzi wa gazeti hili umebaini kuwa CCM kwa sasa inatumia kila mbinu bila kujali madhara yatakayowapata wananchi ili mradi kuhakikisha CHADEMA inasambaratika kabla ya 2015.

Bonyeza Read More Kuendelea



Chanzo chetu kimedokeza kuwa baada ya mipango mingi kukwama dhidi ya CHADEMA, vigogo wa serikali na CCM wameshauri mikakati hiyo igeuziwe bungeni ili kudhibiti wabunge wa CHADEMA.
Uimara wa CHADEMA umeshamiri zaidi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 baada ya kupata wabunge wasiopungua 48 kutoka wabunge 11 mwaka 2005-210.
“Kwa sasa chama chetu kinakatisha tamaa maana viongozi wetu ni kama wamechanganyikiwa na hivyo wanaibua mbinu za kitoto wakidhani wanaweza kuisambaratisha CHADEMA.
“Kumbuka walikuja na wazo la kutaka Bunge lisionyeshwe moja kwa moja wakisingizia kuwa wabunge wa CHADEMA wanafanya vurugu na kutukana lakini limeshindikana baada ya Spika kubaini wabunge wenye shida ni wa CCM,” kilisema chanzo hicho.
Tanzania Daima Jumatano pia limedokezwa na baadhi ya wabunge wa CCM kutoridhishwa na mwenendo wa baadhi ya mawaziri wakati wa kuhitimisha hoja zao, wanatumia muda wote kujibu hotuba ya maoni ya msemaji wa upinzani na kuacha kufafanua za wabunge wengine.
Wabunge hao wanasema kuwa hotuba za wapinzani ni maoni mbadala na ushauri kwa serikali, hivyo wajibu hoja wanapaswa kuchagua mambo ya kuchukua na kufanyia kazi badala ya kuishia kuwashambulia CHADEMA na kushindwa kueleza serikali imefanya nini.
Kutokana na vitendo vya vurugu za udini vinavyoanza kushika kasi katika maeneo mengi nchini, CCM imeanza kukosa kauli kulizungumzia jambo hilo ambalo mara zote imekuwa ikilitumia kama silaha ya kuvidhoofisha vyama vya upinzani.
Kwa sasa wabunge wa upinzani hususan CHADEMA, wameikalia kooni serikali ya CCM bungeni kila wakati wakiitaka ifanye kila mbinu kutokomeza vurugu za kidini na za kisiasa.
Mwaka 2005 wakati CUF ikiwa chama kikuu cha upinzani nchini, CCM ilieneza chuki kwa wananchi ikidai CUF ni chama cha Waislamu wenye itikadi kali wenye asili ya Pemba.
Na muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu, aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Omary Mahita, alijitokeza mbele ya waandishi wa habari akiwa na visu alivyodai vimeingizwa nchini na CUF ili kufanya vurugu.
Madai hayo ya CUF yalihamia kwa CHADEMA baada ya chama hicho kuonyesha upinzani mkubwa kwa CCM mwaka 2010. Viongozi wakuu wa serikali na CCM wameuaminisha umma hadharani kuwa CHADEMA ni chama cha Wakristo, Wakatoliki na Wachagga.
Sasa kauli hizi zinaitesa CCM baada ya wananchi kuanza kubaguana kwa misingi ya udini na ukabila.
Chanzo chetu kimedokeza kuwa kete hiyo ya udini haina tena tija kwa CCM na katika kujinasua ilijaribu kuibua tuhuma za ugaidi kwa kuidhoofisha CHADEMA lakini baada ya mjumbe wa Baraza Kuu wa CHADEMA, Mabere Marando, kufichua siri za mkakati huo, mpango huo umeyeyushwa.
Mbunge mmoja machachari wa CCM ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, aliliambia gazeti hili kuwa kwa sasa chama hicho kimebakiza silaha moja ya mchakato wa Katiba mpya ili kuisambaratisha CHADEMA.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, CCM ilidhamiria na kupanga mbinu za kuvuruga uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya Katiba makusudi ili kuhakikisha inaingiza watu wake wengi kwa lengo la kukamilisha ajenda yao.
“Utaona hata juzi bungeni wakati tukipitisha makadirio ya Wizara ya Katiba na Sheria, wabunge na mawaziri walichachamaa kuwa kuikejeli CHADEMA na kupongeza uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza, wanajua kuwa wamefanikiwa ngazi ya kwanza,” alisema.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, CCM imepanga kutumia sababu za hapa na pale ili kuchelewesha mchakato huo kwa lengo la kumwongezea muda wa miaka miwili zaidi Rais Jakaya Kikwete.
Kwamba katika muda huo, CCM inataka kuhakikisha inatengeneza tuhuma za kuidhohofisha CHADEMA ili kufikia uchaguzi mkuu, wananchi wakione chama hicho hakifai.
“Umesikia wanataka kuleta muswada wa kuzuia mikutano ya kisiasa na maandamano. Hapa wanalengwa CHADEMA maana kusema kweli hawa jamaa wamefanya mikutano mingi ya kujieneza mikoani hadi ngazi za shina ambazo CCM ilikuwa ikitambia,” alisema.

No comments:

Post a Comment